Featured Posts

Showing posts with label Regia Mtema. Show all posts
Showing posts with label Regia Mtema. Show all posts

Wednesday, January 25, 2012

Makala Yangu Katika Toleo la Wiki Hii la Gazeti la Raia Mwema: "Rais Kikwete amefungua milango"


Rais Kikwete amefungua milango

Rais Kikwete msibani kwa Marehemu Mbunge Regia
Rais Kikwete msibani kwa Marehemu Mbunge Regia
KWA mara ya pili ndani ya takriban kipindi cha wiki moja, Tanzania imepoteza wabunge wawili. Kabla majonzi hayajatuisha kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia CHADEMA, Regia Mtema, taifa likapatwa na msiba mwingine wa Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CCM, Jeremiah Sumari.
Kila kifo kinaacha pengo lakini kifo cha kiongozi (awe wa familia kama mzazi au wa jamii) kinaacha pengo linalowagusa na kuwaathiri wengi. Japokuwa yayumkinika kuhisi kuwa katika zama hizi za siasa za kuendekeza maslahi kuna wanaofurahi vifo vya viongozi kwa vile vitatoa nafasi ya wao kugombea, ukweli unabaki kuwa ni vigumu kupata mrithi atakayelingana kwa kila kitu na marehemu (hasa katika utekelezaji wa majukumu).
Kama nilivyoandika katika makala ya wiki iliyopita kuhusu kifo cha Regia, njia bora ya kumuenzi marehemu Sumari ni kudumisha mema yote aliyofanya wakati wa uhai wake. Kwa wanaofikiria kumrithi nafasi yake (na kwa atakayeteuliwa kumrithi nafasi ya Marehemu Regia) changamoto kubwa itakuwa kwenye kuwaenzi viongozi hao kwa kuwajibika ipasavyo. Japo utendaji kazi bora wa kiongozi anayerithi madaraka kutoka kwa kiongozi marehemu hauwezi kurejesha uhai, kwa kiasi fulani unasaidia kupunguza machungu ya wananchi walioathiriwa na pengo lililotokana na kifo husika.
Katika mila na desturi za kiafrika, shughuli ya msiba inatawaliwa na majonzi na kwa kiasi kikubwa ni kumbukumbu kwa kila aliyehai kuwa sote “tulitoka kwenye udongo na tutarejea kwenye udongo.” Misiba inapaswa kutukumbusha kuwa sote ni wasafiri na kila nafsi ya mmoja wetu itaonja mauti.
Moja ya matukio yaliyotawala msiba wa Regia ni habari kwamba Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbroad Slaa, alikwepa kusalimiana na Rais Jakaya Kikwete. Habari hiyo ilichukua uzito mkubwa kiasi cha kukaribia kufunika tukio la huzuni lililowakutanisha viongozi hao huko Ifakara.
Kwa sababu anazozijua mwenyewe, jamaa mmoja aliamua kusambaza waraka katika blogu kadhaa ndani na nje ya nchi kukemea kitendo hicho cha Dk.  Slaa. Mtu huyo ambaye hakufanya jitihada za kuficha itikadi yake ya siasa, akaenda mbali zaidi na kudai kuwa kilichosababisha Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA kutosalimiana na Rais ni amri iliyotolewa na mwenza wa Dk. Slaa (Josephine).
Pengine kwa kuelewa kuwa kukalia kimya jambo hilo kungeibua maneno zaidi, hatimaye Dk. Slaa alieleza kilichomfanya ashindwe kusalimiana na Rais Kikwete. Kwa wanaojua protokali, mtu hakurupuki tu na kwenda kusalimiana na kiongozi mkuu wa nchi hasa ikizingatiwa kuwa kumkaribia kiongozi huyo (hata kama ni kwa nia nzuri) kunawafanya walinzi wake watafsiri kama tishio la usalama kwake.
Kadhalika, Dk. Slaa alieleza bayana kuwa kilichompeleka Ifakara ni kumzika Regia na si vinginevyo. Kwa lugha nyingine, alimaanisha kuwa isingehitaji kutokea kifo cha mbunge au kiongozi wa chama ndipo “mahasimu wawili” (kama ‘wazushi’ wa habari hiyo walivyojaribu kutuaminisha) wakutane na kupeana mikono.
Lakini kama kuwasuta wanaokuza matukio madogo, siku chache baadaye vyombo vya habari vilitawaliwa na picha inayomwonyesha Rais Kikwete na Dk. Slaa wakipeana mikono baada ya mazungumzo kati ya Rais na viongozi wa CHADEMA yaliyofanyika Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam.
Sijui waliozusha kuwa Josephine alimkataza Dk. Slaa wanasemaje kuhusu hilo. Labda watazusha kuwa alimtoroka mwenza wake kama sio kuzusha kuwa kiongozi huyo wa CHADEMA aliamua kuambatana na viongozi wenzie Ikulu ili kujisafisha kutokana na tukio la Ifakara.
Inasikitisha kuona mambo ya msingi yakigubikwa na porojo zisizo na mashiko. Binafsi, moja ya mambo ya msingi yaliyonigusa na kunipa matumaini mapya ni jinsi Rais Kikwete na takriban uongozi wake mzima (serikalini na huko CCM) walivyoweza kuweka kando tofauti za kiitikadi na kumzika Regia kama kiongozi wa Watanzania na si mbunge wa CHADEMA pekee.
