Featured Posts

Showing posts with label EDWARD LOWASSA. Show all posts
Showing posts with label EDWARD LOWASSA. Show all posts

Thursday, November 28, 2013

Makala yangu ktk RAIA MWEMA Toleo la 27.11.13: "Nani Kinara wa CCM Urais 2015 - Part Two"


MAKALA hii ni mwendelezo wa ile iliyochapishwa katika toleo lililopita la gazeti hili, iliyobeba kichwa cha habari ‘Nani kinara wa CCM urais 2015?’
Lakini kabla sijaingia kiundani, nadhani ni vema nikarejea nilichoandika katika makala iliyopita kuhusu kukua kwa uwezekano wa CCM kubaki madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao. Wiki iliyopita ilishuhudia chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, kikiingia katika mtafaruku mkubwa ambao licha ya kutishia uhai wake unazidi ‘kupapalia’ mazingira mwafaka ya ushindi kwa CCM.
Awali, CHADEMA ilitangaza kuwavua madaraka viongozi wake waandamizi watatu, Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba na kuwapa siku 14 kujieleza kwa nini wasivuliwe uanachama baada ya kupatikana kwa nyaraka inayodaiwa kulenga kukihujumu chama hicho.
Jumapili iliyopita, Zitto na Kitila waliitisha mkutano na waandishi wa habari ambao kimsingi haikusaidia japo kupunguza moto unaozidi ‘kuunguza nyumba ya CHADEMA.’ Kwa kifupi, wanasiasa hao wawili walipinga vikali shutuma zilizoelekezwa kwao na kuhalalisha kile kilichotafsiriwa na uongozi wa chama hicho kama hujuma, huku wao wakibainisha kama matumizi ya demokrasia kwa minajili ya kuiboresha CHADEMA.
Pasi haja ya kuingia kwa undani katika sokomoko hilo, ni wazi kwamba uamuzi wa kuwavua madaraka viongozi hao na msimamo uliotolewa na ‘wahanga’ hao unaendeleza mapambano ya madaraka ndani ya CHADEMA. Kubaki au kuondoka kwa akina Zitto hakuwezi kukirejesha chama hicho katika mahala kilipokuwa. Kibaya zaidi, japo hakuna tathmini yoyote iliyokwishafanywa kuhusu athari za mgogoro huo, ni wazi Watanzania wengi wameanza kupoteza matumaini kwa chama hicho kilichotarajiwa sio tu kutoa upinzani mkubwa kwa CCM bali pia hata kuweza kuingia Ikulu mwaka 2015.
Nihitimishe suala hili la CHADEMA kwa kutanabaisha kuwa japo inafahamika kuwa lolote linawezekana katika siasa, ukweli kwamba tumebakiwa na takriban mwaka na ushee tu kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, sambamba na ukweli kuwa hakuna dalili ya mgogoro huo wa CHADEMA kumalizika hivi karibuni, itakuwa vigumu mno kwa chama hicho kujipanga upya na vyema, kuweza kutoa ushindani wa maana katika Uchaguzi Mkuu ujao. Nitaijadili kwa kirefu hatma ya CHADEMA katika makala zijazo.
Tukiendelea na mada ya urais kwa tiketi ya CCM, niliahidi kuwa wiki hii nitajadili ‘odds’ (uwezekano wa kufanikiwa au la) zinazowakabili wanasiasa wawili ambao tathmini yangu inawaona kama ndio vinara katika mbio za kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete kupitia CCM, yaani Edward Lowassa na Bernard Membe.
Pengine hadi siku chache zilizopita, kikwazo kikubwa kwa wote wawili kingeweza kuwa uwezekano wa CCM kubwagwa na CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu ujao. Lakini kwa kuzingatia mwenendo ulivyo katika chama hicho kikuu cha upinzani, yayumkinika kuhitimisha kuwa kikwazo hicho ni kama kimekufa kifo cha asili.
Kwa upande wa Lowassa, doa kubwa linaloonekana kuendelea ‘kuchafua’ jina na wasifu wake ni tuhuma za ufisadi wa Richmond. Bila kujali kuwa uamuzi wake wa kujiuzulu uwaziri mkuu kufuatia kashfa hiyo ni ‘kutolewa kafara’ au ‘alivuna alichopanda,’ tafsiri ya haraka kwa wananchi wengi wa kawaida inabaki kuwa ‘ni vigumu kumtenganisha mwanasiasa huyo na moja ya matatizo makubwa kabisa yanayoikabili nchi yetu, yaani ufisadi.’
Ukweli kwamba Tanzania yetu sio tu ni moja ya nchi masikini sana bali pia inazidi kuwa masikini huku ufisadi ukizidi kushamiri, umesababisha kujengeka kwa hisia (pengine zisizopendeza) kuwa kila mwenye uwezo wa kifedha ni fisadi. Hisia hizo hazimsaidii Lowassa ambaye kwa siku za hivi karibuni amekuwa mstari wa mbele katika harambee za kuchangisha mamilioni ya fedha hususan kwenye taasisi za dini. Badala ya ukarimu wake kumjenga kama kiongozi anayejali, kuna wanaotafsiri jitihada zake hizo kama ‘rushwa’ ya kutaka urais mwaka 2015.
Kadhalika, kuna hisia hasi kuwa hata hizo fedha anazotoa kusaidia miradi mbalimbali ‘ni chafu’ kwa maana ya hisia kuwa huenda ni zile zilizotokana na tuhuma za ufisadi. Kibaya zaidi, kutofahamika chanzo cha kinachotajwa kama utajiri mkubwa wa mwanasiasa huyo kunaimarisha hisia hizo za ufisadi.
Vile vile, na hili linawagusa wote-Lowassa na Membe- ukweli kwamba wanasiasa hao wanatajwa kama sehemu muhimu ya ‘mtandao’ uliomwingiza madarakani Rais Kikwete mwaka 2005, unaleta hisia za ‘mvinyo mpya kwenye chupa ya zamani’ (kwa wasiofahamu, thamani ya mvinyo inaelemea sana kwenye ‘ukale’ wake na si upya wake)
Sasa, kama tukiafikiana kuwa mtizamo wa Watanzania wengi ni kuwa utawala wa Kikwete (ambao uliingizwa madarakani na ‘mtandao’ uliowashirikisha Lowassa na Membe) umetawaliwa zaidi na tuhuma za ufisadi huku hali ya maisha ya Mtanzania ikizidi kuwa ngumu, kwa nini basi watu hao wapewe fursa ya kuboronga mambo zaidi?
Faraja kubwa kwa Lowassa (na hata Membe kwa ‘uhusika wake katika mtandao) kuhusu tuhuma za ufisadi ni ukweli mchungu kuwa Watanzania ni wepesi kusahau ‘mabaya.’ Wanasiasa wetu wengi wanafahamu kuhusu udhaifu huo ambao kwa kiasi kikubwa umewasaidia wengi kuendelea kuwapo madarakani licha ya ‘madudu’ yao.
Iwapo ‘kete ya fedha’ niliyobainisha katika makala iliyopita kuwa inamsaidia sana Lowassa itaendelea kutumika, basi kuna uwezekano mkubwa wa mwendelezo wa ‘who cares?’ (nani anajali?) ambapo mahitaji ya muda mfupi kama vile sukari, khanga, mchele na mengine kama hayo yatafunika mahitaji ya muda mrefu kama vile kuondokana na umasikini sambamba, kupambana na ufisadi, na hatma ya taifa letu kwa ujumla.
Kwa upande wa Membe, kikwazo kikubwa kwake ni kutokuwa maarufu ndani na nje ya CCM. Na ukubwa wa kikwazo hicho unatokana na ukweli kwamba ‘mpinzani’ wake, yaani Lowassa, ni mwanasiasa maarufu kuliko wote ndani ya CCM hivi sasa (bila kujali umaarufu huo ni stahili au la). ‘Wajuzi wa mambo’ wanaeleza kuwa inahisiwa Lowassa anaungwa mkono na zaidi ya asilimia 75 ya viongozi wa chama wenye uwezo wa kufanya uamuzi, huku wengi wao wakiwa watu waliofanyiwa fadhila zilizosababisha wawepo madarakani hivi sasa.
Tegemeo pekee kwa Membe dhidi ya Lowassa ni lile nililogusia katika makala iliyopita; nafasi ya Idara ya Usalama wa Taifa katika kumpata mgombea urais ajaye (ndani ya CCM). Kama kuna kitu chochote kinachoweza kumzuia Lowassa kuingia Ikulu, na pengine kumsaidia Membe kupata fursa hiyo, ni pale Idara hiyo itakapoamua ‘kumbeba mwenzao’ (Membe ni shushushu mstaafu). Na hilo si gumu kama inavyoweza kudhaniwa. Moja ya maeneo ambayo mashushushu wetu wanayomudu sana ni hujuma (sabotage) na uzandiki (subversion).
Ni hivi, kwa vile tayari kuna hisia za ‘uchafu’ kuhusu Lowassa (yaani tuhuma za ufisadi) basi haitokuwa vigumu kwa mashushushu kuzikuza na kuziendeleza katika namna ya kile kinachofahamika kama character assassination. Lakini kwa vile Lowassa bado yupo katika ‘himaya’ ya Idara ya Usalama wa Taifa (kama waziri mkuu wa zamani, anapatiwa huduma za ulinzi na Idara hiyo) ni rahisi kwa mashushushu kuibua mengi (ya kweli au hata ya kutunga) dhidi yake, iwapo wataona haja ya kufanya hivyo.
Kwa hiyo, kwa kifupi, kufanikiwa kwa Membe kutategemea kukwama kwa Lowassa. Na pengine katika hatua hii, ni vema nikitanabaisha waziwazi kuwa mwana-CCM anayeongoza katika kinyang’anyiro hicho ni Lowassa akifuatiwa kwa karibu kiasi na Membe.
Nihitimishe makala hii kwa kueleza kuwa mada hii ni endelevu, kwa maana ya kuwa nitaendelea na uchambuzi na mjadala huu kadri tunavyoelekea Uchaguzi Mkuu ujao. Hata hivyo, ninapenda kurejea tena mtizamo wangu kuwa CCM kurejea tena madarakani mwaka 2015 ni janga kwa Watanzania. Chama hicho tawala sio tu kimeishiwa na kila mbinu ya kuongoza nchi lakini pia hakipo kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Na kama uchambuzi huu ulivyoonyesha kuwa uwezekano mkubwa wa aidha Lowassa au Membe kuwa mgombea kwa tiketi ya chama hicho ni kwa aidha fedha au ‘sanaa za giza’, yeyote kati yao atakapopata urais hatokuwa tofauti na utawala uliopo madarakani hivi sasa ambao nao ulitumia mbinu ya ‘mtandao.’
Kwa bahati mbaya au makusudi, watu tuliodhani wangeweza kutusaidia kuiondoa CCM madarakani, yaani CHADEMA, wanaonekana kuwa ‘bize’ kupigana ngwala kugombea madaraka ndani ya chama chao. Sasa kama zoezi dogo tu la kupata uongozi wa chama linasababisha ‘watiane vidole machoni’ kwenye uongozi wa nchi itakuwaje? Ni ukweli mchungu lakini usioepukika na hivyo ni vema kujiandaa kisaikolojia kuendelea kuwa chini ya utawala wa CCM (ninatamani kuwa na suluhisho mbadala lakini sijalipata hadi muda huu)

