Featured Posts

Thursday, October 14, 2010

Urban Pulse Yawaletea Ratiba ya Tour ya UK ya Msanii DIAMOND


Urban Pulse Creative inawaletea Urban Tour ikimshirikisha msanii Diamond aka mzee wa mbagala pamoja na first lady wa Urban Pulse Fyah Sis mwezi Novemba Ndani ya UK. Show zitafanyika katika miji mitatu ya UK,

6th Nov. 2010
CLUB OPUS
Theatre Distric
Savoy Cresent
Milton Keynes MK9 5UP

12th Nov 2010
THE CLUB
179 – 183 London Road
Croydon, London
CRO 2LR

27th Nov 2010
PANAMA BAR
Gas ST
Birmingham
B1 2JT

Vilevile Urban Tour ikishirikiana na Tanzanian Community itakuwa inafanya Kampeni dhidi ya gonjwa la Malaria ambalo linaangamiza binadamu wengi duniani
Wote mnakaribishwa kuja na kuparty kwa Swaga za Kibongo na UK, badhi ya mapato yatakwenda kuchangia kwenye upambanaji wa Malaria

WOTE MAKARIBISHWA,

BARAKA

URBAN PULSE CREATIVE


Makala Nyingine Mwanana ya Mdau Idd Amiri Kuhusu Vyuo vya Kutengeneza Shahada


Profesa Nkunya na vyuo vya kutengeneza shahada.

Na Idd Amiri



Wiki iliyopita Profesa Mayunga Nkunya, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, aliongea na waandishi wa habari na baadaye akatoa tangazo juu ya kuwepo kwa vyuo vikuu visivyotambulika hapa nchini na huko nchi za nje vinavyotoa shahada za udaktari wa heshima wa falsafa kwa watu mbalimbali mashuhuri hapa nchini na kwingineko barani Afrika hususa ni kwa Wabunge, Mawaziri na hata Marais. Marais wetu wawili nao ni madaktari wa falsafa.

Katika tangazo lake kuhusu kuzuka kwa vyuo hivyo amebainisha kuwa kumekuwa na mbadilishano wa fedha kati ya wahusika na vyuo hivyo na hili ni kwa nia ya kujipa hadhi wasiyositahili waheshimiwa hao kwa wanajamii.

Profesa Nkunya amekuja na kauli hii baada ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi profesa Jumanne Maghembe, kutoa ufafanuzi juu ya kutolewa kwa shahada hizo kutoka katika vyuo hivyo ambavyo kwake yeye hakuviita visivyotambulika au vyuo vya kutengeneza shahada kama profesa Nkunya alivyoviita.

Profesa Maghembe alitoa ufafanuzi katika mkutano wa mwisho wa Bunge La Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko Dodoma, Waheshimiwa aliowataja Profesa Maghembe ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Kwera, Mheshimiwa Chrisant Mzindakaya na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Abeid Karume.

Katika kikao hicho cha Bunge wakati wa kuchangia mijadala mbalimbali Mheshimiwa Juma Ngasongwa, ambaye kwa kiwango cha elimu au usomi ni daktari wa falsafa alilalamika kuwa pamoja na kuwa na shahada nzuri ya udaktari wa falsafa katika uchumi lakini haiitwi Member of the learned brothers!. Mara nyingi wanasheria huiitwa hivyo ingawa binafsi sijui inakuwaje msomi mwenye shahada ya kwanza awe katika kundi hilo na madaktari wa falsafa katika fani nyingine wasiwe katika kundi hilo, Kwa leo hilo siyo sehemu ya mjadala wangu.

Profesa Maghembe alisema kuwa Mheshimiwa Mzindakaya amepewa shahada ya heshima ya udakatari wa falsafa kwa kutambua mchango wake katika upenzi, ujenzi na maendeleo ya viwanda na Mheshimiwa Karume alitunukiwa shahada yake kwa kufanikiwa kutokomeza malaria katika visiwa vya Zanzibar.

Lakini hii si mara ya kwanza kuhojiwa kwa shahada za heshima za watu mbalimbali, katika vikao vya Bunge miaka ya nyuma huko Mheshimiwa Dr. Hansy Kitine aliwahi kuongelea suala hilo na aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu Sayansi na Teknolojia Dr. Pius Sabasi Ng’wandu alimjibu kuwa haoni kama kuna ubaya wowote kwani hakuna madhara kwa mtu kupewa hadhi hiyo. Lakini hoja ya Kitine ilikuwa zaidi kwa maprofesa wa mitishamba. 

Kwa wale waliowahi kutembelea makumbusho ya Bagamoyo watakuwa wanamfahamu Profesa Kejeli, huyu jamaa ni mahiri kwa kuelezea historia ya mji wa Bagamoyo tena kwa kasi ya ajabu, Kumbukumbu za watu, miaka na mahali alizonazo profesa Kejeli kwa kweli zinakuacha mdomo wazi anaposimulia. Nilibahatika kumwuliza ilikuwaje akaitwa profesa alinijibu kuwa alipewa hadhi hiyo na Marehemu Meshack Maganga aliyekuwa Mkuu wa Chuo Cha Uandishi wa Habari Tanzania (TSJ).

Miaka mitatu iliyopita nilikuwa nikifuatilia mwendelezo wa kipindi cha kweli (Reality show) cha kila mwaka cha runinga ya shirika la utangazaji la uingereza (BBC) katika BBC Two, kinachoitwa You’re Fired ambacho huongozwa na Milionea wa Kiingereza Sir Alan Sugar. Lengo la kipindi hiki huwa ni kutafuta mtu mmoja ambaye bila kuangalia kiwango cha elimu yake anaweza kuwa na mbinu za kijasiliamali na kimenejimenti kwa kuwaongoza wenzie katika kutafuta faidi iwe katika hoteli, kiwanda na mahali popote ambapo uzalishaji kwa lengo la kutafuta faidi unafanyika. Mshindi wa mchakato huo huajiriwa katika moja ya makampuni ya milionea huyo na kwa mwaka analipwa paundi za kiingereza laki moja (100,000). 

Ili kufanikisha mkakati wake huo Sir Alan Sugar, aliwagawa washiriki wake wapatao 20 katika makundi mawili ya kila upande watu kumi, akawagawia mtaji wa kuendesha biashara ya kufua nguo ambapo makundi yote mawili yalitakiwa kupita kwa wateja majumbani na kujitangaza na hatimaye wateja walikubali kuwapa nguo zao zikafuliwe na kunyooshwa kwa gharama walizokubaliana.

Hatimaye ikafika wakati wa kuangalia nani kapata nini na kapoteza nini, makundi yote mawili yalipata faidi lakini moja lilipata faidi ndogo na hapo Sir Alan akawa mbogo akitaka kujua nani kasababisha kutopatikana kwa faidi kubwa na kwa bahati mbaya nguo za mmoja wa wateja zilikwenda kwa mteja ambaye siye mwenye nazo!

Katika kutafuta uzembe ulikuwa wapi alijitokeza mshiriki mmoja katika kundi hilo akapaza sauti kuwa tatizo katika kundi lao kuna washiriki ambao siyo wasomi, ndipo Sir Alan akamwuliza kuwa ana elimu ya kiwango gani? mshiriki yule akajibu kuwa ana shahada ya uzamili katika uchumi. Swali la mwisho na ambalo lilimwondoa katika ushiriki ule lilikuwa ametumiaje elimu yake katika kuleta faida, mshiriki akawa kimya na Sir Alan hakuwa na la ziada ila kumfukuza huku akisema wale wafanyakazi wake ambao hawana shahada lakini wanamwingizia faida wana tatizo gani.

