Featured Posts

Showing posts with label RAIA MWEMA. Show all posts
Showing posts with label RAIA MWEMA. Show all posts

Friday, April 25, 2014

Makala yangu ya RAIA MWEMA Toleo la 23.04.14: "Wazimu Huu wa Udini ni Hatari" #KatibaMpya

NI dhahiri sasa kuwa mjadala wa Katiba mpya, hususan kipengele cha muundo wa Muungano, unaelekea kulipeleka taifa mahali pabaya. Japokuwa dalili za Bunge Maalumu la Katiba linaweza kuishia kuwa jukumu ghali kwa walipakodi masikini, hasa baada ya kusikika madai ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuwa posho ya shilingi 300,000 kwa siku haitoshi, lakini Watanzania wengi walikuwa na imani kwamba ‘upepo huo mbaya’ ungepita na hali ingekuwa shwari.
Hata hivyo, kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya. Kinacholeta wasiwasi zaidi kwa sasa ni kuibuka kwa dalili za ubaguzi wa waziwazi, sambamba na jitihada hatari za kumwaga petroli kwenye moto kwa kuingiza udini kwa nguvu kwenye siasa.
Lakini pasi ‘kuuma maneno’ naomba nielekeze lawama zangu kwa Rais Jakaya Kikwete na chama chake - CCM. Pamoja na wasiwasi uliokuwepo awali, kwamba huenda Rais Kikwete angeendeleza desturi iliyoota mizizi ndani ya CCM kwamba kila wazo lililoanzia vyama vya upinzani (kama hilo la umuhimu wa kuwa na Katiba mpya) ni baya, na hivyo angekwamisha uwezekano wa kupata Katiba mpya, alitushtua wengi alipoonyesha dalili za kuwa amepania kwa dhati kuweka historia kwa kufanikisha suala hilo muhimu.
Mambo yalionekana kwenda vizuri licha ya jitihada za hapa na pale ndani ya CCM kulifanya suala la Katiba mpya kuwa la kiitikadi zaidi kuliko la kitaifa. Wengi mtakumbuka vijembe walivyopigwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani walipotaka kukutana na Rais Kikwete. Badala ya kupongeza kile kilichoonekana kama mwanzo mpya wa siasa za maridhiano, baadhi ya wanasiasa huko CCM waliwakebehi wapinzani kuwa wanataka kwenda Ikulu kunywa chai tu!
Dalili za mwanzo kuwa hatma ya suala la Katiba mpya ipo shakani zilianza kujichomoza zaidi baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba kuweka hadharani Rasimu ya Kwanza ya Katiba mpya, ambapo pendekezo la muundo wa Muungano wa Serikali tatu liliwekwa bayana. Taratibu, CCM, chini ya uongozi wa Kikwete, ilianza harakati za chini chini kujaribu kuingilia mchakato wa Katiba mpya, ikiwa ni pamoja na jitihada za kubinafsisha mchakato huo.
Lakini Mungu si Athumani au John, pamoja na vizingiti vya hapa na pale, hatimaye Rais Kikwete alitangaza majina ya wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali ya jamii, kuingia katika Bunge la Katiba. Lakini kabla ya hapo, tayari Rais Kikwete alishatangaza mkoani Mbeya wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM kwamba msimamo wa chama hicho ni Serikali mbili. Japo alitangaza msimamo huo kama Mwenyekiti wa taifa wa CCM, katika mazingira ya kawaida tu, isingewezekana kuwapo kwa mitizamo tofauti kati ya Kikwete wa CCM na Kikwete Rais.
Kuanzia hapo ikawa kama ‘jini lililopo kwenye chupa’ (a genie in the bottle) limefunguliwa. Zikaanza harakati za waziwazi ‘kulazimisha’ matakwa ya chama tawala kwamba muundo wa Muungano lazima ubaki kuwa wa Serikali mbili. Mara zikapatikana taarifa kuwa CCM imetengeneza rasimu yake ya siri.
Mara tu baada ya kikao cha Bunge Maalum la Katiba kuanza, ishara kuwa hali huko mbele inaweza kuwa si shwari zikawa zinajitokeza kila kukicha. Baada ya mshikemshike wa madai ya posho, likaibuka suala la utaratibu wa kupiga kura (yaani kura zipigwe kwa usiri au uwazi.)
Lakini kwa vile tangu awali CCM walionyesha kuwekeza nguvu zao kubwa katika suala la muundo wa Muungano wakitaka Serikali mbili, suala hilo limeteka takriban kila kipengele cha Katiba mpya, na kwa bahati mbaya au makusudi, mjadala wa muundo wa Muungano unazidi kutishia umoja na mshikamano wa taifa letu.
Japo lugha za matusi na kashfa si jambo geni kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri, hali imezidi kuwa mbaya kwenye kikao cha Bunge Maalumu la Katiba, tunasikia baadhi ya wajumbe wakiwatuhumu wenzao kuwa mashoga, huko wengine wakienda mbali na kuhoji Uafrika wa wenzao. Lakini kama nilivyobainisha hapo juu kuwa tumeshazoea matusi na lugha chafu bungeni, kuna waliokuwa na imani kuwa “wakimaliza kutukanana, watarejea kwenye suala lililowakutanisha huko Dodoma.”
Mara vikaanza kuibuka vitisho kuwa iwapo Katiba mpya itaridhia Serikali mbili, jeshi litatwaa madaraka. Na aliyeanzisha vitisho hivi si mwingine bali Rais Kikwete katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge hilo la Katiba, wiki chache zilizopita.
Lakini wakati Rais Kikwete aliliongelea suala hilo katika jukwaa la kisiasa (bungeni), mmoja wa wasaidizi wake akaamua kulitoa suala hilo katika anga za siasa na kulipeleka kwenye nyumba za ibada. Hapa ninamzungumzia William Lukuvi.
Inaniwia vigumu kupata maneno stahili ya kumwelezea mwanasiasa huyo ambaye ghafla ametokea kuwa mtu mwenye kauli chafu, hatari na za kiharamia.
Huyu mtu bila aibu wala uoga amediriki kwenda kanisani na kutangaza waziwazi kuwa jeshi litaasi pindi uamuzi wa kuwa na Serikali tatu utakapopitishwa. Naomba nitamke bayana kwamba nahisi Lukuvi ana matatizo kutokana na hatua yake ya kwenda kanisani kufanya mahubiri ya kushawishi jeshi kuasi.
Lakini anayempa jeuri Lukuvi ni Rais Kikwete, kwani naye aligusia suala hilo kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la Katiba. Kwa hiyo anachofanya Lukuvi ni kusambaza tu ujumbe ulioanzishwa na Rais Kikwete.
Na wakati Rais Kikwete akiwakemea “wanasiasa wanaomtukana Nyerere na Karume” amekalia kimya matusi ya Lukuvi kwa Mwenyezi Mungu (naam, kutumia nyumba ya ibada kujenga chuki na kuhamasisha uasi wa jeshi ni matusi kwa Mungu.)
Ni watu wenye upeo mdogo tu watakaochukia kusikia kwamba Nyerere na Karume wana mchango katika matatizo tuliyonayo kuhusu Muungano, hasa kwa uamuzi wao wa kulifanya suala hilo kama lao binafsi bila kuangalia madhara yake miaka kadhaa ijayo.
Mara kadhaa Rais Kikwete amekuwa akiasa kuhusu athari za kuchanganya siasa na dini. Amewahi kudai kuwa kuna maadui wa nje wanaotumia suala la dini kwa minajili ya kututenganisha.
Lakini kipi cha kushangaza ilhali kwenye chaguzi kadhaa wamekuwa wakitumia nyumba za ibada kupandikiza chuki dhidi ya wapinzani wao?
Japo hainisumbui sana iwapo Katiba mpya haitopatikana, napata wasiwasi kuona uhuni wa kisiasa (political thuggery) ukihalalishwa kwa kisingizio cha ‘kuhubiri athari za Serikali tatu.’
Lakini nani wa ‘kuokoa jahazi’? Rais Kikwete anakemea wanaowatukana Nyerere na Karume, lakini anapuuza matusi ya wasaidizi wake kwa Jaji Warioba.
Nimalizie makala hii kwa kumkumbusha Rais Kikwete kwamba mwakani ataondoka madarakani na kurejea uraiani. Asipotengeneza mazingira mazuri kwake na kwa Watanzania, janga hili linalopikwa na akina Lukuvi litamwathiri naye pia.
Ni muhimu kwa Rais kuweka kando ushabiki wa kisiasa na kuchukua hatua za makusudi kuepusha nchi kutumbukia kwenye machafuko yanayochochewa na mahubiri ya ubaguzi na kuitumia dini kwa minajili ya kisiasa.

Friday, April 18, 2014

Makala yangu Ktk RAIA MWEMA la 16.04.14: "Mafuriko Dar na Kauli za Nyodo za Meya @JerrySilaa"

