Featured Posts

Wednesday, June 27, 2007

REST IN PEACE,AMINA.

MUNGU AILAZE MAHALI PEMA PEPONI ROHO YA MAREHEMU AMINA CHIFUPA

Ni vigumu kuamini lakini ndio imetokea.
Bwana ametoa Bwana ametwaa
Kila mmoja atamkumbuka Amina
Hasa katika vita yake dhidi ya wauza unga
Rest in peace,Amina

Yatasemwa mengi
Yakiwamo na ya uzushi
Hiyo haitusaidii
Sana itazidisha hudhuni
Tumwombee apumzike kwa amani

Zitasomwa rambirambi
Za wabunge na mawaziri
Lakini ili zisiwe za kinafiki
Aloanzisha AMINA muyaenzi
Kwa maslahi ya wananchi

REST IN PEACE,AMINA

Wednesday, June 20, 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-68

Asalam aleykum,

Kwanza napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wote wanaotembelea blogu yangu.Nina furaha kusema kuwa wakati naandaa makala hii blogu hiyo ilikuwa imeshatembelewa na watu 1015 kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni.Inanipa moyo sana kupata idadi hiyo ya wageni na napenda kuwakaribisha wale wote ambao hawajawahi kuitembelea blogu hiyo.Pamoja na hayo,nakaribisha maoni,mijadala na hata kunikosoa pale ambapo msomaji anadhani haafikiani nami.Pamoja na kupata nafasi ya kusoma makala mpya na za nyuma,blogu hiyo ina viunganishi (links) kadhaa vya tovuti mbalimbali za Kitanzania kuhusu habari na burudani.Karibuni sana.

Hivi karibuni serikali ya Uingereza imetangaza nia yake ya kuwaadhibu ipasavyo wale wote wanaopatikana na hatia ya kuwadhalilisha watoto kijinsia (paedophiles).Ni kwamba mtu atakaekutwa na hatia hiyo atadungwa kemikali flani ambayo itampunguzia tamaa ya kuwamendea watoto wadogo.Kwa “kizungu” wanaita “castration” ila tafsiri ya Kiswahili nayoifahamu sio mwafaka kuiandika hapa,ila nachoweza kusema ni kuwa kemikali hiyo inatarajiwa kuwafanya wahalifu hao kuwa kama wanaume wasio na uwezo wa kufanya tendo la ndoa.Nadhani msomaji wangu mpendwa unajua msamiati gani ni mwafaka hapo.Habari hii imenikumbusha mchapo mmoja niliopewa miaka kadhaa iliyopita kwamba katika maeneo flani ya mwambao wajuzi wa “teknolojia asili” (ndumba) wana mbinu ya kuhakikisha kuwa “vyao haviguswi na atakayethubutu kuvigusa atalijua jiji.”Ni kwamba katika kuhakikisha kuwa “mali zake” haziibiwi,mume “anamfunga” mkewe,yaani anamfanyia utaalam flani wa asili ambapo pindi mtu akitembea na mwanamke huyo anaathirika kwa namna flani (kwa mfano,sehemu zake za siri “zinaingia mitini” au mwizi huyo na mwanamke husika wanagandana kama gundi hadi wanafumaniwa).Hadi naondoka sehemu hiyo sikuweza kuthibitisha ukweli wa habari hiyo ila nachokiri ni kwamba utaalamu wa asili upo sana ila tu mara nyingi unatumika ndivyo sivyo.Pengine wakati nasi huko nyumbani tunasubiri teknolojia ya kemikali mamlaka zinazohusika na kuhakikisha kuwa watoto hawaangukii mikononi mwa “paedophiles” zinaweza kuomba msaada wa wataalamu hao wa asili ili kuwalinda watoto wetu.Hiyo ni nyepesi nyepesi,usidhani nimeishiwa na hoja za msingi.

Katika kupitapita kwenye magazeti ya hapa nilikutana na habari moja iliyonifanya niwashangae wanaopanga baadhi ya sera za nje za Marekani.Hivi msomaji mpenzi unafahamu kuwa mtu anayemnyima usingizi Joji Bushi na serikali yake,gaidi nambari wani Osama bin Laden,“alitengenezwa” na Wamarekani haohao?Ni stori ndefu ila kwa kifupi ni kwamba wakati wa “Vita Baridi” kati ya Marekani (na washirika wake) dhidhi ya wafuasi wa Ukomunisti wakiongozwa na Urusi (enzi hizo USSR),Marekani ilikuwa ikitoa sapoti kwa watu na vikundi kadhaa kwa lengo la kuzuia Ukomunisti usienee zaidi.Miongoni mwa watu hao ni Osama bin Laden ambaye pamoja na kundi la Taliban walipewa misaada ya hali na mali na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa ajili ya kufanikisha ushindi kwenye vita kati ya mujahidina wa Afghanistan na Urusi.Katika kuidhibiti Urusi,washirika wake na Ukomunisti kwa ujumla,CIA ilikuwa tayari kufanya lolote lile wakati mwingine pasipo kutafakari nini kitatokea iwapo matokeo yatakuwa tofauti na matarajio ya plani zao.Na ndivyo ilivyokuwa huko Afganistan.Baada ya majeshi ya Urusi kushindwa vita hiyo na baada ya “Vita Baridi” kumalizika,Marekani haikuwahitaji tena Osama,Taliban na vikundi vingine vya mujahidina,na kwa upande mwingine Osama na washirika wake nao walisharidhika na ushindi wao dhidi ya Urusi na walishakuwa na nyenzo za kutosha kuanzisha ngwe nyingine ya mapambano dhidi ya “wafadhili” wao Marekani na wale wote waliowaona kuwa ni maadui wa Uislam.

