Featured Posts

Showing posts with label UFISADI. Show all posts
Showing posts with label UFISADI. Show all posts

Thursday, June 12, 2014

Habari na picha: Huku nchi ikiwa taabani kifedha, angalia matumizi haya ya vigogo wa juu CCM

Wakati taarifa zinatanabaisha kuwa nchi yetu ipo hoi kifedha,

Embedded image permalink

 huku deni la taifa likizidi kupaa, na serikali ikikuna kichwa kutengeneza bajeti ya kueleweka kwa mwaka ujao wa fedha, 

Embedded image permalink
haya ndio matumizi ya viongozi wajuu wa chama Tawala CCM



CHANZO: Jamii Forums

Nakuachia wewe msomaji na kila anayeipenda Tanzania kwa dhati kutoa hukumu hapo mwakani katika uchaguzi mkuu.

Thursday, March 06, 2014

Shamba la Bibi: Utapeli mwingine kama wa Richmond na EPA, mabilioni yachotwa kinyemela BOT

Wakati haijafahamika nani aliyelipwa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa kwenye akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutokana na mvutano baina ya Tanesco na Kampuni ya IPTL, imebainika kuwa Bunge liliwahi kuagiza fedha hizo zisichukuliwe mpaka mitambo ya IPTL itakapokuwa chini ya Tanesco mwakani.
Hiyo imo katika taarifa ya iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2007.
Hata hivyo, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alithibitisha jana kuchotwa kwa Dola za Marekani 122 Milioni (Sh195.2 bilioni) katika akaunti hiyo, lakini akakataa kutaja nani hasa aliyelipwa.
Mkataba wa miaka 20 baina ya IPTL na Tanesco ulisainiwa mwaka 1995 na ulitakiwa kuisha 2015 na mitambo hiyo kuwa mali ya Tanesco.
Hata hivyo, ukiwa umebaki mwaka mmoja kumalizika, imebainika kuwa mitambo hiyo imeuzwa kwa Kampuni ya Pan African Power, ambayo inatarajiwa kuingia mkataba mwingine na Tanesco ili iwauzie umeme.
Ndulu alisema fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Dola za Marekani 22 milioni na Sh161 bilioni za Tanzania ambazo zote kwa pamoja ndizo zilizofikisha jumla ya Sh195.2 bilioni.
Vyanzo vingine vilitoa takwimu mbili tofauti, kimoja kikisema kiasi cha fedha hizo kilifikia Dola za Marekani 270 milioni na kingine Dola 250 milioni. Kuhusu nani mwenye mamlaka ya kutoa fedha hizo, Profesa Ndulu alisema kwa mujibu wa mkataba wa kufunguliwa kwa akaunti ya fedha hizo, ni Wizara ya Nishati na Madini pamoja na IPTL.
“Hakuna mtu mwingine anayeweza kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo zaidi ya hao, kwa hiyo hao ndiyo waliosaini kutolewa kwa hizo fedha na taratibu zote zilifuatwa,” alisema Profesa Ndulu.
Alipoulizwa ni nani aliyelipwa fedha hizo, Profesa Ndulu alisema IPTL ndiyo iliyokuwa na mamlaka ya kusema ni nani alipwe na ilifanya hivyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi alipoulizwa juu ya fedha hizo alisema: “Kwa kawaida huwa nina majibu mafupi sana, lakini kwa kuwa mmeamua kuandika uongo, endeleeni, siwezi kukujibu chochote wasiliana na hao IPTL wakujibu.”
Hata hivyo, haikuwa rahisi kumpata kiongozi wa IPTL kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tayari kampuni hiyo ni mufilisi.
Msimamo wa Bunge
Ripoti ya POAC inasema Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) aliorodhesha matatizo ya mkataba kati ya Tanesco na IPTL na kuangalia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mipango ya kununua mitambo hiyo na kuibadilisha iwe inatumia gesi badala ya mafuta mazito.
“Mgogoro uliopo hivi sasa kati ya Tanesco na IPTL unahusu kiwango cha malipo ya uwekezaji yaani capacity charges ambacho IPTL walikuwa wanalipwa na Tanesco. Kwa mujibu wa mkataba huo, capacity charge inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji wa asilimia 30 na mkopo wa asilimia 22.31.
Baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa, ilikubalika kuwa mtaji uliowekezwa uwe ni Dola za Marekani 36 milioni.
Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa Tanesco iligundulika kuwa IPTL haikuwekeza fedha hizo, bali Sh50,000,” inasema ripoti hiyo.
Ilisema kuwa, mpaka kufikia Mei 2008, Tanesco ilikuwa imeilipa IPTL Sh221 bilioni tangu ilipoanza uzalishaji umeme Januari 2002.
Kamati iliagiza: “Wanasheria wa Tanesco na Serikali watumie ushahidi wote uliopo kuhakikisha kuwa kiwango cha fedha kilichopo kwenye akaunti maalumu (Escrow) ndicho hichohicho kitumike kumaliza madeni yaliyopo na vilevile kufanyia marekebisho mitambo hiyo ili itumie gesi,” inasema taarifa hiyo.
Pendekezo hilo lilipitishwa na Bunge huku POAC ikitoa maelekezo kwa Gavana Ndulu kuwa fedha zilizopo Escrow zisitumike kwa namna yoyote ile bila mitambo ya IPTL kuwa ya umma na kubadilishwa na kutumia gesi asilia.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa POAC, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema ameshtushwa na taarifa za kutolewa kwa fedha hizo kinyemela.
“Tunaitaka Serikali kutoa taarifa kama kweli hizo fedha zimetolewa, kwa sasa siwezi kutoa msimamo wetu kwa kuwa hatujakaa kama kamati, tunatarajia kuitisha kikao cha dharura Dodoma kuzungumzia suala hili,” alisema Zitto.
 CHANZO: Mwananchi

Wednesday, August 28, 2013

NCHI INAUZWA: Mwarabu wa Oman anayedai kuwekeza wa Airport Dar ALISHAINGIA MITINI kuhusu ATCL


Naomba niwe mkweli. Kila nikiskia Mwarabu flani anawekeza sehemu, hisia ya kwanza ni jinsi twiga na wanyama pori wetu wanavyotoroshwa na Waarabu...na sakata la Loliondo lililopelekea kifo cha mwandishi mahiri wa habari za Uchunguzi, Marehemu Stan Katabalo.