NIANZE kwa kutoa pole kwa Watanzania kwa janga la mafuriko ambalo linaendelea kusababisha madhara makubwa katika maeneo mbalimbali huko nyumbani.
Japo taarifa zinazosikika zaidi kuhusu mafuriko hayo ni za hali ilivyo Jijini Dar es Salaam, taarifa zinaonyesha kuwa janga hilo linaendelea kusababisha madhara katika sehemu nyingine mbalimbali za nchi yetu.
Kwa vile Taifa bado lipo katika kipindi cha majonzi kufuatia wenzetu kadhaa waliokwishapoteza maisha kutokana na mafuriko hayo, sambamba na maelfu waliopoteza mali zao, inaweza kuwa si wakati mwafaka sana kuanza kunyoosheana vidole. Hata hivyo, kituko kimoja kilichojitokeza mwishoni mwa wiki iliyopita kinaleta haja ya kuwekana sawa wakati tunakabiliana na janga hili.
Jumamosi iliyopita, kulipatikana taarifa iliyoambatana na picha inayomwonyesha Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, akiwasili mjini Mwanza kwa shughuli za kichama. Ikumbukwe kwamba siku hiyo hali ilikuwa mbaya sana Jijini Dar es Salaam kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kuonyesha sehemu mbalimbali huko nyumbani.
Ili kukupa mlolongo sahihi wa matukio, naomba ninukuu kauli husika kuhusiana na tukio hilo. Awali, kutokana na kushangazwa na uwepo wa Meya Silaa jijini Mwanza huku wananchi wake wakikabiliwa na janga la mafuriko, nilibandika picha iliyoambatana na maelezo
Meya wa Ilala Jerry Silaa katika shughuli za kichama muda huu huko Mwanza,” na kuuliza “Mheshimiwa, una taarifa za mafuriko Dar?” Kisha nikaandika tena, “Hawa ndio viongozi wenu. Manispaa ya Ilala ipo katika mafuriko, Meya wa Ilala Jerry Silaa yupo kichama Mwanza.
Baada ya muda mfupi, Meya Silaa alijibu, namnukuu,
Nakuomba radhi kama ungependa niwe Dar nikizuwia mvua isinyeshe.” Kisha akaandika tena “I hate cheap politics (nachukia ‘siasa nyepesi’). Mabonde yote yamejengwa. Mnategemea mito itapumulia wapi? I have remarkable record kwenye rescue missions (nina rekodi ya kupigiwa mfano kwenye jitihada za uokoaji.)” Lakini hakuishia hapo, akaendelea kudai kwamba, “Kwangu wahanga (wa mafuriko) ni kwa wanaoathirika kwa madaraja kukatika iliyosababishwa na watu kujenga mabondeni.” Na katika ‘kuhitimisha’ mjadala huo, Meya Silaa akatoa tuhuma kwamba “Najua viongozi wengi huwa wanaombea watu hata wafe wakabebe jeneza kuonekana wanajali lakini ni unafiki.”
Naomba niweke wazi ya kuwa sina tatizo na Meya Silaa binafsi ila kwa hakika kauli zake zilizosheheni dharau na kiburi zilinikera sana. Na si mimi pekee bali Watanzania kadhaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii pia walishutumu kauli za kiongozi huyo wa Manispaa ya Ilala.
Hata hivyo, pamoja na ushauri wa wengi kwamba hata kama hakuwa na nia mbaya katika kauli hizo basi labda aombe radhi, Mheshimiwa huyo alipuuzia ushauri huo. Mie ni muumini mkubwa wa uhuru wa kujieleza. Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba uhuru pasi nidhamu ni uhuni. Japo kila kiongozi ana uhuru wa kujieleza kama mwananchi yeyote yule, uhuru huo unaambatana na wajibu wa kiongozi husika kwa umma.
Kwa busara za kawaida tu, shughuli za kichama zilizompeleka Meya Silaa huko Mwanza hazikuwa na uzito mkubwa zaidi ya janga la mafuriko Jijini Dar es Salaam ambapo manispaa ya mheshimiwa huyo ilikuwa ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa sana.
Lakini busara zaidi zingeweza kutumika baada ya mheshimiwa kutambua kuwa suala hilo limezua hisia hasi miongoni mwa wananchi, na angeweza kujibu kistaarabu tu, kwa mfano, “ninatarajia kurejea Dar es Salaam  haraka kushirikiana na wananchi wenzangu katika janga hili” badala ya kauli ya kebehi kuwa ‘anaomba radhi kwa anayependa awepo Dar es Salaam  kuzuwia mvua isinyeshe.’
Hivi Rais Jakaya Kikwete alipofanya ziara ya maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na mafuriko hayo alifanya hivyo ili kuzuwia mvua au mafuriko hayo? Na je Makamu wa Rais Dk. Bilal na viongozi wengineo walionusurika katika ajali ya helikopta wakati wakitaka kuanza ukaguzi wa athari za maafa ya mafuriko walitarajia wangezuwia mafuriko hayo?
Ninaamini Meya Silaa anafahamu fika kwamba tunapokwenda kuwajulia hali wagonjwa haimaanishi kuwa tutawaponyesha, tunapokwenda misibani haimaanishi kuwa tutawafufua marehemu. Kumjulia hali mgonjwa au kujumuika msibani ni ustaarabu tuliyojijengea katika mila zetu kuonyesha kuwa TUNAJALI. Na kisaikolojia inaonyesha kuwa mhanga wa tukio lolote lile hupata faraja pindi anapotambua kuwa kuna wanaomjali.
Katika moja ya majibu yangu kwake, nilimfahamisha bayana Meya Silaa kwamba tatizo kubwa la wengi wa viongozi wetu ni kuzowea kusifiwa tu lakini wakikosolewa hukimbilia kudai ni ‘cheap politics.’
Waingereza wanasema “wrong is just that, wrong” (kisicho sahihi kipo hivyo hivyo, hakipo sahihi). Kiongozi kuzipa kipaumbele shughuli za kichama ilhali wananchi wanahangaika na janga la mafuriko si sahihi, na hakuna excuse katika mazingira ya aina hiyo.
Japo Meya Silaa anaweza kuwa sahihi kulaumu ujenzi wa mabondeni kama moja ya sababu zinazochangia mafuriko, lakini kwa hakika mamlaka husika kwa mfano Manispaa ya Ilala inayoongozwa na Meya Silaa zinahusika kwa namna moja au nyingine. Kuwalaumu tu wakazi wa mabondeni hakuwezi kuleta ufumbuzi wa tatizo. Ni muhimu kuelewa kwanini wakazi hao wa mabondeni wanaendelea kuishi maeneo hayo licha ya tishio la mafuriko.
Kwa uelewa wangu, wengi wao ni masikini ambao wanaoishi katika ‘nyumba za mbavu za mbwa’ na ni vigumu mno kwao kumudu kununua ama kujenga nyumba bora katika maeneo salama, achilia mbali huo uwezo wa kununua japo kiwanja.
Lakini eneo jingine ambalo pengine Meya Silaa hawezi kuligusia ni ujenzi unaokiuka taratibu za mipango-miji, unaofanywa na matajiri ambao fedha zao zinawawezesha kupindisha kila aina ya sheria. Wanaoishi mabondeni ni wahanga wanaathiriwa zaidi na kanuni za kiasili za maji kujaa kwenye mabonde, lakini ujenzi holela unaoathiri mfumo wa maji taka ni uingiliaji wa makusudi wa jitihada za binadamu kukabiliana na mafuriko.
Mvua ikinyesha maji yanajaa, na kwa vile mitaro inayopaswa kuyaongoza maji hayo katika maeneo maalumu imezibwa, maji hayo yatamwagikia eneo lolote lile, hata kama si bondeni.
Kuhusu kauli za Meya Silaa, nilimfahamisha kwamba ana bahati ni meya wa manispaa nchini Tanzania kwani laiti angekuwa  meya kwa hapa Uingereza, kisha akaenda mji mwingine kwa shughuli za kichama ilhali wananchi wake wanakabiliana na janga la mafuriko, kungekuwa na uwezekano mkubwa wa harakati za kumng’oa madarakani. Moja ya sifa ya uongozi si tu kujali wananchi bali pia kuonyesha uongozi hasa katika nyakati za majanga.
Kauli hizo zisizopendeza za Meya Silaa zimekuja katika kipindi ambacho Taifa letu lipo katika mchakato wa kupata Katiba mpya. Pengine tukio hili laweza kuwa angalizo muhimu kuhusu Katiba hiyo mpya.
Kwa mfano, je, Katiba hiyo itamwezesha mwananchi wa kawaida kumwajibisha kiongozi ‘mwenye kauli zisizofaa’? Suala hapa si tu katika kauli za kiongozi (iwapo zinafaa au la) bali suala zima la uwajibikaji.
Nimalizie makala hii kwa kurejea kauli ya Rais Jakaya Kikwete wakati alipofanya ziara katika maeneo mbalimbali kuangalia athari za mafuriko, kwamba “mafuriko hayaepukiki na wajibu wa Serikali ni kuwasaidia waathirika.”
Mafuriko kama maji kujaa kutokana na wingi wa mvua hayaepukiki, lakini mafuriko kama ukosefu wa miundombinu bora ya kukabiliana na mafuriko ni suala lililo ndani ya uwezo wetu. Kuna tofauti kati ya mafuriko yanayosababishwa na maji kuvuka kingo za Mto Kilombero huko Ifakara, na mafuriko katika maeneo yasiyo mabondeni jini Dar yanayochangiwa na mfumo duni wa kushughulikia majitaka.
Na japo ninaafikiana na kauli ya Rais kwamba wajibu wa serikali ni kuwasaidia waathirika (sijui ni wapi hao tukirejea kauli ya Meya Silaa) lakini kuna mengi yaliyo ndani ya uwezo wa serikali yanayoweza kupunguza idadi ya waathirika wa majanga kama mafuriko. Kubwa zaidi ni kujijengea uwezo wa kukabiliana na majanga badala ya kusubiri janga litokee ndipo tuanze kutafutana. 

Friday, April 11, 2014

Makala yangu ktk RAIA MWEMA Tole la 09/04/14: "Sakata la Muungano- Si kila jambo jema ni sahihi"

