Featured Posts

Showing posts with label Mwigulu Nchemba. Show all posts
Showing posts with label Mwigulu Nchemba. Show all posts

Sunday, January 19, 2014

Baraza Jipya la Mawaziri: JK afanya utani mbaya, amteua Mwigulu Nchemba kuwa Naibu Waziri wa Fedha




UCHAMBUZI WA HARAKA:

Yaelekea matatizo ya uchumi wetu si miongoni mwa mambo yanayomnyima usingizi Rais Jakaya Kikwete, ndio maana amefanya kituko cha mwaka kumteua Mwigulu Nchemba kuwa Naibu Waziri katika Wizara hiyo nyeti. Ila mzaha huo ni wa kimkakati zaidi. CCM inahitaji fedha kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2015. Hadi hapo si tatizo, lakini tatizo lipo kwenye kupata fedha hizo kwa njia halali. Ninatafsiri uteuzi wa Mwigulu kwenda Wizara ya fedha kuwa ni sehehmu ya mkakati wa kuiwezesha CCM kupata fedha za uchaguzi mkuu ujao. Tutegemea EPA nyingine? Time will tell.

Adam Malima kupelekwa Wizara nyeti ya fedha si jambo la kushangaza, ikizingatiwa yyeye na JK wanatoka mkoa wa Pwani na ukaribu wao. Sijui nini kilichopeleka Juma Nkamia kupewa uwaziri wa Michezo, lakini majibu anayo JK mwenyewe.

BOTTOM LINE: Tatizo sio mawaziri bali Kikwete mwenyewe. Mbunge wa Ubungo aliwahi kuingia matatani alitamka bayana kuwa JK NI DHAIFU lakini ukweli unabaki kuwa ukweli, na alichosema Mnyika ndo ukweli wenyewe. Mawaziri wanaweza kubadilishwa kila wiki, lakini as long as kiongozi wao ni dhaifu, basi tuendelee kutarajia yaleyale yanayopelekea kabineti kubadilishwa mfululizo kama safari za JK nje ya nchi.

Na kwa waliodhani Pinda angeng'oka walikuwa wanaota ndoto za mchana. Pinda ni nyenzo muhimu kwa JK, ni mtu anayebeba lawama za bosi wake. Madudu yakifanywa na JK,lawama zinaelekezwa kwa Pinda.

Tuombe Mungu 2015 ifike mapema, JK amalize majaribio yake ya urais, labda nchi yetu itapata mwelekeo mpya.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

MABADILIKO HUSIKA NI HAYA HAPA CHINI

- Hakuna Mabadiliko Ofisi ya Rais

- Ofisi ya Makamu Wa Rais - Naibu Waziri Kitwanga amehamishwa na nafasi yake imejazwa na Mhe. Ali Mwalimu

- Mwigulu Nchemba amekuwa Naibu Wizara ya Fedha (Sera). Aliyekuwa nafasi hiyo sasa ni Waziri Kamili
- Uchumi na Mapato sasa anatoka Janet Mbene na inajazwa na Adam Malima

- Asharose Migiro sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria

- Ulinzi na Kujenga Taifa => Hussein Mwinyi

- Mambo ya Ndani - Mathias Chikawe

- Afya na Ustawi wa Jamii - Naibu wake sasa ni Waziri Kamili; naibu wa sasa ni Dr. Kebwe S. Kebwe

- Mulugo ameondoshwa rasmi serikalini. Nafasi yake imejazwa na Jenista Muhagama

- Pindi chana amejaza nafasi ya Ummi Mwalimu - Jinsia na watoto

- Mifugo na Maendeleo ya Mifugo - Titus Kamani atakuwa Waziri mpya. Naibu ni Telele na hivyo Wizara nzima imepata mawaziri wapya

- Ole Medeye OUT - Simbachawene kachukua nafasi yake (Naibu wa Prof. Tibaijuka)

- Naibu Kilimo - Zambi

- Habari - Naibu ni Juma Nkamia

- Nyalandu amekuwa Waziri Kamili. Naibu ni Mahmood Hassan Mgimwa

- Muhongo na Naibu wake wamebakizwa. Nishati atachukua Charles Kitwagwa akiichukua toka kwa Simbachawene