Kwa kifupi, picha iko hivi: Mwaka jana Rais Jakaya Kikwete alipokwenda huko Uarabuni, aliwahamasisha wafanyabiashara wa huko kuja kuwekleza Tanzania akidai kuwa nchi yetu ina "fursa zisizo na kikomo" (unlimited opportunities) kwa Waarab hao.

Kufuatia ziara hiyo ya JK na wito wake kwa Waarabu hao, siku chache baadaye (Januari mwaka huu) zikapatikana taarifa kuwa kundi la wafanyabiashara wa Oman likiongozwa na kampuni ya AL-HAYAT DEVELOPMENT AND INVESTMENT COMPANY wanapanga kuwekeza dola za kimarekani milioni 100 kufufua shirka la ndege la Tanzania (ATCL), na memorundum of understanding ikasaniwa kati ya ATCL na bosi wa kampuni hiyo ya Oman Sheikh Salim Al-Harthy

Hata hivyo, mwezi Juni mwaka huu, Naibu wa Mawasiliano na Uchukuzi, Dkt Charles Tizeba, aliliambia Bunge kuwa 'mwekezaji huyo wa Oman ameingia mitini' Kadhalika, Naibu Waziri huyo alieleza kuwa hakukuwa na makubaliano yoyote yaliyosainiwa kati ya 'wawekezaji' hao na ATCL

Cha kushangaza, vyombo mbalimbali vya habari huko nyumbani vimeripoti jana kuwa mtu yuleyule SHEIKH SALIM AL-HARTHY na kampuni ileile ya AL-HAYAT DEVELOPMENT DEVELOPMENT AND INVESTMENT COMPANY inatarajia kuufanyia ukarabati Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar, kwa kutumia uwekezaji wa dola za Kimarekani milioni 100.

Hivi ndugu msomaji, hata tukiweka kando rekodi ya 'wawekezaji' wa Kiarabu katika kuhujumu uchumi wetu, inaingia akilini kweli kwa mtu yuleyule aliyeleta uzushi kuhusu uwekezaji kwenye ATCL, na kisha kuingia mitini, kukabidhiwa dhamana ya kuifanyia ukarabari aiport yetu kuu?

'Mwekezaji' huyo Mwarabu alinukuliwa na gazeti moja akida (nanukuu)

 Nimekuja kuwekeza hapa kwa kuitikia mwito wa Rais Jakaya Kikwete, amechoka sana inabidi sisi tumsaidie, ana nia nzuri ya kuhakikisha nchi hii inakuwa kiuchumi inabidi tumsaidie kuwekeza katika maeneo kama haya” alisema. Katika hatua nyingine mwekezaji huyo ametangaza kuwekeza ndege nane kwenye Shirika la Ndege la Tanzania(ATCL), mradi ambao unatarajiwa kugharimu dola za Marekani 100 milioni.

Tafadhali zinatia maneno hayo ya rangi nyekundu.

Cha kusikitisha zaidi, ni ukweli kwamba hata Waziri pekee anayeonekana kupigania haki za wanyonge, Dkt Harrison Mwakyembe, naye kaingia mkenge kwa kumsapoti Mwarabu huyo, na kunukuliwa akisema kuwa serikali imefanya kazi kubwa ya kuvutia wawekezaji hao...





Thursday, July 18, 2013

Mgeni Njoo Mwenyeji Apone,Obama Njoo, Fisadi Apone: UFISADI WA KUTISHA KWA MGONGO WA ZIARA YA OBAMA



 
Ufisadi ujio wa marais

*Hazina yatumia Shilingi bilioni 8
*‘Wajanja’ watafuna mamilioni
*Vifaa vya Obama vyaokoa jahazi
*Vinyago vyagharimu Sh milioni 30
*Sare, mikoba, vyagharimu mil. 400/-
*Karamu, chupa za kahawa, miavuli mil. 390/-
*Burudani ya muziki yatafuna milioni 195

Na Waandishi Wetu

Mkutano wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue), uliomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, umeigharimu Serikali Sh bilioni nane.

Hata hivyo, mamilioni ya fedha hizo yameishia mikononi mwa watumishi kadhaa wa Serikali kupitia zabuni tata walizotoa kwa kampuni mbalimbali.

Baadhi ya vifaa vilivyoorodheshwa kwenye zabuni hizo, ama havikuwasilishwa, au viliwasilishwa shughuli ikiwa imeshamalizika, na sasa vimetunzwa kwenye maghala. Miongoni mwa vifaa hivyo ni shehena kubwa ya bendera za Tanzania ambazo zimetunzwa katika chumba ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Wahusika wakuu kwenye ulaji huu ni maofisa kadhaa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa waliokuwa waratibu wa ugeni huo. Katibu wa Bodi ya Zabuni katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Onesmo Suka, ni miongoni mwa maofisa wanaokabiliwa na wakati mgumu kueleza mchanganuo wa zabuni ulivyokwenda.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umeonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha cha Sh bilioni nane ni mbali kabisa na kile kilichokusanywa kutoka kampuni na mashirika mbalimbali ya umma.

Imebainika kuwa hadi Juni 5, mwaka huu, fedha taslimu zilizokusanywa ni Sh milioni 170 kutoka kampuni saba. Wachangaji wa kiasi hicho na kiwango kikiwa kwenye mabano ni Kampuni ya Simu ya Tigo (Sh milioni 80), PPF (Sh milioni 20), PSPF (Sh milioni 20) na LAPF (Sh milioni 20). Benki Kuu (BoT) ilitoa Sh milioni 10, Barrick Gold (Sh milioni 15) na Benki ya Azania (Sh milioni 5).

Kampuni tatu zilikubali kutoa vifaa. Vodacom iliamua kuchangia masuala ya ICT, Masasi Foods walitoa maji ya kunywa, ilhali Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) lilitoa fulana na zawadi ndogo ndogo.