KWA familia nyingi huko nyumbani, takriban kila usiku huambatana na kukusanyika mbele ya runinga kuangalia tamthilia mbalimbali.
Hali kama hiyo hujitokeza pia mchana wa mwisho wa wiki ambapo tamthilia hizo hurejewa kwa kujumuisha ‘vipande’ vya wiki nzima.
Nyingi ya tamthilia hizo huwa katika lugha ya kigeni, lakini wengi wa wanaozifuatilia wanamudu kuzielewa bila matatizo. Hata hivyo, yayumkinika kuhisi kwamba hata magwiji wa ufuatiliaji wa tamthilia hizo sasa wanapata wakati mgumu si tu kufuatilia bali hata kuelewa ‘tamthilia’ nyingine ndefu inayoendelea huko Dodoma. Hapa ninamaanisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba.
Pengine ni vema nikawakumbusha wasomaji msimamo wangu kuhusu suala la Katiba mpya, ambao nimeutanabahisha katika makala zangu kadhaa zilizopita.
Kwanza, pamoja na kutambua haja ya kuwa na Katiba bora zaidi ya tuliyonayo sasa, ukweli kwamba matatizo mengi yanayoikabili nchi yetu hayatokani na ukosefu wa sheria bali usimamizi na utekelezaji wake, sioni jinsi Katiba mpya (kama itapatikana) itakavyoweza si tu kuwa ‘mwarobaini’ wa matatizo yetu bali pia kuheshimiwa.
Pili, muundo wa Muungano ndio suala linaloonekana kutawala mjadala wa Katiba mpya, na ninarejea tena kukiri kwamba ninachoona muhimu kwangu si idadi ya serikali zinazounda Muungano- ziwe mbili kama ilivyo sasa, tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, au hata serikali moja kama inavyodaiwa kuwa ndio ‘muundo halisi’ wa Muungano- bali jinsi serikali husika inavyoweza kutimiza majukumu yake na kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi.
Kwahiyo basi, kwa lugha nyepesi, msimamo wangu katika suala hili la muundo wa Muungano ni “wowote ule utakaowapatia Watanzania wanachostahili.” Na kwa hakika, malumbano yanayoendelea kuhusu suala hili la muundo wa Muungano yamegubika masuala mengine muhimu yaliyoleta haja ya kuwa na Katiba mpya.
Sasa, kwa vile mazingira yanaashiria kwamba kupatikana au kutopatikana kwa Katiba mpya kunategemea muafaka katika suala hilo la muundo wa Muungano, basi hata sie ‘tusiolitilia maanani sana’ tunalazimika kulijadili kwa marefu na mapana. Hiki ni kikwazo ambacho bila kukivuka chaweza kuondoa uwezekano wa kupatikana Katiba mpya.
Mwanzoni mwa makala hii, nimefananisha kikao cha Bunge Maalumu la Katiba na tamthilia. Lakini kichekesho ni kwamba wakati tamthilia nyingi za kigeni zinazotawala kwenye runinga za huko nyumbani zinaeleweka licha ya kuwa katika lugha za kigeni, hii ya Bunge la Katiba si tu inazidi kutoeleweka bali inapoteza ladha kila kukicha.
Hakuna haja ya kurejea mlolongo wa matukio yaliyokwishakujitokeza katika Bunge hilo, hasa kwa vile takriban yote yanakera; kuanzia madai ya nyongeza ya posho hadi Bunge hilo kugeuka ulingo wa kuonyeshana umahiri wa vijembe na lugha zisizopendeza.
Lakini sasa kuna suala jipya ambalo si tu linazidisha ugumu wa mjadala wa muundo wa Muungano bali pia linatishia hata uhai wa Muungano wenyewe. Suala hili ni nyaraka mbalimbali za kuthibitisha uhalali/uhalisia wa Muungano.
Ningependa kukiri kwamba sielewi nyaraka hizo za Muungano ni ngapi, lakini ninachofahamu ni kwamba moja ni hiyo inayofahamika kama Hati ya Muungano. Sasa, katika mazingira yanayoweza tu kuonekana katika filamu ya kutisha (horror movie), sahihi ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere inaonyesha dalili ya ‘kuchakachuliwa.’ Mlolongo wa maswali unaibuka hapo: je, sahihi hiyo imechakachuliwa au hati nzima imechakachuliwa na ndiyo maana sahihi inazua utata? Nani aliyefanya ‘uhuni’ huo? Na kubwa zaidi, kwa nini?
Lakini ukidhani kizaazaa pekee ni katika suala hilo la sahihi ya Nyerere tu, basi subiri mpaka utakapofahamu kwamba madai kuwa Hati ya Muungano ambayo awali ilidaiwa ipo Umoja wa Mataifa (UN) nayo yana walakini baada ya UN kudai haina hati hiyo. Swali jingine, iko wapi? Kwa nini ilidaiwa ipo UN ilhali si kweli? Nani huyo anayedanganya? Kwa nini?
Kabla ya kuandika makala hii nimekutana na maelezo ya mchambuzi mmoja kwenye mtandao mmoja wa kijamii akieleza kwamba kwa uelewa wake, hati iliyowasilishwa katika Bunge Maalumu la Katiba huko Dodoma, na yenye sahihi za Nyerere na Pius Msekwa sio ‘Hati ya Muungano’ (Articles of the Union) bali ni Sheria ya Muungano (the Act of the Union) iliyotungwa na Bunge wakati huo kupitisha Articles of the Union, na kusainiwa na Nyerere na Msekwa (kama Katibu wa Bunge wakati huo).
Na hata hati hiyo ingekuwa ndio Hati halisi ya Muungano, bado kuna tatizo jingine la sahihi za Nyerere na Msekwa kuwa na walakini. Kadhalika, inaelezwa kwamba hati hiyo imeongezwa maneno ‘kwa kompyuta’ japo kila mwenye uelewa anafahamu kwamba kompyuta hazikuwapo nchini katika miaka hiyo ya 1960.
Mchambuzi huyo anahitimisha kwamba hati ‘zilizotoweka’ ni nakala halisi ya Serikali ya Tanganyika, nakala halisi ya SMZ, nakala halisi ya Bunge la Tanganyika, nakala halisi ya Baraza La Wawakilishi, nakala halisi ya Mwanasheria Mkuu, nakala halisi ya Nyerere, na nakala halisi ya Karume.
Maswali kadhaa yanajitokeza, ikiwa ni pamoja na, je nakala hizo ‘zimetoweka’ kweli au hazijawahi kuwapo? Nani anahusika na kutoweka huko? Kwa nini? Na maswali mengine lukuki.
Vilevile, gazeti moja la Kiingereza la huko nyumbani, katika toleo lake la juzi, liliripoti kwamba aliyekuwa Katibu wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Salum Rashid, alieleza kwamba Mzee Karume hakuwahi kusaini hati yoyote kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Utata huo unaogubika uhalali na/au uhalisia wa Muungano umenifanya kuhisi kwamba kuna mtu/watu fulani mahala fulani anadanganya/wanadanganya. Swali: ni nani? Na kwa nini anadanganya/wanadanganya?
Niliwahi kuandika katika moja ya makala zangu huko nyuma kwamba pamoja na nia nzuri ya kuunganisha Tanganyika na Zanzibar, Nyerere na Karume walikosea kufanya suala hilo kama la ‘wao binafsi’ na si la Watanganyika na Wazanzibari wote.
Pamoja na dhamira zao nzuri, sidhani kama viongozi hao waliangalia mbali zaidi ya ajenda ya umoja na mshikamano, hivyo kutotilia maanani uwezekano wa matatizo ya kisheria au hata ridhaa ya wananchi huko mbele. Na, binafsi naona mapungufu haya kama moja ya vyanzo vikuu vya matatizo ya Muungano.
Lakini pengine badala ya kuwalaumu waasisi hao wa Muungano ni muhimu kutambua mazingira ya kisiasa ya wakati huo. Hicho kilikuwa kipindi cha kujenga Taifa, huku mfumo wa kisiasa ukiwa hauruhusu mawazo tofauti na ya watawala. Hivi tumeshawahi kujiuliza wazo la kuunganisha Tanganyika na Zanzibar lilikuwa la kidemokrasia kiasi gani, kwa maana ya kusaka ridhaa ya wadau halisi wa Muungano huo, yaani Watanganyika na Wazanzibari?
Kwa bahati mbaya (au kwa makusudi), kwa kiasi kikubwa chama tawala CCM kinataka kurejea kosa hilohilo lililopelekea kuzaliwa Muungano ‘wenye matatizo.’ Wanataka kulazimisha matakwa yao ya muundo wa Muungano wa serikali mbili. Kuna busara moja inafundisha hivi, “Si kila tendo jema ni sahihi. Kwa mfano, kumpa chakula ‘kigumu’ mtu mwenye njaa ni tendo zuri, lakini kumpa chakula kingi kigumu mtu mwenye njaa kali ni hatari kwani inaweza kumfanya mtu huyo kuvimbiwa na hata kupoteza maisha.”
Dhamira ya CCM kutaka kunusuru muundo wa sasa wa Muungano (wa serikali mbili) inaweza kuwa nzuri. Lakini kulazimisha dhamira hiyo (pasi kujali uzuri wake) ni jambo hatari. Na hata kama CCM walitaka kulazimisha dhamira yao hiyo basi angalau wangejiandaa vya kutosha badala ya kukurupuka, na sasa tunashuhudia matatizo mengine makubwa zaidi yanayozua utata wa Muungano mzima wanaotaka kuinusuru.
Nihitimishe kwa kuishauri CCM na wote wanaotaka kulazimisha muundo wa Muungano wa serikali mbili, kwamba suluhu pekee ni kwa suala hilo kupelekwa kwa wananchi ili hatimaye waamue kuhusu muundo wa Muungano wanaotaka. Na si tu kulipeleka suala hilo kwa wananchi bali pia kutowatisha kwa minajili ya kuwalazimisha wafuate matakwa ya chama hicho tawala.
Ni ushauri mwepesi lakini kila anayeijua CCM anafahamu kuwa ni chama ‘kisichoshaurika’ wala ‘kuambilika.’ Kwao, wapo tayari Watanzania wakose Katiba mpya iwapo dhamira ya chama hicho kung’ang’ania muundo wa Muungano wa serikali mbili itakwama.
Kama ambavyo hata tukipata Katiba mpya inaweza kutokuwa na manufaa pasipo nia ya dhati kuiheshimu na kuitekeleza kwa ufanisi, pasipo nia ya dhati ya kusaka muafaka katika suala la muundo wa Muungano na hatma ya Katiba mpya kwa ujumla, kikao cha Bunge Maalumu la Katiba kitaishia kuwa tamthilia ambayo si tu inakera bali pia ya gharama kubwa kwa wananchi.
PENYE NIA PANA NJIA

Saturday, April 05, 2014

Makala yangu ktk RAIA MWEMA Toleo la 02.04.14: "Ajali Sasa Zimezoeleka Kama Mgao wa Umeme"