Ungedhani kuwa Marekani ingejifunza kutokana na maamuzi yake ya “kuangalia leo pasipo kufikiria kesho itakuwaje”.Majuzi nimesoma gazeti la Guardian la hapa Uingereza na kukuta taarifa kuwa Marekani imeandaa mpango wa kuvisaidia vikundi vya madhehebu ya Sunni nchini Iraki ili vipambane na wapiganaji wa Al-Qaeda waliojazana nchini humo.Matarajio ni kwamba vikundi hivyo vya Wa-Sunni vitaweka mbele maslahi ya taifa lao la Iraki dhidi ya wapiganaji wa Al-Qaeda ambao wengi wao wametoka nje ya nchi hiyo kuja kupambana na Wamerekani.Wasiwasi wa baadhi ya wachambuzi wa mambo ya usalama ni kwamba hata kama mpango huo utafanikiwa,hali itakuwaje iwapo misaada ya kifedha na silaha kwa vikundi hivyo itavipa jeuri vikundi hivyo kuanzisha “mtanange” mwingine dhidi ya Wa-Shia au Wa-Kurd iwapo Al-Qaeda wataondoka Iraki?Na kuna uhakika gani kuwa baada ya kupata misaada ya kutosha vikundi hivyo vya Wa-Sunni havitawageuka wafadhili wao na kuungana na makundi mengine kupambana na Wamarekani?

Kana kwamba hiyo hazitoshi,kuna taarifa kwamba CIA imekuwa inaendesha mkakati wa siri kuwarubuni baadhi ya Wasudan kuingia kwenye mpango ambao watapatiwa mafunzo ili baadaye wapenyezwe kwenye vikundi vya Kiisalam vyenye jitihada kali hususan Al-Qaeda.Dada mmoja anayefanya utafiti kuhusu hali ilivyo huko Darfur anadai kuwa Marekani inahusika kwa namna moja au nyingine katika machafuko yanayoendelea huko ambapo kwa mujibu wa utafiti wake,licha ya Marekani kuwa na uwezo wa kusaidia kudhibiti vikundi vinavyoendesha unyama katika eneo hilo imeamua kutofanya lolote kwa inavihitaji vikundi hivyo kuisaidia Marekani kudhibiti tishio la ugaidi kutoka vikundi visivyodhibitiwa katika nchi ya jirani ya Somalia.Nchi hiyo ambayo kwa miaka nenda rudi imekuwa ikiendeshwa kiholela na vikundi vya “mabwana vita” (warlords) inahesabiwa na Marekani kuwa ni tishio kubwa kwa vile ni rahisi kwa Al-Qaeda na wafuasi wake kupata hifadhi pasipo bughudha yoyote ile.

Kuhusu huko nyumbani,nimeshtushwa na mpango uliotangazwa na Waziri wa Fedha,Zakia Meghji,ambapo katika utekelezaji wake,baadhi ya waagizaji bidhaa kutoka nje wataweza kuingiza mizigo yao nchini pasipo mizigo hiyo kufanyiwa ukaguzi.Mpango huo unaweza kusababisha balaa kubwa kwa sababu zilizo wazi kabisa.Sote tunafahamu kuwa pamoja na sheria zilizopo bado kuna watumishi wasio waadilifu ambao kwa kuthamini matumbo yao wamekuwa wakizembea kukagua bidhaa zinazoingia nchini na hivyo kufanya nchi yetu kujaa bidhaa kadhaa kutoka nje ambazo hazina ubora unaostahili.Sasa kwa mpango huu wa Meghji kuna hatari kubwa zaidi ya hofu ya bidhaa zisizostahili kwani upo uwezekano wa wajanja flani kuingiza unga (sio wa ugali bali madawa ya kulevya) na hata silaha kwa kutumia mwanya huo wa kutokaguliwa bidhaa zinazoingizwa nchini.Hivi kuna uhakika gani kuwa utaratibu huo utawahusu wanaodaiwa kuwa na rekodi nzuri ya kulipa kodi au wawekezaji wa dhati?Tunafahamu kuwa baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakichuma chapchap wakitumia msamaha wa kodi (tax holiday) halafu wanaingia mitini.Sasa wawekezaji wa namna hiyo wakipewa fursa nyingine ya kuingiza bidhaa pasipo ukaguzi hawawezi kutumia fursa hiyo kuingiza visivyofaa kuingizwa nchini?Kwa uchungu gani hasa walio nao kwa nchi yetu?Maana kama wangekuwa na uchungu basi wasingekimbia nchini au kubadili majina ya biashara zao baada ya kumalizika kwa “tax holidays” wanazopewa kwa nia nzuri tu ya kuwatengenezea mazingira mazuri ya uwekezaji.Hivi kweli kuna mfumo thabiti (fool proof) wa kuhakikisha kuwa watu wenye nia mbaya na nchi yetu hawatawatumia wafanyabishara wanaodaiwa kuwa na rekodi nzuri ya kulipa kodi kuingiza mizigo hatari kwa mfano silaha?