Hadi Juni 5, mwaka huu, kampuni tano zilikuwa zikisubiri uamuzi wa Bodi. Kampuni hizo ni Mac Group, CBA Bank, PBZ Bank, Nokia-Siemens na Shirika la Hifadhi la Taifa (NSSF).

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa kampuni nne zilishindwa kuchangia kwa kile kilichoelezwa kwamba ni uwezo wake mdogo kifedha. Kampuni hizo ni TanzaniteOne inayochimba tanzanite Mererani; IBM, Infrotech ba Diamond Trust Bank.

Wafanyabiashara nguli nchini hawakuachwa nyuma kwenye michango hiyo, ingawa taarifa zinasema wapo waliokataa kutoa. Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote, Balozi Ombeni Sefue, aliagiza wafanyabiashara kama Said Bakhresa na Mohamed Dewji wafuatiliwe kwa karibu ili waweze kutoa michango. 

Hata hivyo, aliyekuwa Mkuu wa Sekretarieti ya Smart Partnership Dialogue, Victoria Mwakasege, anasema kwamba baadhi ya wafanyabiashara, wakiwamo kina Dewji, hawakuchangia. Hakutoa sababu za kushindwa kwao. 


Sokomoko la matumizi mabaya ya fedha

Uchunguzi umethibitisha kwamba Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote, hakuridhishwa kabisa na namna zabuni zilivyotolewa.

Kwenye kikao cha mwisho, Sefue, kwa maandishi, alisema ingawa yeye ameshiriki katika Kamati ya Uendeshaji, hakubaliani na bajeti pamoja na mchanganuo wa zabuni ulivyokosa uwazi.

Sefue amenukuliwa akisema ni jambo gumu kwake kukubaliana na ununuzi huo kwa vile hapakuwapo mchanganuo wa kuthibitisha namna mamilioni ya fedha yalivyotengwa kuwalipa wazabuni na bei za vifaa vilivyohitajika.

Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya kikao kilichofanyika Juni 17, vinasema Balozi Sefue, aliweka wazi msimamo wake baada ya kuona taratibu za ununuzi zikiwa zimekiukwa, na kwamba baadhi ya vitu vilivyoorodheshwa, vilikuwa ni “vichekesho”.

“Mimi sitaki nihusishwe na jambo hili, waliolifanya wanapaswa wenyewe wabebe msalaba huu, mchanganuo uletwe ili kuonyesha nini kinanunuliwa kwa kiasi gani badala ya utaratibu huu wa kuorodhesha vitu na kuweka gharama,” alinukuliwa aking’aka Balozi Sefue.

Kampuni zilizopata zabuni

Mmoja wa maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wamesema wazi kwamba fununu za kufanyika kwa mkutano wa Smart Partnership zilipoenea, watu wengi walipigana vikumbo wakitaka wapewe zabuni. 

Kampuni ya Luma International Ltd ilipewa zabuni ya kusambaza vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 391.1 Baadhi ya vitu hivyo ni vipeperushi, bendera za Tanzania (kubwa na ndogo), suti kwa watu wa protoko, sare kwa watu wa mapokezi, mabegi kwa wageni mashuhuri na wageni wa kawaida, na beji.

Kampuni ya Softel Trading Company Limited ilipewa zabuni ya Sh milioni 392.6 kusambaza picha za mapambo ukumbini, miavuli (1,500), chupa za kahawa (800), vikombe vya kahawa (800), kalamu za zawadi (2,000) na vishikio vya funguo (800).

Kampuni hiyo hiyo ilipewa zabuni nyingine ya Sh milioni 48.25 kwa ajili ya kufanya kazi za usanifu kwa kutumia kompyuta na uchapaji wa mabango madogo madogo.

Kana kwamba haitoshi, kampuni hiyo hiyo ya Softel Trading Company Ltd ilipewa zabuni ya thamani ya Sh milioni 254 kwa ajili ya kutengeneza mabango makubwa 40. Wakati mkutano ukiwa unafanyika Dar es Salaam, iliamuriwa kwamba mabango hayo yasambazwe katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Zanzibar.

Kampuni ya Wild Cat Publishing ilishinda zabuni ya Sh 278,409,409,269 kwa ajili ya kuandaa machapisho 1,000 ya mkutano. Yalitakiwa yahusu masuala ya kiasiasa, kiuchumi, fedha, teknolojia, mawasiliano, usafirishaji, kilimo, ujenzi, afya na elimu, utalii, n.k.

Kampuni ya tano iliyoshinda zabuni ni ya Big Mama’s Woodworks ambayo ilipangiwa Sh milioni 29.96 kwa ajili ya kutengeneza zawadi za vinyago 60 yenye urefu wa sentimita 15 na upana wa sentimita 12 kila kimoja. Pia ilitakiwa itengeneze vinyango vinne vyanye urefu wa sentimita 150 na upana wa sentimita 35.

Kwenye masuala ya burudani, kampuni ya Prime Time Promotion ilijipatia zabuni ya Sh milioni 194.7. 

Kwenye orodha ya ugawaji zabuni, kampuni ya True Colour Entertainment Group ilizawadiwa zabuni ya Sh milioni 50 kwa ajili ya kuandaa na kuonyesha jarida. Ingawa haikufafanuliwa, hii yawezekana ndilo lile jarida lililoonyeshwa kwenye Ukumbi Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, siku ya ufunguzi wa Mkutano wa Smart Partnership. Lilihusu wanyamapori na vivutio kadhaa vya utalii vinavyopatikana hapa nchini.

Zabuni ya nane ilitolewa kwa kampuni ya Simply Computers (T) Ltd. Iligharimu Sh milioni 187.478. Ilitakiwa kusambaza kompyuta kubwa mbili, idadi kama hiyo kwa kompyuta za ukubwa wa kati na projekta nne.

Kampuni hiyo hiyo ya Simply ilipata zabuni nyingine yenye thamani ya Sh milioni 210.198 kwa ajili ya kusambaza kompyuta tano za mezani, laptop (5), laptop za sekretarieti na mkutano (14), mobile computing equipment (14), black and white printer (2), colored printer (2), kompyuta za mezani (nyingine 5), colored printer (nyingine 2) na flash disk (32).