KATIKA  taifa la ‘nani-anajali?’ (a who-cares nation) ajali zimeanza kuzoeleka kama mgao wa umeme,” ni ujumbe nilioandika juzi katika mtandao fulani wa kijamii baada ya kusoma habari kwamba matukio mawili ya ajali yamegharimu maisha ya Watanzania wenzetu 33.
Ujumbe huo ulibeba mambo mawili ya msingi. Kwanza, ni kasumba inayozidi kushamiri miongoni mwa Watanzania ya kupuuzia masuala ya muhimu kwao binafsi na kwa taifa lao. Mifano ni mingi lakini hapa nitabainisha michache.
Kama kuna vitu viwili vinavyonikera mno katika mitandao ya kijamii ni malalamiko yasiyoisha ya watumia huduma mbalimbali huko nyumbani. Maeneo mawili yanayozalisha walalamikaji wengi ni mgao wa umeme na huduma duni za baadhi ya kampuni za simu za mkononi.
Katika tatizo la mgao wa umeme, wengi wa walalamikaji hutumia lugha kali na hata matusi dhidi ya Tanesco, kana kwamba kwa kufanya hivyo shirika hilo la umeme litaona aibu na kuacha tabia inayoelekea kuwa ya kudumu sasa ya kukata umeme mara kwa mara, wakati mwingine mara kadhaa ndani ya siku moja.
Huwa najiuliza, hivi kitu pekee wananchi hawa wanachoweza kufanya ni kuitukana tu Tanesco? Lakini pengine kundi linaloweza pia kubebeshwa lawama licha ya wananchi hao ‘walalamishi’ ni wanasheria na wanaharakati wa haki za watumia huduma (consumer rights).
Kundi hili linajumuisha watu wanaojua sheria zinazomlinda mlaji (consumer), na laiti wangeguswa na tabia hii ya Tanesco basi ni dhahiri wangeweza kufungua kesi zinazofahamika kisheria kama class action. Kesi za aina hii ambazo ni maarufu zaidi nchini Marekani hufunguliwa na kundi kubwa la watu wanaowakilishwa na mwanasheria mmoja au kundi la wanasheria, dhidi ya mtu au taasisi.
Kwa mfano, mwaka 2008 wateja kadhaa wa kampuni moja ya huduma za mawasiliano nchini Marekani, AT&T, walifungua kesi dhidi ya Shirika la Ushushushu la nchi hiyo (NSA) wakilituhumu kwa vitendo vya kunasa mawasiliano na kufuatiliaji nyendo zao (surveillance).
Japo walalamikaji katika kesi hiyo walishindwa mahakamani, lakini mfano huo umelenga kuonyesha jinsi watumia huduma huko kwa wenzetu wanavyosaka haki zao. Japo mimi si mtaalamu wa sheria, je hakuna uwezekano wa kufungua kesi kama ya aina hiyo (class action) dhidi ya wahusika wote wa mgao wa umeme?
Kwa wanaolalamika kuhusu huduma zisizoridhisha za baadhi ya makampuni ya simu (hivi kuna hata moja isiyolalamikiwa?), wala haihitaji class action bali uamuzi tu kwamba “ninaachana nanyi kwa sababu mnaniona kama mteja nisiye na thamani kwenu.”
Hiyo ikizua kitu kinachojulikana kama domino effect (yaani kama goroli zikiwa kwenye mstari, ukiipiga moja inaisukuma nyingine, na nyingine, na kadhalika) hatimaye kampuni husika itabaini kwamba uhai wake upo hatarini laiti isipojirekebisha.
Kichekesho ni kwamba ‘domino effect’ iliyopo huko nyumbani miongoni mwa wateja wasioridhishwa na huduma za baadhi ya makampuni ya simu ni mtu mmoja kuitukana kampuni husika, na mwingine kufanya hivyo, na kadhalika.  Na wasichotaka kujifunza kwa watangulizi wao ni ukweli kwamba hasira hayajawahi kuleta ufumbuzi wa tatizo lolote mahali popote pale.
Lakini kama nilivyoeleza mwanzoni mwa makala hii, mada ya wiki hii ni kuhusu kukithiri kwa ajali na mwamko mdogo miongoni mwa Watanzania kukabiliana na janga hilo ambalo kwa kiasi kikubwa linazuilika. Ndiyo, wanasema ‘ajali haina kinga’ lakini pindi ukiruhusu basi la abiria ambalo si tu linatumia injini ya ‘kibajaji’ lakini injini hiyo pia imechakachuliwa, ni wazi pindi basi hilo likipata ajali hatuwezi kudai kwamba ‘ajali haina kinga.’
Huo ni mfano wa kufikirika tu lakini ukweli unaochukiza ni kwamba asilimia kubwa ya vyombo vya usafiri wa abiria havipaswi japo kubeba majani ya kulisha mifugo au hata takataka. Sasa kwanini vyombo hivyo vya usafiri vinaruhusiwa kuwa barabarani?
Majibu mawili makuu ni aidha vinamilikiwa na vigogo ambao askari wa usalama barabarani hawawezi kuomba rushwa au kama mmiliki ni ‘mtu wa kawaida’ basi ni halali kwa askari kudai rushwa na kisha kuviruhusu viendelee na safari.
Wanasema ‘rushwa ni adui wa haki’ lakini kisichosemwa sana ni kwamba rushwa ni janga hatari kama ukimwi au ugaidi, vyote vyaweza kugharimu maisha ya watu wasio na hatia.
Na hata pale chombo cha usafiri kinapokuwa imara (kwa maana kinaweza kumudu kusafirisha abiria bila matatizo), tatizo jingine ni madereva. Katika mazingira ya kawaida tu, mtu akikesha baa kisha akaamka na mabaki ya pombe ya jana kichwani, anaweza kuwa na wakati mgumu kutembea kwa miguu achilia mbali kumudu kuendesha usafiri mwepesi kama pikipiki au hata baiskeli. Sasa dereva wa basi la abiria anaporuhusiwa kuendelea na safari huku ana ‘faida kichwani’ ni wazi kwamba hatma ya safari hiyo ni kama bahati nasibu.
Kwa nini madereva wasiostahili kuwao barabarani (maana hata mwendesha guta au bajaji akiwa na uwezo wa kuhonga trafiki ataruhusiwa kuendesha basi la abiria, hata kama hana leseni wala ujuzi stahili) wanaruhusiwa? Jibu ni lilelile: aidha chombo cha usafiri anachoendesha ni cha kigogo hivyo trafiki hawawezi kumdai rushwa au dereva anamudu kuwapatia trafiki haki yao ya rushwa.
Lakini kwa upande mwingine ni abiria wenyewe kutolipatia kipaumbele suala la usalama barabarani. Ni jambo la kawaida kusikia abiria wakipiga mayowe kwenye basi pindi dereva wa basi, kwa mfano, anapolikosakosa gari jingine barabarani, lakini hakuna ‘nguvu ya umma’ (kwa maana ya abiria kwa umoja wao ndani ya basi hilo) itakayotumika kumdhibiti dereva huyu. Na si kwamba abiria hao wanasafirishwa bure kiasi cha kuhofia kuwa “tukimbana dereva aendeshe kwa umakini atatushusha njiani.”
Kilichoniuma zaidi baada ya kusoma habari hiyo kuhusu wenzetu 33 waliopoteza maisha kutokana na ajali ni jinsi habari yenyewe ilivyoonekana ya kawaida miongoni mwa Watanzania wengi. Hata kwenye vyombo vya habari, magazeti mengi yalitawaliwa na habari kuhusu vituko vinavyoendelea kwenye Bunge Maalumu la Katiba huko Dodoma badala ya kulipa uzito janga hilo la kitaifa.
Katika salamu zake za rambirambi kwa wahanga wa moja ya ajali hiyo, Rais Jakaya Kikwete alieleza kwamba “vifo hivyo si vya lazima” na “ameshtushwa na kusikitishwa.” Lakini je inatosha tu kushtushwa na kusikitishwa ilhali, Mungu aepushie mbali, tuendelee kutarajia ajali zaidi hadi hapo hatua madhubuti zitakapochukuliwa ikiwa pamoja na kulifanya tatizo la ajali ‘zinazoepukika’ kuwa janga la kitaifa?
Lakini wakati Rais Kikwete anastahili pongezi kwa angalau kutoa salamu hizo za rambirambi, Watanzania wengine ukiachilia mbali wahanga wa ajali hizo, walifanya nini? Pitia pitia yangu kwenye mitandao ya jamii ilionyesha kuwa janga hilo lilikamata hisia za watu wachache sana ukilinganisha na, kwa mfano, klabu ya Liverpool ya hapa Uingereza kufanikiwa kushikilia usukani wa Ligi Kuu, au kimuhemuhe cha mpambano wa Ligi ya Mabingwa wa soka wa Ulaya kati ya Manchester United ya hapa na Bayern Munich ya Ujerumani  jana.
Inasikitisha kuona Tanzania yetu inazidi kuwa taifa la ‘who cares?’ (nani ajali?). Na kwa kiasi kikubwa tatizo hili linaanzia kulekule kwenye kutokujali haki au stahili zetu binafsi. Ni wazi kuwa familia isiyojali inaweza ‘kuzaa’ ukoo usiojali, na hatimaye uwezekano wa kabila lisilojali, na hadi kufikia hapa tulipo: taifa lisilojali.
INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO

Friday, March 28, 2014

Makala yangu ktk RAIA MWEMA Toleo la Machi 26, 2014: " Si serikali 1,2 au 3, Bali Shibe"