Mwisho,wakati naungana na Watanzania wenzangu kuipongeza Taifa Stars kwa mafanikio yake,napenda kumpongeza Mheshimiwa Anne Kilango kwa kilio chake ambacho naamini ni cha kila Mtanzania mwenye mapenzi na nchi yetu kuhusu hao wanaofanya maamuzi ambayo matokeo yake yanaiathiri nchi yetu.Maamuzi hayo ambayo unaweza kabisa kudhani kuwa yamefanyikia baa huku mtu akiwa “matingas” ni pamoja na kuingia mikataba ya ajabu kuliko ile aliyofanya Karl Marx na machifu wetu ambao hawakuwa na ujuzi wowote kuhusu suala la mikataba.Mama Kilango anawaomba viongozi wa namna hiyo wamuogope Mungu na kuionea huruma nchi yetu,mie nakwenda mbali zaidi ya hapo kwa kuwaombea mabaya wale wote ambao wanathamini sana matumbo yao na nyumba ndogo zao kuliko maisha ya Watanzania wenzao.Mungu awalaani na ikiwezekana wapate adhabu yao hapahapa duniani ili iwe funzo kwa wengine.

Alamsiki

Friday, June 15, 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-67

Asalam aleykum,

Enzi za Ujamaa na Kujitegemea tulikuwa tukiambiwa kuwa ubepari ni unyama.Bado naamini kuwa kauli hiyo ni sahihi hadi kesho.Nimeikumbuka kauli hiyo baada ya kuona kipindi cha “Witness” kwenye kituo cha runinga cha Aljazeera English ambapo mada ilikuwa maendeleo ya sekta binafsi ya afya nchini India.Nchi hiyo inasifika hivi sasa kwa kutoa huduma bora za afya hasa kwa wageni ambao wanakimbia gharama za afya kwenye nchi zao ili kupata unafuu huko India.Lakini wakati “watalii” hao wa afya wananufaika na unafuu huo,maelfu kwa maelfu ya Wahindi wasio na uwezo wanaishia kukodolea tu majengo ya hospitali hizo kwa vile hawana uwezo wa kumudu gharama za tiba.Kibaya zaidi,jitihada za hospitali hizo za kisasa kutoa “msaada wa kibinadamu” kwa wagonjwa wasio na uwezo wa kumudu gharama zinaishia mikononi mwa wajanja wachache ambao badala ya msaada huo kuwafikia walengwa,wengi wa wanaonufaika ni wale wenye mahusiano na watawala ambao ndio wanaopendekeza nani apatiwe msaada wa tiba ya bure.Wamiliki wa hospitali hizo wanatetea uamuzi wao wa kutoza gharama za juu kwenye tiba wanazotoa kwa kigezo kwamba gharama za uendeshaji ni za juu sana na wanategemea zaidi teknolojia kutoka nje ya nchi hiyo ambayo pia ni ghali.

Niliona taarifa nyingine Skynews kuhusu kushamiri kwa biashara ya mafigo ya binadamu huko Pakistani. “Watalii” wa afya (watu wanaosafiri kutoka nchi moja kwenda nyingine kutafuta huduma nafuu za afya) wamekuwa wakimiminika katika hopsitali moja nchi humo kwenda kununua mafigo ya bei rahisi.Gharama ya matibabu ni pauni za Kiingereza 3,500 lakini wanaouza mafigo hayo huambulia pauni 800 tu.Hicho ni kiwango kikubwa sana kwa watu hao kwani inakadiriwa kuwa kwa baadhi yao itawachukua zaidi ya miaka kumi kufikisha kiwango hicho cha fedha iwapo watategemea vipato vyao kiduchu katika kazi zao za kila siku,nyingi zao zikiwa ni mithili ya utumwa.Lakini fedha hizo wanazolipwa ambazo kwa wengi ni kama kushinda bingo flani huishia kwenye matibabu zaidi kwani sote tunafahamu kuwa mwili ni kama gari,ukishakongoroa kifaa kimoja basi unakuwa ushaharibu “balansi” ya mwili mzima.Matokeo yake ni mzunguko usioisha.Baba anauza mafigo yake,anapata fedha ambazo mwanzoni zinaonekana kama ukombozi kwa familia,lakini muda si mrefu afya inaanza kudhoofika,fedha iliyopatikana kwenye kuuza mafigo inaanza kurejea hospitali alikouza mafigo,hatimaye inalazimu mama au mtoto naye auze mafigo ili kumuda gharama za matibabu ya baba,na hadithi hiyo inaendelea mithili ya Isidingo (hivi imeshafikia mwisho?).Mmiliki wa hospitali hiyo ya kipekee nchini Pakistan anatetea uamuzi wake wa kununua mafigo akidai kuwa anatoa huduma kwa jamii mara mbili:kuokoa maisha ya watalii wa afya ambao wanahitaji mafigo kwa udi na uvumba,na kuwakwamua watu walio hohehahe ambao mtaji wao ni mafigo yao.Alipoulizwa kuwa anachofanya sio sawa na “kumwibia Pita ili kumlipa Paulo” mmiliki huyo alidai kuwa yeye anajiona ni mkombozi kwa makundi yote mawili:wanaohitaji mafigo na wanaohitaji hela.