Soma zaidi kuhusu:

- See more at: http://raiamwema.co.tz/nani-kinara-wa-ccm-urais-wa-2015-ii#sthash.RAQui2j5.dpuf

Sunday, November 24, 2013

Makala yangu ktk RAIA MWEMA Toleo la 20.11.13: "Nani kinara wa CCM urais wa 2015?"


KAMA nilivyoahidi katika makala yangu ndani ya toleo lililopita la gazeti hili maridhawa, wiki hii nitafanya uchambuzi kuhusu kinyang’anyiro cha kumpata mgombea urais kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2015.
Kwa wanaofuatilia safu hii, niliwahi kugusia mada hii katika toleo la Oktoba 26, 2011 ikibeba kichwa cha habari “Mizengwe na mitego ya mgombea urais kutoka CCM.” Mengi yametokea kati ya wakati huo na sasa, na kwa vile Uchaguzi Mkuu unazidi kujongea, nimeona ni muhimu kurejea tena mada hii.
Pengine msomaji unaweza kubaini mabadiliko kidogo katika mtizamo wangu kuhusu uwezekano wa CCM kung’oka madarakani 2015. Ninaomba kukiri kwamba chokochoko zisizo na msingi zinazoendelea ndani ya chama kikuu cha upinzani (na tegemeo la wengi kuiondoa CCM madarakani, CHADEMA, zinanifanya nikubaliane na ukweli mchungu kuwa fursa za chama tawala kushinda tena katika uchaguzi mkuu ujao zinazidi kuongezeka.
Na moja ya mambo ya kusikitisha zaidi kuhusu CHADEMA ni kuibuka kwa kundi la ‘wahuni wa kisiasa’ waliojipachika joho la uanaharakati. Kwa wababaishaji hao, kuanza kukubalika kwa chama hicho kumetoa fursa kwao kufahamika kwa namna moja au nyingine. Ni tatizo lilelile sugu katika jamii yetu la kusaka umaarufu hata kwa mambo ya kipuuzi, Waingereza wanasema ‘famous for nothing.
Sasa ‘wahuni’ hawa wamebinafsisha ajenda ya CHADEMA kupambana na ufisadi na kujipa hakimiliki kuwa wao pekee ndio wenye uelewa na mbinu za kukiwezesha chama hicho kufanikisha ajenda hiyo. Pasi kujali madhara ya uhuni wao kwa hatma ya chama hicho, wamejikuta wakitumiwa na maadui wa CHADEMA kwa njia isiyo ya moja kwa moja - kwa ‘remote control.’
Lakini kuashiria kuwa chama hicho kina wakati mgumu japo uongozi wake wa juu unaendeleza porojo za “njama za CCM na Usalama wa Taifa,” imefika mahala Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya mkoa anabandika tuhuma nzito dhidi ya Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, kwenye blogu yake. Hivi pamoja na madudu ya CCM unatarajia ‘utoto’ wa aina hiyo?
Tuelekee huko CCM sasa. Kwanza ninaomba kuweka bayana kuwa uchambuzi huu umeelemea katika uelewa wangu wa siasa za huko nyumbani, maongezi yangu na watu walio karibu na siasa hizo, na taarifa mbalimbali katika vyombo vya habari (vya ‘asili’ na vya ‘kisasa’)
Kwa mtizamo wangu, hadi muda huu wanasiasa wawili wanaoongoza katika kinyang’anyiro cha kumpata mrithi wa Rais Jakaya Kikwete hapo 2015 ni aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Kwa ‘pembeni’ kidogo kuna Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta. Kimsingi, majina mengine yanayosikika kama William Ngeleja, John Magufuli na wengineo ni ya ‘kuchangamsha gumzo’ zaidi kuliko kuwa na uzito wowote wa maana.
Pengine baadhi ya wasomaji wangetamani nisiandike hivi lakini kimsingi hauepukiki, kama mazingira yatabaki kama yalivyo muda huu (constant) ni vigumu kwa mwanasiasa yeyote yule ndani na nje ya CCM kumzuia Lowassa kuwa rais mwaka 2015. Ninaomba nikiri kuwa ninatamani isiwe hivyo (kwa sababu binafsi ninaamini kuwa hafai kuwa Rais) lakini ukweli una tabia moja: kuuchukia hakuufanyi uwe uongo.
Turufu kubwa ya Lowassa ni uwezo wake mkubwa wa kifedha japo mwenyewe amekuwa akikanusha na kudai kuwa mamilioni anayoyamwaga katika harambee mbalimbali ni michango ya rafiki zake (hajawahi kuwataja wala kutueleza vyanzo vya utajiri wao).
Inaelezwa pia kuwa mwanasiasa huyo amejijenga mno ndani ya CCM kiasi cha kuwa sahihi kuhitimisha kuwa ana nguvu zaidi ya Mwenyekiti wa Taifa, Kikwete.
Sasa, huhitaji japo kozi ya muda mfupi ya siasa za nchi yetu kufahamu kuwa katika zama hizi fedha ndio nyenzo muhimu zaidi ya kumwezesha mwanasiasa kushinda uchaguzi kuliko kitu chochote kile. Mpigakura mwenye njaa hana habari na sera ya chama bali anachofikiria ni pishi ya mchele, doti ya khanga au kilo ya sukari.
Kwa upande wa Membe, turufu zake muhimu zaidi ni tatu. Kwanza, nafasi yake kama Waziri wa Nje inamweka karibu sana na Rais Kikwete kwani wanasafiri pamoja takriban katika kila ziara ya Rais nje ya nchi. Huhitaji kuwa mdadisi kufahamu kuwa watu wanaosafiri pamoja kwa miaka 10 mfululizo wana ukaribu kiasi gani.
Pili, kuna taarifa zisizo rasmi kuwa Membe anaungwa mkono na familia ya Kikwete. Katika moja ya mahojiano, mmoja wa watoto wa Kikwete, Ridhiwani, alikiri bayana kuwa anadhani Membe anaweza na anafaa kuwa Rais. Siasa za kifamilia zinaweza kubadilika lakini kwa angalau kwa sasa hali ipo hivyo.
Tatu, na kwangu hii ndio turufu muhimu zaidi, Membe ni ‘shushushu mstaafu.’ Pengine ni vigumu kuelezea kwa undani umuhimu wa kigezo hiki, lakini kwa kifupi, ni vigumu sana kwa mwanasiasa kuingia Ikulu pasi kuungwa mkono na Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi husika (angalau katika ‘demokrasia changa’). Mashushushu, kama watumishi wengine wa vyombo vya dola, wana tabia moja ya kumuunga mkono ‘mwenzao.’
Lakini sambamba na hilo ni kile kinachofahamika kama ‘sanaa za giza’ (dark arts), yaani kwa lugha ya kawaida, zile mbinu zinazosababisha kura kuyeyuka katika mazingira ya ajabu. Tukiamini kuwa mashushushu watamuunga mkono Membe, kwa nini basi wasiende mbali zaidi kuhakikisha kuwa anashinda kwa ‘gharama yoyote’ (na ‘gharama’ hapa si lazima iwe fedha)?
Kwa hiyo licha ya uwezo mkubwa wa kifedha wa Lowassa (tukiweka kando kukanusha kwake kuwa yeye si tajiri), Membe anaweza kumshinda kwa mbinu (ambazo kwa mtizamo wangu zinaweza kuhusisha watumishi wa sasa na wa zamani wa Idara ya Usalama wa Taifa)
Kuhusu Sitta, nafsi yangu inanituma kuamini kuwa haitokuwa jambo la kushangaza endapo miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 tukakutana na kichwa cha habari kama hiki “Sitta: Lowassa ni chaguo la Mungu.” Kwa nini nina hisi hivyo? Binafsi ninamwona kama mwanasiasa asiyeaminika, anayeendeshwa na siasa za kusaka umaarufu na hata ‘rahisi kutulizwa.’ Kwa kifupi, Sitta anaendeshwa zaidi na imani (kuwa anaweza kuwa rais) kuliko uhalisia.
Kwa Sumaye, japo pengine ni mapema mno ‘kumpuuza,’ nafasi pekee ya yeye kuwa rais ni nje ya CCM. Tatizo kubwa kwa mwanasiasa huyu ni kwamba lugha anayoongea haieleweki ndani ya chama hicho. Naam, amejitokeza kuwa msemaji wa wanyonge na mkemeaji mkubwa wa ufisadi lakini sote tunafahamu kuwa hiyo sio sera ya CCM (angalau kwa vitendo na si kauli za majukwaani).
Nafasi hairuhusu kuangalia ‘odds’ dhidi ya Lowassa na Membe (ninataraji kufanya hivyo katika matoleo yajayo), lakini muda mfupi kabla ya kuandaa makala hii nilishiriki katika mjadala mzito kuhusu hatma ya Tanzania yetu hususan jinsi ya kuzuia uwezekano wa kumpata Rais atakayetokana na rushwa. Pia tulijadili tatizo la rushwa na namna ya kulimaliza.
Kwa bahati nzuri, mjadala huo uliofanyika katika mtandao wa kijamii wa Twitter ulimvutia mwanasiasa kijana na Mbunge wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki, Abdullah Mwinyi. Kwa kifupi, alitueleza kiini cha tatizo la rushwa, na nini kinaweza kufanyika kupambana na tatizo hilo sugu. Bila kuingia undani kuhusu mjadala huo, ulipofikia tamati takriban kila mshiriki alikiri kuwa “kumbe CCM bado ina hazina zaidi ya hayo majina tunayoyasikia kila siku.”
Je, wanasiasa kama Abdullah, mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi wanaweza kuwa chaguo mbadala (alternative choice) hasa ikizingatiwa kuwa hawana ‘mawaa’ kama ya Lowassa au Membe (nitayajadili mbeleni)?
Nihitimishe makala yangu kwa kusisitiza jambo moja: japo kwa jinsi hali ilivyo ni muhimu kujiandaa kisaikolojia kuiona CCM ikiendelea kuwa madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu ujao, bado kuna umuhimu mkubwa kwa chama hicho kikongwe kupumzishwa kwani kimeshindwa kazi.
Si Lowassa, Membe, Sitta au Sumaye anayeweza kuibadili CCM irejee misingi aliyoasisi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Tegemeo dogo katika chama hicho ni damu mpya kama za akina Abdulla Mwinyi, japo pengine ni mapema mno kuhitimisha hilo.
ITAENDELEA...