Mshiriki aliyekuja kushinda na hatimaye kuajiriwa kwa mshahara wa paundi 100,000 alikuwa ni yule aliyekaa chuo kikuu kwa miezi mitatu na kuacha kwa sababu alionyesha kuwa ana mbinu za kijasiliamali na kimenejimenti za kuweza kuzalisha faida katika kampuni.

Sasa nirejee kwenye usomi na shahada za bandia na za kweli, hapa najiuliza maswali mengi lakini kwa uchache ni inawezekana vipi kwa msomi ambaye ni profesa kuteuliwa kuwa waziri wa mawasiliano na uchukuzi na baada ya muda Fulani anapoondoka wizara ile mashirika karibu yote katika ile wizara yanakuwa taabani? Msomi mwingine ambaye ni profesa anaanzisha taasisi isiyokuwa ya kiserikali huku fedha zote za kuendeshea taasisi hiyo zikitoka nje kwa wahisani wake, anajenga jumba lake kubwa la kifahari, ananunua gari la kifahari pia na anasomesha watoto wake ughaibuni na katika kufanikisha mradi anaendesha utafiti ambao mara zote ni kuangalia kama mwanasiasa fulani anapendwa na watanzania au la? Fikra zangu duni ni kuwa baada ya kuwa mtu yeyote amesoma na kuwa na hadhi ya profesa na chuo kumkubali nadhani anatakiwa kuonyesha kwa vitendo thamani ya elimu aliyopata.

Kwahiyo unaweza kujiuliza kutokana na yale niliyoeleza hapo juu kuwa hii ndiyo gharama ya kodi za watanzania walizotumia kumlipia yeye wakati akisoma inasaidia nini kujua kuwa fulani anapendwa au hapendwi? Unakuwa na msomi mwingine ambaye ni daktari wa falsafa na waziri vilevile lakini hajui hata kutoka Mwenge jijini Dar es Salaam hadi jimboni kwake ni kilomita ngapi na huyu ndiye anayetakiwa kusimamia ujenzi wa barabara? Jambo linalonipa taabu ni kama kwa utashi wangu niwape heshima ya usomi waheshimiwa hawa? Upo mfano mmoja hivi inakuwaje kwa msomi kung’ang’ania kufanya kazi katika chuo kimoja tu wakati anaweza kusaidia mahala pengine hata kama siyo kwa kufundisha, kwanini msomi kama huyu asifanye kazi nyingine yoyote zaidi ya kufundisha na kufanya utafiti ambao matumizi yake ni yamkini?

Kwa bahati mbaya nimekuwa nikijikuta nawasilikiza au kuwatazama wasomi mbalimbali wakiongea katika runinga na redio na wengi ni wakosoaji wazuri, kuna wakati Mzee Ali Hassani Mwinyi alipokuwa rais wa Tanzania alikuwa na mshauri wa uchumi ambaye ni profesa na ni huyo huyo leo hii anasema kuwa serikali inategemea sana misaada katika bajeti yake na ijaribu kuja na mbinu za kujitegemea, lakini wote tunajua jinsi nchi hii ilivyopoteza viwanda na raslimali chungu mbovu wakati msomi huyu alipokuwa msahuri wa mzee ruksa.

Wakati Rais Jakaya Kikwete akitoa hutoba ya kulivunja Bunge, Mjini Dodoma kulikuwa na wasomi wawili ambao walialikwa na Runinga ya Taifa(TBC) ili watoe tathmini yao kutokana na hutoba ile na kwa kuwa ilikuwa na takwimu nyingi hapo ulikuwa ni uwanja wao. Kilichonishangaza ni moja wa wasomi wale alipokuwa akiunga mkono takwimu zile kwa kusema kuwa zinatokana na utafiti uliofanyika wakati hali halisi haiendani kabisa na yaliyokuwa yakitoka kwenye takwimu zile, hii ilinipa simanzi sana.

Kwa mfano, katika hotuba ile kulitajwa kuwa umasikini umeshuka kwa kiwango cha kuridhisha na kwa bahati mbaya wiki ile ile katika kituo kingine cha televisheni ilionyesha mama moja akiwa katika kijiji kimoja wilayani Kyela akiomba msaada wa kujengewa nyumba na wazungu waliokuwa katika ziara ya kujifunza maisha ya watu wa nchi hii. Mama yule ana watoto saba ambao bado hawajawa na uwezo wa kujitegemea, yeye mwenyewe ni mgonjwa, nyumba anayoishi ipo mbioni kudondoka, katika hali ile takwimu za Mheshimiwa zilizopata baraka za wasomi zilikuwa sahihi kweli?

Nirudi kwa kuuliza swali usomi wake umeisaidiaje nchi hii? Kuwa daktari wa falsafa, profesa kama hakuna ulichosaidia kupambana na matatizo ya watanzania na kwa bahati mbaya ukafanya mambo kama siyo msomi bado ni hasara kwa taifa.

Kwa wale tunaofuatilia mienendo ya hawa wote wawili naamini hatuna shaka kwa sababu zilizotolewa na vyuo hivyo kuamua kuwaenzi kwa kwatunuku shahada za falsafa za udaktari wa heshima kwani michango yao tumeiona na hata profesa Maghembe alikubaliana na vyuo hivyo kutoa shahada hizo.

Hivi Karume kuitwa daktari kwa kuwaondolea wazanzibari gonjwa linalotafuna maisha ya watu chungu mbovu katika nchi za kitropiki kuna ubaya? Wasomi wanaotambulika kwa kupitia vyuo vinavyotambulika mbona wameshindwa kuwaangamiza wale mbu pale Hospitali ya taifa Muhimbili? Mzindakaya kuanzia kwenye uanzishaji wa SIDO hadi kuwa na kiwanda chake mwenyewe hilo ni tatizo? Wasomi wangapi hatujui wameifanyia nini nchi hii?

Ninao mfano moja wa kijana aliyemaliza masomo yake kutoka chuo cha maji pale ubungo, jijini Dar Esa salaam, miaka ya mwanzo ya themanini aliporudi kijijini kwake mkoani Iringa alijaribu kufanya matembezi katika moja ya milima inayozunguka kijiji chake, kwa bahati nzuri alifanikiwa kuona chemchem ya maji katika moja ya milima ile, wazo likamjia akawasilisha serikalini na wanakijiji wakafanya harambee ya kuchimba mtaro wa kupitishia mabomba ya maji na yeye akatumia utaalamu wake kukinga maji yale ili yatiririke kuelekea vijiji vya karibu.

Kwa bahati nzuri serikali ilimsikia na kwa juhudi na maarifa aliyokuwa nayo mradi ule unatoa maji kwa vijiji zaidi ya 10 leo hii na hakuna hata siku moja maji yamekatika na wanachi wanaulinda mlima ule kama almasi yao.  Baada ya mradi ule kufanikiwa aliendelea kufanya kazi katika miradi ya maji sehemu mbalimbali nchini na kila alipokwenda na kuondoka wananchi walimlilia, je huyu akipewa shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa kuna tatizo?

Kuna wakati niliwahi kuuliza swali kwa raia moja wa nchi za magharibi kuwa kwanini Waziri Mkuu wa Uingereza wakati huo Gordon Brown, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, Condereza Rice hawapendi kuitwa kwa majina ya kisomi ya Daktari na profesa wakati wanasitahili hivyo kwa elimu zao, alinijibu kuwa siyo vizuri kuitwa msomi na kesho yake ukafanya mambo kama siyo mtu aliyekwenda shule.