 
 “HIVI ujumbe aliotoa Rais Jakaya Kikwete alipohutubia Bunge la Katiba Ijumaa ulikuwa wa Rais? Mwenyekiti wa CCM? Mtanganyika au Mtanzania wa kawaida?”,  niliuliza swali hili katika mtandao mmoja wa kijamii baada ya kuchanganywa na hotuba hiyo.
Lakini siku chache baadaye, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu, ‘alijibu’ swali hilo kwa namna fulani. Akizungumza na moja ya magazeti ya huko nyumbani, Salva aliushutumu Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwa kile alichoeleza kuwa ni kuendeleza propaganda, na kubainisha kuwa “Rais kama Mtanzania ana haki ya kutoa maoni yake.
Wakati ninakubaliana na maelezo hayo, sote tunafahamu kuwa shughuli iliyompeleka Rais Kikwete katika Bunge hilo la Katiba ni kulizindua, si kutoa maoni yake. Ninaamini kwamba kama ilivyokuwa kwa Watanzania wengine, Rais alikwishakupewa nafasi ya kutoa maoni yake huko nyuma, na hakukuwa na haja ya kutumia tukio hilo la uzinduzi wa Bunge la Katiba ‘kutoa tena’ maoni yake.
Kwa upande mwingine, binafsi sikushangazwa na msimamo wa Rais Kikwete hususan kwenye hoja ya muundo wa Muungano. Kwa wenye kumbukumbu nzuri watakumbuka kwamba wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya, Rais Kikwete kama Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho tawala aliweka bayana msimamo wa CCM kuwa ni muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Sasa kwanini ilitarajiwa kwamba angebadili msimamo siku ya uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba?  Ni muhimu pia kukumbuka kwamba wazo lenyewe la mabadiliko ya Katiba halikuanzia CCM (angalau kipindi hiki, na tukiweka kando harakati za ndani ya CCM kama zile za kundi la G55) bali kwa vyama vya upinzani hususan, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kuna baadhi ya wachambuzi wanaokwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa hata huko kwa wapinzani kulikoanzia wazo hilo la Katiba mpya, msukumo ulikuwa zaidi katika mazingira ya chaguzi, hususan Uchaguzi Mkuu, baada ya kuonekana bayana kwamba Katiba iliyopo inatengeneza mazingira magumu ya ushindani halisi wa kisiasa (au kwa lugha nyingine, ni vigumu mno kukiondoa chama tawala madarakani katika mazingira ya Katiba iliyopo).
Mara kadhaa huko nyuma nimebainisha msimamo wangu kuhusu suala la Katiba mpya. Japo ninaafiki kwamba Katiba tuliyonayo ina mapungufu ya kutosha na kuna umuhimu mkubwa wa kuibadilisha, ninapata shida sana kuona jinsi kuja kwa Katiba mpya kutakavyoweza kumsaidia Mtanzania wa kawaida anayeandamwa na umasikini unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na ufisadi.
Tatizo jingine linaloninyima shauku ya kuona Katiba mpya inapatikana ni ukweli mchungu kwamba kwa kiasi kikubwa tatizo linaloikabili nchi yetu si ukosefu wa sheria bali usimamizi na utekelezaji wake. Hivi tumewahi kujiuliza kwamba kama sheria zilizomo kwenye Katiba iliyopo (na ni muhimu kutambua kuwa Katiba ni ‘sheria mama’) hazisimamiwi ipasavyo na kupuuzwa mara kadhaa, kuna mwamana (guarantee) gani kwamba sheria zitakazokuwemo katika Katiba mpya zitaheshimiwa?
Kati ya sababu za msingi zinazochangia kero za Muungano ni hiyohiyo ya kupuuza sheria. Wakati Rais Kikwete anahubiri faida za Muungano wa serikali mbili, alishindwa kabisa kukemea uvunjifu wa sheria (Katiba) ulioruhusu Zanzibar kujipa hadhi ya nchi ndani ya nchi. Kwa makusudi, mjadala kuhusu muundo wa Muungano unakwepa kujadili Marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 ambayo hayakuingizwa kwenye Katiba ya Muungano.
Uvunjifu huo wa Katiba kwa maana ya kuruhusu kuundwa kwa nchi yenye Rais wake, bendera yake, wimbo wake wa Taifa, Katiba yake, nk (Zanzibar) ndani ya nchi nyingine (Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania) ulifanyika wakati wa utawala wa Rais huyuhuyu tuliyenae sasa (Jakaya Kikwete), na si yeye wala washauri wake, kwa mfano ‘wakereketwa wa Muungano kama Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, waliodiriki kukemea jambo hilo.
Japo binafsi sipingi wala siungi mkono muundo wa Muungano wa serikali mbili au tatu (au hata wa serikali moja) kwa sababu kwangu cha muhimu ni function (kazi) na sio form (muundo), kinachofanyika sasa kwa kung’ang’ania muundo wa serikali mbili uliogubikwa na matatizo yanayoweza kuepukika ni kuahirisha tu tatizo. Ni wazi tatizo hilo litarejea kwani busara zinaeleza kwamba haiwezekani kuua wazo ‘lililoiva’ (you can’t kill an idea whose time has come).
Hatuwezi kutatua tatizo kwa kuficha tatizo jingine. Katika mazingira ya kawaida tu, ilipaswa mjadala kuhusu muundo wa Muungano uambatane na kuwekwa wazi kwa nyaraka zilizounda Muungano huo (Articles of the Union) ambazo zimeendelea kufanywa siri kubwa.
Hata kwa sisi tusiohangaishwa sana na muundo wa Muungano tunadhani kwamba pengine chanzo kikubwa cha ‘kelele zisizoisha’ kuhusu Muungano ni ukweli kwamba waasisi wa Muungano huo, Mwalimu Julius Nyerere na  Sheikh Abeid Karume, walifikia mwafaka wa kuunganisha nchi hizo kana kwamba yalikuwa makubaliano ya watu binafsi na si ya wananchi wote wa nchi hizo mbili. Sina hakika ni Watanganyika na Wazanzibari wangapi waliopewa fursa ya kuafiki au kupinga suala hilo la Muungano.
Na kama alivyofanya Rais Kikwete katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba, uhai wa Muungano umeendelea kutegemea zaidi kuogopana, hadaa na vitisho (hususan ile ya takriban kila Rais kudai hayupo tayari Muungano uvunjike mikononi mwake).
Muungano katika muundo wake wa serikali mbili unaweza tu kusalimika iwapo matatizo yanayoukabili yatajadiliwa kwa uwazi pasi kuchelea matokeo ya kufanya hivyo. Iwapo kuujadili Muungano kwa uwazi kutasababisha uvunjike-alimradi kwa amani-basi na iwe hivyo. Iwapo kuujadili kwa uwazi kutauimarisha (na hii ndio njia mwafaka) basi tusipoteze muda na tufanye hivyo sasa.
Ni kichekesho kwa chama tawala CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete, kujaribu kuuhadaa umma kuhusu utatuzi wa matatizo ya Muungano ilhali kimsingi kinachofanyika ni ‘kuvuta muda’ (buying time) pasipo jitihada zozote za makusudi kufanyika kuimarisha Muungano huo.
Kama tunataka tuwe na Muungano wenye maana halisi ya muungano basi ni muhimu kwa kila raia wa nchi hizi mbili ajisikie huru awapo upande wowote wa Muungano. Vilio vya Watanzania Bara kwamba wanapokuwa Zanzibar wanajiona kama ‘raia wa kigeni’ visipuuzwe, kwa sababu ni vitu kama hivi vinavyoweza kuzua ‘muundo wa lazima’ wa Muungano pasi kujali vitisho vya watawala.
Nihitimishe makala hii kwa kukumbushia kwamba muundo wa Muungano ni kimoja tu kati ya vipengele vingi vilivyomo kwenye Rasimu ya Katiba mpya. Ni muhimu pia kutambua kuwa matatizo ya msingi yanayoikabili nchi yetu- kwa mfano umasikini wa kupindukia na ufisadi unaoshamiri kwa kasi- hayatokani na muundo wa Muungano wa serikali mbili na pengine hata muundo wa Muungano wa serikali tatu hauwezi kuyatatua.
Wakati Watanzania wakitafakari na kujadili hotuba ya Rais Kikwete, baadhi ya magazeti mwanzoni mwa wiki hii yaliripoti taarifa za kigogo mmoja wa Ikulu kufanya jitihada ya kumtoa rumande mmoja wa wafanyabiashara watuhumiwa wakubwa wa madawa ya kulevya anayeshikiliwa na polisi huko Lindi. Je muundo wa Muungano unashughulikia vipi uhuni wa aina hii?
Masuala kama utawala bora, haki za makundi ‘ya wanyonge’ (vulnerable groups), haki za huduma muhimu kama afya, elimu, nishati, na habari yana umuhimu mkubwa pengine zaidi ya aina ya Muungano tunaotaka.
Ndiyo maana nimeeleza hapo juu kwamba la muhimu zaidi kwangu ni function(s) na si form(s) za serikali kama taasisi inayoongoza nchi.
Kuwa na serikali mbili, au serikali tatu, au serikali moja kuna faida tu kwa mwananchi kama kunamwezesha kujipatia mahitaji yake muhimu kwa haki na kumfanya ajione ‘mdau halisi’ wa nchi husika. Vinginevyo, badala ya serikali 2, 3 au 1, kwa mwananchi huyo asiye na uhakika wa mlo wake ujao na ambaye ustawi wake unatarajia kudra za Mwenyezi Mungu, anachoona ni kama kuna serikali 0.

Thursday, March 13, 2014

Makala yangu RAIA MWEMA 12.03.14: "Katiba bora au bora Katiba: Mpira mezani kwa Kikwete"

NIMEKUTANA na habari ya kushtua inayohusu jaribio la kumdhuru mkuu wa zamani wa Majeshi ya Rwanda, Jenerali Faustine Kayumba Nyamwasa anayeishi kama mkimbizi Afrika Kusini.
Habari hiyo ilieleza kuwa watu sita wametiwa nguvuni wakituhumiwa kuhusika na jaribio hilo, na watatu kati yao ni Watanzania. Nikabaki ninajiuliza, “baada ya Tanzania yetu kuchafuliwa na habari za       Watanzania wanaosafirisha madawa ya kulevya, sasa tumehamia kwenye ku-export (kusafirisha nje) wauaji (assassins)”
Baadaye nikajaribu kuamsha mjadala kuhusu suala hilo katika mtandao mmoja wa jamii (social media), na baadhi ya walioshiriki mjadala huo walionyesha wasiwasi wao iwapo watu hao watatu waliokamatwa ni Watanzania kweli au walikuwa wakitumia tu hati za kusafiria za Tanzania.
Pengine ni mapema mno kufahamu ukweli halisi wa suala hili hasa kwa vile uchunguzi bado unaendelea, lakini kimsingi habari hiyo ni mwendelezo wa ‘sifa zisizopendeza’ zinazoiandama nchi yetu.
Nimewahi kueleza katika makala zangu mbalimbali kuhusu tabia niliyojijengea ya kuanza siku yangu kwa kupitia mitandao mbalimbali ya huko nyumbani ili kufahamu kinachoendelea. Na mara baada ya kumaliza kusoma habari hiyo inayomhusu Jenerali Nyamwasa, rafiki wa zamani wa Rais wa Rwanda Paul Kagame aliyegeuka kuwa mmoja wa mahasimu wake wakubwa, nikakumbana na ‘filamu mbaya’ inayozidi kutawala vichwa vya habari, kuhusu maendeleo ya kikao cha Bunge la Katiba.
Ninaiita filamu mbaya kwa sababu japo vikao vya Bunge letu vimekuwa mahiri zaidi kwa vituko kuliko kuzungumzia masuala lukuki yanayomhusu Mtanzania, kinachoonekana ni kama Bunge la Katiba linajaribu kuchuana na ‘Bunge la kawaida’ kwa vituko.
Na pengine bila kuumauma maneno ni vema nikitanabahisha kuwa kama ilivyo katika vikao vya ‘Bunge la kawaida,’ chanzo kikubwa cha mambo yote ya kukera yanayojitokeza katika Bunge la Katiba ni kasumba ya chama tawala CCM kutanguliza maslahi ya kiitikadi mbele ya maslahi ya Taifa.
Baada ya kumalizika ‘kinyemela’ kwa mjadala mkali kuhusu posho ya wajumbe wa Bunge hilo la Katiba (madai yalikuwa kwamba kiwango cha posho cha shilingi 300,000 kwa siku hakitoshi), suala ‘jipya’ linalotishia hatma ya Bunge hilo ni kuhusu utaratibu wa kupiga kura- iwe siri au ya wazi.
Binafsi ninaunga mkono hoja ya kura ya siri kwa sababu moja ya msingi- katika mazingira ya siasa za vitisho na ubabe, namna pekee mpigakura anaweza kuwa huru kutumia haki yake ya kupiga kura ni kwa kupiga kura ya siri.
Na utaratibu wa kura ya siri umekuwa ukitumika katika ngazi mbalimbali, ndani na nje ya anga za kisiasa. Tunapochagua viranja-iwe shule ya msingi au sekondari, na tunapochagua viongozi vyuoni, kura hupigwa kwa siri. Kisiasa, chaguzi katika takriban ngazi zote-iwe ni udiwani au urais, kura hupigwa kwa siri. Sasa kwanini kwenye suala muhimu la Katiba mpya kura iwe ya wazi?
Nimeeleza kuwa chanzo cha tatizo ni CCM. Na sababu kubwa kwa chama hicho kuwa chanzo cha tatizo ni kasumba iliyozoeleka ndani ya chama hicho tawala kubinafsisha kila suala linalomhusu Mtanzania. Baada ya kuanzishwa mchakato wa kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba, CCM ikabinafsisha zoezi hilo na kutengeneza ‘rasimu mbadala’ ambayo kwa bahati nzuri ‘ilivuja’ na umma ukapata nafasi ya kutambua hila mbaya za chama hicho.
Kwa CCM, Katiba mpya inapaswa kupatikana kulingana na matakwa ya chama hicho. Na ili matakwa hayo yatimie, ni lazima nguvu, vitisho na hujuma vitumike kuhakikisha kuwa kila mjumbe kutoka chama hicho anatekeleza msimamo utakaolinda matakwa hayo, iwe ni kwa manufaa ya Mtanzania au la. Kuwa na msimamo wa pamoja si vibaya lakini ni muhimu msimamo huo uzingatie matakwa ya wengi.
Lakini kuilaumu CCM kana kwamba ni familia ya mtu mmoja ni kutoitendea haki. Hizo taarifa kwamba kuna baadhi ya wajumbe kutoka chama hicho wamedhamiria kupigania haki zao za kupiga kura kwa utashi wao na si kwa kushinikizwa na ‘msimamo wa pamoja,’ ni ishara tosha kuwa miongoni mwa wana-CCM kuna wanaotaka kuona demokrasia ikizingatiwa sambamba na haki ya kikatiba ya kufanya maamuzi pasipo kuingiliwa na mtu mwingine ilimradi kufanya hivyo hakuvunji sheria za nchi.
Kwa hiyo tunaweza kuilaumu CCM kwa umoja wake lakini ndani yake kuna wenye mtizamo wa kitaifa badala ya kiitikadi.
Lakini kama kuna mtu anayepeswa kubebeshwa lawama zote basi ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, ambaye kwa hakika ni kama anapelekeshwa tu  na wanaoitwa ‘wahafidhina’ ndani ya chama hicho.
Tangu mwanzo wa mchakato wa kupata Katiba mpya, Rais Kikwete ameonyesha kuyumba kimsimamo, ambapo mara kadhaa anapozungumzza kama Rais ameonyesha kutambua umuhimu wa zoezi hilo la upatikanaji wa Katiba mpya lilizingatie matakwa ya Watanzania wote pasi kujali tofauti zao za kiitikadi, lakini anapozungumza kama kiongozi mkuu wa CCM anaonekana kutaka kuwaridhisha wahafidhina wanaotamani kuona Katiba mpya ikizingatia matakwa yao binafsi.
Hili limezungumzwa mara nyingi (na kukanushwa mara nyingi pia) kwamba tatizo kubwa linaloathiri utendaji kazi wa serikali ya Rais Kikwete ni ombwe la uongozi. Yeye kama Mkuu wa nchi na Mwenyekiti wa chama tawala akiamua kuwa “ninataka tupate Katiba mpya itakayozingatia matakwa ya Watanzania wote” na itakuwa hivyo.
Lakini hilo haliwezekani kwa sababu upande mmoja, Kikwete anataka kuweka historia nzuri ya kuwaletea Watanzania Katiba mpya inayokidhi matakwa yao, lakini kwa upande mwingine anataka kuwafurahisha wana-CCM wenzie wanaotaka Katiba mpya itokane na matakwa ya chama hicho.
Kama nilivyomuusia katika makala yangu moja ya hivi karibuni, ni muhimu kwa Rais Kikwete kuangalia kalenda na kuhesabu siku zilizobaki kabla hajastaafu. Muda mfupi baada ya kustaafu atakuwa mwananchi wa kawaida tu, na asipokuwa makini, mara baada ya kustaafu anaweza kuandamwa kutokana na maamuzi mabaya yaliyofanyika wakati wa utawala wake.
Ndiyo, Mwalimu Nyerere, na marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa walishiriki kufanya baadhi ya maamuzi ambayo pengine hayakuzingatia maslahi ya Watanzania wote kwa ujumla- kwa kutanguliza maslahi ya chama tawala pekee- lakini zama za Nyerere, Mwinyi na Mkapa ni tofauti na tulizo nazo sasa.
Japo Watanzania tunasifika kwa ‘upole’ ambao baadhi ya watu wanautafsiri kama ‘ugoigoi wa kuruhusu mambo yasiyofaa yatokee pasi wahusika kuchelea matokeo,’ kizazi hiki cha Facebook, Twitter na nguvu za mitandao ya kijamii, sambamba na jitihada za kuelimisha umma kuhusu haki zake ni tofauti sana na huko nyuma.
Kwa vile kwa hali ilivyo sasa kikwazo kikubwa ni mtizamo fyongo wa CCM kutaka kubinafsisha mchakato mzima wa kupata Katiba mpya, Rais Kikwete ana nafasi nzuri ya kuingilia kati na kuwaelimisha wana-CCM wenzie kuwa “tuache maji yafuate mkondo.”
Ni muhimu kutambua kuwa matakwa ya CCM kung’ang’ania muundo wa serikali mbili (na hili ndilo linalowaogopesha kuhusu kura ya siri) hayawezi kuua dhamira ya wanaotaka Muungano wa serikali Tatu.
Ni lazima Kikwete na CCM wafahamu kuwa moja ya vyanzo vya matatizo ya Muungano ni ‘usiri’ uliotawala katika upatikanaji wa Muungano huo. Usiri huo unathibitishwa na ukweli kwamba wajumbe wa Bunge la Katiba watajadili muundo wa Muungano huo bila kupatiwa ‘Articles of the Union’ (aidha kwa vile nyaraka hiyo haipo au kama ipo, basi ikiwekwa hadharani itazua sokomoko kubwa). Kwanini Turejee makosa hayohayo yanayoufanya Muungano wetu kuwa moja ya kero kubwa za siasa za Tanzania yetu?
Nimalizie makala hii kwa kuueleza bayana kuwa nimeanza kujiandaa kisaikolojia kuona Bunge la Katiba likitafuna mabilioni ya fedha za walalahoi wa Kitanzania na kuishia kuwa kumbukumbu mbaya tu ya vioja, vituko na kila jambo linalozifanya siasa zetu kuonekana za kibabaishaji.
Kama CCM haitoacha ‘uhuni’ wake, na kwa hakika kama Rais Kikwete hatoingilia kati kuhakikisha Katiba mpya yenye kujali maslahi ya Watanzania wote inapatikana, basi labda tutakachoishia kuambulia ni Katiba mpya kwa jina lakini fyongo na isiyo na manufaa kwa Mtanzania.
Mpira upo mezani kwa Rais Kikwete: akitaka asimamie maslahi ya Watanzania bila kujali tofauti ya itikadi zao za kisiasa, tutapata Katiba mpya ya kweli. Aking’ang’ania kutaka kuwaridhisha ‘wahafidhina’ ndani ya CCM, Katiba mpya itabaki kuwa kitendawili.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/katiba-bora-au-bora-katiba-mpira-mezani-kwa-kikwete#sthash.1H7l4BPB.dpuf