- See more at: http://raiamwema.co.tz/nani-kinara-wa-ccm-urais-wa-2015#sthash.fO09a0nd.dpuf

Saturday, June 02, 2012

Kikwete Amuunga Mkono Lowassa

 
AKIRI TATIZO LA AJIRA KWA VIJANA KUWA BOMU, ASEMA LISIPOTATULIWA LITALETA MACHAFUKO BARANI AFRIKA

Peter Saramba na Mussa Juma, Arusha
RAIS Jakaya Kikwete amekiri kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ni tatizo kubwa na kwamba lisipotafutiwa ufumbuzi wa kudumu linaweza kusababisha vurugu, machafuko na uasi wa umma, hata kwa nchi zinaoongozwa kwa misingi ya kidemokrasia, kama inavyotokea sasa katika nchi za Kiarabu.

Onyo hilo la Rais Kikwete linafanana na lile ambalo limekuwa likitolewa mara kwa mara na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, lakini, linapingana na kauli ya Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka ambaye Machi 21 mwaka huu, alimjibu Lowassa akisema, "Kitendo cha wanasiasa kuendelea kusema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu linalosubiri kulipuka, siyo kweli."

Jana akifungua mkutano wa mwaka wa Magavana wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) Jijini Arusha, Rais Kikwete alisema moja ya sababu kuu ya machafuko yanayoshuhudiwa sasa kwenye ukanda wa nchi za Kiarabu, ni matokeo ya ukosefu wa ajira kwa vijana na watu kukata tamaa.

“Siyo kweli kwamba machafuko yanayoshuhudiwa kwenye nchi za Kiarabu ni matokeo ya Serikali za nchi hizo kukaa madarakani kwa kipindi kirefu kama wengi wanavyodhani. Ukweli ni kwamba hayo ni matokeo ya ukosefu wa ajira na watu kukata tamaa ya maisha,” alisema Rais Kikwete.

Alisema bila kutafutia ufumbuzi wa haraka, tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana ambao wengi hukimbilia mijini kusaka hali bora ya maisha, hata nchi zenye kuongozwa kidemokrasia, zinaweza kukumbwa na machafuko na uasi wa umma.

Rais alitumia fursa hiyo kuishukuru Denmark kwa kutoa fedha za kusaidia Mfuko wa Ajira kwa Vijana barani Afika, akisema ni moja ya mapendekezo kadhaa yaliyotolewa na kamati maalum ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya kiuchumi barani Afrika ambayo yeye na Rais wa AfDB, Dk Donald Kaberuka, walikuwa wajumbe.

Mapema Rais wa Ivory Coast, Allasane Ouattara aliyehudhuria mkutano huo aliunga mkono kauli hiyo ya Rais Kikwete kwa kusisitiza kuwa vijana lazima wawekewe mazingira mazuri na kuwezeshwa kukabiliana na kumudu changamoto za kiuchumi, kitamaduni na kiteknolojia wanazokabiliana nazo.

“Lazima wasaidiwe na wawekewe mazingira bora ya kupata fursa za ajira na kujiajiri, bila kufanya hivyo ni kukaribisha matatizo na machafuko yanayotokana na ongezeko la mahitaji na kukata tamaa katika miji yetu inayokua kila kukicha kutokana na ongezeko la vijana wanaosaka ajira na maisha bora,” alisema Rais Ouattara.

Rais Ouattara aliyetumia muda mwingi kumshukuru Rais Kikwete na viongozi wenzake wa Kiafrika kwa kusaidia upatikanaji wa amani nchini mwake alitaja changamoto kadhaa zinazokabili Bara la Afrika, kuwa ni mabadiliko ya tabia nchi, ukame, uhaba wa chakula na ukosefu wa amani kwa baadhi ya sehemu.

Mambo mtambuka 
Ili kukabiliana na tatizo hilo, Rais Kikwete alitaja mambo kadhaa yanayopaswa kufanyika ikiwa ni pamoja na kukuza na kuboresha sekta ya kilimo kwa kuongeza uwekezaji na kuacha kutegemea kilimo cha mvua badala yake itumie fursa ya vyanzo vingi vya maji.

“Bara la Afrika linaweza kuzalisha mazao ya kilimo na kujitosheleza kwa chakula na kubakisha ziada ya kuuza nje hadi kuwa ghala la chakula duniani iwapo uwekezaji katika sekta ya kilimo utapewa kipaumbele,” alisema Rais Kikwete.

Kuhusu miundombinu, Rais Kikwete aliipa changamoto AfDB kuongeza juhudi katika ufadhili na udhamini wa miradi ya maendeleo barani Afrika, ikiwemo miradi ya miundombinu aliyosema ni moja ya changamoto zinazokwaza maendeleo ya Afrika.

Alisema pamoja na kukwaza mawasiliano kwa njia ya barabara, reli na anga, uduni wa miuondombinu pia huchangia bei kubwa ya bidhaa na huduma katika nchi za Kiafrika kutokana na gharama kubwa ya usafirishaji.

Rais Kikwete alisema uwepo wa miundombinu ya uhakika siyo tu itawahakikishia wakulima vijijini soko na bei ya uhakika kwa mazao na bidhaa zao, lakini pia itapunguza kasi ya watu kuhamia mijini inayozikabili miji mingi barani Afrika.

Akizungumzia uwekezaji katika nyanja ya uchumi mdogo, Rais alisema  uwekezaji huo ndiyo njia pekee ya kuboresha na kuinua uchumi wa watu wa kawaida huku ikitumia vema soko lake la ndani kwa kutumia bidhaa zinazopatika barani humo badala ya kuendelea kutumia fedha nyingi kuagiza bidhaa kutoka nje, hata zile zinazopatikana nchi jirani.

Rais Kikwete alisema ili kupiga hatua kimaendeleo, Afrika kupitia AfDB na wahisani wengine wa ndani na nje lazima iwekeze katika ujenzi na uboreshaji wa miuondombinu ambayo ni nyenzo muhimu kimaendeleo.

Kuhusu sekta ya utali, alisema licha ya  Afrika kujaliwa vivutio vingi vya utalii, sekta hiyo bado haichangii kikamilifu uchumi wa bara hilo kutokana na kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo miundombinu mibovu, ukosefu wa safari za ndege za kimataifa na bei kubwa ya safari ndege chache za kimataifa zinazofanya safari zake barani Afrika.