Lakini hoja ya Profesa Nkunya ni kama hapendezwi na tunu wanazopata watu mbalimbali kutoka katika vyuo visivyotambulika na kwa hili yuko sahihi, angependa shahada hizi zitolewe zaidi kwa wale wanaosomea kwa kukaa vyuoni na kusimamiwa na wahadhiri na kwa vile huwezi kupata shahada ya udaktari wa falsafa bila kufanya utafiti kwa vigezo vilivyowekwa na chuo ni dhahiri ni lazima uhenyeke au utaabike kabla hujavaa joho hilo.

Kwangu mimi ambaye siyo msomi sioni tofauti yoyote kati ya viwanda vya kutengeneza shahada kama profesa Nkunya alivyoviita na vyuo vinavyotambulika. Lazima tukubali kuwa Vyuo vyetu ni mahali pa kwenda kuchukua vyeti ili kupata ajira kwa sababu hilo ndilo sharti kubwa kuwa na elimu ya shahada ya kwanza, ya pili, tatu hadi mwisho na hii yote inategemea mshahara atakaolipwa mtarajiwa kwa elimu yake na majukumu atakayopangiwa na ofisi inayomwajiri.

Hapa ni kama mashindano ya Bongo Star Search kwani aliyeshinda mwaka jana amefanya kazi yoyote ya muziki? Si ni fedha tu ndizo zinazotafutwa kipaji ni jambo la wengine, unaweza kuiga mwanamuzi unayempenda na kumudu vizuri ili watu wakupigie kura upate mahela! Na kwa upande wa shahada ni hivyo hivyo kinatafutwa cheti kwa gharama yoyote iwe kwa kuiba mitihani, kuhonga mwalimu kwa fedha na ngono, kukodi mtu akufanyie mtihani, kunakili utafiti wa mtu mwingine na hata kukodi mtu wa kufanya utafiti wenyewe suala ni maisha nani anabisha?

Siyo siri kuwa kupata shahada hakuendani na hadhi au muktadha na mantiki ya shahada hiyo, tujiulize wakati tuna wanasheria wenye shahada lukuki inakuwaje mikataba ya madini inakuwa kama ya akina Mangungo wa Msovelo? Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuwa chafu na wahasibu wasomi ndiyo hao? Waandishi wa habari wanaofanya uandishi wa habari kama maofisa uhusiano wa makampuni na shahada zao? Makocha wa mpira wasioleta kombe hata moja la kimataifa huku wakitaka waitwe super coach? Wahandisi wa barabara zinazoharibika siku ya kwanza ya ufunguzi na shahada zao? Wahandisi wa maji wanaotandaza mabomba ya maji wakati wakijua kuwa hakuna maji yatakayotoka na shahada zao? Fani zote zina matatizo na ni wasomi wa vyuo vyetu tunavyovipenda sana na kuviita vinatambulika. Kutambulika kwa chuo bila ufanisi ni sifuri tu. Kama wasomi wetu wangekuwa wanaonyesha mifano kwa wasiosoma ingekuwa ni halali kuwanyooshea kidole wanaofanya ujanja wa kielimu. Msomi hawezi kutuonyesha jinsi alivyoweza kutumia elimu yake kuwa na shamba lenye mazao na mifugo iliyonona kila siku anafanya utafiti ili kiwe nini?

Kwa hapa nirudi miaka ya nyuma kwa upande wa Mahakama, kulikuwa na Mawakili ambao watu wengi walipenda kwenda kuwaona wakitoa hoja zao mahakamani kwa mfano, akina Murtaza Lakha, Ismail Mukhadam, Francis Uzanda na baadaye wakaja akina Abasi Mselem, Dr. Masumbuko Lamwai na Michael Wambali.

Wakati huo mashahidi walikuwa na wakati mgumu sana kwa waheshimiwa hawa kwa hoja na maswali waliyokuwa wakiwatupia wakati wakitoa ushahidi wao mahakamani nilitegemea leo tungekuwa na wanasheria wakali zaidi ya hawa lakini hilo halipo na bado tuendelea kuzalisha kundi la werevu ambao ni members of the learned brothers kila mwaka katika vyuo mbalimbali hapa ndani na nje ya nchi kwani sivinatambulika kwenye mafaili yetu!

Kwa waandishi wa habari ambao kwa kweli kwa wakati huo kulikuwa hakuna hata chuo kimoja ambacho kilikuwa kikitoa shahada za uandishi wa habari watawakumbuka akina Stanley Katabalo na John Rutayisingwa, hawa wote ni marehemu kwa sasa kwa jinsi walivyoweza kuandika habari za uchunguzi wa kikachero na kuwafanya wasomaji wa magazeti kufuatilia habari zao kila magazeti yalipokuwa yakitoka, naye Mnenge Suluja alivyokuwa akiandika habari za mahakamani na kumfanya msomaji ahisi kama alikuwepo mahakamani siku ya shauri. Leo tunao wenye shahada si ndiyo! Habari gani ambayo wameandika ikionyesha kuwa inaendana na usomi wao?

Nimeanzisha mjadala huu ili wachangiaji wengine wanisaidie kupata picha halisi ya viwanda vya kutengeneza shahada na vyuo vinavyotambulika kwani mimi siyo msomi na sina nia mbaya ya kuleta utetezi wa shahada za heshima tatizo langu ni ujinga na uelewa mdogo nilio nao, bado sielewi tofauti iko wapi na nini mchango wa wale tunaowaita wasomi waliobobea katika maendeleo ya nchi hii?


Waweza kunisaidia kwa hili kwa kuniandikia barua pepe kwa anwani hii kilindi80@yahoo.co.uk

ASANTE SANA MDAU IDD KWA MAKALA HII MWANANA.WADAU WENGINE PIA MNAKARIBISHWA KUTUMA MAKALA ZENU AU CHOCHOTE KILE CHA MANUFAA KWA JAMII.

Makala Maridhawa ya Mdau Idd Amiri Kuhusu Ujasusi



Tunahitaji taasisi ya kijasusi ya uchumi na biashara?

Na Idd Amiri

Julai mosi mwaka huu soko la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki lilianza rasmi, soko hili linajumuisha nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Ni soko ambalo moja ya mihimili yake ni kuruhusu bidhaa kuuzwa au kusafirishwa toka nchi moja mwanachama kwenda nyingine pasipo kutozwa kodi.

Wakati huo huo wiki iliyopita Jumuiya ya Uchumi na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ilitimiza miaka 30 toka ianzishwe ambayo Tanzania ni Mwanachama. Malengo na Madhumuni ya Jumuiya zote mbili ni kama yanafanana ingawa kuna tofauti za hapa na pale. Wakati Tanzania inajitoa kutoka Umoja wa soko la pamoja la ushuru na forodha kwa nchi za kusini na mashariki mwa Afrika(COMESA) ilikuwa na nia ya kujiimarisha zaidi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) kama alivyotamka wakati huo aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Idd Simba.

Lakini mwanachama mwingine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya bado ni mwanachama wa COMESA na hata Zambia ambayo ni mwanachama wa SADC bado ni mwanachama wa COMESA vile vile. Nchi zote mbili zimeendelea kuwepo katika Jumuiya hizo kwa maslahi ya kiuchumi zaidi. Kwa Tanzania bado hatujapata kuelezwa au kuona faida za moja kwa moja ambazo kama nchi imepata kwa kuwepo katika Jumuiya ya SADC kwa kipindi chote cha Miaka 30 iliyopita ingawa wanasiasa na baadhi ya wachumi wanaendelea kuhudhuria vikao vya Jumuiya hii. SADC ilitokana na nguvu ya kisiasa ya wakati huo ya nchi zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi kusini mwa Afrika.