Napopata mapumziko baada ya “kubukua” kwa nguvu huwa napendelea kuiangalia dunia kupitia macho ya runinga.Na “hobi” yangu hiyo inanikutanisha na habari za aina mbalimbali,za kuchekesha na za kuhudhunisha,za kufundisha na za kutia ghadhabu.Iliyonipa ghadhabu hivi karibuni ni taarifa ya kiuchunguzi ya BBC kuhusu makampuni yajulikanayo kama “vulture fund companies” (makampuni yanayozengea mizoga).Haya ni makampuni yaliyoshamiri sana kwenye nchi za magaharibi na walengwa wake wakuu ni nchi masikini za dunia ya tatu.Makampuni haya yanaishi kwa kununua madeni ya nchi masikini kwa bei nafuu halafu katika yanaishia kutengeneza mamilioni ya dola.Yule “mtu mfupi” wa Zambia,Frederick Chiluba, ambaye tulikuwa tukiambiwa kuwa ni mlokole, amejikuta akiumbuka baada ya kubainika kuwa alikula dili na “vulture fund company” flani ya Marekani ambapo kampuni hiyo ilinunua madeni ya nchi hiyo na kisha kutoa teni pasenti ya nguvu kwa Chiluba.Yaani wanachofanya wenye kampuni hizo ni hivi:wewe una deni la shilingi laki moja lakini huna uwezo wa kulilipa au unasuasua kulilipa.Mie nalinunua deni hilo kwa anayekudai,bei ya kulinunua deni hilo ikiwa ni poa.Kwa hiyo mie nageuka kuwa ndie naekudai.Hadi hapo hakuna tatizo,lakini ujanja uko kwenye ukweli kwamba mengi ya makampuni hayo yanafanya biashara zake kwa siri na shughuli zake haziko wazi sana kisheria.Na hapo ndipo “dili za kuuza nchi” zinapojitokeza.Unajua kuna tofauti kati ya kudaiwa na taasisi “ya kueleweka” kama benki na kudaiwa na “mjanja” flani wa mtaani.Kibaya zaidi ni kwamba hao wadaiwa hawatoi fedha zao mfukoni,bali ni fedha za walipa kodi (wananchi).Kwahiyo,kwa upande mmoja kuna kampuni ya kiujanjaujanja ambayo haijali taratibu za kisheria za madeni na ulipwaji wake na kwa upande mwingine ni mdaiwa ambaye anatumia nafasi kudili na “mdai poa” kujitengenezea fedha kadhaa,ambapo mwisho wa dili pande zote mbili zinanufaika,huku walipa kodi wakizidi kuumia.

Unaweza kujiuliza kwanini makampuni haya hayadhibitiwi ilhali yanaendesha shughuli zao katika nchi tunazoamini kuwa zinafuata utawala wa sheria.Jibu ni jepesi:sheria za kuyabana makampuni hayo ziko “luzi” sana kiasi kwamba ni sawa na hakuna sheria kabisa.Pia kuwepo kwa makampuni hayo kunayanufaisha sana mashirika ya kimataifa katika kupata fedha zao walizokopesha kwa nchi masikini.Kadhalika,mengi ya makampuni hayo yana mahusiano ya karibu na mashirika ya kimataifa yanayotoa mikopo kwa nchi masikini.Kadhalika,baadhi ya viongozi wa nchi masikini wamekuwa wakihusishwa na umiliki wa makampuni haya.Hiyo ndio dunia tunayoishi ambayo mwenye nacho anataka zaidi ya alichonacho na asiyenacho ananyang’anywa hata kile kidogo kabisa alichonacho.

Huko nyumbani nako kuna mambo.Nilisoma sehemu flani kwamba Wizara ya Miundombinu inaanda utaratibu wa kuwa na teknolojia ya kufuatilia matumizi ya magari ya serikali.Wazo zuri kama lingekuwa halihusishi fedha,tena mamilioni ya fedha.Hivi jamani namna bora ya kufuatilia matumizi ya mali yako si kuhakikisha sheria zilizopo zinafuatwa?Unadhani kuna dereva ambaye akielezwa bayana kwamba atatimuliwa kazi pindi gari la umma analoendesha likionekana mtaani saa 2 usiku atathubutu kukiuka amri hiyo?Unadhani jeuri ya madereva hao inatoka wapi?Mjuzi mmoja wa udereva wa magari ya umma aliwahi kuninong’oneza kuwa madereva na masekretari ni “wasiri” muhimu sana kwa mabosi.Hao ndio wanaojua nyumba ndogo za mabosi wao,ndio wanapokea meseji na kupeleka mizigo na hata kwenye madili ya mabosi wao huwa wanahusika kwa namna moja au nyingine.Leo utabuniwa mradi wa kudhibiti magari ya umma kesho utabuniwa mradi wa kuhakikisha wafanyakazi wanaripoti ofisini muda stahili.Yote ni mawazo mazuri kama malengo ni kuongeza tija na sio kuongeza matumizi yasiyo ya lazima.Jamani,tuionee huruma nchi yetu!

Mwisho,ni bajeti ya mwaka ujao wa fedha.Kwa kuongeza kodi kwenye mafuta inamaanisha kuwa bei za bidhaa na huduma kadhaa zitapanda,kuanzia nyanya magengeni hadi usafiri wa daladala na mikoani.Mikakati ya kupambana na umasikini inaweza kuwa na wakati mgumu kufanikiwa pale gharama za maisha zinazidi kupaa.Cha muhimu hapa sio kulaumiana bali kuangalia nini cha kufanya.Bajeti imeshasomwa na matokeo yake yanafahamika (mfano,uwezekano wa kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma).Cha kufanya ni kuhakikisha kuwa walafi wa faida hawatumii mwanya huo kuwaminya walalahoi.Wananchi wataumia vya kutosha tukiwaachia wafanyabiashara wajipangie bei za bidhaa na huduma au tukitegemea nguvu ya soko katika kudhibiti bei. “To hell with” (ifie mbali) hekaya za soko huria.Iwe hivi,mamlaka husika zitamke bayana kuwa bei ya kitu flani isidhidi kiasi flani,kama hutaki tunafunga biashara yako.Sema huo ni udikteta,lakini kuna dhambi gani ya kuwa dikteta kwa maslahi ya wengi wasiojiweza?Udikteta usiokubalika ni ule wa dhidi ya watu wengi na sio huo naoshauri ambao ni kwa manufaa ya watu wengi.

