
Subscribe to our newsletter to get the latest updates to your inbox. ;-)
Your email address is safe with us!
Na Boniface Meena
TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini(Takukuru) imetangaza kutoa donge nono kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi (DPA) wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba ambaye hadi hivi sasa hajulikani halipo.
Wakati Takukuru ikifikia hatua hiyo, tayari kuna wananchi ambao wametoa taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuwa wanaweza kutoa taarifa za alipo Liyumba. Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana Afisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani alisema wameamua kutangaza doge nono ambalo hakulitaja ni kiasi gani cha fedha ili wananchi wasaidie kupatikana kwa Liyumba. Alisema Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Dk Edward Hoseah ,anakaribisha watu ambao wanaweza kutoa taarifa au kusaidia alipo Liyumba ili aweze kukamatwa.
"Kuna wananchi tumesikia wako tayari kuisaidia Takukuru, tunawakaribisha na Dk Hoseah anawakaribisha ili waweze kutusaidia na donge nono litatolewa kwa atakayesaidia kukamatwa kwa Liyumba," alisema Kapwani.
Wakati Takukuru ikifikia maamuzi hayo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema kama Takukuru itahitaji msaada wa Wizara hiyo kumtafuta Liyumba iko tayari kutoa msaada huo.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili Waziri wa Wizara hiyo, Lawrance Masha alisema wakipewa maombi ya kumtafuta Liyumba, watasaidia kumtafuta kwa kuwa wote ni Serikali. "Juzi nilitoa tamko kuwa hatujaletewa maombi ya kumtafuta, lakini Takukuru wakituletea tutafanya hivyo, kwa kuwa sisi ni Serikali," alisema Masha.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifuta dhamana ya Liyumba Februari 19 na kutoa amri ya kuwakamata wadhamini wake ambao walikamatwa siku hiyohiyo na baadaye kuachiwa. Wadhamini hao ni wafanyakazi wa BoT Benjamin Nduguru (mhasibu wa benki hiyo) na Agaterus Oto (Afisa Usalama wa ndani wa benki hiyo).
Hata hivyo, licha ya mahakama kufuta dhamana kuwakamata wadhamini hao, ilitoa amri ya kumtafuta na kumkamatwa Liyumba.Liyumba pamoja na aliyekuwa Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka wameshitakiwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka yao katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo na kuisababishia hasara serikali jumla ya Sh221 bilioni.
Liyumba alipewa dhamana na Hakimu Mkaazi wa Kisutu, Hadija Msongo kwa kutumia hati ya nyumba yake iliyoko Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam yenye thamani ya Sh800 milioni, ambayo hata hivyo ililalamikiwa na upande wa mashitaka kwamba imetolewa katika mazingira tata kwa kuwa haijafikisha kiwango cha Sh50 bilioni walizotakiwa kutoa
Juzi Wakili wa serikali, Prosper Mwangumila aliileza mahakama kwamba, Liyumba bado hajapatikana. Hakimu alisema amri ya kumkamata Liyumba bado inaendelea na ya kuwakamata wadhamini imesitishwa hadi kesi itakapotajwa Februari 24, mwaka huu.
Katika hatua nyingine Mawakili wanaomtetea mtuhumiwa huyo waliulalamikia upande wa mashitaka kwa kitendo chake cha kuwanyanyasa ndugu wa mtuhumiwa huyo ambapo walidai kuwa uliwanyang’anya baadhi ya mali zao.
Mmoja wa mawakili hao wa utetezi, Majura Magafu aliiomba mahakama kutoa amri ya kuutaka upande wa mashitaka kuacha kuinyanyasa familia ya Liyumba na kwamba warudishe gari ya mmoja wa wadhamini ambayo waliikamata. Akijibu hoja hiyo, Hakimu Msongo aliutaka upande wa utetezi kama una maombi yoyote kuyapeleka kwa utaratibu wa mahakama kwa kuwa juzi haikuwa tarehe ya kesi.