Lengo la kuleta mada hii katika safu hii ni kujaribu kuona kama wanaohusika na sera katika Serikali ya Tanzania wamekuwa wakifanya utafiti wa kutosha kwa nia ya kujua faida halisi za kuwa katika jumuiya yoyote kabla ya kujiingiza au imekuwa ni kufuata mkumbo. Faidi kubwa ambayo kama nchi inaingia katika jumuiya yoyote siyo siasa na maneno ya kuremba, kinachotizamwa zaidi ni kuendeleza ajira kwa watu wa nchi ile na hivyo kujenga usitawi wa kiuchumi na kijamii mengine huwa ni ziada tu, kwa mfano Afrika ya Kusini kwa kuwa Mwanachama wa SADC imefanikiwa kuuza bidhaa za viwanda kwa kiasi kikubwa sana kwa nchi hizi bila mizengwe na hivyo kujenga, kulinda, kupanua na kuimarisha mfumo wa ajira katika nchi ya Afrika ya Kusini, suala hapa ni uhakika wa kuwepo kwa soko la bidhaa zake ili kuneemesha watu wake na kupunguza vurugu za kijamii ambazo huchochewa na kutokuwepo kwa ajira.

Kumekuwa na mazoea ya kufikiri kuwa kuendelea kwetu kunategemea kujiingiza katika jumuiya hizi kwani wenzetu katika nchi zao wamekuwa na ujanja wa kutoa maelezo mengi kama vile kupitia SADC au EAC kutakuwepo na maendeleo ya Sekta ya nishati, barabara, Afya na mambo chungu mbovu lakini mwishoni mwa siku tunajikuta kama umeme, maji, barabara na vinginevyo tunajitafutia wenyewe kwa sababu kila nchi inataka kupata soko kwa mwenzie na hivyo haiko tayari kusaidia kuondoa matatizo ya umeme kwa mwenzie kwani kwa kufanya hivyo itakuwa inamwendeleza kiviwanda na hatimaye itakosa mahali pa kuuza bidhaa zake. Ni jambo liliowazi kuwa kama viwanda vya Tanzania havifanyi vizuri Afrika ya Kusini itafurahi vile vile Kenya itafanya inafurahi zaidi.

Hapa lipo angalizo dogo tu, Kenya inapanua Bandari yake ya Mombasa kwa sababu bidhaa nyingi ambazo zingepitia Dar Es Salaam kwa sasa zinapitia huko hivyo basi haitaki kumwamsha aliyelala ingawa ni Mwanafrika Msahariki mwenzie!

Nikirejea katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, yapo masuala mengine kama kuruhusu watu wa nchi hizi kusafiri, kuishi katika nchi nyingine na kupata ajira pasipo vikwazo kwa kazi za aina fulani, soko la ajira lililo huru na yapo mambo mengine mengi ambayo sina shaka wananchi katika nchi hizi wanayajua kwani tunaambiwa serikali zote tano zimefanya juhudi kubwa kuwafahamisha watu wake ingawa bado nina mashaka juu ya hili.

Nia yangu katika kuzungumzia suala hili la kuwemo katika Jumuiya hizi za ushirikiano ni kujaribu kuamusha hoja ya kuwa na Economic Intelligence au taasisi ya uchunguzi wa kijasusi wa uchumi na biashara ambayo kuna wakati ilipendekezwa na Mheshimiwa mmoja ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini haikuuungwa mkono na Waheshimiwa wengi na hatimaye ilikufa kifo cha mende.

Najua kuwa zipo taasisi zinazofanya tafiti (Think Tank) mbalimbali katika masuala ya uchumi na biashara hapa nchini lakini bado kunahitajika uamusho wa kujua nia ya wanaoshawishi kuwepo kwa jumuiya hizi, kwa sababu Kenya ambayo ndiyo ilikuwa kinara wa kuvunjika kwa iliyokuwa Jumuiya Afrika Mashariki wakati huo ndiyo hiyo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Jumuiya ya sasa inafanikiwa tena kwa kasi ya ajabu na tumekwishaona kuwa yenyewe ndiyo inayofaidi sana na kuwepo kwake!

Taasisi hii ingekuwa inakusanya taarifa mbalimbali kutoka kwa nchi hizi ili kujua baadhi ya mambo ya msingi ambayo kwa kila nchi inayahitaji au ilikuwa inafikiri itapata faida ikiwa itaingia katika soko hili au lile na mengine ambayo labda kwa ujanja inayaweka kando ili kufunika kombe ili mwanaharamu apite na wakati mwafaka ukifika iyaibue. Kazi yake ingekuwa kujua nini msimamo wa kila nchi na kuwasilisha taarifa yake kwa wajumbe wetu ambao wanaingia katika vikao mbalimbali vya majadiliano kwa nia ya kulinda maslahi ya Taifa na siyo kwenda kukusanya posho za vikao na masurufu ya safari.

Wakati haya na mengine yakiendelea kuna habari kuwa kuna majadiliano yanaendelea ili watalii wanaotembelea nchi hizi washukie nchi yoyote na kwenda popote katika nchi hizi bila kufuata taratibu za kimipaka kwa Watalii.

Kenya kwa muda mrefu imekuwa ikitangaza kuwa Mlima Kilimanjaro upo nchini humo na kwa kutumia shirika lake la ndege na mawakala mbalimbali wa utalii imefanikisha hilo na wakazi wa nchi za magharibi wanaotembelea Afrika Mashariki kwa nia ya kufanya utalii wameamini hivyo na wameutumia uwanja wa ndege wa Nairobi kama njia ya kwenda kupanda na kuuona mlima Kilimanjaro. Nenda nchi yoyote barani Ulaya uone maajabu ya matangazo hayo ndipo utaposhindwa kuelewa kama kweli tuna watu katika taasisi zetu zinazoshughulika na utalii kwa nini hawabishi na wao kutoa matangazo yanasema siyo kweli kuwa Mlima Kilimanjaro uko Kenya!

Hili likikubaliwa itakuwa faida kubwa kwa Kenya ambayo miaka nenda miaka rudi imedanganya watalii wa nchi zote duniani kuwa mlima Kilimanjaro upo kwake na siyo Tanzania na hivyo imefanikiwa sana kuteka makundi ya watalii kutoka sehemu mbalimbali duniania, kwa kukubaliana na hili Kenya haitakuwa na kazi nyingine ya kuutangaza mlima Kilimanjaro kwa hadaa tena, kazi imekwisha!

Wakati Kenya inaendelea na mikakati yake hiyo kwetu tumelala usingizi fofo na hakuna anayebisha si tunahudhuria vikao ili tulipwe posho kuna ubaya ugani? Wenzetu wa Kenya huwa wanatusoma mapema kuwa tunataka nini na wao wachukue vipi kile wanachokihitaji. Wengi tunaona jinsi Jumuiya hii inavyowanufaishi wao zaidi kuliko sisi.

Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na kutoelewana kwa nchi mbili wanachama za Tanzania na Kenya katika suala la kuuza meno ya tembo yaliyopo katika maghala mbalimbali hapa nchini, wakati Tanzania inataka kuuza meno hayo imekuwa ikitafuta kibali kutoka katika shirika lisilo la kiserikali la Kimataifa la CITES ambalo huwa linajishulisha zaidi na kuzuia uvunaji wa wanyama au viumbe walio katika hatari ya kutoweka duniani.