Thursday, May 09, 2013

Makala yangu Ktk RAIA MWEMA Toleo la Mei 8, 2013: "Kama ya udini, sumu ya ugaidi nayo itatugharimu"


HUU ni mwendelezo wa makala ya iliyopita iliyojaribu kujadili mwelekeo wa mageuzi ya kisiasa huko nyumbani tangu yaruhusiwe takriban miaka 20 iliyopita.
Pamoja na mambo mengine, katika makala hiyo nilibainisha waziwazi kuwapo kwa wanasiasa watatu waandamizi wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), ambao binafsi ninawaona kama kikwazo kwa ufanisi wa mageuzi hayo, sambamba na kuwa hatari kwa ustawi wa Taifa.
Niliwataja wanasiasa hao kuwa ni Stephen Wassira, Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba. Kwa bahati nzuri, kati ya nilipoandika makala hiyo na sasa kumejitokeza majina mengine ya viongozi wa CCM wenye mtizamo na vitendo kama wa hao watatu, na hilo linalazimisha kupanua zaidi wigo wa mjadala huu.
Lakini kabla sijarukia majina hayo mapya ni vema nikiendeleza pale nilipoishia katika makala iliyopita, ambapo baada ya kuwajadili Wassira na Nape, inabidi kumwangalia Mwigulu Nchemba.
Ninapata shida kumwelewa mwanasiasa huyu. Wasifu wake unaonyesha kuwa ni mtu aliyeelimika lakini matendo yake yanakinzana kabisa na uelewa wa mtu wa kiwango cha aina yake ya elimu.
Kati ya vitendo vingi vinavyokera kama ni kweli amefanya yeye, ni kumvisha mbwa bendera ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwenye mkutano wa hadhara. Sijui lengo lilikuwa kuwafananisha CHADEMA na mbwa au ni mwendelezo tu wa siasa mufilisi za wanasiasa wetu? Lililo wazi ni kuwa mtu mwenye uelewa tu wa kawaida hawezi kufanya kitendo cha aina hiyo.
Lakini pengine tukio litakalobaki vichwani mwa Watanzania wengi kuhusu Mwigulu na siasa zake za chuki (hususan dhidi ya CHADEMA) ni hili la ‘tuhuma za ugaidi dhidi ya Wilfred Lwakatare.’
Nisingependa kujadili kwa undani suala hili kwa vile tayari lipo mahakamani (japo majuzi baadhi ya wabunge wameamua kupuuza busara hiyo – hatuwezi kuwalaumu sana kwani yayumkinika kuhitimisha kuwa kuna uhaba mkubwa wa busara miongoni mwa wabunge wetu).
Kwa kufuatilia mtiririko wa suala la Lwakatare, ni rahisi kuhitimisha uhusika wa Mwigulu katika aidha kutengeneza mkakati fyongo wa kujenga picha kuwa CHADEMA ni chama cha kigaidi au kutumia mkakati huo kupigia mstari ajenda hiyo ya ugaidi.
Kwamba Mwigulu ameshaashiria mara kadhaa kuwa na uelewa wa uwepo wa ‘video ya Lwakatare’ hata kabla haijawekwa mtandaoni si jambo la kujadili tena. Labda tunachopaswa kujiuliza ni kama uhusika wa Mwigulu katika mkakati huo ni ajenda yake binafsi ya chuki dhidi ya CHADEMA au ni ajenda ya CCM.
Majuzi, uongozi wa CHADEMA ulitoa tamko linaloonyesha ‘mtandao’ mpana wa wahusika wa mkakati huo, ambapo licha ya Mwigulu, CHADEMA iliwataja watu wengine kadhaa wakiwemo watumishi waandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Kimsingi, hata kama CHADEMA wasingemtaja Mwigulu, au hata kama mwenyewe asingebainisha huko nyuma kuwa ana mkanda wa video unaothibitisha ‘mipango ya ugaidi’ ya CHADEMA, mtu yeyote anayefuatilia siasa za Tanzania kwa karibu, au anayemfahamu vyema mwanasiasa huyo, asingeshindwa kuhisi kuwa anahusika kwa namna moja au nyingine.