Mara kadhaa nimekuwa nikishutumiwa kwa kumkosoa au kumlaumu Rais Kikwete. Lakini siku zote nimejitahidi kusisitiza kuwa lawama hizo na kukosoa hakumaanishi chuki au husuda bali ni kwa minajili ya ustawi wa taifa letu.
Natambua kuna uwezekano wa baadhi ya wasomaji kuhisi nimefikia hatua ya kumpongeza Rais Kikwete kwa vile tukio husika linaihusu CHADEMA (ambayo nimekuwa nikituhumiwa kuipendelea na baadhi ya watu, huku wengine wakidai mimi ni mwanachama wa chama hicho.)
Yeyote aliyesoma salamu za rambirambi zilizotolewa na Rais Kikwete kwenda kwa familia ya marehemu Regia na CHADEMA hatoshindwa kubaini kuwa zilikuwa zimetoka moyoni kwa dhati. Hakukuwa na hata chembe ya tofauti za kiitikadi bali hisia za kibinadamu pindi zinapopatikana habari za kifo.
Naomba nisisitize kuwa tukio hilo sio pekee au la kwanza kwa Rais Kikwete kuonyesha kile wanachokiita Waingereza ‘human side’ (ubinadamu wake, kwa tafsiri isiyo rasmi). Mara nyingi mkuu huyo wa nchi ameonyesha kuguswa kwa dhati kila anapokuwa kwenye matukio ya huzuni.
Japo wakati mwingine huishia kulaumiwa kuwa ‘haisaidii kuonyesha uchungu ilhali janga husika lingeweza kuzuilika’ (kwa mfano kwenye matukio ya milipuko ya mabomu huko Mbagala na Gongo la Mboto), hiyo haindoi ukweli kuwa ameguswa na matukio hayo.
Lakini pamoja na pongezi hizi kwa Kikwete na CCM kwa ujumla pengine ni muhimu kukumbushana kuwa kama tunaweza kushikamana wakati wa misiba kwa nini basi iwe vigumu kufanya hivyo nyakati nyingine?
Kwa lugha nyingine, kwa nini tusubiri hadi kiongozi wa chama cha upinzani afariki ndipo tuonyeshe kuwa tofauti za kiitikadi haziondoi ukweli kuwa sote ni Watanzania tunaoweza kutofautiana kimtizamo au kiitikadi pasipo umuhimu wa ‘kuong’oana’ macho.
Japo Kikwete si mahiri katika kuendekeza siasa za uhasama (aidha kwa vile si muumini wa dhana hiyo au anatumia wasaidizi wake kukwepa lawama zinazoweza kuelekezwa kwake), kiujumla chama anachoongoza, yaani CCM, kimekuwa kikifanya jitihada kubwa kuuaminisha umma kuwa vyama vya upinzani ni mithili ya mikusanyiko ya maharamia wasioitakia mema nchi yetu.
Ukisikiliza hotuba za baadhi ya viongozi wa CCM wanapovizungumzia vyama vya upinzani unaweza kabisa kutamani kwenda Idara ya Uhamiaji kuhoji iwapo viongozi hao wa upinzani ni raia halisi wa nchi hii. Hivi haiwezekani kukosoana pasipo kupandikiza chuki ya uadui miongoni mwetu?
Katika tafiti za kitaaluma, kuna hatua ambapo mtafiti huwezi kubashiri matokeo ya utafiti husika kwa kuzingatia dhana alizotengeneza (hypothesis). Japo makala hii si sehemu ya utafiti lakini ningependa kutengeneza dhana kuu mbili zinazoweza kubashiri matokeo fulani.
Ya kwanza, kwa vile Rais Kikwete na CCM wameweza kututhibitishia kuwa tofauti zao za kiitikadi na CHADEMA si za kiadui, na ndio maana wameshiriki kikamilifu katika msiba wa marehemu Regia, Tanzania inaingia kwenye zama mpya za siasa za upendo na kukosoana kistaarabu.
Ya pili, kwa vile siku chache baada ya msiba wa mbunge wa CHADEMA, Rais Kikwete aliwaalika viongozi wa CHADEMA kufanya majadiliano nao, tunaanza kushuhudia ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Rais (na pengine CCM kwa ujumla) katika uongozi wa nchi.
Matokeo yanayotarajiwa ni kwamba badala ya muda mwingi wa ujenzi wa taifa letu kutumika kunyoosheana vidole, kuitana majina ya ajabu ajabu na upuuzi mwingine, sasa tunaweza kuona uongozi wa nchi ukifanya kazi bega kwa bega kwa lengo la kuikomboa Tanzania yetu kutoka katika lindi la umasikini (licha ya rasilimali lukuki tulizojaliwa) na kuunganisha nguvu kukabiliana na kundi la maharamia walioigeuza nchi yetu kuwa ‘shamba la bibi’ kwa ufisadi.
Unaweza kudhani labda aya tatu za hapo juu nimeziandika nikiwa ndotoni. La hasha. Kila nililoandika linawezekana kwani sababu (ya kushirikiana) ipo, na uwezo wa kufanya hivyo upo (kama ilivyothibitika katika tukio hilo la msiba wa marehemu Regia), ila kinachokosekana ni nia tu.
Ni matarajio ya safu hii kuwa Rais Kikwete (ambaye naamini anasoma makala hizi au anasimuliwa na wasaidizi wake) hatorudi nyuma katika kufungua sura mpya ya siasa za maelewano na ushirikiano kwa manufaa na ustawi wa Tanzania yetu. Penye nia pana njia.