Tanzania na Kenya wote ni wanachama wa Taasisi hii, Tanzania inataka kuuza meno hayo ili fedha zitakazopatikana ziweze kusaidia katika kupambana na vitendo vya ujangili vinavyoendelea katika mbuga na hifadhi zake za kitaifa. Kenya inapinga kwa kudai kuwa kwa kuuza meno hayo kutachochea vitendo vya ujangili katika mbuga zake na inaishauri Tanzania ichome kwani hata yenyewe ilifanya hivyo miaka ya nyuma na hivyo majangili watakosa upenyo wa kuendesha shughuli zao.

Hizi ni nchi mbili ndugu na marafiki ambazo zipo katika jumuiya moja, zinapingana kwa jambo moja ambalo zingekubaliana wala kusengekuwa na aibu ya ujumbe wa Tanzania kwenda kwenye mkutano wa CITES uliofanyika mwezi wa julai huko Doha, Quatar na kuangukia patupu baada ya Kenya kuendesha kampeni ya kuhakikisha kuwa Tanzania haipati kibali kutoka kwa wanachama wengine wa CITES ili iweze kuuza shehena ya meno ya tembo.

Ni kwa kuona mambo haya mawili ndipo nilipoamua kaundika makala haya ili kuwaamusha walio katika serikali wasiendelee kulala na kuamini kuwa wako na jirani na ndugu mwema wakati ukweli wa mambo hauko hivyo. Jirani yetu ni mjanja sana na anajua nyendo zetu.

Nikianza na lile la kwanza la meno ya tembo utaona kuwa Kenya ilishakuwa na msimamo wa kupinga mapema pale tu Tanzania ilipoanza kusambaza habari zake chini kwa chini kuwa inataka kuuza shehena ya meno yake ya tembo. Sababu kubwa ni kuwa Kenya inataka kulinda mbuga zake na kwa hilo hakuna ujomba wa Afrika Mashariki hapa. Swali la kujiuliza ni je, tunao watu ndani ya serikali ambao kazi yao kubwa ni kufanya ujasusi wa kiuchumi na kibiashara wa kujua nani analenga kuzuia maslahi yetu ya kiuchumi na kibishara kabla hatujayaweka wazi?

Jibu la swali hili ni kuwa hatuna watu wa aina hiyo na ndiyo sababu tumefika tulipo kwa sasa na aibu tuliyo nayo. Watu wa kazi hii wapo katika kila nchi duniani hasa ile inayolenga kulinda utaifa wake katika ajira, maliasili, teknolojia, viwanda, sayansi na katika yale mambo yote ambayo kwayo inaamini yana maslahi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Tumekabidhi utaifa wetu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC wakati wenzetu wanaendelea kulinda maslahi yao ya kiuchumi na kibiashara kwa nia ya ustawi wa viwanda vyao na Mataifa yao.

Katika majadiliano ambayo yanaendelea kuhusu Soko la pamoja la Afrika Mashariki aliyewahi kuwa Waziri wa Utawala Bora katika Serikali ya Awamu ya tatu ya Benjamini Mkapa, Dk. Hassy Kitine alisema kuwa unapotafuta uhusiano na mtu masikini lazima ujiulize kuwa muda mwingi atataka kusaidiwa na wewe na ni hivyo hivyo Tanzania ilitakiwa kuunda jumuiya ya soko la pamoja na nchi tajiri za kiwango chake za Kongo DRC na Angola na siyo hizi za Afrika Mashariki ambazo kilaslimali zinaitegemea Tanzania.

Maneno ya Dk. Kitine yalinifanya nitafute baadhi ya watu ambao wamewahi kufika na wengine kuishi nchini Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo, maelezo waliyonipa yanakubaliana na DK. Kitine, ni nchi zenye utajiri wa maliasili na kama soko la bidhaa za vyakula huko ni mahali pake. Tatizo ni kuwa zote mbili hazikuwa kuiomba Tanzania kuunda umoja wa aina fulani na hivyo hivyo Watanzania tuliolala hatukuona utajiri wa wenzetu.

Majasusi wa shughuli za biashara na uchumi wanaliona hili ni halali kabisa kwani hata Biblia imeagiza hivyo pale Canaan alipokwenda kutafuta nchi ya asali na maziwa, Ipo mifano mingi lakini kwa uchache nitachukua kwa nchi za Marekani na Ufaransa ambapo Mwandishi wa Habari za Kijasusi na Ulinzi wa Gazeti la Daily Telegraph, nchini Uingereza Michael Smith katika kitabu chake The Spying Game, the secret history of British Espionage, anabainisha kuwa mnamo mwaka 1971 Ufaransa kwa kutumia taasisi yake ya kijasusi SDECE (Service de Documentation Exeterieure et de Contre-Espionage) aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Alexandre de Marenches aliongoza shughuli za kijasusi na kufanikiwa kuujua mapema mpango wa Marekani wa kushusha thamani ya sarafu yake ya dola na kwa kufanya hivyo Wizara ya fedha ya Ufaransa ilitengeneza faidi kubwa katika soko lake la fedha.

Utafutaji wa Habari za siri kuhusu masuala ya kifedha, kiuchumi, maendeleo ya Viwanda na Sayansi na teknolojia katika Ulinzi na usalama yaliendelea kwa Ufaransa dhidi ya Marekani hata pale mwaka 1981 SDECE ilipobadili jina na kuitwa DGSE (DirectionGenerale de la Securite Exterieure) ambapo Mkurugenzi wake Mkuu wakati huo Pierre Marion alifanikiwa kupata taarifa za ushindani wa kibiashara katika mauzo ya ndege kwa India na kuipiku Marekani na Urusi wakati ambapo zote zilikuwa zikiwania biashara hiyo na baadaye kwa maneno yake mwenyewe akasema “Siyo jambo la kawaida kuwa tunafanya shughuli za kijasusi dhidi ya nchi hizi kwani kisiasa na kijeshi ni marafiki lakini katika mashindano ya kiuchumi na kiteknolojia ni washindani wetu.”

Vile vile kwa Ufaransa nayo ilipata pigo pale mwaka 1994 wakati Waziri Mkuu wa wakati huo Edouard Balladur aliposafiri kwenda Jeddah, Saudi Arabia kusaini mkataba wa dola bilioni sita ambapo Ufaransa ingeiuzia Saudia meli za kivita na makombora na pia kubadilisha ndege za abiria za shirika la ndege la nchi hiyo kutoka zile zilizotengenezwa Marekani ili kuipa bishara hiyo Airbus ambayo ni kampuni ya Ulaya ambapo Ufaransa ina hisa.

Mkataba huo haukusaniwa kwani mashirika ya kijasusi ya Marekani yakiongozwa na CIA (Central Intelligence Agency) yalipata habari za kina kuhusu mpango huo na Serikali ya Marekani ikiongozwa na Bill Clinton iliitia shinikizo serikali ya Saudia na Clinton alipimpigia simu Mfalme Fahd na mabadiliko yakafanywa ili Makampuni ya Kimarekani ya Boeing na Mcdonnell Douglas yakafanikiwa kupata mkataba huo na hatimaye kuiuzia Saudia ndege za kiraia na kijeshi.

Si hivyo tu hata katika majadiliano juu ya makubaliano ya kibiashara katika shirika la maendeleo ya bishara la kimataifa la wakati huo yaani GATT Marekani na Ufaransa kila moja ilikuwa ikitafuta siri za mwenzake ili kujua msimamo wa mwenziwe kabla ya kuhudhuria vikao vya Shirika hilo. DGSE iliwahi kuitisha mkutano wa wandishi wa habari na kuwafahamisha kuwa ilikuwa imemkamata jasusi moja kutoka CIA ambaye alikuwa akitoa hongo ya fedha kwa ofisa moja wa Ufaransa aliyekuwa akijua siri na msimamo wa nchi hiyo kuhusu mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea wakati huo.