Friday, March 07, 2014

Makala yangu Ktk RAIA MWEMA Toleo la 05.03.14: "USHOGA: Haramu Isikwaze Halali,Halali na Isikwaze Haramu"

MWISHONI mwa wiki iliyopita kulijitokeza malumbano makali, hususan katika mtandao wa kijamii wa Twitter, kuhusu suala la ushoga.
Sina hakika mjadala huo ulianza vipi lakini ninadhani kwa upande mmoja ulichochewa na sakata linaloendelea kati ya serikali ya Uganda na baadhi ya nchi za Magharibi baada ya Rais wa nchi hiyo, Yoweri Museveni, kusaini muswada unaopiga marufuku ushoga kuwa sheria inayoambatana na adhabu kali. Kwa upande mwingine, nahisi mjadala huo ulichangiwa na majadiliano yanayoendelea katika Bunge la Katiba huko Dodoma, ambapo suala la haki za mashoga limejichomoza.
Kwa upande wa Bunge la Katiba, kuna tuhuma kuwa ‘ajenda ya ushoga’ imeletwa makusudi kwa minajili ya kuepesha (divert) mtizamo wa Watanzania katika ‘masuala ya msingi zaidi’ yanayopaswa kujadiliwa katika Bunge hilo maalumu.
Lakini pengine kabla sijaingia kiundani katika mada hii ni vema nikaweka bayana msimamo wangu kuhusu suala hili la ushoga. Huko nyuma niliwahi kuandika makala iliyozungumzia mjadala wa ushoga, makala iliyobeba kichwa cha habari “Tatizo ni unafiki wetu, sio ushoga.”
Hoja kubwa ya ‘wapinzani wa haki za mashoga’ ni kwamba suala hilo haliendani na mila na desturi zetu. Lakini kabla ya kwenda mbali, hivi hizo mila na desturi zetu ni zipi hasa? Mara kadhaa tumekuwa tukiwalaumu ‘wazungu’ kwa kuiangalia au kuizungumzia Afrika kana kwamba ni kijiji kimoja kikubwa kinachoundwa na familia moja kubwa. Wengi wetu tumekuwa mahiri kuwakumbusha ‘wazungu’ kwamba Afrika ni mkusanyiko wa mataifa zaidi ya 50, na ndani ya mataifa hayo kuna makabila lukuki yenye mila na desturi tofauti.
Sasa tukirejea kwa Tanzania yetu, hivi ‘mila na desturi za Kitanzania’ ni zipi hasa? Naomba ieleweke kwamba sikatai kwamba tuna mila na desturi bali ninapata shida kuelewa hizo ‘mila na desturi za jumla’ zinazofuatwa na kila Mtanzania.
Kuna hoja nyingine inahusu imani za kidini, kwamba “katika dini zote, ushoga ni haramu.” Tunarejea palepale. Kwa sababu dini fulani zinasema kitu hiki ni haramu haina maana basi kila mtu (asiye muumini au hata muumini wa dini hiyo) lazima aafiki mtizamo huo. Tukumbuke kuwa dini ni imani, na imani hailazimishwi. Sasa kwa vile Tanzania yetu si nchi ya kidini, japo wengi wa Watanzania wana dini, kinachotakwa haramu katika dini fulani si sheria inayopaswa kufuatwa na kila Mtanzania.
Maana kama kila matakwa ya dini lazima yafuatwe kama sheria ya nchi, hali itakuwaje katika suala kama la ulaji wa nyama ya nguruwe ambayo ni ruhusa kwa Wakristo lakini ni haramu kwa Waislamu? Tupige marufuku ulaji wa nyama ya nguruwe kwa vile ni haramu kwa Waislamu au turuhusu kwa vile ni halali kwa Wakristo? Usuluhishi unapatikana katika busara za kutambua haki na wajibu: uhalali usikwaze haramu na haramu isikwaze halali.
Wakati mjadala huo wa ushoga unaendelea huko Twitter, muungwana moja alinihoji iwapo msimamo wangu kuhusu haki za mashoga unatokana na uwepo wangu huku Uingereza. Nikamjibu kuwa mie ni muumini wa haki za binadamu, na haki hizo ni pamoja na za mashoga.
Mwingine akaenda mbali na kuhoji iwapo nami ni shoga eti kwa sababu ninawatetea sana. Nilimuuliza, hivi tunavyopambana dhidi ya ujangili na kupigania haki za uhai wa tembo wetu, kwa mfano, basi nasi ni tembo?  Kuna vijana wanaopigania haki za wazee, wasio na ulemavu wanaopigania haki za walemavu, na wanaume wanaopigania haki za wanawake. Ni suala la imani.
Ninaendelea kuamini kuwa kwa mtu ambaye si shoga, sioni kwanini asumbuliwe na haki za mashoga. Ni haki za mashoga, sio za wewe usiye shoga. Kwanini basi zikusumbue? Oh dini yako inakataza. Sawa, lakini dini fulani inakataza kula nguruwe lakini yako inaruhusu. Oh mila na desturi zinakataza, vipi kwa asiyehusika na mila na desturi hizo?
Waingereza wana msemo ‘two wrongs don’t make a right’ ambao kwa tafsiri isiyo rasmi ni unamaanisha ‘kwa vile kosa la kwanza limeachwa kama si kosa, haimaanishi kosa la pili nalo liachwe pia.’  Msemo huu unatumika sana dhidi ya wanaohoji “kwanini hizo mila na desturi zikumbukwe kwenye suala la ushoga pekee na sio dhidi ya ufisadi, biashara ya dawa za kulevya, ukahaba na mengine kama hayo?”
Wapinzani wa haki za mashoga wanadai “kwa vile hatutilii mkazo kuhusu imani za dini zetu na mila na desturi zetu kupambana na maovu mbalimbali katika jamii, haimaanishi tusikemee ushoga.” Sawa, lakini haki za mashoga zinachangia vipi uwepo wa mgawo wa umeme usiokwisha? Au mashoga wanachangiaje kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya? Na ni kwa vipi mashoga wanahusika na kuzaliana kwa kasi kwa matapeli wa kisiasa katika mfumo wa siasa wa nchi yetu?
Ninatambua kuwa msimamo wangu katika suala hili sio popular (unaoafikiwa na wengi). Ninatambua pia kuwa kuna wasomaji watakaoniona mtu wa ajabu kabisa kwa kutetea haki za mashoga. Ninahisi pia kuna watakaodhani kuwa labda ‘nimechanganyikiwa.’ Sina tatizo na mtizamo huo kwa sababu ni matumizi ya haki na uhuru wao. Na ndio moja ya faida kubwa za haki na uhuru: kufanya hata kile ambacho mtu mwingine hakiafiki. Sasa, kama sio tu tunapenda haki na uhuru, kwanini tuchukie vitu hivyo hivyo kwa wenzetu?
Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuhusu ukweli huu ambao pengine ni mchungu kwa wapinzani wa haki za mashoga: Sio tu kwamba Tanzania yetu ina mashoga bali pia kasi ya kukua kwa ushoga ni kubwa. Na hata miongoni mwa wapinzani wa ushoga kuna mashoga pia lakini wanaotumia fursa hiyo ya kupinga ushoga kwa minajili ya kuficha ‘siri’ yao. Tunaweza kuendelea kudai ‘ushoga ni haramu...mila na desturi zetu zinapinga ushoga...” lakini hiyo haiondoi ukweli kuwa ushoga upo na mashoga wapo.
Wito wangu kwa ‘wapinzani’ wa ushoga sio wabadili mtizamo wao bali kama kweli wanaoongozwa na dini au mila na desturi kupinga ‘laana’ ya ushoga, basi ni vema pia wakielekeza hasira zao dhidi ya majanga ya kitaifa kama vile ufisadi na biashara ya madawa ya kulevya, sambamba na usaliti katika uhusiano au ndoa (suala maarufu la ‘nyumba ndogo’ na ‘mambo mengine yasiyofaa.’