Ni rahisi kuhitimisha kuwa ajenda kuu kichwani mwa Mwigulu ni kuiangamiza CHADEMA kwa namna mbaya kabisa. Chuki za mwanasiasa huyo kwa CHADEMA ni kubwa zaidi ya waliyokuwa nayo Watanzania dhidi ya mkoloni, kaburu au nduli Idi Amin.
Lakini wakati ninamshutumu Mwigulu ni vema kujiuliza, “Je uongozi wa juu wa CCM, ikiwa ni pamoja na Rais Kikwete, wana mtizamo tofauti na wa Mwigulu?” Au “je Mwigulu anatumia tu vibaya nafasi yake ndani ya chama hicho au anatekeleza tu matakwa na maelekezo ya chama hicho tawala?”
Ni vigumu kuamini kuwa Mwigulu haungwi mkono na viongozi wenziwe wa CCM (ukiweka kando Wassira na Nape) kwa sababu laiti ingekuwa hivyo basi angeshakemewa au ‘kuwekwa sawa.’
Vyovyote ilivyo, hatua iliyofikiwa na Mwigulu na wenzie kutengeneza mazingira ya uhalifu (criminalisation) dhidi ya CHADEMA yaweza kuwa na madhara yasiyokusudiwa. Nimeandika mara kadhaa kuwa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa kwa CHADEMA kunatokana na udhaifu, ubabaishaji, uzembe, ufisadi, nk ndani ya CCM.
Kinachokiweka CHADEMA karibu na Watanzania wengi hivi sasa ni mafanikio ya chama hicho kuwaonyesha bayana wananchi jinsi CCM ilivyoifikisha nchi hapa tulipo, kwa kuibua ufisadi unaowahusisha baadhi ya viongozi wa CCM na kupigania marekebisho ya kimfumo (kwa mfano marekebisho ya Katiba) yatakayoleta uongozi wa hali na wa uadilifu.
Kwa kukihujumu CHADEMA, Mwigulu na wenziwe wanaweza kuwa wanawahujumu Watanzania, kwa sababu wakati CCM kimekuwa kikiwashawishi Watanzania kuwa CHADEMA hakifai, wenzao wa CHADEMA nao wamekuwa wakiwaamsha Watanzania kuhusu hali ilivyo sasa na hatma ya nchi yao, na nini kinapaswa kufanyika kuifikisha Tanzania yetu mahali inapostahili.
Ninatafsiri mkakati wa kufanya CHADEMA kionekane chama cha kigaidi umelenga kujenga hoja mbadala dhidi ya ile ya CHADEMA kuwa CCM ni chama cha mafisadi. Kwamba CHADEMA wakisema “CCM ni mafisadi” CCM nao watakuwa na cha kusema, kuwa “CHADEMA ni chama cha kigaidi.” Ikumbukwe, kabla ya ‘mkakati huu wa ugaidi’ CCM ilijaribu bila mafanikio kujenga picha kuwa CHADEMA ni chama cha kifamilia, baadaye kikabila, na hatimaye cha kidini. Mkakati huo wa kuifanya CHADEMA ionekane chama cha kidini umechangia sana kutufikisha katika vuguvugu la udini linaloendelea huko nyumbani. 
Nitahitimisha makala hii katika toleo lijalo kwa kuhusisha hatari ya vitendo vya Wassira, Nape na Mwigulu na uhuni unaoendelea huko bungeni, sambamba na kujadili kwa kifupi ‘nyongeza katika orodha ya wanasiasa hatari’ (yaani zaidi ya hao watatu, na kuwatupia macho Spika Anne Makinda, Naibu wake Job Ndugai na mbunge Peter Serukamba ambaye ameweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kutumia ‘the F-word’ katika Bunge tukufu la Jamhuri ya Muungano).
Kwa kifupi, kilichojiri bungeni hivi karibuni ni mwendelezo tu wa yale yanayofanywa na akina Wassira, Nape na Mwigulu kwenye harakati zao za kila siku za kuendeleza siasa za chuki. Wanapuliza sumu nje ya bunge lakini upepo umefanikiwa kurejesha sumu hiyo ndani ya bunge, na kwa hakika hatma ya taasisi hiyo tukufu-na nchi yetu kwa ujumla si njema.
Itaendelea.

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India