Kwa wale wanaofuatilia habari za mataifa mbalimbali watakuwa wanajua kuwa Japan ina taasisi yake ya ujasusi wa kiuchumi na kibiashara(JETRO) toka mwaka 1958 ambayo iko chini ya Wizara ya Viwanda na Bishara ni kwa kupitia taasisi hii Japan imefanikiwa sana kuhodhi masoko ya vifaa vya electoniki na magari hadi katika masoko yenye masharti magumu na vikwazo ya Ulaya na Marekani.

Hivyo basi hata Tanzania kwa kuangalia mifano hiyo ni dhahiri kuwa ujumbe wa Tanzania uliokuwa umeongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Shamsa Mwangunga na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dr. Ladislaus Komba, ulitakiwa kujua mapema ni nchi ngapi na zipi zilikuwa na msimamo tofauti na Tanzania na ingetumia mikakati gani kuzima misimamo kinzani wakati wa mkutano wenyewe kwa kuendesha kampeni ya nchi kwa nchi ili kuhakikisha kuwa inasonga mbele.

Waliporejea nchini wote wawili waliitisha mkutano na waandishi wa habari, kuelezea kile kilichowasibu na wakaahidi kuwa wataendelea na mapambano ya kuhakikisha kuwa wanauza shehena hiyo ya meno ya tembo, lakini kama hawatakuwa na mkakati mbadala ya ule walioutumia itakuwa ni vigumu sana kushinda vita hiyo. Bila kufanya hivyo itakuwa mchezo wa kuvaa suti na kusafiri Business Class katika ndege kwa gharama za watanzania bila kuleta tija.


Wapiganaji husema: “Huwezi kwenda kupigana na adui usiyemjua uwezo wake.” Ni kwa kutumia watu ambao wako tayari kulinda maslahi yetu ndipo tutakuwa taifa lenye heshima mbele ya wengine. Watu hawa watakuwa watoa habari tu na watawapa wale wanaohusika katika majjadiliano ili kusoma alama za nyakati kwa upande mwingine.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingene inapasa kutambua kuwa siyo kila utuchekeaye ana mapenzi na sisi kwani upo msemo wa kiswahili usemao hapendwi mtu ni pochi tu na pochi letu sisi ni raslimali zetu ambazo kwa wingi wake yapo mataifa mengi yanatolea macho. Watu wetu wengekaa katika ofisi za ubalozi hadi kwenye migodi ya dhahabu, almasi, tanzanite, rubi na kote kule ambako kizazi hiki na kijacho kinategemea kuvuna maliasili hizo. Kuwa na Economic Intelligence siyo kwa majirani tu hata katika mataifa yaliyoendelea ambapo watakuwepo wachambuzi wa mambo kujua nia ya dola fulani kwetu ni ipi?

Niandikie kilindi80@yahoo.co.uk 

ASANTE SANA MDAU IDD KWA DARASA HILI MARIDHAWA.WADAU WENGINE WENYE MADA KAMA HII AU NYINGINEZO MNAKARIBISHWA KWA MIKONO MIWILI

Mafanikio ya JK: Maisha Bora kwa Wastaafu wa Afrika Mashariki Yamewezekana (PICHA)

Wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa wamejilaza tayari 'kusulubiwa na gari la upupu' la FFU.Kosa lao ni kufuatilia haki na stahili zao.

Wazee wetu wakipiga swala.Hivi Kikwete angewakalia kooni mafisadi wa Kagoda na wana-EPA wengine kisingepatikana japo kiasi cha mboga kuwatuliza wazee wetu hawa?

Katika moja ya hotuba zake Bungeni,Kikwete alikumbushia umuhimu wa haki za kinadamu za mafisadi.Vipi kuhusu haki za msingi za wazee hawa wasio na hatia?

Picha ya juu na chini: Wazee wetu wakijipoza kwa mlo baada ya awamu nyingine ya danadana za kupata haki zao.Natumaini wazee hawa wanafahamu nani ni kikwazo cha ufumbuzi wa tatizo lao.Haya ndio Maisha Bora aliyowaahidi Kikwete mwaka 2005.Na hiyo ndio Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya ya kutatua kero zenu.Bado mnatafuta sababu za ziada za kumnyima kura?

Picha kwa Hisani ya MICHUZI JUNIOR (Jiachie).Maelezo ya picha ni yangu binafsi.

Tumwenzi Baba wa Taifa Kwa Kutimua Mafisadi Oktoba 31


Siku kama leo,mwaka 1999 Tanzania ilimpoteza muasisi wa taifa,Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.Kilichowaliza Watanzania wengi ni hofu na mashaka kuhusu hatma ya taifa lao.Pamoja na mapungufu yake ya kibinadamu,Mwalimu alijitahidi kadri awezavyo "kuita koleo ni koleo na sio kijiko kikubwa".Ni katika ujasiri huo wa Mwalimu ndipo alisimama kidete mwaka 1995 kukataa jitihada za Jakaya Kikwete na Edward Lowassa kuingia Ikulu.Miaka 10 baadaye,huku Mwalimu akiwa kaburini,Jakaya Kikwete na swahiba wake Lowassa walifanikiwa kuukwaa uongozi wa Taifa letu.

Bahati nzuri,Mungu hamfichi mnafiki.Japo leo hii Mwalimu ni marehemu na hana namna ya kuwalaumu Watanzania kwa kupuuza ushauri wake kuhusu Kikwete na Lowassa,uamuzi wa wanasiasa hao wawili kupuuza ushauri wa Mwalimu na hatimaye kuwania na kushinda uongozi wa juu wa taifa letu umetusaidia kufahamu kwanini Nyerere aliwapinga in the first place.Bahati nzuri zaidi,Lowassa alikuwa majeruhi wa papara zake,na akalazimika kujiuzulu baada ya kuliingiza taifa kwenye mkenge wa kusaini mkataba na kampuni ya briefcase ya Richmond.Bahati mbaya,na kutokana na Katiba yetu kumlinda rais kupita kiasi,Kikwete alisalimika japo haihitaji utafiti wa kichakachuaji wa Redet au Synovate kutambua kuwa Richmond na mrithi wake Kagoda,kama ilivyo kwa skandali za EPA,Meremeta,Tangold,nk ni ishu zilizokuwa na baraka za mkuu wa nchi,yaani Jakaya Mrisho Kikwete.

Miaka mitano ya utawala wa Kikwete inapaswa kuwafumbua macho kwanini Nyerere hakutaka Kikwete awe rais.Na kama tuna imani na Nyerere hadi leo,basi tutazidi kuonekana watu wa ajabu iwapo tutatoa nafasi nyingine kwa Jakaya kulikongoroa taifa letu.Wasiwasi wa Nyerere kwa Kikwete ulielemea zaidi kwenye aina ya watu waliomzunguka mwanasiasa huyu.Kwa bahati mbaya,Nyerere hakuwa hai mwaka 2005 kushuhudia namna Kikwete alivyotumia kila aina ya hila na hujuma kukwaa urais akisaidia na kila aina ya binadamu huku wengi wao wakiwa ni watu hatari kabisa kwa ustawi wa taifa letu.Watu hao ambao hawana tofauti na kundi hatari la Mafia bado wapo na ndio wanaohangaika huku na kule kuhakikisha 'mlinzi' wao-Kikwete-anarejea tena madarakani kwa vile wanafahamu laiti mzalendo kama Dokta Wilbroad Slaa akiingia Ikulu basi makazi ya mafisadi hao yatakuwa Keko kama sio Segerea...