Lowassa na ajira
Novemba 15, mwaka jana akiwa katika harambee ya ujenzi wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Makasa, Parokia ya Nyakato, Mwanza, Lowassa alionya kuhusu tatizo hilo na kulitaka Kanisa lisaidie kujenga vyuo vya ufundi.

Alitoa takwimu akisema utafiti wa mwaka 2006, ambao hata hivyo, hakusema ulifanywa na taasisi gani, ulionyesha kuwa tatizo hilo kwa sasa limekuwa na kufikia asilimia 15 huku likigusa zaidi vijana wenye umri wa miaka kati ya 15 hadi 24 ambao ndiyo nguvukazi ya taifa.

Novemba 29, mwaka huo wa jana akiwa harambee ya ujenzi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Amani Sabasaba, Singida, Lowassa alionya tena kuhusu tatizo hilo la ajira. 

Mwezi Machi mwaka huu akiwa katika sherehe za uzinduzi wa Jimbo jipya la Kanisa Katoliki Ifakara alirejea kisema: “Nawaomba maaskofu katika miradi yenu mlipe kipaumbele suala la tatizo la ajira kwa vijana.... hili kama tulivyosema ni bomu linalosubiri kulipuka...”

Hata hivyo, kauli hiyo mpya ya Lowassa, ilijibiwa na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana Gaudensia Kabaka Machi 21 akisema, "Siyo kweli  kudai Serikali hayaijafanya kitu, wanakuwa hawaitendei haki na kuongeza kwamba, utafiti uliofanywa na wizara yake kwa kushirikiana na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), unaonyesha kuwa tatizo hilo limepungua kwa asilimia 1.2.

CHANZO: Mwananchi

Thursday, May 24, 2012

Makala Yangu Ndani ya RAIA MWEMA Mei 23 "Uamuzi mgumu na ujasiri wa kisiasa"