Wakati akitoa dhamana hiyo Februari 17, mwaka huu, Hakimu Msongo alisema mshitakiwa huyo, atakuwa nje kwa dhamana ya Sh882 milioni wakati mahakama inajiridhisha na hati nyingine zilizopingwa na upande wa mashitaka. Alisema mshitakiwa atatakiwa kutimiza masharti ya dhamana ya kiasi kilichobaki cha Sh54,417,344,800.23 endapo mahakama itabaini kuwa hati hizo zina kasoro.
Hata hivyo baada ya kutolewa maamuzi hayo Wakili wa serikali Justus Mulokozi alisema hawajaridhika na maamuzi yaliyotolewa na kwamba watakaa kuyajadili na kuyatolea maamuzi. Upande wa mashitaka ulipinga kupokelewa kwa hati 10 kati ya 11 zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi kwa madai kuwa zina kasoro, zikiwemo za kuwa na mali zisizokuwa za kudumu kama mbuzi, ng’ombe na kuku.
Siku mbili baada ya mtuhumiwa huyo kuachiwa huru na mahakama kutokana na kutimiza masharti, mahakama ilitoa amri ya kukamatwa tena jambo lilosababisha wadhamani wake kushikiliwa kwa muda na kisha kuachiwa.
Liyumba na Kweka walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza , Januari 27, mwaka huu kwa tuhuma za kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia hasara serikali kiasi cha Sh 221 bilioni. Kweka bado hajapata dhamana.CHANZO: Mwananchi Jumapili
CCM yamjibu Dk. Kitine
na Edward Kinabo
SIKU moja baada yaMkurugenzi mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini, Dk. Hassy Kitine, kudai nchi inaendeshwa kienyeji na kukilalamikia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuwakumbatia wanachama wake wanaokabiliwa na kesi za ufisadi, chama hicho
kimesema hakiwezi kuwavua nyadhifa hizo, kwa sababu kesi zao bado ni tuhuma tu.
Sambamba na hilo, CCM imesema kauli ya Dk. Kitine kwamba nchi inaendeshwa kienyeji ni maoni yake binafsi, kwani hayana ukweli. Msimamo huo wa CCM ulitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, alipozungumza na Tanzania Daima, akijibu shutuma nzito zilizotolewa juzi na Dk. Kitine dhidi ya serikali.
“Sisi tunasema, yeye kama raia ana haki ya kutoa mawazo yake, na hiyo ndiyo demokrasia. Lakini si lazima kila anayetoa mawazo yake yawe sahihi. Mtu anaweza kujiuzulu nafasi yake kupisha uchunguzi ufanyike, hiyo haimaanishi kwamba hilo jambo amelifanya kweli.
“Uchunguzi unapofanyika kuna mambo mawili yanaweza kutokea, la kwanza huyo mtu anaweza kubainika alifanya hicho kitu na la pili anaweza kuonekana hana hatia.
“Hatuwezi kuwavua watu uanachama au nyadhifa zao ndani ya chama kwa sababu hiyo tu. Yeye aliyesema hivyo atutajie ni kiongozi gani wa serikali ambaye pia ni kiongozi wa chama, ameshathibitika kuwa hana maadili halafu kama chama tumeendelea kumwacha. Atuambie…..hakuna,” alisema Chiligati.
Alipoulizwa kwanini CCM isiwafukuze uanachama na kuwavua nyadhifa zao za kichama na ubunge, baadhi ya viongozi wake, ambao tayari serikali ya chama hicho ilisharidhika kwamba walikiuka maadili ya uongozi kwa kutumia vibaya madaraka yao, hata ikaamua kuwafungulia kesi, alisema: “Hatuwezi kuwachukulia hatua kwa sababu kesi zao bado ni tuhuma tu. Wakithibitika kama kweli walifanya hivyo, hatutawaacha,” alisema Chiligati.
Chiligati alipinga madai ya nchi kuongozwa kienyeji na kusisitiza kuwa kauli ya Dk. Kitine, haina ukweli wowote.
Alisema nchi inaongozwa vizuri kwa kufuata utawala wa sheria na mihimili yote ya dola, ikiwemo utawala, Bunge na Mahakama, inafanya kazi zake vizuri. Alibainisha kuwa kielelezo kuwa nchi haiongozwi kienyeji, ni amani na utulivu vilivyopo nchini, kwani kama nchi ingekuwa inaongozwa kienyeji kusingekalika.