Alamsiki

Sunday, June 10, 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-66

Asalam aleykum,

Pengine hii ni tetesi ambayo ungependa kuisikia.Kuna habari kwamba Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair ambaye anastaafu rasmi mwezi huu ana mpango wa “kubadili dhehebu.”Blair ni muumini wa Kanisa la England (Church of England) wakati mkewe,Cherie,ni Mkatoliki.Inasemekana kuwa miongoni mwa ziara za mwisho za Blair akiwa Waziri Mkuu ni kwenda Vatican kukutana na Papa Benedikti,na “wambea” wanadai katika ziara hiyo Blair atajiunga rasmi na Kanisa Katoliki.Taarifa zaidi zinadai kuwa licha ya kujiunga na Kanisa hilo,Blair pia anataka kuwa deacon (kwa mujibu wa tafsiri kwenye kamusi ya English-Swahili neno hilo linamaanisha shemasi,japo upeo wangu mdogo wa Ukatoliki unaniambia kuwa ushemasi ni hatua moja kabla ya upadre).Enewei,ni vizuri kwa Blair kumrejea Bwana kwa namna yoyote ile inayofaa hasa baada ya kuboronga kwenye sera yake ya Iraki ambapo wengi wetu tunafahamu matokeo yake.

Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu mchakato wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya “chama dume” CCM.Watu wanapigana vikumbo kuhakikisha wanaibuka videdea kwenye kinyang’anyiro hicho.Na wale wanaojua kutumia midomo yao kutengeneza fedha,basi huu ni wakati wa kuchuma hasa.Nadhani wapo wanaoombea kuwa tuwe na chaguzi kubwa kila wiki maana sio siri kwamba chaguzi zinawanufaisha wengi.Ita rushwa,takrima au ukarimu lakini hilo sio nalotaka kulizungumzia kwani linahitaji makala nzima.Unajua wakati mwingine ni vigumu sana kutofautisha rushwa na ukarimu.Hivi kijana anapotoa ofa za chipsi kuku na bia kwa mrembo anayemtamani anakuwa anatoa rushwa akubaliwe kimapenzi au anafanya ukarimu ili “somo lieleweke”?Na mgombea anapotumia “ukarimu wa kisiasa” kuwakamatisha mafedha wapiga kura wake ili apate uongozi anakuwa anatoa rushwa au anakuwa mkarimu kwa wapiga kura hao?Tutalijadili hilo siku zijazo kwani kama nilivyosema awali mjadala huo unahitaji muda na nafasi ya kutosha.

Kumekuwa na maneno ya chinichini na ya waziwazi kuhusu hofu ya “watoto wa vigogo” kuiteka CCM hasa baada ya baadhi ya watoto wa wanasiasa wetu kuchukua fomu za kugombea uongozi kwenye nafasi mbalimbali za chama hicho tawala.Mmoja ambaye nadhani ametajwa sana ni Ridhiwani Kikwete.Kwa wafuatiliaji wa makala zangu watakumbuka kuwa nilishawahi kuelezea huko nyuma “mkutano” wangu na kijana huyo kwenye hafla moja ya Watanzania mjini Manchester,hapa Uingereza.Katika makala hiyo nilielezea namna nilivyovutiwa na namna Ridhiwani alivyo,yaani kama si kufanana na baba yake,JK,isingekuwa rahisi kuhisi kuwa kijana huyo ni mtoto wa Rais.Yaani tofauti na mazowea yetu ambapo tumezowea kuona watoto wa vigogo wakijifanya tofauti na sie tunaotoka familia za kawaida,mtoto huyo wa JK alionekana kuwa “down-to-earth” kweli kweli.Tulipokutana nilimfahamisha kuwa kwa hakika anatoa picha nzuri sana sio kwa familia yake tu bali pia hata kwa familia za viongozi wengine.Nakumbuka alinieleza kwamba tangu utotoni amekuwa akiamini kwenye jitihada zake binafsi na wala sio nafasi ya mzazi au familia yake.

Sasa wapo waungwana ambao wanadhani kuwa kijana huyo anaweza kutumia jina la baba yake ili kukwaa madaraka.Kwanza binafsi sioni kosa kwa mtoto wa kiongozi kugombea uongozi wa aina yoyote ile kwani hiyo ni haki yake ya kidemokrasia na kikatiba.Iwapo wapiga kura watashawishika kumpa kura kwa vile ni mtoto wa Rais,haitakuwa kosa kwani naamini kuwa kwenye kampeni zake ananadi sera zake na wala sio mahusiano yake na JK.Joji Bush,rais wa sasa wa Marekani ni mtoto wa rais aliyepita wa nchi hiyo,na hakuna anayelalamika kwani Bush mtoto aliingia madarakani kwa jitihada zake binafsi ikiwa ni pamoja na kuuza sera zake vizuri dhidi ya wagombea wengine.Nadhani hofu kwamba madaraka yanazunguka miongoni mwa familia flani haina uzito sana kwani la muhimu kwa kiongozi sio familia anayotaka bali uwajibikaji wake.Naomba nisisitize kuwa simpigii debe Ridhiwani au mtoto yoyote yule wa kigogo kwani hata kama ningetaka kufanya hivyo mie sio mpiga kura kwenye mikutano ya chaguzi za CCM.