Uamuzi mgumu na ujasiri wa kisiasa

Evarist Chahali
Toleo la 240
23 May 2012
WIKI iliyopita, Rais wa Marekani, Barack Obama, aliingia kwenye vitabu vya historia ya taifa hilo kwa kuwa kiongozi wa kwanza kuunga mkono ndoa za watu wa jinsia moja. Kwa muda mrefu Obama alikuwa aidha akipinga suala hilo nyeti au kuchelea kuweka wazi msimamo wake.
Tayari suala hilo la ndoa za jinsia moja limezua mgawanyiko mkubwa wa kimtizamo ingawa kura mbalimbali za maoni zinaonyesha kuwa msimamo huo ‘mpya’ wa Obama hautoathiri kwa kiasi kikubwa maamuzi ya wapigakura katika uchaguzi mkuu wa Marekani unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa kura za maoni za hivi karibuni, takriban asilimia 60 ya Wamarekani wanasema kitendo cha Obama kuunga mkono ndoa za mashoga hakitowashawishi kumpigia au kutompigia kura.
Lakini moja ya makundi ambayo yanaonyesha kuguswa na suala hilo ni Wamarekani Weusi. Kama ilivyo kwetu Waafrika, Wamarekani Weusi wamekuwa wapinzani wakubwa si tu wa ndoa, bali hata uhusiano wa kawaida wa watu wa jinsia moja. Mara kadhaa wasanii wengi wa muziki wa kufokafoka (hip-hop/rap), ambao ni maarufu kwa Wamarekani Weusi, wamekuwa wakilaumiwa kwa tungo zao zenye kuonyesha bayana upinzani dhidi ya ushoga.
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, baadhi ya viongozi wa makanisa ya Wamarekani Weusi wameeleza bayana kuwa hawamuuingi mkono Obama katika suala hilo, huku wengine wakitishia kutompigia kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Japo Obama anaendelea kuungwa mkono na kundi hilo (la Wamarekani Weusi) huku akionekana kuwa ni ‘mwenzao’, kura za maoni zinaonyesha kuwa asilimia 49 inampinga katika msimamo wake kuhusu ndoa za mashoga kulinganisha na asilimia 43 ya Wamarekani Weupe.
Obama mwenyewe amekiri kuwa anafahamu bayana msimamo wake huo utawaudhi baadhi ya wanaomuunga mkono. Lakini akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha luninga cha ABC cha Marekani, Rais huyo alieleza kuwa inamwia vigumu kuendelea na ‘sintofahaumu’ katika ‘ubaguzi’ dhidi ya mashoga ilhali Wamarekani kadhaa anaowaongoza wamo kwenye kundi hilo.
Alifafanua kuwa kama mzazi, alikuwa anapata wakati mgumu kutokuunga mkono ndoa za mashoga ilhali wanae Sasha na Malia wana  baadhi ya marafiki zao ambao wazazi wao ni mashoga.
Kadhalika, alieleza kuwa ilikuwa inamsumbua pia kuendelea kutokuunga mkono ndoa za mashoga huku baadhi ya makundi muhimu katika nchi hiyo, kwa mfano, wanajeshi wanaolitumikia taifa hilo kwa uadilifu mkubwa, yakijumuisha mashoga.
Lengo la makala hii si kumuunga mkono au kumpinga Obama katika msimamo wake huo kwa ndoa za mashoga bali kupigia mstari nafasi ya ujasiri katika uongozi.
Kama alivyokiri mwenyewe kuwa anafahamu bayana uamuzi wake wa kutangaza hadharani msimamo wake kuhusu ndoa za mashoga utawakera wengi, na pengine kumgharimu katika uchaguzi mkuu ujao, lakini Obama ameweza kufanya ujasiri wa kusimamia kile anachokiamini.
Japokuwa kuna baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaotafsiri hatua hiyo ya Obama kama kigeugeu-kwa maana alishawahi kuwa mpinzani wa ushoga- huku wengine wakidai hatua hiyo ni ‘janja yake’ tu kusaka kura za mashoga, jambo la msingi hapa ni ukweli kwamba amediriki kuweka kando uoga (huku akijua madhara) na kuweka wazi wapi anasimamia katika suala hilo.
Kwa upande fulani, uamuzi huo unaweza kumnufaisha dhidi ya mpinzani wake mtarajiwa kutoka chama cha Republicans, Mitt Romney, ambaye kama ilivyo kwa wahafidhina wengi, suala la ushoga ni kama laana.
Sasa, kwa vile moja ya misingi muhimu ya taifa la Marekani ni uhuru wa mtu kufanya apendacho alimradi havunji sheria, sambamba na kupinga ubaguzi wa aina yoyote ile, Obama na wanaomuunga mkono wanaweza kuutumia upinzani wa Romney dhidi ya ndoa za mashoga kama mfano hai wa jinsi mgombea huyo (mtarajiwa) na chama chake cha Republicans walivyobobea kwenye ‘ubaguzi na kuminya uhuru’  wa Wamarekani.
Kwa mtizamo wangu, ujasiri alionyesha Obama (bila kujali kama naafikiana au ninapingana naye katika suala la ndoa za mashoga) ninaulinganisha na kauli za hivi karibuni za aliyekuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa sasa wa Monduli (CCM), Edward Lowassa. Naomba niweke wazi kuwa ninaamini wasomaji wengi wa makala hizi wanafahamu fika msimamo wangu dhidi ya Lowassa, hususan kuhusiana na tuhuma za ufisadi. Lakini msimamo huo haumaanishi nichelee kumuunga mkono pale anapoonyesha ujasiri wa kisiasa.
Kwa muda mrefu sasa, Lowassa amejitokeza kuwa mmoja wa wanasiasa wachache ndani ya CCM wanaoeleza waziwazi mapungufu ya chama hicho na jinsi yanavyoliathiri taifa kwa ujumla. Lakini kama ilivyozoeleka, msimamo huo (ambao hapa ninauita ujasiri) umemfanya mwanasiasa huyo aonekane kama kiumbe hatari kabisa kwa ustawi na uhai wa chama hicho tawala.