Upungufu uliojitokeza

Pamoja na mamilioni hayo kupitishwa kwa ajili ya mkutano huo lakini bado kulikuwa na upungufu mkubwa katika utendaji hususani katika utoaji wa vitambulisho.vitabulisho wa

JAMHURI lilishuhudia baadhi ya wageni wakiwemo mabalozi kutoka katika mbalimbali Askari wa Jeshi la Polisi usalam wa taifa madereva wa Idara mbalimbalia za Serikali wakiendelea kusota kwa ajili ya kupata vitambulisho hivyo .

Kadhia hiyo pia ilimpata Katibu Mkuu Kiongozi, Sefue ambaye alifika katika Ukumbi wa Kalimjee saa nne asubuhi ambapo wafanyakazi wa waliokuwa wakihusika na utoaji wa vitambulisho hawakumjali jambo ambalo liliwasahangaza wengi waliokuwepo hapo. 

Wengi wao walihoji uelewa wa wahudumu hao katika utendaji wao na kama kweli walikuwa hawamjui kiongozi huyo au ilikuwa ni dharau.

Sefue alikaa katika eneo hilo kwa zaidi ya nusu saa na kuondoka katika ukumbi huo huku akiwa hana kitambulisho hadi anaingia ukumbini wa Kimataifa wa Walimu Nyerere. Saa kumi jioni.

Wengine waliofika katika ukumbi huo na kupata kadhia hiyo ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana na mwenzake ambaye JAMHURI hailikufanikiwa kupata jina lake

Dk. Bana na mwenzake walifika na kujitambulisha kwa mmoja wahudumu katika ukumbi huo lakini mhudumu huyo baada ya kutekeleza shida yao, alianza kueleza matatizo yaliyoikumba idara hiyo ya vitambulisho.

“Jamani idara hii ina matatizo kwani hatukuwa tumejipanga kila mtu yuko kivyake ndio maana mnaona huduma imesimama kama mnavyoona hakuna majina hapa, mafaili yako tupu na wahusika hawapo kinachotakiwa ni kufika hapa na kuhakikisha jina lako na pia unakwenda kupiga picha pale lakini hadi sasa hatujapata majina je nyinyi mlijiandisha,” anasema mhudumu huyo. 

Hata hivyo kauli hiyo ilimuudhi, Dk. Bana na mwenzake hivyo alimtaka mhudumu huo kutozungumza upungufu wa idara hiyo mbele ya wageni waliofika katika ukumbi huo, kwani kufanya hivyo ni aibu na haukuwa wakati wake kinachotakiwa kutoa vitambulisho. 

Mhudumu huyo ambaye JAMHURI halikufanikiwa kupata jina leke alionekana kukerwa kauli hiyo aliendelea kuzumgumzia upungufu huo pamoja na Dk. Bana mwenzake kunyamaza. Waliondoka katika eneo hilo kwa miadi ya kurudi baadae.


Viongozi ‘warushiana mpira’

Utata kuhusu uhalali wa fedha zilizotumika kununua vitu hivyo, usiri kwenye utoaji zabuni na upungufu mkubwa uliojitokeza kwenye shughuli nzima ya mkutano huo, ni mambo yanayowasumbua sasa viongozi serikalini.

Wakati Katibu Mkuu Kiongozi akijitoa kwenye sakata hilo na kumsukumia Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule; Haule anasema yeye hahusiki. Badala yake anasema anayepaswa kuulizwa mambo yote yalivyokwenda ni Mkuu wa Sekretarieti ya Smart Partnership Dialogue, Mwakasege.

Kwa upande wake, Mwakasege anaruka kwa kusema Sekretarieti ambayo yeye alikuwa Katibu haikuhusika kwa namna yoyote na masuala ya zabuni. Akasisitiza kwa kusema, “Huyo anasema uniulize mimi (Haule), mwulize yeye. Mimi nilihusika na logistic, sisi tulipeleka mahitaji, kwenye zabuni hatukuhusika kabisa. Kilichofanyika ni sisi kukabidhiwa vitu kulingana na mahitaji. Yeye ndiye mwenye masurufu, ndiye anayejua hesabu zote za wizara.”

CHANZO: Gazeti JAMHURI

Friday, July 05, 2013

Makala yangu Ktk Gazeti la RAIA MWEMA Toleo la Julai 3, 2013: "Tumepoteza fursa kwa Obama"