Nilipokuwa Mlimani (UDSM) mwalimu wangu wa Sosholojia Padre John Sivalon aliwahi kutueleza darasani kwamba suala la watu wa familia au ukoo mmoja kushika au kupeana madaraka ni kitu cha kawaida huko Marekani,alimradi hakuna sheria iliyokiukwa.Alisema labda tofauti kati ya huko Marekani na Afrika ni ukweli kwamba kwa wenzetu huko mtu anapopata nafasi kwa vile ni ndugu ya mtu flani basi anajitahidi kuhakikisha hamuangushi huyo nduguye.Unajua kwa wenzetu sifa ya familia au ukoo ni jambo muhimu sana.Sasa kama mtoto wa kiongozi atapata nafasi kwa vile baba yake ni flani,anahakikisha kuwa anawajibika kwa nguvu ili kulinda heshima ya baba yake huyo pamoja na familia na ukoo kwa ujumla.Na kikubwa wanachoangalia wenzetu ni uwezo wa mtu na wala sio familia au ukoo anaotoka.Pia ikumbukwe kuwa kwa mgombea kuwa mtoto wa kiongozi haimaanishi kuwa atajipigia kura mwenyewe bali hilo ni jukumu la wapiga kura ambao ili wamchague ni lazima waridhishwe na uwezo wa mgombea huyo

Pia yatupasa tukumbuke kuwa kuna familia au koo ambazo siasa iko damuni.Na ipi ni njia bora ya kuendeleza utamaduni wa familia au ukoo kama sio kushiriki kwenye mazoezi halali ya kidemokrasia kama chaguzi?Inawezekana ukoo wa akina Kikwete una damu ya siasa,na kama msemo wa Kiswahili usemavyo kuwa maji hufuata mkondo,naamini kuwa mtoto wa JK kufuata hatua ya baba yake kwenye fani ya uongozi wa kisiasa ni jambo zuri.Wenzetu huku Ughaibuni wanapenda kuangalia vipaji vya watoto wao na mchango wa vipaji hivyo katika familia au ukoo,na hatimaye kuviendeleza vipaji hivyo

Jingine ambalo naamini litanifanya nitofautiane na wenzangu wengi ni kuhusu marupurupu ya wabunge ambayo imefahamika kuwa yataongezeka katika mwaka ujao wa fedha.Awali mie nilikuwa miongoni mwa wale wanaoamini kuwa wabunge wanalipwa fedha nyingi zaidi ya wanazostahili.Mawazo hayo yalibadilika baada ya kuongea na Mheshimiwa flani mmoja ambaye alifanikiwa kuingia bungeni mwaka jana kwa tiketi ya CCM (naomba nisimtaje jina).Mheshimiwa huyo ambaye ni rafiki yangu wa karibu alinieleza mambo ambayo niliyashuhidia kwa macho yangu binafsi.Alinimabia kuwa ubunge ni jukumu linalohitaji moyo hasa kwa wale ambao majimbo yao yanakabiliwa na matatizo mbalimbali.Nilishuhudia kwa macho yangu namna wapiga kura walivyokuwa wakimiminika nyumbani kwa Mheshimiwa huyo kuomba misaada mbalimbali hususan ya kifedha.Aliniambia,(na mwenyewe nilishuhudia) Chahali watu wanalalamika wanaposikia sie wabunge tunaomba tuboreshewe maslahi yetu lakini hawajui namna gani “familia zetu zinavyotanuka” baada ya kupata ubunge.Wapiga kura wanakuwa sehemu ya familia kwani inamwia vigumu mbunge kuwatelekeza watu wanaodamka asubuhi kuja nyumbani au ofisini kwa mbunge huyo wakiomba msaada mmoja au mwingine.Akiwatosa atakuwa anajichimbia kaburi la kisiasa katika uchaguzi ujao lakini licha ya hilo,kwa mila na desturi zetu za Kitanzania inafahamika kuwa tunawajibika kuwasaidia wale wasiojiweza hata kama kwa kufanya hivyo tutakuwa tunajiathiri sie wenyewe.Nafahamu kuwa wapo wabunge ambao inawezekana hawatoi misaada kwa wapiga kura wao lakini hapa nazungumzia kila nilichokiona kwa macho yangu mwenyewe.Na kwa vile ubunge sio kazi ya kuhubiri injili ambayo mshahara wake ni peponi bali ni jukumu ambalo kwa mwajibikaji halisi linamaanisha “kuufutua” ukoo (kuongezeka idadi ya wanaokutegemea) basi nadhani uamuzi wa serikali kuboresha maslahi ya waheshimiwa wabunge ni sahihi.