Majuzi, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alinukuliwa akimpinga Lowassa kutokana na kauli yake katika mkutano wa hadhara huko Mto wa Mbu, Arusha, kuwa tatizo la CCM ni uongozi kuacha kusimamia misingi. Katika majibu yake kwa Lowassa, Mukama alimtaka mbunge huyo wa Monduli kushughulikia matatizo jimboni kwake kwanza.
Kuna wanaotafsiri kuwa msimamo wa Lowassa kukikosoa chama chake ni sehemu tu ya mikakati yake ya kuwania urais mwaka 2015. Lakini wanaofikiria hivyo wanapaswa kumtendea haki mwanasiasa huyo hasa kwa vile hajatangaza kuwa atagombea urais katika uchaguzi mkuu ujao. Kadhalika, ni muhimu kutanua upeo wetu na kuzichambua kauli za Lowassa pasipo kuzihusisha zaidi na malengo yake ya baadaye ya kisiasa.
Kimsingi, tukiweka kando hisia za ‘unafiki wa kisiasa’, anayoongea Lowassa kuhusu CCM ni ya kawaida sana kwa maana kwamba kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufikiri anaelewa ‘mchango wa CCM katika kukwaza maendeleo ya nchi yetu.’
Kama chama tawala, CCM haiwezi kujinusuru dhidi ya shutuma kwamba inachangia sana kukwaza jitihada za kulikwamua taifa kutoka kwenye lindi la umasikini unaochangiwa zaidi na vitendo vya ufisadi.
Kwamba Lowassa ni mmoja wa wana-CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi si sababu ya kumfanya mwanasiasa huyo kutozungumzia suala hilo. Na hata hizo tuhuma dhidi yake zinaweza kukosa nguvu kwa vile CCM yenyewe imeshindwa kuchukua hatua zozote dhidi yake.
Makala hii haina maneno ya kuitia moyo CCM katika msimamo wa baadhi ya viongozi wake wanaokerwa na kauli za Lowassa, hasa ikizingatiwa kuwa anachofanya mwanasiasa huyo ni kuwakilisha tu mtizamo wa Watanzania wengi (ikiwa ni pamoja na wana-CCM) dhidi ya chama hicho tawala. CCM inaweza hata kumtimua Lowassa lakini isipojirekebisha, kuna kila dalili kuwa itang’olewa madarakani huko mbeleni.
Japo ninaelewa msimamo wa Mukama kwamba kama kiongozi wa CCM Lowassa anapaswa kuongelea matatizo ya chama hicho kwenye vikao vya ndani, kimsingi hilo ni moja ya vyanzo vya matatizo yanayosababisha watu kama Lowassa kuamua kuweka hadharani matatizo hayo.
Ni hivi, kama chama hicho kina matatizo, kisha yanazungumzwa kwenye vikao vya ndani na hayapatiwi ufumbuzi, kwa nini basi kiongozi asishawishike kuyaongelea matatizo hayo hadharani?
Halafu kuna suala la maslahi ya taifa dhidi ya maslahi ya chama. Kwa vile CCM ni chama tawala, kila inachofanya au kuzembea kufanya kinaligusa taifa moja kwa moja. Kwa mantiki hiyo, wakati Mukama anaweza kuyaona matatizo ya CCM kuwa ni suala la kichama, kiuhalisi matatizo hayo si tu yanaligusa taifa bali pia ni suala la kitaifa. Na kwa vile Tanzania ni yetu sote, basi ni sahihi na halali kwa kila Mtanzania, ikiwa ni pamoja na Lowassa, kuyaongelea matatizo yanayolisumbua taifa letu pasi uoga wa kumuudhi mtu flani.
Naomba kuhitimisha makala hii kwa kurejea kuweka bayana msimamo wangu kuwa lengo halikuwa kuunga mkono msimamo wa Obama kuhusu ndoa za mashoga wala kugeuka muungaji mkono wa Lowassa (japo vyote si dhambi).
Makala hii imelenga kuwapongeza wanasiasa hao kwa ujasiri wa kuweka wazi misimamo yao hata pale kufanya hivyo kunapoweza kuwaingiza matatizoni. Kinyume cha ujasiri ni uoga na unafiki, na sote tunafahamu kuwa kiongozi mwoga na/au mnafiki si tu hawezi kusimamia yale anayoamini lakini pia ni kikwazo katika jitihada za kuleta mabadiliko muhimu kwa anaowaongoza.

Friday, March 09, 2012

Utata watanda afya ya Lowassa

Wednesday, 07 March 2012 19:31

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa
ATHIBITISHA YUKO HOSPITALINI, ASEMA ASINGEPENDA KUELEZEA KWA UNDANI KUHUSU AFYA YAKE  
Ramadhan Semtawa
UTATA umegubika afya ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa baada ya taarifa mbalimbali kueleza kuwa yuko hospitalini nchini Ujerumani kwa matibabu.Takriban juma moja sasa kumekuwa na taarifa mbalimbali zikizungumzia afya ya Lowassa lakini hakukuwa na taarifa rasmi kutoka chanzo chochote kati ya Serikali, familia yake au Bunge kuzungumzia afya ya Mbunge huyo wa Monduli.

Jana, Lowassa akizungumza na mwandishi wetu kwa simu alisema kwamba yuko hospitali, bila kufafanua kuwa ni nje au ndani ya nchi, wala kueleza kinachomsibu.

Mahojiano hayo kati ya Lowassa na mwandishi wetu yalikuwa kama ifuatavyo:

Swali: Asalaam alaykum Mheshimiwa Lowassa.
Jibu: Waalaykum Salaam.

Swali: Mimi naitwa... (jina la mwandishi) kutoka gazeti la Mwananchi. Kwanza pole kwa matatizo ya kiafya yanayokusumbua.
Jibu: Ahsante.

Swali: Nimekupigia pamoja na kukupa pole, nilitaka kujua unaendeleaje na matibabu?
Jibu: Niko hospitalini kwa sasa naomba niache mambo mengine tutaongea baadaye.

Swali: Lakini, ni matibabu gani hasa unayopata?
Jibu: ... (akimtaja mwandishi) naomba niache niko hospitalini sasa hivi mambo mengine tuongee baadaye.