Tuweke kando siasa za haiba.Tuweke kando tabasamu mwanana la Jakaya Kikwete-tabasamu linalowanufaisha zaidi mafisadi kuliko walalahoi.Tuweke kando hayo maji ya bendera ya CCM waliyokunywa wakereketwa.Tuangalie mwelekeo wa taifa letu.Tujiulize hatma ya taifa hili huku tukitambua kuwa hatuna pa kukimbilia pindi Kikwete na watu wake wakituingiza matatizoni zaidi ya ilivyo sasa.

Kampeni zinazoendelea zimeshashuhudia kila aina ya ufisadi unaofanywa na wafuasi wa Kikwete.Wengi wao hawafanyi uhuni huo kwa vile wanampenda Kikwete bali wanalinda nafasi zao na maslahi yao.Hawako tayari kuona Dokta Slaa anaingia Ikulu kwa vile wanafahamu bayana kuwa "watanyang'anywa mapande makubwa ya keki ya taifa" wanayoyafakamia kwa ulafi mkubwa.

Njia bora ya kumwenzi Baba wa Taifa ni kusema HAPANA kwa ufisadi na mafisadi.Na njia ya kufanya hivyo ni kupiga KURA NYINGI ZA HAPANA KWA KIKWETE na CCM yake.Watanzania wasitegemee miujiza kutoka kwa mtu huyu aliyetuthibitishia bayana kuwa hajui chanzo cha umasikini wa nchi yetu,asiyehitaji kura za Wafanyakazi,anayedhani mimba za wanafunzi wa kike ni kimbelembele chao tu,anayeamini kuwa waathirika wa ukimwi wameukwaa ugonjwa huo kwa kimbelembele chao,na asiyetaka kuomba msamaha kwa wimbo la ufisadi lililoshamiri katika miaka yake mitano ya utawala.

Naamini Baba wa Taifa angekuwa hai leo,angesimama hadharani na kumkataa Kikwete kwa vile sababu zilizopelekea amkatae 1995 sio tu bado zipo bali zimethibitika kwa vitendo kati ya 2005-2010.Uhuru uliopiganiwa na Nyerere na wenzake haukumaanisha uhuru wa mafisadi kama mmiliki wa KAGODA ambaye hadi leo anahifadhiwa na Kikwete na wasaidizi wake.

Ewe Mtanzania,unataka Kikwete na CCM wafanye nini zaidi hadi ufikie hatua ya kusema SASA YATOSHA (Enough is enough)?Kama kosa lilishafanywa 2005 kwa kumpa nafasi ya majaribio na amefeli,hakuna haja ya kumpa fursa ya kurejea tena.Na bahati nzuri safari hii tuna Mtanzania mzalendo (Dokta Slaa) ambaye ujasiri wake kama mbunge umefunika utendaji wa Kikwete,Lowassa,Chenge,Rostam Aziz,Karamagi,Kingunge,Msabaha,Marehemu Ballali,Idris Rashid,Basil Mramba,Yona na wababaishaji wengineo.Katika uchaguzi huu hatuna sababu ya kutojikwamua na makucha ya ufisadi kwa vile tuna alternative iliyo bora ambayo ni Dokta Slaa.

NJIA PEKEE YA KUMWENZI MWALIMU NI KUENZI BUSARA ZAKE ZA KUMKATAA KIKWETE MWAKA 1995.TULIPUUZA BUSARA HIZO MWAKA 2005,PENGINE KWA VILE NYERERE HAKUWEPO KUTUONYA.LAKINI MUNGU AMETUSAIDIA KUTONYESHA BAYANA KWANINI NYERERE ALIMKATAA KIKWETE.KWAHIYO,NJIA MWAFAKA YA KUMWENZI BABA WA TAIFA (NA KUMWOMBA MSAMAHA KWA KUPUUZA USHAURI WAKE WA 1995) NI KUMWONDOA KIKWETE MADARAKANI KWA NJIA YA KURA HAPO OKTOBA 31.KUMWONDOA KIKWETE NDIO NJIA MWAFAKA YA KUONDOKANA NA UFISADI.YEYE NDIO SHINA NA HAO WAPAMBE NI MATAWI TU.TUKIONG'OA SHINA LA UFISADI BASI MMEA MZIMA WA UFISADI UTAKUWA HISTORIA.

INAWEZEKANA.TIMIZA WAJIBU WAKO

Tuesday, October 12, 2010

Mashushushu Wanajiandaa Kuchakachua Matokeo ya Uchaguzi?


Nimekumbana na post ifuatayo hapo Jamii Forums.Naiwasilisha kama ilivyo kisha tujiulize kwa pamoja (kama tuhuma hizo ni za kweli) wanafanya hivyo kwa faida ya nani?

Taarifa ya Siri - Mikakati ya Kuiba Kura Inavyoendelea USALAMA WA TAIFA
Napenda kuwajulisha mikakati michafu ya kupora na kuzuia maamuzi ya umma yanayofanywa na ccm kwa uratibu wa usalama wa taifa. Baada ya kubaini dalili za kuanguka vibaya katika uchaguzi wa mwaka huu idara ya usalama wa taifa imeandaa mikakati ya kuiba kura ili kuzuia chadema msiingie ikulu. Mikakati hii inaeleweka vizuri kwa tume ya taifa ya uchaguzi ambayo inashirikiana bega kwa bega na idara ya usalama wa taifa kumtengenezea jk ushindi bandia wa 80%. Wana hakika watanzania watagundua wizi huo na watakataa matokeo ndiyo maana kwanza waliwatumia viongozi wa dini waliotembelea makao makuu ya chadema wawasihi chadema wakubali matokeo yatakapotangazwa na juzi wamelitumia jeshi kutisha wananchi watakaoamua kupinga matokeo ya kupikwa yanayoandaliwa na nec/usalama wa taifa. Majid Kikula ambaye ni government security officer ndiye mratibu wa zoezi la kuiba kura, ni mtaalamu aliyebobea katika kazi za aina hii aliratibu vizuri zoezi kama hilo mwaka 2005. Pia mwaka 2007 alitumwa kenya kwenda kumsaidia kibaki kupora ushindi wa odinga.
Kikula anatumia muda wake mwingi hivi sasa ofisi za tume ya uchaguzi kwa ajili ya uratibu wa uvurugaji daftari la kudumu la wapiga kura akiifanya kazi hiyo kwa karibu na baadhi ya watendaji wa nec na maafisa kadhaa wa usalama wa taifa kutoka kurugenzi ya IT ya idara ya usalama (DITA) ambao wako ndani ya nec kwa zaidi ya miezi sita sasa, nitawapatia majina yao. Pia kuna vijana wataalamu wa IT waliochukuliwa kutoka maeneo mbalimbali wamepewa nyumba upanga mtaa wa undali shughuli kubwa wanayofanya ni kuandaa utaratibu wa ku-access remotely daftari la kudumu la wapiga kura. Hawa wanafanya kazi chini ya Salva Rweyemamu na Mindi Kasiga kutoka kurugenzi ya mawasiliano ikulu. Wapo vijana kadhaa leo nawapa majina ya wawili; Maharage Chande na Edgar Masatu wanafanya kazi kwa karibu na Nzowa wa idara ya usalama ambaye ndiye aliyeratibu shambulio la kumwagiwa tindikali Kubenea. Pia kuna kundi linalojumuisha wataalamu wa printing wa kiwanda cha uchapaji cha usalama wa taifa kilichopo MALINDI ambao hivi karibuni walikuwa mjini tanga kwa semina fupi ya jinsi ya kughushi kura kupitia fake ballot paper, timu hii inaongozwa na ndg SINYAU.
Kwa hiyo utaona kwamba imeandaliwa mikakati mingi kuufanikisha uovu huo ili mmoja ukikwama basi mwingine utatumika ila wameamua ni lazima jk ashinde kwa 80%. Ndani ya idara ya usalama wa taifa maafisa wengi wamechoshwa na uongozi mbovu wa ccm hivyo wanataka mabadiliko ya uongozi idara imechukua hatua kadhaa kuhakikisha maafisa wote wa idara wanampigia kura jk, wote wameagizwa kuwasilisha vitambulisho vyao vya kupigia kura ili vinakiliwe namba ili atakayepigia upinzani afukuzwe kazi baada ya uchaguzi. Fuatilieni kwa karibu haya niliyowaeleza nimeyapata kwa nafasi yangu ndani ya tiss. Huyu KIKULA mfuatilieni kwa  karibu ni hatari. HAKIKISHENI DUNIA NA WATANZANIA WOTE WANAJUA MAPEMA HILA HIZI. Jambo la kujiuliza maafisa usalama wa taifa wanafanya nini ndani ya tume ya uchaguzi wakati huu.