“Kwa mfano, hilo alilosema nchi inaongozwa kienyeji, maana yake nini? Nchi kuongozwa kienyeji maana yake hakuna mfumo wa utawala kabisa, hakuna utawala wa sheria. Mahakama hazipo wala Bunge halipo…serikali haipo.
“Kungekuwa na hali hiyo, ingekuwa sawa na kusema nchi inaongozwa kienyeji. Lakini sisi hatujafikia hatua hiyo. Bunge lipo, Mahakama ipo, Serikali ipo. Utawala wa sheria. Nchi haiongozwi kienyeji, ndiyo maana kuna amani na
utulivu,” alisema Chiligati.
Mbali ya CCM kutoa kauli hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliunga mkono kauli ya Dk. Kitine.
“Mzee Kitine ameongea jambo ambalo ninaliongea kila siku kwamba, kuna tatizo kubwa serikalini. Tuhuma za ufisadi zimeshamiri sana, watendaji hawachukui maamuzi, wanasiasa wenye nyadhifa serikalini wamejaza nafasi na hawako tayari kuwajibika. Tunahitaji muafaka wa kitaifa kwenye mambo mengi,” alisema Zitto. Alisema ili mambo yaende vizuri, Tanzania inahitaji kelele za wazee wastaafu kama Dk. Kitine, wasimamie kunena na kushauri na hata kukemea na wananchi wawapigie kura wabunge wengi wa upinzani ili Bunge liwe na meno.
Juzi, Dk. Kitine alisema taifa linakabiliwa na tatizo la uongozi, ambalo halijawahi kutokea katika historia ya nchi. Kada huyo wa siku nyingi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyewahi kuwa mbunge wa Makete, mkoani Iringa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, chini ya uongozi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alisema nchi imekuwa ikiendeshwa kienyeji, kwa sababu ya kuporomoka kwa maadili ya uongozi.
“Hali tuliyofikia si nzuri, tena niseme ni mbaya sana. Kuna kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya uongozi. Na hii nawaambia, nchi haijawahi kuwa katika hali mbaya huko nyuma kama ilivyo sasa. Kwa hali tuliyofikia ni ngumu kurekebisha maadili ya uongozi."
“Tatizo kubwa ni viongozi kukosa integrity (uadilifu). Kwanza ni integrity ya viongozi wenyewe, pili ni commitment (wito), tatu ni nationalism (utaifa). Haya ndiyo yalikuwepo wakati wa Mwalimu,” alisema Dk. Kitine. Alisema baadhi viongozi wa serikali wamepoteza sifa kuu tatu za uongozi ambazo ni kuwa na uadilifu, wito na kuweka mbele
utaifa, sifa ambazo alisema ndizo zilikuwa nguzo ya uongozi wakati wa Serikali
ya Awamu ya Kwanza, chini ya Baba wa Taifa, hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alisema uteuzi mbaya wa viongozi hususan uteuzi wa mawaziri, umechangia
kupatikana kwa viongozi wasio waadilifu, wengi wao wakijihusisha na vitendo vya rushwaCHANZO: Tanzania Daima
IFUATAYO NI HABARI ILIYOBEBA MATAMSHI YA DR KITINE.![]()
MKURUGENZI Mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk. Hassy Kitine, amesema taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la uongozi, ambalo halijawahi kutokea katika historia ya nchi.
Kitine ambaye aliiongoza idara hiyo nyeti kwa karibu miaka 30 zama za Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, alisema ukosefu huo wa uongozi umesababisha nchi iongozwe kienyeji.
Kachero huyo namba moja kwa miaka mingi, ambaye alilazimika kujiuzulu wadhifa wa uwaziri wa nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa, mwishoni mwa miaka ya 1990 kutokana na kuhusishwa na kashfa ya mkewe kufuja fedha za umma kiasi cha shilingi milioni 40, alirejea kutoa kilio chake cha miaka mingi cha kuporomoka kwa maadili ya uongozi nchini.
Kitine ambaye aliwahi pia kuwa Mbunge wa Makete kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitoa matamshi hayo mazito katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na waandishi wa vyombo kadhaa vya habari.