HATIMAYE Rais Barack Obama amezuru Tanzania. Ukweli kwamba Obama ana asili ya Afrika unafanya ziara yake katika baadhi ya nchi za bara hilo iwe na mvuto wa kipekee.
Lakini pengine tukiweka kando furaha ya kutembelewa na Rais wa kwanza wa Marekani ambaye ni Mmarekani Mweusi, na ukweli kwamba ni tukio kubwa kutembelewa na kiongozi wa taifa hilo lenye nguvu kubwa kabisa duniani, ni muhimu kuangalia masuala mengine ya maana zaidi kuhusiana na ziara hiyo.
Pengine kabla sijaingia kiundani katika mjadala huu nisimulie mkasa mmoja ulionikumba huko kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Jumatatu, mara baada ya Obama kuwasili jijini Dar, nilijikuta nikiingia kwenye ‘vita ya maneno’ na mwandishi wa habari mmoja wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ambaye ni Mtanzania kama mie.
Kilichosababisha vita hiyo ya maneno ni kuchukizwa kwake na tweets zangu ambazo kwa kiasi kikubwa zilielemea kwenye kuangalia masuala mazito zaidi ya ziara hiyo badala ya mashamushamu yaliyoambatana nayo. Kwa mfano, nilijaribu kuamsha udadisi kuhusu namna Mtanzania wa kawaida atakavyonufaika na ziara hiyo.
Kadhalika nili-retweet tweets mbalimbali za watu mbalimbali waliokuwa wakiiangalia ziara ya Obama kwa mtazamo tofauti; hususan katika masuala ya haki za binadamu, rushwa, nk. Hilo halikumpendeza muungwana huyo, na akanishambulia vikali huku akinituhumu kuwa sina uzalendo na ‘ninatumiwa na wazungu’ (japo naye ni mwajiriwa wa shirika la wazungu).
Vyovyote vile; hatimaye niliamua kumpuuza tu kwani licha ya yeye kuwa mwanahabari (ambaye kimsingi angepaswa kuthamini uhuru wangu wa kujieleza), alionekana kama anakandamiza haki yangu ya kikatiba kutoa mawazo alimradi hayamkashifu au kumtusi mtu.
Kituko hicho ni moja tu ya vilivyoambatana na ziara ya Obama. Juzi, siku kiongozi huyo alipowasili Tanzania, angalau magazeti mawili makubwa ya Marekani - The New York Times na USA Today, yalikuwa na habari nzito kuhusu Tanzania.
Magazeti hayo, kwa kutumia waandishi wake waliokuja huko nyumbani kufanya ‘coverage’ ya ziara ya Obama, yaliandika masuala mbalimbali yanayotia walakini taswira ya nchi yetu.
Kwa kutegemea mahojiano waliyofanya na watu wa kada mbalimbali huko nyumbani, magazeti hayo yalizungumzia tukio la kutekwa Dk. Ulimboka, mauaji ya Padre Evaristus Mushi huko Zanzibar, shambulio la bomu huko Arusha, na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuruhusu polisi wawapige wananchi ‘wakorofi.’
Tofauti na magazeti hayo makubwa ndani na nje ya Marekani, mengi ya magazeti yetu ya huko nyumbani (ukiondoa gazetihili maridhawa) yalionekana kuelekeza akili zao zote kwenye lojistiki ya ziara ya Obama, hususan kwenye suala la usalama wake.
Habari zilizotanda kwenye magazeti yetu kuhusu ziara hiyo zilielemea zaidi kwenye idadi ya magari katika msafara wa Obama, ndege zilizokuja (na ukubwa wake), wingi wa mashushushu, na mambo mengine kama hayo.
Ndio, Watanzania walistahili kufahamishwa kuhusu namna Rais wa Marekani anavyolindwa, lakini wangependa zaidi kufahamu ziara hiyo ina manufaa gani kwa nchi yao.
Kadhalika, wananchi hao wangeweza kutendewa fadhila kubwa na magazeti yetu laiti yangeiga mfano wa Ney York Times na USA Today kwa kuitumia ziara ya Obama kuijulisha dunia kuhusu masuala mbalimbali yanayotukwaza kimaendeleo, kwa mfano ufisadi, ukiukwaji wa haki za binadamu, nk.
Lakini tunaweza kwenda mbele zaidi ya kuwalaumu baadhi ya waandishi wetu wa habari wanaohangaika na sensational stories pasi kujali ukosefu wa manufaa yake kwa umma. Tukumbuke ni majuzi tu, nchi yetu ilipata ugeni mwingine mkubwa kimataifa baada ya kutembelewa na Rais Xi Jinping wa China. Taarifa za serikali zilieleza kuwa katika ziara hiyo mikataba kadhaa ilisainiwa kati ya nchi hizo mbili (China na Tanzania). Hadi leo mikataba hiyo imebaki kuwa siri.
Pengine hali itakuwa tofauti katika ziara hii ya Obama kutokana na ukweli kwamba wenzetu wa China bado wanaendekeza sana usiri, suala la haki za wananchi kupewa au kupashana habari halipewi fursa.
Kwa Marekani, labda tutakachofichwa ni mikataba ya siri ya kiusalama, lakini katika hali ya kawaida tunaweza kufahamishwa maafikiano mengi kati ya nchi hiyo na yetu kufuatia ziara ya Obama.
Lakini tatizo kubwa, na ambalo binafsi linanifanya niione ziara ya Obama kama tukio tu la kufurahiwa lakini linaloweza kutokuwa na maana yoyote, ni ukweli kwamba umasikini wetu hautokani na ukosefu wa misaada kutoka kwa mataifa wafadhili.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, kwa muda mrefu Tanzania imeshikilia nafasi ya tatu duniani-baada ya Afghanistan na Iraki- kwa kupokea misaada ya kimataifa.
Sana sana umuhimu wa misaada hiyo inaonekana zaidi katika matumizi ya anasa ya watawala wetu-magari na samani za thamani kubwa zaidi ya wanazotumia wafadhili wetu – badala ya nchi yetu kujikwamua katika lindi la umasikini.
Japo ni jambo jema kumsikia Obama akionyesha nia ya kushirikiana na nchi yetu na nyinginezo za Afrika katika kuleta maendeleo, ‘ukweli mchungu’ ni kwamba dhamira hiyo nzuri itakwazwa na majambazi wanaosubiri kwa hamu ‘fedha za Obama’ zidondoke ili nao wazihamishie kwenye akaunti zao huko Uswizi au kisiwa cha Jersey, kama sio kuongeza idadi ya magari na mahekalu yao ya kifahari, na pengine hata idadi ya ‘nyumba ndogo’ zao.
Sitaki kuamini kuwa Obama na Wamarekani wenzie hawafahamu hilo; bali wanaona ni tatizo dogo ukilinganisha na faida watakayopata kwa kufunguliwa milango ya kuvuna raslimali zetu; hususan gesi na mafuta.
Si kwamba Obama hakuwa na taarifa kuhusu hali ya ufisadi, ukiukwaji wa haki za binadamu na demokrasia unavyoiathiri nchi yetu na watu wake; bali yayumkinika amezingatia ukweli kwamba “kama wenyewe hawajali kuhusu hatma ya nchi yao na vizazi vijavyo, kwanini mimi nijali?”
Nimalizie makala hii ‘kuwapoza’ wanahabari walioelekeza macho yao kwenye mashamushamu yaliyoambatana na ziara ya Obama badala ya kuangaza kwenye masuala ya msingi zaidi. Huenda wanahabari hao walifanya hivyo kwa kutambua kuwa “Obama atakuja, atatengeneza mazingira kwa Wamarekani kuchuma raslimali zetu, na ataondoka akituacha na umasikini, ufisadi na porojo zetu.”
Wanasema “kwenye ukosefu wa habari ya maana, vioja/mbwembwe au shamrashamra hugeuka habari ya maana.”
Mwisho, asante Rais Obama angalau kwa kututembelea. Hata hivyo, wakati umeondoka huku tukitamani Tanzania yetu iwe taifa la fursa lukuki kama Marekani, sie tunaelekea kubaki ‘taifa lenye fursa lukuki kwa mafisadi.
Na kinachokaribia kulingana na ‘American Dream’ kwa Tanzania yetu ni kiu ya mafisadi kuifilisi nchi yetu kwa ulafi mkubwa na haraka iwezekanavyo.
MUNGU IBARIKI TANZANIA