Mwisho,nadhani uamuzi wa Katibu wa Bunge kuwapiga stop wanahabari kuhudhuria vikao vya kamati za bunge sio wa busara.Hao ni wawakilishi wetu,na tunapaswa kujua namna wanavyojadili masuala mbalimbali yanayotuhusu.Kwani kuna siri gani ambazo zinaathiriwa na kuwepo kwa waandishi wa habari wakati wa vikao vya kamati za bunge?Natumaini kuwa hatua hiyo itakuwa ya muda tu,na pia nataraji wabunge wetu wataikemea kwani nao wanavihitaji sana vyombo vya habari katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alamsiki

Monday, June 04, 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-65

Asalam aleykum,

Miongoni mwa mambo niliyozungumzia katika makala iliyopita ni namna “ugonjwa” wa “reality television” ulivyoenea huku ughaibuni.Kwa waliosahau, “reality tv” ni vipindi kwenye televisheni ambavyo hujaribu kuonyesha maisha ya mshiriki/washiriki kwenye kipindi hicho katika hali halisi.Hivi ni vipindi ambavyo kwa mfano hufuatilia maisha ya mwanamke mjamzito kwa miezi kadhaa hadi pale anapojifungua.Au wakati mwingine huonyesha maisha ya kundi flani likiwa limefungiwa sehemu flani huku kamera zikifatilia masaa 24 (mfano vipindi vya Big Brother).Nilieleza pia kuhusu mpango wa kampuni ya Endemol ya Uholanzi (ambayo hutengeneza vipindi vya runinga) kuandaa kipindi cha “Big Donor” ambapo washiriki wangeshindana kupata figo la mwanamama mmoja anayesubiri kufa kwa kansa.Endemol sasa wameibuka na kudai kuwa mpango wa kuwa kipindi hicho ulikuwa “hewa” (feki).Wanadai kuwa nia ya kuitangaza plani hiyo ilikuwa kutoa changamoto kwa wananchi kuhusu kuchangia viungo kwa wale wenye kuvihitaji.Wanajua wao kama hiyo ni kweli au porojo tu.

Pamoja na ukweli kwamba baadhi ya watu wanaviona vipindi vya “reality” kama vyenye nia ya kuwatumia washiriki wa vipindi hivyo kwa manufaa ya waaandaaji,vipo vipindi kadhaa vya “reality” ambavyo vinatoa mafundisho kwa jamii.Hapa ntazungumzia vipindi vitatu vyenye mantiki inayofanana.Kuna wakati flani,Michael Portillo,mmoja wa wanasiasa maarufu hapa UK aliamua kushiriki kwenye kipindi ambacho mama mwenye nyumba alimwachia mwanasiasa huyo jukumu la kutunza watoto kwa siku kadhaa.Ulikuwa ni mtihani kweli kwa Portilo ambaye pia ni mbunge katika chama cha kihafidhina cha Conservatives.Kuna wakati mtazamaji angejikuta anamwonea huruma mbunge huyo jinsi alivyokuwa “akipelekeshwa” katika jukumu la kutunza watoto hao.Lakini kipindi hicho kilipoisha,Portillo alieleza kuwa amejifunza mambo mengi sana katika muda aliokaa na watoto hao ikiwa ni pamoja na kutambua kuwa kwa mama siku moja ya ulezi wa watoto ni zaidi ya majukumu ya ofisini.

Pia kuna kipindi kingine kinaitwa “wife swap.”Kipindi hicho huonyesha familia mbili zikibadilishana wake (mamsapu) na waume,ambapo mara nyingi familia hizo huwa zinatoka katika “backgrounds” tofauti kabisa (kwa mfano,familia inayoamini katika kuishi “fast life”-kinywaji,sigareti,muziki mkubwa,nk-na familia ya kilokole,au kwa mfano wa huko nyumbani,familia kutoka “ushuani” Oysterbay na nyingine kutoka Kimbiji).Katika kipindi hicho mke kutoka familia “iliyozowea raha” au inayoishi kwa kufuata “sheria kali” anaonjeshwa joto ya jiwe kwenye upande mwingine wa maisha,huku mume nae akienda kuonja ladha ya maisha ambayo ni tofauti kabisa na yale aliyozowea.Hebu fikiri mume aliyezowea kushinda baa akila kinywaji na kuvuta sigara moja baada ya nyingine anakwenda kuishi kwenye familia ya kilokole ambayo pombe na sigara ni dhambi kubwa pengine zaidi ya kuua.Au pale mke aliyezowea kufanyiwa kila kitu na hauzigeli anajikuta anawajibika kupika chakula,kulaza watoto na kufanya majukumu mengine ya ndani ambayo kwake ni sawa na ndoto ya mchana.Japo kuna wakati “swap” (mbadilishano) huo hupelekea kuleta songombingo za hali ya juu,mwishoni washiriki hukiri kuwa wamejifunza vitu vingi kwa kuishi maisha ambayo wamekuwa wakiyasikia au kuyaona kwenye runinga tu.
Kipindi cha tatu ambacho kilinivutia sana ni kile cha “Young Black Farmers” kilichoshirikisha kundi la vijana weusi “watukuku” tisa kutoka South London (hilo ni eneo la jiji hilo ambalo ni lazima uwe “ngangari” ili umudu maisha).Vijana hao ambao miongoni mwao kulikuwa na wauza unga, “mateja” (wabwia unga),makahaba,vibaka na matapeli,walipelekwa kwenda kuishi kwenye ranchi ya Wilfred Emmanuel-Jones,Mwingereza Mweusi ambaye alikuwa anaendesha shughuli za kilimo na ufugaji wa kibiashara kwenye eneo lililojaa watu weupe la Devon.South London imejaa watu weusi,na kwa vijana wengi wa maeneo hayo wazo la “kujichanganya” na watu weupe ni la mbali sana labda iwe kwenye usafiri,shuleni au ofisini.Sasa wazo la kuishi Devon ambako wengi wa wakazi wake hawajawahi kuwa na rafiki Mweusi,lilikuwa ni kama ndoto isiyoweza kuwa kweli.Vijana hao walitakiwa kutekeleza majukumu kadhaa hapo Devon na mshindi angeibuka na skolashipu ya kujifunza mambo ya kilimo na ufugaji hapo kwenye ranchi.Kwa lugha nyingine,ushindi katika zoezi hilo ulimaanisha kuepuka maisha waliyozowea vijana hao huko South London ya kukimbizana na polisi,kukwepa vita vya magenge na adha nyingine za maisha ya “kigetogeto.”Wapo walioachia ngazi siku za mwanzo tu,lakini wengine waliamua kupambana na ugumu wa kumkubalisha mtu mweupe aamini kuwa hata kijana Mweusi anayeamka kwa brekifasti ya “kokeni” anaweza kuwa mtu bora mwenye kujua majukumu yake katika jamii.Mwishoni mwa kipindi alipatikana mshindi mmoja ambaye nadhani alikuwa kibaka kabla ya kwenda hapo kwenye ranchi.Kwa wengine,licha ya kushindwa wote walikubali kuwa maisha ya kijijini hapo yamewapa fundisho kubwa sana maishani mwao.Na japo takriban wote walionyesha kukata tamaa siku walipowasili kijijini hapo kwa mara ya kwanza,siku ya kuondoka ilikuwa ni majonzi makubwa kwao kwani ilikuwa ni kama wameonjeshwa pepo na sasa wanarudi tena ahera.