Lowassa alitoa majibu hayo majira ya saa nane mchana na alipopigiwa tena saa 10.20 jioni, alijibu kama ifuatavyo:

Swali: Naam, Mheshimiwa Lowassa nimekupigia tena mimi... (mwandishi akajitambulisha).
Jibu: ... Unataka nikuambie nini tena? Nilishakwambia niko hospitalini niache!

Swali: Sawa, natambua uko hospitalini, lakini wewe ni kiongozi ambaye umewahi kuwa Waziri Mkuu, hivyo Watanzania wangependa kujua maendeleo ya afya yako kutokana na utata ulioibuka na kama je, umelazwa hapo hospitalini au uko katika matibabu ya kawaida?
Jibu Niache, ninachokwambia niko hospitalini sasa unataka nini tena? Nisingependa kuzungumzia afya yangu kwa undani.

Bunge

Akizungumzia suala hilo juzi, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah alisema ofisi hiyo haijapata maombi rasmi ya mbunge huyo kwenda nje kwa ajili ya matibabu.

Dk Kashillilah alisema kwa utaratibu, Ofisi ya Bunge inashirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kuwapeleka wabunge wanaoumwa nje ya nchi baada ya kupata rufaa ambayo inatokana na ushauri wa kitaalamu wa madaktari wa ndani.

Alisema hadi juzi, hakuwa akijua aliko Lowassa na kama ana matatizo ya kiafya kama inavyozungumzwa au la: “Mimi ndiyo Ofisi ya Bunge na ndiyo nakwambia hatujapata maombi ya kutaka mheshimiwa Lowassa apelekwe nje ya nchi.”

Mtendaji huyo mkuu wa Bunge alisema wapo baadhi ya wabunge ambao huwa wanakwenda nje kwa vipindi maalumu kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kawaida wa afya baada ya matibabu lakini, katika orodha hiyo Lowassa hayumo.

“Tunao utaratibu wa baadhi ya waheshimiwa wabunge kwenda nje kwa mujibu wa ratiba zao kwa ajili ya kufanyiwa uangalizi wa kawaida wa afya zao. Lakini, hadi sasa (juzi) katika orodha hiyo mheshimiwa Lowassa hayumo,” alisema Dk Kashillilah.

Hata hivyo, kwa mujibu wa nafasi yake ya utumishi serikalini aliyokuwa nayo, Lowassa anaweza kupata matibabu nje ya nchi kwa kupitia utaratibu wa Serikali bila ya kuhusisha Bunge.

Juhudi za kupata Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda au Naibu wake, Dk Lucy Nkya zilishindikana kutokana na simu zao kufungwa na kutopatikana ofisini.