Tuesday, April 02, 2013

Dear Rais Kikwete, shuhudia nchi yetu inavyobakwa mchana kweupe (Onyo: ufisadi wa kutisha)



Kampuni ya Mohamed Enterprises yauziwa viwanja kinyemela
*Bandari watumbua zaidi ya bilioni 1.5, waendesha miradi hewa
*Mabosi wanachomeka watumishi hewa, wanavuta mishahara




Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2011; imeendelea kufichua namna kundi la watumishi wa umma na wafanyabiashara wakubwa wanavyoitafuna Tanzania. Utouh aliwasilisha taarifa hiyo bungeni mwishoni mwa wiki. Fedha na mali za umma zenye thamani ya mabilioni ya shilingi, ama zinaibwa au zinachukuliwa kwa namna ambayo ni vigumu kuamini kama kweli viongozi wakuu wa kitaifa wana dhamira ya kutokomeza ufisadi uliovuka mipaka. 


Kuuzwa kwa viwanja, majengo ya Serikali 
CAG amebaini kuwa kiwanja kilichopo katika Kitalu Na. 10 katika Barabara ya Nyerere, kimeuzwa kwa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) kinyemela. Amesema wakati uuzaji kiwanja hicho ulipaswa uratibiwe na Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC - mrithi wa PSRC), kazi hiyo ilifanywa na watu wasiokuwa na mamlaka kisheria. 
Nyaraka za mawasiliano kati ya MeTL, Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina zinazohusiana na uuzaji kiwanja hicho, zinaonyesha kuwa Wizara ya Fedha na Msajili wa Hazina ndiyo waliojihusisha moja kwa moja katika uuzaji wa mali hiyo ya umma, kwa kutoa maelekezo kwenye menejimenti ya CHC. Bodi ya Wakurugenzi haikushirikishwa kabisa. 
Hatimaye kiwanja hicho kiliuzwa kwa MeTL kwa Sh bilioni 2.046 bila kufuatwa kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2005. 
Katibu wa Waziri aamuru kampuni ilipwe Sh bilioni 2.34
Utata wa matumizi mabaya ya fedha za umma, umemkumba aliyekuwa Katibu wa Waziri mwenye dhamana ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji kuhusu kiwanja namba 192 kilichopo Barabara ya Nyerere. Alimwandikia barua Mwenyekiti wa PSRC ailipe kampuni ya DRTC Sh milioni 954.72. 
Hata hivyo, Meneja Mkuu wa DRTC akamwandikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC akitaka alipwe haraka kiasi cha Sh bilioni 2.349. Kwenye barua hiyo, Meneja wa DRTC alisisitiza kuwa malipo hayo ni maelekezo kutoka serikalini, licha ya ukweli kwamba yalikuwa ni makubwa kuliko madai halisi na akalipwa. 
Kuuzwa kwa jengo la kampuni ya umma ya TMSC
Jengo la kampuni ya Tanzania Motors Services (TMSC) lipo katika kitalu namba 24 katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam. Jengo hilo liliuzwa kwa kwa kampuni ya Saddiq Super Service Station (SSSS) kwa Sh bilioni 1.3. Kampuni hiyo ilitoa malipo ya awali ya asilimia 10, yaani Sh milioni 130. Baadaye Wizara ya Fedha ikaitaarifu CHC kuwa Serikali imeghairi kuliuza jengo hilo lililopo kitalu namba 24 kwa kampuni ya SSSS. Wizara ya Fedha ikaitaka CHC ikubaliane na SSSS kuwafidia, kwani tayari kampuni hiyo ilishatoa kianzio cha Sh milioni 130. 
Kuona hivyo, kampuni ya SSSS ikawasilisha madai ya kulipwa fidia ya Sh bilioni 3.894 kwa ajili ya kupoteza biashara yake na Sh milioni 500 kama fidia kwa usumbufu. Hatimaye ikaamuliwa kuwa SSSS ilipwe Sh milioni 964 ambamo ndani yake kulikuwa na Sh milioni 130 ilizotoa awali na gharama za usumbufu. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha alikuwa Mwenyekiti wa kikao kilichoidhinisha malipo hayo. Akawasilisha katika Wizara ya Fedha ambayo yeye ni kiongozi, ili ilipe kiasi hicho cha fedha kwa maelekezo ya kikao alichokiongoza yeye mwenyewe. 
Kwa uamuzi huo, Wizara ya Fedha ikailipa moja kwa moja SSSS Sh milioni 964.2; ilhali kama ni malipo, basi yalipaswa kufanywa na CHC. Malipo hayo, kwa mujibu wa taarifa ya CAG, yanaibua maswali juu ya dhamira ya Wizara ya Fedha kulipa fedha hizo haraka haraka bila kuishirikisha Menejimenti wala Bodi ya Wakurugenzi ya CHC. 
Malipo ya kushangaza kwa kampuni ya Tantrack
Tantrack Agencies ilikuwa mpangaji katika jengo la TMSC lilipo kitalu namba 24, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam. Ilipanga kwa miaka miwili kuanzia Julai Mosi 1993. Kampuni hiyo inasema ilitumia Sh milioni 24 kukarabati jengo kwa wakati wote wa mkataba wake wa upangaji, licha ya ukweli kwamba jambo hilo halikuwamo kwenye mkataba iliyoingia na TMSC. Ikakataa kulipa ada ya pango ikisema fedha hizo zilizotumika kwenye ukarabati zitambuliwe kuwa ndiyo ada ya pango. 
Tantrack ikafungua kesi ya madai namba 257 ya mwaka 1995 katika Baraza la Nyumba Mkoa wa Dar es Salaam (DRHT) dhidi ya TMSC, kwa kigezo kwamba TMSC ilikuwa ikivunja makubaliano. Ilifanya hivyo baada ya TMSC kuiandikia barua ikiipa notisi ya miezi sita ihame kutokana na kutotekeleza makubaliano ya mkataba. 