Ningekuwa na uwezo ningeandaa kipindi kama hicho huko nyumbani.Ningemchomoa kigogo mmoja kutoka kwenye shangingi lake lenye kiyoyozi masaa 24 halafu ningempeleka Manzese Kwa Mfuga Mbwa akaone shida ya maji huko,asome kwa koroboi kwa vile kama ilivyo sehemu nyingi za uswahilini Tanesko huwa wanajiamulia tu kukata umeme bila taarifa,na asubuhi ashuhudie namna gani ilivyo vigumu kubanana kwenye daladala (kama atafanikiwa kupanda,na iwapo kitambi chake kitastahimili m-banano huo),halafu nimtembeze kwenye mitaa aone namna watu wanavyopigwa “roba za mbao” kirahisi,ningempitisha Uwanja wa Fisi aone vibinti vidogo kabisa vinavyotumikishwa kama makahaba.Na pengine ningemchomoa bimkubwa mmoja kutoka ushuani Masaki halafu nimpeleke Sofi Majiji (tafuta kwenye ramani ya nchi yetu ufahamu nazungumzia sehemu gani).Ningemtaka aende na watoto wake kisha watoto hao wa “kishua” waende ziara ya angalau wiki moja kwenye “shule halisi za msingi vijijini”,wamsikilize mwalimu wakiwa wamekalia matofali huku mama yao akiwa ameenda porini kutafuta kuni na akirudi aende kisimani kuchota maji.Ningetaka mama na watoto hao waonje ladha ya namna ya kubalansi maisha kwa shilingi mia tano kwa siku na kula ugali na matembele yasiyo na chumvi wala hayajaungwa kwa vile shilingi alfu haitoshi.Halafu wakishaumwa na mbu waende zahanati ya kijiji,wapange foleni masaa kadhaa kisha “watolewe upepo” kupimwa maleria,halafu waandikiwe dawa ambazo hazipo hapo kwenye zahanati.Pia ningemkurupusha kigogo mmoja wa NGO ya UKIMWI nimpeleke akaishi na waathirika “halisi” wa ugonjwa huo (na sio wale “walengwa” kwenye ripoti za mwaka),akaone maana halisi ya unyanyapaa,aone namna gani madawa ya kuongeza maisha (ARVs) yalivyo adimu,na pengine aangalie kama kweli akirejea ofisini NGO yake iendelee kudai kuwa ipo kwa ajili ya kuhudumia waathirika wa UKIMWI au ipo kwa ajili ya kuhudumia “kifriji” chake na nyumba ndogo yake.Nadhani vipindi hivyo vingetoa fundisho kubwa sana.

Mwisho,nimechekeshwa na habari moja kwamba wana-CCM huko Ulanga na Kilombero wanataka kuwashtaki wabunge wao eti kwa vile wameshindwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho.Nimecheka kwa vile wanaolalamika ndio haohao waliowapa ubunge walalamikiwa.Hivi wanaolalamika walijiuliza vya kutosha kabla ya kupiga kura kuwa wanayoahidiwa na walalamikiwa yatatekelezwa au yanatekelezeka?Hivi waliusikia vizuri ule wimbo wa “ndio mzee” wa Joseph Haule (Profesa Jay wa Mitulinga) ambapo mgombea ubunge anaahidi kutatua matatizo ya usafiri kwa kuleta helikopta?Nadhani wapiga kura wana tatizo la kuamini neno “NITAFANYA…” badala ya “NILIFANYA…”Yaani kigezo cha kumchagua mtu kisiwe atafanya nini bali ameshafanya nini.Mmoja wa walalamikiwa hao amenukuliwa akisema kuwa kazi ya kuleta maendeleo si ya mbunge pekee.Angalau ameongea kistaarabu kuliko Mheshimiwa mmoja (mbunge wa zamani jimbo moja la Dar) ambaye aliposikia wapiga kura wanamlalamikia aliwapa kitu “laivu” kwamba walimchagua kwa hela zake alizowapa wakati wa kampeni,sasa wanapolalamika wakati wameshakula hela hizo wanamtaka yeye afanye nini!

Alamsiki

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India