“Hali tuliyofikia si nzuri, tena niseme ni mbaya sana. Kuna kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya uongozi.Na hii nawaambia, nchi haijawahi kuwa katika hali mbaya huko nyuma kama ilivyo sasa. Kwa hali tuliyofikia, ni vigumu kurekebisha maadili ya uongozi.
“Tatizo kubwa ni viongozi kukosa integrity (uadilifu). Kwanza ni integrity ya viongozi wenyewe, pili ni commitment (wito), tatu ni nationalism (utaifa). Haya ndiyo yalikuwepo wakati wa Mwalimu,” alisema Dk.Kitine.
Akizungumza kwa kujiamini kama ilivyo kawaida yake, Kitine alisema viongozi wengi wa serikali wamepoteza sifa kuu tatu za uongozi ambazo ni kuwa na uadilifu, wito na kuweka mbele utaifa, sifa ambazo alisema ndizo zilikuwa nguzo ya uongozi wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, chini ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“That was possible (hilo liliwezekana) chini ya Mwalimu. Kama alikuwa akifanya kosa, basi kosa hilo lilikuwa likitokea tu wakati akifanya jambo kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. "
“Philosophy (falsafa) ya Mwalimu, ilikuwa kwanza Mungu, pili Tanzania, halafu yeye binafsi. Kila kiongozi anayetofautiana na Mwalimu tu hulifikisha taifa hili kubaya, if you differ with him, utaishia kubaya,” alisema Dk. Kitine akionyesha hali ya masikitiko.
Alisema uteuzi mbaya wa viongozi, hususan ule wa mawaziri, umechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa viongozi wasio
waadilifu, wengi wao wakijihusisha na vitendo vya rushwa. “Haiwezekani viongozi wakateuliwa kwa misingi ya mitandao …sijui, kwa msingi wa politics of division (siasa za makundi) ndani ya chama. Haiwezekani nchi ikaendeshwa kienyeji. Integrity should be number one (uadilifu unapaswa kuwa kitu cha kwanza kuzingatiwa). "
“Mtu anajiuzulu, anafukuzwa uwaziri kwa sababu ya kashfa, kwa sababu ya kukosa maadili, halafu anabakia kuwa mbunge na mjumbe wa kamati kuu ya chama, nini hii? Hii haifai. Waziri akikosa uadilifu anatakiwa aondolewe mara moja nyadhifa nyingine zote alizobakiwa nazo. Nadhani hii itasaidia,” alisema Dk. Kitine pasipo kutaja jina la kiongozi yeyote.
Kitine ambaye wakati wote wa mazungumzo yake alisema alikuwa anataka kujadili masuala muhimu na si watu, alieleza namna asivyo na imani na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na tatizo la rushwa kubwa. Kwa mujibu wa kachero, mwanasiasa na mwanazuoni huyo, hatua hizo ambazo zinahusisha baadhi ya watu wenye majina makubwa kufikishwa mahakamani, zimechukuliwa kwa ajili tu ya maandalizi ya uchaguzi ujao.
“Nilikuwa kiongozi wa kwanza kuzungumzia rushwa kubwa miaka 10 iliyopita. Nilisema ndiyo inayovuruga uchumi kuliko hata rushwa ya
nesi, hakimu, polisi,.… hakuna hata mkubwa mmoja aliyekamatwa. Ilinigharimu sana, na mimi nilipata adhabu ya kuzuiliwa kikao kwa miezi miwili, kama huyu nani huyu, Zitto (Kabwe). Wakati huo ilikuwa ndani ya CCM".
“Mimi nadhani hatua hizi zinazochukuliwa hazilengi kukomesha tatizo la rushwa, ni siasa tu za uchaguzi,” alisema Dk. Kitine.
Alipoulizwa nini kifanyike ili kukabiliana na tatizo hilo la uongozi mbaya, pamoja na mambo mengine, alielekeza changamoto zake kwa Idara ya Usalama wa Taifa.
“Usalama wa Taifa should be completely clean (unapaswa kuwa safi kabisa). Idara hii inatakiwa kuwa, juu ya mambo ya rushwa, iwe safi kabisa. Usalama wa Taifa ndiyo unayoteua viongozi, ndiyo inayoshirikiana na rais kwa kumshauri katika kuteua mawaziri. Sasa kama Usalama wa Taifa ukiwa mchafu ndio tunapata viongozi wala
rushwa. Nafikiri vigezo vinavyotumika kuteua viongozi pia vina matatizo,” alisema Dk. Kitine.