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/uhalali-usikwaze-haramu-na-haramu-isikwaze-halali#sthash.tuSqf3kJ.dpuf

Friday, February 28, 2014

Makala yangu ktk RAIA MWEMA Toleo la 26.02.14: "Anayeona Posho ni ndogo ajitoe"

HUYU naye vipi? Mhasibu mzima anapenda basi la wafanyakazi! Hana japo pikipiki na bado anaishi nyumba ya kupanga. Ama kweli kwenye miti hakuna wajenzi...”.  Hii ilikuwa kauli ya mfanyakazi mwenzangu wakati nilipokuwa mwajiriwa wa taasisi moja ya umma huko nyumbani.
Mhasibu aliyekuwa akiongelewa ni kijana mmoja ambaye baada ya kuhitimu masomo Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na kurejea kazini alipandishwa cheo katika idara ya uhasibu katika taasisi hiyo. Yayumkinika kuhitimisha kuwa miezi kadhaa ya mwanzo baada ya kuwa mhasibu, kijana huyo aliandamwa sana na wengi wa wafanyakazi wenzake, ‘kosa’ lake pekee likiwa ‘kuishia maisha ya kawaida kulingana na kipato chake.’
Tofauti na kijana huyo, katika taasisi hiyo kulikuwa na jamaa mmoja ambaye japo hakuwa mhasibu kitaaluma, ndiye aliyekuwa na jukumu la usimamizi wa fungu la fedha kwa ajili ya matumizi ya mkurugenzi mkuu wa taasisi hiyo, hususan safari za nje ya nchi. Sehemu kubwa ya fedha alizokuwa akisimamia ndugu huyo zilikuwa za kigeni.
Huyu bwana alikuwa na uwezo mkubwa mno kifedha japo mshahara wake ulikuwa wa ‘kawaida’ tu. Alikuwa na misururu ya magari ya thamani huku ikidaiwa kuwa alikuwa na idadi kubwa ya nyumba jijini Dar es Salaam. Mfanyakazi huyu alikuwa akinyenyekewa hata na baadhi ya mabosi wake.
Baada ya muda, inaelekea huyo mhasibu kijana alizidiwa na kebehi dhidi yake, na akaanza ‘kuishi kihasibu,’ na taarifa zilizopatikana zilionyesha kuwa alianza kununua nyumba, magari na hata matumizi yake yalibadilika yakawa makubwa. Na sifa zikaanza kumiminika kwake, na kama ilivyokuwa kwa yule ‘mhasibu’ wa mkurugenzi mkuu, naye akaanza kunyenyekewa.
Ninakumbuka kuhusu ‘kituko’ hiki kwa vile kilitokea mbele ya macho yangu katika taasisi niliyokuwa nimeajiriwa. Lakini kimsingi hali hiyo ilikuwa kama ya kawaida kwenye taasisi nyingi tu, za umma na za binafsi.
Huo ndio ‘ukweli mchungu’ kuhusu Tanzania yetu. Mhasibu atakayeishi kulingana na kipato chake (na mishahara ya wahasibu wengi ni ya kawaida kwa vile uhasibu si ‘fani adimu’- rare profession- kama urubani yenye mshahara mkubwa.
Huko mitaani hali ni mbaya zaidi ambapo wahalifu wanatukuzwa; wauza madawa ya kulevya wamepachikwa ‘uzungu’ na kuitwa ‘wazungu wa unga.’ Wananyenyekewa kama miungu-watu. Kwa hakika Tanzania yetu inaweza kuwa sehemu muafaka ya kuthibitisha ule msemo wa Kiingereza kuwa crime pays (uhalifu unalipa).
Utakutana na mtu ambaye hana shughuli ya kueleweka lakini ana fedha nyingi mno; hajaachiwa urithi mkubwa, hajawahi kushinda bahati nasibu, na kubwa zaidi hana kazi wala biashara ya kueleweka. Uwezekano pekee wa ‘utajiri’ wa mtu huyu ni kujihusisha na uhalifu kwa sababu fedha hazianguki kutoka hewani kiasi cha kuwa na mtu mwenye fedha nyingi lakini hana chanzo cha mapato.
Nikirejea kwenye uzoefu wangu huko nyumbani, kuna wakati niliwahi kufanya kazi na watumishi wa chombo kimoja cha dola (yaani kazi iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya chombo hicho na taasisi niliyokuwa nikiitumikia wakati huo). Hali huko ilikuwa mbaya zaidi ambapo mtendaji aliyechukia rushwa alionekana kama adui wa watendaji wenzie.
Kisingizio kikubwa kilikuwa maslahi madogo na mazingira magumu ya kazi. Nilichojifunza kwao ni kwamba ilikuwa vigumu sana kuwa mzalendo katika chombo hicho cha dola kwa sababu rushwa ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya watumishi wake.
Mara nyingi tumekuwa tukiilaumu serikali na taasisi zake, wanasiasa na watawala wetu kuhusu kuporomoka kwa uadilifu sambamba na kushamiri kwa uhalifu. Lakini pengine mara nyingi zaidi ni nadra kwetu kama wananchi kujiuliza kuhusu nafasi zetu kupambana na au kuchochea kuporomoka huko kwa maadili na kushamiri kwa uhalifu. Ni vigumu kuuchukia uhalifu, kwa mfano, ilhali ndoto zako ni kuishi maisha ya kifahari kama anavyoishi mhalifu fulani.
Ninaambiwa kwamba baadhi ya wahalifu huko nyumbani wamekuwa na nguvu kubwa zaidi ya watawala wetu kiasi kwamba vyombo vya dola vinaogopa kuwagusa wahalifu hao. Na bahati nzuri kwao, baadhi yao wamefanikiwa kujenga ushirikiano na watu wa karibu wa familia za watawala wetu ambao wanatumiwa na wahalifu hao kama kinga dhidi ya hatua za kisheria.
Sasa kama katika hali inayokera na kukatisha tamaa tunaelekea kuruhusu na kuhalalisha upatikanaji kipato kwa njia zisizo halali, na kisha kuwaabudu wahalifu kana kwamba ni miungu-watu na kuwaenzi kwa ‘nyadhifa kama ‘mzungu wa unga’ au ‘pedejee,’ kwanini tunatahayari kusikia taarifa kwamba wajumbe wengi wa Bunge la Katiba wanalalamika kuwa posho ya shilingi 300,000 kwa siku haitoshi?
Hivi katika mazingira ya kawaida tu, tutarajie lipi kwa mjumbe wa Bunge la Katiba aliyeteuliwa na Rais  ‘anapogusana mabega’ (rubbing shoulders) na wajumbe walioingia katika Bunge hilo kama wabunge ‘wa kawaida’ wanaolipwa zaidi ya shilingi milioni 10 kwa mwezi?
Kwamba kama serikali ina uwezo na jeuri ya kulipa mamilioni hayo kwa wabunge zaidi ya 300 kila mwezi kwa miaka mitano, kwanini basi nao wasidai japo ‘kipande kiduchu cha keki hiyo ya taifa’?
Naomba ieleweke bayana kwamba si kuwa ninaafiki madai ya wajumbe hao wa Bunge la Katiba wanaodai waongezewe posho, bali ninachojaribu kubainisha hapa ni ukweli kwamba kelele za wajumbe hao zinaakisi hali halisi huko mtaani. Kama ni sahihi kwa wahalifu kuenziwa huko mtaani, kwanini basi ‘waheshimiwa hawa wa muda mfupi’ wasitumie fursa hiyo kujinufaisha?
Nchi yetu imekuwa kama msitu (jungle) ambapo kanuni pekee inayotawala ni ubabe: kula au uliwe. Na katika mazingira ya namna hiyo ni vigumu kweli kwa uzalendo au wazalendo kusalimika. Ndiyo maana niliposikia jina la mwanadada mzalendo, Maria Sarungi, kuwa miongoni mwa wajumbe walioteuliwa kuwa wajumbe wa Bunge la Katiba nilitamani kungekuwa na angalau makumi kadhaa ya watu kama yeye.
Simsifii bali mwanadada huyu amekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya mtandaoni inayoitwa 'Badili Tanzania' (Change Tanzania), ambayo kimsingi inahimiza mabadiliko ya kifikra, kitabia na vitendo kwa jamii badala ya kutilia maanani kuwategemea wanasiasa au taasisi za kisiasa kuleta mabadiliko chanya kwa nchi yetu.
Ikumbukwe kuwa kati ya mafanikio makubwa ya kampeni ya Change Tanzania ni kupinga ongezeko la kodi kwa kadi za simu (SIM card tax) ambapo hatimaye ilifutwa baada ya kilio cha umma kupitia kampeni hiyo kusikika kwa watawala.
Alipotajwa kuwa mmoja wa wajumbe wa Bunge la Katiba sikumpongeza, na hadi leo sijatoa pongezi zangu kwake. Sababu kubwa ya kuhifadhi pongezi zangu ni kwamba yeye ni mithili ya mwanasoka bora ambaye kwa hakika ni lazima achaguliwe katika timu ya taifa. Na tunapoongelea soka, kuna mfano mzuri hapa: mwanasoka Mtaliano Mweusi, Mario Balotelli, aliwahi kunukuliwa akisema kwamba anapofunga bao huwa hashangilii kwa sababu hiyo ni kazi yake. Na akasema ‘umeona wapi msambazaji barua wa posta anashangilia anapofikisha barua kwa mhusika? Huwezi kumshangilia kutimiza jukumu lake.”
Bunge la Katiba lilipaswa kuundwa na wazalendo wanaofikiria hatma ya taifa letu na si ‘nani atalipwa ada ya mwanangu wakati ninashughulikia mchakato wa Katiba mpya’ au wanaodhani posho ya ujumbe wa Bunge la Katiba ni fursa ya kuwabadilishia maisha yao (iwe kuwaongezea fedha au kuongeza idadi ya nyumba ndogo).
Tumeruhusu ‘uhuni’ katika shughuli hiyo muhimu kwa hatma ya taifa letu, na ndiyo maana tunashuhudia mtu kama Emmanuel Makaidi akigeuza mchakato wa kupata Katiba mpya kuwa fursa ya kiuchumi kwa familia yake kwa kumteua mke wake kuwa mjumbe mwenza katika Bunge hilo.
Bunge la Katiba lilihitaji akina Maria Sarungi wengi, yaani watu ambao historia ‘inawapendelea’ (kwa maana kwamba kuna mifano hai ya uchungu wao kwa Watanzania wenzao)’.  Bunge hilo halikustahili kuwa fursa kwa wababaishaji wanaodai eti waongezewe posho kwa vile wameambatana na wanasheria wa kuwashauri wakati wa mjadala wa Katiba mpya.
Kwa vile uteuzi wa wajumbe wa Bunge hilo haukufanywa kwa mtutu wa bunduki kuwa ‘lazima uwe mjumbe hata kama posho haitoshi’ ni vema kwa wanaodhani posho haitoshi wakajiuzulu na kurejea makwao.
Nimalizie makala hii kwa kuwaasa Watanzania wenzangu kujiandaa kisaikolojia kupokea Katiba mpya ‘fyongo au ‘bomu’ kwa sababu wengi wa wanaotuwakilisha katika mchakato wa kupata Katiba hiyo wapo huko Dodoma kwa maslahi yao binafsi. Yayumkinika kuhisi kwamba mjadala wa Katiba huo utakuwa mrefu, si kwa minajili ya kupata muafaka wenye maslahi kwa taifa bali ukweli kwamba urefu wa mjadala utamaanisha urefu wa posho pia.
Ningetamani sana kuhitimisha makala hii na ‘pendekezo la maana’ lakini nafsi inanisuta: ukipanda upupu shambani kamwe usitarajie kuvuna maharagwe.' Kinachojiri katika Bunge la Katiba Dodoma kinaakisi kinachojiri katika maisha yetu ya kila siku mtaani, na tusipoamua kwa dhati kubadili mtizamo wetu dhidi ya ‘wazungu wa unga’ na ‘mapedejee’ basi tusitarajie miujiza kwa watu wanaoteuliwa katika ‘nafasi za ulaji’ kama ujumbe wa Bunge la Katiba.