Sunday, October 10, 2010

Siku Maalum Kabisa: Tarehe 10 Mwezi wa 10 Mwaka Elfu Mbili na 10 (10.10.10 au10/10/10 au 10-10-10)



Muda maalum kabisa utakuwa hapo saa 4 na dakika kumi na sekunde kumi,ambapo saa na tarehe itakuwa 10.10.10 10.10.10.Tukio hili ni la nadra kupita kiasi na litajiri tena baada ya miaka 100,yaani karne nzima kutoka sasa

Saturday, October 09, 2010

Wapiga Kura Wanapaswa Kuwaumbua Wachakachuaji wa REDET


Majuzi tumemsikia Mwenyekiti Mwenza wa REDET,Dokta Benson Bana akilipuka tena na utafiti wao wa kuchakachua kuhusu mwenendo wa uchaguzi,ambapo kwa mujibu wao wanadai mgombea wa CCM,Jakaya Kikwete anaongoza kwenye kura za maoni.

Huko nyuma nilishawahi kuandika post moja kuhusu Dokta Bana,na tabia yake ya ulipukaji.Katika post hiyo nilikuwa nazungumzia kauli ya Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba tuhuma zilizokithiri dhidi ya ufisadi zinaweza kusababisha taifa kukosa viongozi wazuri.Yani mhadhiri mzima alikosa busara ya kufahamu kuwa kukalia kimya ufisadi hakuwezi kusababisha taifa kupata viongozi wazuri.

Bana na Redet yake wanadhani Watanzania ni wajinga ndio maana wakakurupuka na uchakachuaji huo wakiamini wanaisaidia CCM na Kikwete.Sio ubishi wala kulazimisha matokeo tunayotaka sie bali hali halisi ya mwenendo wa kampeni inaonyesha dhahiri kuwa CCM na Kikwete wamekaliwa kooni na Dokta Wilbroad Slaa na Chadema,huku uthibitisho mkubwa ukiwa kwenye vioja kama kauli ya vitisho ya Mnadhamu Mkuu wa JWTZ Brigedia Jenerali Shimbo.

Hivi huyo Kikwete angekuwa 'anapendwa' na zaidi ya asilimia 70 ya wapiga kura watarajiwa (potential voters) angekuwa anahangaika huku na kule ku-recycle lundo la ahadi zake za mwaka 2005?

Lakini tungetarajia nini kutoka kwa Dokta Bana na REDET yake?Waseme umaarufu wa Kikwete umeshuka?Waseme Dokta Slaa anaongoza kura za maoni?Hayo hayawezekani katika utawala huu wa kifisadi unaotaka kusikia habari njema tu hata kama hazina ukweli.Tunafahamu kuwa Synovate walishindwa kutueleza nani anaongoza kura za maoni kwa vile CCM ilihofia matokeo ya ripoti hiyo yangewaadhiri.Sasa kwa vile REDET 'wameshafungulia mbwa' sintoshangaa Synovate nao wakikurupuka na ripoti yao iliyochakachuliwa itakayoonyesha Kikwete na CCM wanaongoza.

Haina haja ya kuwashutumu wachakachuaji hawa.Dawa yao iko kwa wapiga kura waliochoshwa kuona nchi yao ikigeuzwa maabara ya uchakachuaji kwenye kila eneo.Hebu pata picha iwapo kila Mtanzania aliyechoshwa na ufisadi akipiga kura ya kuwaadhibu mafisadi na hatimaye Kikwete akan'goka madarakani,Dkt Bana na REDET yake watakuwa katika hali gani!

Hilo linawezekana.Wapiga kura wasianze kukata tamaa kuwa CCM wataiba kura.Of course wataiba lakini ili 'kura zitoshe' watalazimika kufanya wizi wa 'mchana mweupe' (day light robbery) jambo ambalo sio rahisi sana,japo linawezekana.Wanaweza tu kuchakachua matokeo kama,kwa mfano Dokta Slaa akipata asilimia 51 na Kikwete asilimia 49.Hapo watarejea uchakachuaji kama ule wa Zanzibar.Lakini kama ni tofauti ya double digits,wanaweza kupatwa na kigugumizi katika kufanikisha ujambazi huo.

Ni muhimu kutovunjwa moyo na hujuma hizi.Yatupasa kufahamu kuwa Kikwete na CCM yake ni kama mgonjwa mahututi ambaye yuko tayari hata kuning'inia kwenye uzi ili asalimike.Tutashuhudia vituko zaidi ya huo uchakachuaji wa REDET au vitisho vya akina Brigedia Shimbo.Cha muhimu ni kusimamia dhamira yetu.

Inawezekana.Timiza wajibu wako

Friday, October 08, 2010

Urban Pulse na ASET Wanawaletea Ziara ya Msanii Diamond Hapo Novemba

Image and video hosting by TinyPic


Urban Pulse Creative ikishirikiana na Aset Inapenda kuwataarifu wadau wote wa Music wa bongo Flava na Hip Hop kuwa imeandaa tamasha maalum linaloitwa URBAN TOUR ambapo msanii Diamond kutoka bongo anayetamba na kibao chake cha Mbagala atakuwepo hapa ukerewere kuanzia mwezi wa November mwaka huu. Wasanii wengine ni Pamoja na First lady wa Urban Pulse Mish Ze Fyah Sis UK Artist anayetamba na single yake Freedom na I don't give a damn.



Tamasha Hili ni kwa ajili ya kuchangia Vita Dhidi ya Malaria Afrika. Diamond ni ambassador wa Malaria Tanzania na ndiye atakekuwa akiwakilisha.
Shows Hivi zitafanyika tarehe 6th Nov Milton keynes, 12th Nov London and 27th Nov Birmingham.
Stay tune kwa habari zaidi.

Asanteni,

Urban pulse Creative.

Makala Yangu Katika Jarida la RAIA MWEMA

Katika toleo la wiki hii la jarida la Raia Mwema nazungumzia kuhusu tuzo ya milenia,msaada tuliopewa na Waingereza baada ya kuridhishwa kwao na "nidhamu na matumizi yetu" na sifa alizomwaga Obama kuhusu "utawala bora".Cheki makala hiyo hapa bila kusahau makala na habari nyingine motomoto ndani ya jarida hilo maridhawa.

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India