Kada huyo wa CCM ambaye kitaaluma ni mchumi na mwanasheria, akizungumzia hali ya uchumi nchini, alisema kwa kiasi kikubwa uchumi umeshikiliwa na wageni kuliko wazawa, na kuelezea kusikitishwa kwake juu ya kuwepo kwa pengo kubwa kati ya matajiri na maskini.
Akitoa mfano alisema, miongoni mwa mambo yanayoonyesha kuparaganyika kwa mambo ni kukithiri kwa idadi ya ombaomba mitaani. “Mwalimu asingeruhusu watu hawa waombeombe barabarani. Kazi za Watanzania ni udereva teksi, daladala, mabasi, kazi ya uboi ndani ya nyumba na kazi ya kufagia barabarani. Hizi ndizo kazi za Watanzania na hawa ndio wenye mali."
“Uchumi huu wa Watanzania si wa kwao. Watanzania ambao ni matajiri hawazidi hata watano. Hakuna sera bora za kusaidia kutumia
maliasili zetu ili zitupe fedha ya kujenga shule, madaraja, hospitali…..”
alisema Dk. Kitine. Akizungumzia utendaji wa kazi wa Bunge katika kusimamia utendaji wa serikali, Kitine alisema kazi inayofanywa na taasisi hiyo hivi sasa ni kubwa kuliko ilivyopata kuwa wakati wowote huko nyuma.
Hata hivyo katika kuusifia utendaji wa kazi wa Bunge, aliupongeza mchango mkubwa na muhimu wa wabunge wa upinzani katika kuiimarisha taasisi hiyo muhimu. “Ni Bunge zuri kuliko lilivyowahi kuwa huko nyuma. Linaonyesha kila dalili za uhuru. Upinzani unafanya kazi nzuri. Bunge liko wazi zaidi na wabunge wanatoa michango mingi yakinifu, yenye manufaa kwa taifa. Likiendelea hivi tutafika mahali pazuri,” alisema.CHANZO :Tanzania Daima
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Haroun Ali
Suleiman, amesema haoni sababu ya kujiuzulu wadhifa huo kwa madai ya wanafunzi
wengi Zanzibar kufanya vibaya katika mitihani yao ya kidato cha nne.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, alisema utamaduni kama huo haupo Zanzibar na
wangejiuzulu mawaziri wengi wa elimu waliopita akiwamo Katibu Mkuu wa CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad.
Waziri Suleiman ametoa kauli hiyo huku kukiwa
na malalamiko kutokana na matokeo mabaya ya mitihani, huku baadhi ya wanasaisa
wakimtaka awaombe radhi Wazanzibari na kutangaza kuwajibika kutokana na
kusimamia vibaya sekta hiyo.
Alisema
kimsingi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inapaswa kupongezwa kutokana na
mafanikio inayopata katika sekta ya elimu, ikiwamo kuongezeka kwa shule za
serikali kutoka sita kabla ya Mapinduzi hadi 134 hivi sasa.
Inashangaza kuona watu wamekuwa wepesi wa
kulaumu pale matokeo yanapokuwa mabaya, lakini yanapokuwa mazuri hushindwa kumpa
sifa anazostahili. Tangu kushika wadhifa huo mwaka 2001, kuna
mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa vile kiwango cha kufaulu kimeongezeka
kutoka asimilia 77.3 mwaka 2000 hadi asilimia 84.6 mwaka 2007.
Matokeo mabaya yaliyojitokeza mwaka huu si jambo
geni kwa vile wanafunzi wamekuwa wakifanya vizuri katika baadhi
ya wakati na mara nyingine kufanya vibaya. Akiwa ameshikilia takwimu za kufaulu
wanafunzi tangu mwaka 1971, alisema hata yeye hakufurahishwa na kiwango cha
kufaulu kuanguka mwaka huu kutoka asilimia 84. 6 hadi 77.3.
Mwaka 1982
wakati Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa Waziri wa Elimu
Zanzibar, kiwango cha kufaulu kilishuka zaidi hadi asilimia 64.4.