Thursday, February 20, 2014

Makala yangu RAIA MWEMA Toleo la 19.02.14: "Amri Hii ya Kikwete (CCM Iache Unyonge) Yaweza kumwandama ataporudi Uraiani"

KABLA ya kuanza kuandika makala hii nilikutana na habari moja mtandaoni iliyonifanya nijiulize  iwapo Rais Jakaya Kikwete anapata muda wa kuangalia kalenda kufahamu muda uliobaki kabla hajamaliza muhula wake wa pili na wa mwisho wa Urais.
Habari hiyo ilihusu hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa mjini Dodoma kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ambapo aliwataka wanachama wa chama hicho kuacha unyonge na kusema uvumilivu una kikomo chake.
Tunashindana na wenzetu wagomvi, maana wao ugomvi ndiyo sehemu ya mwongozo wa kufanya kazi ya siasa...Tulizungumza nalo hilo kwenye Kamati Kuu, tulikubaliana kuacha unyonge. Ndiyo, kwenye Kamati Kuu tumekubaliana, tumesema jamani watu wote waende wakaseme tumekubaliana kuacha unyonge,” alinukuliwa Kikwete ambaye licha ya kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.
Kwa kifupi, Rais Kikwete ametoa ruhusa kwa wana-CCM kukabiliana na alichokiita tabia ya ugomvi ya vyama vya upinzani. Kwamba wana-CCM wachukue sheria mkononi pindi wakihisi wanafanyiwa ugomvi na wapinzani. Kwa lugha nyingine, jukumu la ulinzi na usalama katika shughuli zinazokihusu chama hicho zimeporwa kutoka vyombo vya dola na kukabidhiwa kwa wanachama wa chama hicho tawala.
Kwa tafsiri pana, iwapo wana-CCM ‘wataacha unyonge’ na kufanya mashambulizi ya kujihami dhidi ya wapinzani (yaani hata kama wapinzani hawajafanya ‘ugomvi’ wowote) bado watakuwa na ‘haki’ kutokana na ruhusa hiyo waliyopewa na Rais Kikwete.
Kadhalika, vyombo vya dola vitakuwa na wakati mgumu kuchukua hatua dhidi ya wana-CCM watakaowashambulia wapinzani kwa sababu amri ya kufanya mashambulizi hayo ina baraka za Rais ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu.
Hivi kweli Rais Kikwete hatambui kuwa amebakiwa na takriban miezi 20 tu kabla ya kuwa ‘raia wa kawaida tu’ ambaye anaweza kuwa miongoni mwa wahanga wa ruhusa hiyo ya vurugu aliyowapa wana-CCM wenzake?
Na hata kama angekuwa amebakiwa na miaka mingine mitano katika Urais, haihitaji busara kutambua kuwa ni rahisi kuruhusu uvunjifu wa sheria kuliko kuzuwia. Ni rahisi kwa Rais Kikwete ‘kuwapa rungu’ wana-CCM kupambana na wapinzani lakini ni vigumu mno kuwazuwia kutotumia ruhusa hiyo.
Binafsi ninadhani kinachomsumbua Rais Kikwete ni ‘kofia mbili za uongozi katika Taifa,’ yaani Urais na Uenyekiti wa Taifa wa CCM. Na suala hili la ‘unyonge wa wana-CCM’ si pekee linaloonyesha jinsi ‘kofia mbili’ zinavyomtesa Rais Kikwete.
Angalia suala la Katiba Mpya: anapozungumza nje ya hadhara za ki-CCM, Rais anaonekana kuwa na dhamira ya dhati kuona Katiba mpya inapatikana kulingana na matakwa ya Watanzania wote.
Lakini ukisikiliza hotuba zake mbele ya wana-CCM wenzake, inakuwa mwendelezo uleule wa kuweka mbele itikadi za kisiasa hata pale inapohitaji kutanguliza maslahi ya Taifa.
Kimsingi ‘kofia mbili’ hazipaswi kuwa tatizo iwapo kasumba ya kuweka mbele siasa katika kila jambo itaepukwa. Rais anaweza kabisa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria pasipo hofu ya kuathiri nafasi yake kama Mwenyekiti wa Taifa wa chama anachoongoza.
Na kwa kumrahisishia kazi, CCM inafahamika kwa ‘mshikamano’ wake, na ni dhahiri kuwa Rais ana nafasi kubwa ya kuungwa mkono na chama chake katika uongozi wake, na wakati huohuo Rais imara anatengeneza mazingira ya uenyekiti imara ndani ya CCM hivyo kuondoa uwezekano wa upinzani ndani ya chama.
Sitaki kabisa kudhani kuwa baada ya ruhusa hiyo kwa wana-CCM wenzake kuacha unyonge, Rais Kikwete atahamia kwa Watanzania na kuwaruhusu kuacha unyonge dhidi ya mafisadi, wafanyabiashara ya madawa ya kulevya na  majangili.
Lakini hata asipotoa ruhusa ya aina hiyo, uamuzi wake wa kuwakabidhi wana-CCM majukumu ya vyombo vya dola unaweza kuvuka mipaka ya kisiasa (yaani CCM dhidi ya wapinzani) na kuchukua sura ya kitaifa, kwani wahanga wa ufisadi, madawa ya kulevya, ujangili, nk ni Watanzania wote pamoja na hao wana-CCM.
Ruhusa hiyo ya Rais Kikwete kwa wana-CCM kuacha unyonge na kukabiliana na wapinzani si tu ni fyongo lakini pia imekuja wakati mbaya. Macho  na masikio ya Watanzania wote yameelekezwa Dodoma kufuatilia Bunge la Katiba ambalo limeanza kukiwa na matarajio Katiba mpya itaimarisha umoja na upendo miongoni mwa Watanzania.
Na kwa upande mwingine, kauli hiyo ya Rais Kikwete inaturejesha kwenye suala nililozungumzia katika makala yangu ya wiki iliyopita nikieleza kuwa tatizo kubwa la Katiba tuliyonayo na zilizotangulia huko nyuma ni utekelezaji wake.
Ni wazi kuwa Rais Kikwete anafahamu kwamba wenye jukumu la kukabiliana na ‘wagomvi’ wa CCM si wana-CCM bali vyombo vya dola. Huo ndio utawala wa sheria kwa mujibu wa Katiba. Inapotokea matamshi yetu yakaonyesha kuwa kuna ruhusa kwa wananchi kupora wajibu wa vyombo vya dola katika kulinda amani na usalama, tutarajie nini kutoka kwa mwananchi wa kawaida?
Kutarajia kwamba Rais Kikwete atabadili kauli yake ya ‘ruhusa kwa wana-CCM kuacha unyonge dhidi ya tabia ya ugomvi wa wapinzani wa chama hicho’ ni sawa na kutarajia ujangili utakwisha kwa vile Rais amedai serikali inawafahamu vigogo 40 wanaoendesha biashara hiyo haramu. Labda kinachoweza kutokea ni ‘kucheza na maneno’ na kuwalaumu waandishi wa habari kuwa “walinukuu vibaya.”
Nimalizie makala hii kwa kumkumbusha Rais Kikwete kuwa bado ana nafasi nzuri ya kujitengenezea mazingira mazuri ya ‘kustaafu kwa amani’ pindi atapomaliza muhula wake wa Urais mwakani.
Kuruhusu wana-CCM wachukue sheria mkononi dhidi ya ugomvi kutoka kwa vyama vya upinzani ni kuruhusu uvunjifu wa sheria.

- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/amri-hii-yaweza-kumfuata-kikwete-uraiani#sthash.9f8lBlwU.dpuf

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India