Wakati hayo yakiendelea, jengo la TMSC likauzwa kwa njia ya mnada kwa African Terminal Limited (ATL) kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa Sh milioni 3. CHC ikapeleka vielelezo vyake mahakamani ikionyesha mkataba ulivyokuwa kati yake na Tantrack. Kabla rufaa haijasikilizwa, ATL ikaweka pingamizi. Sasa ni miaka 15 suala hilo likiwa halijaamuliwa. 
CAG anasema imebainika kuwa kuna uzembe na kutowajibika kwa pande zote mbili zinazopambana kwenye mgogoro huo. 
Utata Kitalu namba 33 kilichotwaliwa na Kampuni ya Maungu Seeds
PSRC iliingia makubaliano na kampuni ya Maungu Seeds, kwa ajili ya kununua kiwanda cha Mzizima Maize Mill kilichopo Kitalu namba 33, Barabara ya Saza katika Eneo la Viwanda Chang’ombe jijini Dar es Salaam. 
Makubaliano hayo yalitiwa saini Septemba 1, 2004; na gharama ya ununuzi ilikuwa Sh milioni 620. Malipo yalikuwa yafanywe kwa awamu tatu. Maungu ikaanza kulipa Sh milioni 200 na kutoa dhamana ya benki (TIB) ya Sh milioni 420. 
Ikakubaliwa kuwa PSRC ingeikabidhi kampuni ya Maungu kiwanda hicho ndani ya miezi mitatu baada ya kutiliana saini ya ununuzi, na kwamba Maungu ingekabidhiwa nyaraka zote baada ya kukamilisha malipo. Iliyokuwa PSRC ikashindwa kukabidhi kiwanda kwa mujibu wa makubaliano kwenye mkataba kutokana na kwamba, kiwanda kilikuwa rehani kwa kampuni ya CDC London ya Uingereza tangu mwaka 1959. 
Hatimaye, ilipofika Aprili 26, 2006 rehani ikawa imeondolewa, lakini tayari muda wa dhamana ya benki ulikuwa umekwisha. Kiasi cha Sh milioni 420 kikawa hakijalipwa. Mwaka 2010 kampuni ya Maungu ikafungua kesi ya madai na ikaamuriwa kuwa ipewe hati ya eneo yenye namba 6639. PSRC (CHC) ikaamuriwa iilipe Maungu Sh milioni 200 haraka. Fedha hizo ni zilezile ilizokuwa imetoa kama malipo ya awali na ikarejeshewa. 
Kimsingi, Maungu ikawa haijalipa chochote, lakini ikawa imepewa kiwanda cha Mzizima bure kabisa bila kulipa kiasi chochote kwa mali hiyo ya umma. 
Madeni ya Simu 2000 yafutwa kienyeji
CAG ameonyesha wasiwasi mkubwa kwa uamuzi wa CHC wa kufuta madeni mengi ya iliyokuwa kampuni ya Simu 2000. Kampuni hiyo iliundwa na kuongozwa na familia ya Mama Anna Mkapa, kwa ajili ya kuuza zilizokuwa mali za Shirika la Posta na Simu. Kuna habari kwamba familia hiyo ilijitwalia mali kadhaa zenye thamani ya mabilioni ya shilingi. Miongoni mwa majengo yaliyouzwa ni maghorofa yaliyopo Ilala. 
Ulaji Chuo cha Ubaharia (DMI)
Ukaguzi uliofanywa na CAG umebaini kuwa Sh milioni 83.96 zimelipwa kama takrima na fedha za kujikimu kwa viongozi bila kuidhinishwa na mamlaka za kisheria. Katika malipo hayo, maofisa wa Wizara ya Mawasiliano walilipwa Sh milioni 12; na Sh milioni 51.8 zililipwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la DMI kama posho ya madaraka (honorarium), mafuta na posho ya vikao. 
Sh milioni 2.6 zililipwa kwa maofisa wa akaunti wa DMI bila wao wenyewe kuhudhuria vikao; Sh. milioni 10.4 zililipwa kwa watumishi wa DMI kama posho ya kujikimu Juni, 2009 bila wenyewe kuhudhuria kile kilichoitwa kuwa ni kikao cha kikosi kazi cha kupitia mitaala ya DMI. 
Katika hatua nyingine, DMI ilipokea Sh milioni 385 kwa ajili ya kuwalipa wadeni wake, lakini ukaguzi umebaini kuwa ni 205.8 pekee zilizotumika. Wafanyakazi 12 wa DMI wamelipwa mishahara ya ngazi ya PGSS 5 na zaidi bila kuidhinishwa na Baraza DMI. Aidha, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala amekuwa akijilipa mshahara kwa kiwango cha PHTS ambacho hakikuidhinishwa. 
Kompyuta za msaada zaibwa, zanyofolewa vifaa
Ukaguzi umebaini kuwa Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza, kilitoa msaada wa kompyuta 25 kwa DMI kwa ajili ya maktaba yake. DMI ilimlipa wakala wa utoaji vifaa hivyo bandarini Sh milioni tatu Desemba 7, 2007. Lakini hadi ukaguzi unafanywa, kompyuta hizo zilikuwa hazijawasilishwa kama ilivyotarajiwa. 
Baadaye imebainika kuwa kati ya kompyuta hizo, ni kompyuta 13 pekee zilizowasilishwa katika maktaba, na kwamba ni kompyuta nne pekee zinazoweza kukarabatiwa. Kompyuta kenda haziwezi kutengenezwa kutokana na kuibwa vifaa muhimu kama Ram, Processors, Hard disks, Power Supply na Mother Boards. 
Bohari ya Dawa (MSD) inaingiza vifaa feki
Pamoja na kuwapo upotevu wa mamilioni ya shilingi zinazotolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, CAG amebaini kuwa baadhi ya vifaa na dawa vinavyosambazwa na MSD havina ubora. Ametoa mfano wa mashine za kupima shinikizo la damu na vifaa vinavyotumika kubebea wagonjwa. 
Pia dawa kama kwinini imebainika kuwa inasambazwa nyingine ikiwa na ubora wa hali ya chini, kutokana na pengine kutohifadhiwa vizuri. Aidha, ukaguzi umebaini kuwa vitambaa vinavyotumika kunyonya damu wakati wa upasuaji huwa vipo chini ya kiwango. 