Haroun
alisema hivi sasa kuna sababu mbalimbali zinazochangia wanafunzi kutofanya
vizuri ikiwamo upungufu wa vitendea kazi, uhaba wa vifaa vya sayansi pamoja na
walimu wa masomo hayo.
Hata hivyo, alisema Serikali ya Zanzibar kwa
kushirikiana na Serikali ya Marekani imeanza kuchukua hatua za kuondoa uhaba wa
vifaa, ikiwamo vitabu vya sayansi na kujenga shule za sekondari 19 ambazo kila
wilaya itanufaika hapa Zanzibar.
Hadi ifikapo mwaka 2010 tatizo kwa
baadhi ya wanafunzi kukaa chini litakuwa limekwisha pamoja na kuwapo uwiano kati
ya idadi ya wanafunzi na walimu katika darasa. Hivi sasa serikali inaendelea na
programu ya kusomesha walimu katika ngazi mbalimbali ambao watatumika kufundisha
katika shule za sekondari.
Hata hivyo, ni kweli Zanzibar inakabiliwa na
wimbi la walimu wanaomaliza katika viwango vya shahada kukimbilia ajira binafsi
zenye maslahi zaidi. Ili kukabiliana na tatizo hilo, serikali imeamua kupitia
utaratibu wa malipo kwa walimu kuyaboresha zaidi.
Juzi Chama cha
Wananchi (CUF) kilisambaza taarifa kwa vyombo vya habari kikimtaka waziri huyo
kuwaomba radhi wazee na vijana wa Zanzibar kwa kushindwa kwake kuinua na kukuza
elimu Zanzibar.CHANZO: Tanzania
Daima
JAPO SIAFIKIANI NA HOJA ZILIZOTOLEWA NA MHESHIMIWA HUYU KUTETEA UNGA WAKE,NASHAWISHIKA KUKUBALIANA NAE KWENYE KAULI YAKE KUWA UTAMADUNI WA KUJIUZULU HAUPO (SI ZANZIBAR TU BALI TANZANIA KWA UJUMLA).HEBU TUANGALIE MFANO WA CHAPCHAP HUKO ATCL,UNADHANI KWANINI HADI MUDA HUU HAKUNA ALIYEJIUZULU?MAJUZI MMOJA WA MANAIBU GAVANA BOT AMETAJWA MAHAKAMANI KUWA ANAHUSIKA KWA NAMNA FLANI KWENYE SKANDALI LA EPA,KWANINI HAJAJIUZULU KUPISHA UCHUNGUZI?BAADHI YA WATENDAJI WALIOTAJWA KWENYE TUME YA MWAKYEMBE HAWAJAJIUZULU HADI LEO,KWANINI?JIBU LISILOHITAJI TAFAKURI NI HILO ALOTOA MUUNGWANA HUYO WA ZENJE:HAKUNA UTAMADUNI WA KUJIUZULU.JE CHANZO NI NINI?KWA MTIZAMO WANGU TATIZO LIKO KWA WALIOWATEUA WA HAO WANAOPASWA KUJIUZULU.UTAMADUNI HUU UMELELEWA NA UKWELI MCHUNGU KWAMBA MTU ANAWEZA KUAMUA KUJIUZULU PINDI ANAPOBORONGA JUKUMU FLANI LAKINI ALIYEMTUA HAONI UMUHIMU WA KUFANYA HIVYO.FRANKLY SPEAKING,UKOSEFU WA UWAJIBIKAJI KATIKA MAONEO MBALIMBALI UNACHNGIWA ZAIDI NA TABIA YA KULEANA NA KUBEMBELEZANA KATI YA MABOSI NA WALIO CHINI YAO.LAITI KUNGEKUWA NA KANUNI KWAMBA "UKIBORONGA ,UNAWAJIBIKA.USIPOWAJIBIKA UNATIMULIWA" BASI SI AJABU TUNGESHUHUDIA WABABISHAJI WENGI WAKIACHIA NGAZI KUEPUKA FEDHEHA YA KUTIMULIWA AMBAYO MARA NYINGI HUAMBATANA NA KUNYIMWA MARUPURUPU YA KUMALIZA AJIRA.