Friday, January 20, 2012

Dr Slaa Afafanua Kwanini Hakuweza Kusalimiana na Kikwete Kwenye Msiba wa Regia


Dk Slaa: Kwa nini sikumsalimia JK 


Thursday, 19 January 2012 20:42
Fredy Azzah 
KATIBU Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa  amesema kuwa, hakuweza kusalimiana na Rais Jakaya Kikwete kutokana na Jiografia ya eneo la makaburini lilivyopangwa na watu wa usalama wa taifa pamoja na kamati ya mazishi kutomruhusu kufanya hivyo.

 
Hata hivyo Dk Slaa alisisitiza kuwa, kwa upande wake, kwenye msiba siyo sehemu ya kwenda kwa ajili ya kusalimiana na watu ama kurekebisha mambo yaliyoharibika bali ni sehemu ya kumwombea marehemu.

 “Siyo hulka ya Dk Slaa kutumia misiba kama sehemu ya kusalimiana, wala kutengeza mambo yaliyoharibika, mimi huwa naenda kwenye msiba kwa lengo moja tu la kumwombea marehemu, huwa simtazami hata mtu aliyekaa pembeni yangu,” alisema Dk Slaa alipozungumza kwa njia ya simu  jana.  

Alifafanua kuwa, katika eneo la makaburi kulikuwa na mabanda matano ambayo yalipangwa kwa ajili ya Askofu, Rais, Viongozi wa vyama vya siasa, mwili wa marehemu  na familia na banda jingine lilikuwa la watu wengine waliohudhuria mazishi hayo. 

“Sasa kutoka alipokuwa amekaa Rais mpaka kwenye banda nilipokuwa mimi, kulikuwa na umbali wa karibu  mita 20, sasa mlitaka nikimbie kumsalimia Rais nivunje protokali kisha nikamatwe na usalama wa taifa,” alisema Dk Slaa. Alisema alikuwa mtu wa kwanza kufika makaburini kwa lengo la kuangalia jinsi kaburi la mbunge wa chama chake lilivyochimbwa kisha akaonyeshwa sehemu ya kukaa na watu wa usalama wa taifa.

 Alisema kuwa, hata katika wakati wa kuaga mwili wa Marehemu Regia Mtema, katika ukumbi wa Karejee, kulikuwa na utaratibu kama huo ambapo ilitengwa sehemu ya kukaa Makamu wa Rais, Spika wa Bunge, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na Makamu wake na yeye Dk Slaa akawekewa sehemu yake kama Katibu wa Chama alichokuwa akikitumika marehemu.