CHANZO: Mwananchi

Saturday, December 10, 2011

Uhusika wa Rais Kikwete katika utapeli wa Richmond...kwa mujibu wa Lowassa




Kikwete, Lowassa hapatoshi

Saed Kubenea's picture
Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 November 2011
Printer-friendly versionSend to friend
HATIMAYE Edward Lowassa ametoka hadharani na kuonyesha kuwa anataka kupimana ubavu na Rais Jakaya Kikwete.
Ameeleza hadharani kuwa Rais Kikwete anahusika kwenye mkataba tata wa Richmond/Dowans; lakini pia, kuwa hafuati taratibu katika kuongoza chama chake.
Lowassa ambaye alikuwa nguzo muhimu katika mbio za urais wa Kikwete mwaka 2005, ameonekana kumgeuka waziwazi swahiba wake huyo kwa kuanika kile wachunguzi wanaita “udhaifu katika uongozi.”
Ndani ya kipindi cha siku nne, Lowassa ametoa kauli tatu nzito zinazoonyesha dhahiri ameamua kufanya mapambano na Kikwete.
Akiwa ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lowassa alinukuliwa akieleza hatua kwa hatua namna kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (RDC), ilivyopewa zabuni ya kufua umeme wa dharura nchini.
Lowassa alijiuzulu wadhifa wa waziri mkuu mwaka 2008 kufuatia kashfa ya mkataba wa Richmond, kampuni iliyopewa kwa upendeleo zabuni ya kuzalisha umeme wakati haina fedha, haina uzoefu wala fedha za kufanyia kazi hiyo.
Alikiambia kikao cha NEC mjini Dodoma, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo wewe Rais Kikwete hukulifahamu au hukunituma” kuhusu Richmond/Dowans.
Alisema, “…Mwenyekiti, natukanwa kwa ufisadi wa Richmond wakati wewe unafahamu yalichosababisha kashfa ya Richmond ni makosa ya watendaji walio chini yangu? Sasa kosa langu ni lipi? Ni kule kukubali kuwajibika kwa ajili ya serikali yangu na chama chetu? Kwa nini nihukumiwe kwa kosa hilo?”
Huku akimtolea macho Kikwete alisema, “Unakumbuka vema jinsi nilivyotaka kuvunja mkataba ule. Nilikupigia simu ukiwa nje ya nchi, lakini ukasema umepata ushauri wa kamati ya makatibu wakuu, ushauri ambao ulisababisha mkataba usivunjwe?”
Lowassa alisema Kikwete anafahamu kila kitu kwa kuwa ni yeye aliyeridhia Rostam Aziz kutafuta mbia baada ya Richmond kushindwa kuleta umeme.
“Uliponitaka ushauri wa mtu wa kutusaidia ili kuondokana na aibu ya Richmond kushindwa kutimiza mkataba wake, nilipokutajia jina la Rostam, haraka ulikubali na kusema, naona hilo ni sawa,” alieleza Lowassa kwa njia ya kumsuta Kikwete.
Hatua ya Lowassa kumuingiza Kikwete kwenye tope la Richmond/Dowans imezima moja kwa moja kauli yake iliyodai, “Siwajui wala siwafahamu wamiliki wa makampuni ya Dowans Tanzania Ltd na Dowans Holdings SA.”
Akihutubia kwenye maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, tarehe 5 Februari 2011, mjini Dodoma, Kikwete alikana kufahamu wamiliki wa kampuni hiyo na kwamba hajawahi kuwaona wamiliki wake.
Alisema, “Nataka kuuhakikishia umma kwamba, sihusiki na kampuni hii. Siifahamu na wala sijawahi kuwaona wamiliki wake…Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.”
Kauli ya Kikwete ya kutoitambua Dowans wala wamiliki wake, ilikuwa ni mwendelezo wa kauli kama hizo zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wasaidizi wake, zikilenga kumuondoa kwenye kashfa hiyo iliyomlazimu kuvunja baraza lake la mawaziri.
Akizungumzia kwa undani jinsi Richmond ilivyoingia na jinsi yeye na Kikwete walivyokuwa kitu kimoja kuhakikisha mkataba unasainiwa na kutekelezwa, Lowassa alisema, “Hakuna jambo nililolifanya ambalo Rais Kikwete hukulifahamu.”
Akizungumzia kwa undani suala hilo kwa mara ya kwanza tangu ajiuzulu wadhifa wa waziri mkuu, Februari 2008, Lowassa alisema, “Mwenyekiti kwanza napongeza uamuzi huu wa kurejesha jambo hili katika taratibu za kawaida, lakini napenda kufahamu kwa miezi saba nimetukanwa nikiitwa fisadi, watu wamezunguka nchi nzima kwa fedha za chama, hivi hatukujua kama kuna kamati hizo za maadili?”
Lowassa alikuwa akichangia pendekezo la Kamati Kuu (CC) ya CCM lililotaka kurejeshwa kwa suala la “kujivua gamba” kwenye vikao vya chini vya chama hicho baada ya watuhumiwa, isipokuwa Rostam Aziz, kukataa kuachia uongozi katika chama.
Kikwete alikiambia kikao cha NEC kuwa, uamuzi wa kutaka jambo hilo lirejeshwe kwenye vikao vya chini, umetokana na “taratibu kukosewa.”
Hata hivyo, kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya chama hicho aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu, uamuzi wa Kikwete kulirejesha suala la kujivua gamba kwenye vikao vya chini ulitokana na hofu ya NEC kujaa wajumbe wengi kutoka kwa kundi la Lowassa.
“Unajua mle NEC, Kikwete hana chake. Mle ndani kuna kundi kubwa la Lowassa, ndiyo maana jamaa ameogopa suala hilo la kuvuana magamba lijadiliwe,” ameeleza kiongozi huyo ambaye ni waziri katika serikali ya Rais Kikwete.
Kanuni za CCM zinaeleza kabla ya tuhuma kufikishwa NEC, sharti wale wanaotuhumiwa wapewe haki na fursa ya kujitetea mbele ya vikao vya kamati ya usalama na maadili.
Akifunga mjadala huo kwa angalizo mwanana, Kikwete aliagiza suala hilo lipelekwe kamati ya maadili ambako alitaka kuwasilishwa ushahidi wa vielelezo na siyo hujuma dhidi ya watuhumiwa.
Wakati Lowassa akishusha tuhuma kwa Kikwete, kiongozi huyo wa nchi alionekana kama amepigwa ngazi. Hakukana hata tuhuma moja miongoni mwa yaliyoelezwa na swahiba wake huyo wa zamani.
Kikwete na Lowassa, wamejitambulisha mara kadhaa kuwa ni marafiki, huku mmoja akisisitiza, “Hatukutana barabarani.”
Haijafahamika mahusiano yao yamefikia wapi kwa sasa baada ya Lowassa kumhusisha mwenzake katika kashfa ya Richmond katika kile wachunguzi wanasema amechukua tabia ya “tufe sote au tukose wote.”
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kauli ya Lowassa ambayo ilitolewa mbele ya viongozi wake wakuu, akiwamo rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ililenga kuonyesha udhaifu wa Kikwete ndani ya CCM kwa kuasisi falsafa ya kujivua gamba na kuikimbiza moja kwa moja kwenye CC na NEC, kinyume cha taratibu na kanuni za chama chake.
Kama hiyo haitoshi, juzi Jumapili akiwa mkoani Singida alikokwenda kusimamia harambaee ya kuchangia fedha za ujenzi wa kanisa, Lowassa alinukuliwa akisema, “Kwa vyovyote vile, nitaibuka mshindi dhidi ya vita vya kuvuana magamba.”
Akitiwa moyo na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kati, Ushirika wa Amani, mjini Singida, Eliufoo Sima aliyesema, “suluhu ya mapambano ni kukabiliana nayo,” mwanasiasa huyo alisema, amekuwa akihusishwa na tuhuma ambazo hazina ukweli.
Askofu Sima alisema mapambano katika maisha hayatakwisha na “suluhisho siyo kuyaogopa, isipokuwa kuyatafutia majawabu kwa upole, hekima na utulivu.”
Vita vya magamba viliasisiwa na Kikwete 5 Februari 2011, kabla ya kudakwa na baadhi ya watendaji wa Sekretarieti ya CC ambao kwa miezi saba sasa, wamekuwa wakituhumu Lowassa na wenzake wawili - Rostam Aziz na Andrew Chenge – kuwa mafisadi wanaokidhalilisha chama mbele ya jamii.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa kutoka ndani ya CC zinasema kushindwa kwa Rais Kikwete kutekeleza mkakati wake wa kumfukuza Lowassa ndani ya chama chake, kulitokana na upinzani mkali uliotokea kwenye mkutano wa CC.
“Ni kweli kabisa, ndani ya CC, Lowassa alipata uungwaji mkono mkubwa, kiasi ambacho mwenyekiti alilazimika kulipeleka suala hilo NEC. Alipofika NEC na kuona moto umekuwa mkubwa, ndipo alipoamua kuliondoa na kutaka lifanyiwe kazi kwenye vyombo vya chini,” kimeeleza chanzo kimoja cha gazeti hili.
Amesema wajumnbe wa Zanzibar, wakiongozwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho visiwani, Amani Abeid Karume, muda wote wa mkutano walisimama imara kuhakikisha Lowassa hafukuzwi kwenye chama.
“Kuna wakati watu kutoka Bara walikuwa wanakaribia kushinda. Lakini baadaye Zanzibar wakapata nguvu pale Karume aliposimama na kusema, shutuma zote hizo hazijafuata taratibu,” ameeleza.



CHANZO: Mwanahalisi

Saturday, November 26, 2011

Nova Kambota: VIVA KAMANDA LOWASSA


MKUU NIMEFURAHISHWA NA LOWASSA KUANZA KUANIKA UKWELI KUHUSU RICHMOND KWA KWELI NAONA ANAFANYA KILE NILICHOWAHI KUTABIRI KWENYE MAKALA YANGU YA "LOWASSA SEMA NENO MOJA TU" SASA KWA KULIONA HILO NIMEAMUA KUMTUNGIA SHAIRI HILO HAPO CHINI NAOMBA LITUNDIKE KWENYE BLOG YAKO WADAU WALISOME......


Kalamu yangu nashika, shairi nakutungia
Kamanda umeongea, kiwingu umeondoa
Hukutaka kusinzia,makosa kuyarudia
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Mwananchi nimesoma, la jana nilinunua
Machoya yakatuama, dukuduku umetoa
Uliyosema Dodoma, Kwakweli yanavutia
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Richmond kupasua, mapema uligundua
Kikwete ukamwambia, mkataba kuondoa
Rais akakataa, nini alitegemea?
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Nape akashikilia, lile asilolijua
Mikoani kaambaa, uzushi kang’ang’ania
Jinalo kulichafua, wewe ukavumilia
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Mapema nilitabiri, falsafa nikapinga
Magamba sikukariri, kuvuana sikuunga
Ukweli niliukiri, mantiki iso kunga
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

Beti sita nakomea, kalamu naweka chini
Mengi nimeongelea, soma tena kwa makini
Yatazidi kutokea,kusini kaskazini
Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa.

Shairi limetungwa na Nova Kambota Mwanaharakati,
+255717 709618
Tanzania, East Africa
Jumamosi, November 26, 2011

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India