 “Mimi sipendi kuweka siasa kwenye mambo kama ya msiba, Dk Slaa siyo kichaa siyo kichaa aanze kukimbia kumsalimia Rais. Katika sehemu kama ile Rais huwa anakuja baada ya watu wote wakiwa wameshakaa, yeye ndiye hupita na kuanza kusalimia watu na hamjaona hata sehemu moja aliponyoosha mkono kunisalimia nikamkwepa,” alisema Dk Slaa:

 “Msiba siyo mahali pa kutengeza urafiki, au kutengeza mambo yaliyo haribika, pale ni ibada tu na kumuombea marehemu siyo sehemu ya kufanya siasa” alisisitiza Dk Slaa. Jana baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa, Dk Slaa alishindwa kusalimiana na Rais Jakaya Kikwete katika mazishi ya Regia Mtema yaliyofanyika kijijini kwao Ipangalala Morogoro juzi.Regia alifariki dunia Januari 14 kwa ajali ya gari iliyotokea katika eneo la Ruvu mkoani Pwani.  


CHANZO: Mwananchi

Wednesday, January 18, 2012

Picha za Mazishi ya Marehemu REGIA MTEMA huko Ifakara













Picha zote kwa hisani ya Jamii Forums

Saturday, January 14, 2012

Taarifa Zaidi kutoka Chadema Kuhusu Msiba wa Mheshimiwa Regia Mtema



TANZIA


Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepatwa na majonzi makubwa na kinasikitika sana kwa kifo cha Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa, Mheshimiwa Regia Mtema ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira. Mheshimiwa Regia Mtema amefariki leo tarehe 14 Januari 2011 kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu darajani.
 


Katika uhai wake marehemu Regia Mtema amefanya kazi mbalimbali za kisiasa na kijamii katika taifa. Marehemu Regia Mtema amezaliwa tarehe 21 mwezi Aprili mwaka 1980 na kusoma shule za sekondari kidato cha kwanza mpaka cha sita katika shule ya sekondari ya Forodhani na Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Machame. Marehemu Regia Mtema alipata shahada yake ya kwanza (Bsc Home Economics and Human Nutrition) katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine. 



Mara baada ya kuhitimu masomo yake marehemu Regia Mtema alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na CHADEMA na kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA na baadaye kuteuliwa kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya CHADEMA nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa mbunge wa viti maalum. 



Viongozi wakuu wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Katibu Mkuu Dr. Wilbroad Slaa, wajumbe wa kamati kuu, wakurugenzi wa chama makao makuu na wabunge wamejumuika hivi sasa na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu. 



CHADEMA inatoa pole kwa familia ya marehemu Regia Mtema, wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususani wa Jimbo la Kilombero, wanachama wote wa CHADEMA, jamii ya watu wenye ulemavuTanzania na Watanzania wote kwa ujumla, kutokana na msiba huu wa ghafla katika wakati ambapo mchango wake ukihitajika kwa chama na kwa taifa. 



Taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada ya kukamilisha majadiliano baina ya familia ya marehemu, chama na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 


Mipango ya mazishi ya marehemu inapangwa nyumbani kwa Baba wa Marehemu Regia Mtema, Ndugu Estelatus Mtema, Tabata Chang'ombe. Ratiba ya maziko itatolewa baada ya kukamilika kwa taratibu zinazopangwa na familia ya marehemu, Ofisi ya Bunge na chama. 


Mungu ailaze roho ya Marehemu Regia Mtema, mahali pema peponi. Amina.



Imetolewa na: 

John Mnyika(Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi

Picha kwa Hisani ya Jamii Forums

Breaking News: Mbunge Regia Mtema afariki kwa ajali ya gari



Habari za kusikitisha zilizopatikana kwenye mtandao wa jamii wa Twitter na ukumbi wa mijadala ya mtandaoni wa Jamii Forums zinaeleza kuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chadema,Regia Mtema,amefariki kwa ajali ya gari iliyotokea daraja la mto Ruvu.

Licha ya kifo cha Regia kuwa pigo na pengo kubwa kwa Chadema pia ni msiba mkubwa kwa sie wazawa wa wilaya ya Kilombero,mahali alipozaliwa marehemu na ambapo alipatumikia kwa nguvu zake zote.

Tutawaletea taarifa zaidi kadri zinavyopatikana.

Bwana Ametoa Bwana Ametwaa,Jina lake lihimidiwe Milele.Amen.

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India