Ukaguzi umebaini kuwa Sh bilioni 3.95, dola milioni 9.4 na euro milioni 1.5 ambazo zimetumika bila kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya MSD na hivyo kukiuka Sheri ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 na Kanuni 41 ya Tangazo la Serikali namba 97. 
Aidha, imebainika kuwa MSD imefanya ununuzi kwa zabuni nane huku upitiaji wa zabuni hiyo ukifanywa na mtu mmoja, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Zabuni zilizofikwa na hali hiyo ni za Sh milioni 134.4, dola 10,000 na Euro milioni 1.5. 
Ulaji wa kutisha Bandari ya Dar es Salaam
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) iliingia mkataba na kampuni ya Singapore PTE Limited kwa ajili ya kuweka ‘Radio Data Terminals’ Februari 2010 wenye thamani ya dola 339,600. Punde tu baada ya TPA kupata radio hizo, mambo kadhaa yalianza kujitokeza. 
Kwanza, menejimenti ikabaini kuwa ‘Radio Data Terminals’ hizo  haziwezi kufanya kazi bila kile kinachoitwa kitaalamu kuwa ni ‘Access Points’ (virusha mawimbi). Hatua hiyo ikaifanya PTA iingie mkataba mwingine na Singapore PTE Limited Juni 21, 2010 kwa ajili ya kuweka virusha mawimbi 68 kwa gharama ya dola 399,000. Baada ya kununua vifaa hivyo, ikabainika tena kwamba haviwezi kufungwa juu minara ya iliyokuwapo. Kwa sababu hiyo, PTA ikaingia mkataba mwingine na CATS (T) Limited Septemba 17, 2010 kwa ajili ya kuweka minara mingine kwa gharama ya dola 133,000. 
CAG anasema katika ukaguzi wake kwamba pamoja na kufanya yote hayo, bado ‘Radio Data Terminals’ hazikuweza kufanya kazi kama ilivyokusudiwa, kwa vile ilipaswa iunganishwe kwenye mkongo (fibre optic) kwa gharama ya dola 553,800 za Marekani. Kazi hiyo ikafanywa na EMEC. 
Kwa kifupi, TPA ikajiingiza kwenye gharama za ziada za dola milioni 1.09 na bado kilichokusudiwa hakikuweza kupatikana kwa muda kutoka kwa mkandarasi aitwaye CATS. Hakuna gharama zozote ambazo TPA imeweza kuzidai kutokana na kucheleweshwa au kuingia gharama kubwa kiasi hicho. Hii inatiliwa shaka kuwa ndiyo ulaji wenyewe. 
Sh milioni 100 zaliwa bila jengo la bosi TPA
TPA iliingia mkataba na kampuni ya AF MULT-CON LIMITED kujenga makazi ya Meneja wa Bandari Tanga kwa gharama ya Sh milioni 500. Utangazaji zabuni umebainika kuwa ulifuata taratibu zote. Hata hivyo, CAG amebaini kuwa kuna uzembe katika kufuatilia taratibu za mkataba wa zabuni. CAG mwenyewe alizuru eneo lililokusudiwa kujengwa jengo hilo, na hakushuhudia malighafi wala shughuli yoyote ya kuhalalisha malipo ya Sh milioni 100 ambazo tayari mzabuni alishalipwa. 
Mkataba mwingine wa utata TPA
Wakati wa ukaguzi, CAG alibaini kuwa TPA iliingia mkataba na kampuni ya Chibeshi Construction kwa ajili ya kujenga uzio katika kitalu namba moja kwenye Bandari ya Mtwara. Mkataba huo ulikuwa na thamani ya Sh milioni 679.8. Ulitiwa saini Aprili 14, 2009 na ujenzi ulipaswa ukamilike kwa wiki 26 kutoka siku ya kutiwa saini mkataba. 
Kabla ya mkandarasi kuanza ujenzi, TPA ikaamua kuvunja mkataba huo kwa maelezo kwamba hapakuwapo fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Uamuzi huo ukaifanya TPA iingie hasara ya Sh milioni 92.6 kama adhabu au faini. Ikamlipa mkandarasi. Fedha zikachukuliwa na mkandarasi bila kufanya kazi yoyote. 
Mkataba mwingine wa utata waingiza hasara TPA
Katika ukaguzi, CAG amebaini kuwa PTA iliingia mkataba na kampuni ya WiA kwa ajili ya kuweka mawasiliano ya intaneti katika Makao Makuu ya TPA, na bandari nyingine zilizo chini ya Mamlaka hiyo. Mkataba huo ulikuwa wa miezi mitatu kuanzia Julai 2010. Hata hivyo, mradi huo haukukamilika baada ya muda uliopangwa kumalizika. TPA ikaamua kumwongeza mkandarasi muda hadi Februari 28, 2011 na mkandarasi bado alishindwa. TPA ilipaswa kumtoza mkandarasi kiasi cha dola 95,000 kwa kushindwa kutekeleza mkataba kwa muda, lakini haikufanya hivyo. 
Hazina yalipa mamilioni ya mishahara hewa
Wakati wa ukaguzi, CAG amebaini kuwa Hazina imeendelea kutumia mamilioni ya shilingi kuwalipa wafanyakazi hewa katika taasisi mbalimbali. Katika ukaguzi huo, imebainika kuwa Chuo Kikuu cha Mkwawa (MUCE) kumekuwa na majina 42 ya watu wanaolipwa mishahara licha ya ukweli kwamba si watumishi wa chuo hicho. Imebainika kuwa kuanzia Oktoba 2009 hadi Juni, 2010 MUCE ilipokea Sh milioni 612 na kuwalipa watumishi hewa. 
Katika Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Hazina imeendelea kuwalipa mishahara watu ambao si watumishi chuoni hapo. Baadhi ya waliostaafu na MNMA kupeleka majina yao Hazina, wanaendelea kulipwa. Hali hiyo imesababisha Sh milioni 134.74 zitumike kuwalipa watu ambao si watumishi katika chuo hicho. Fedha hizo hazikurejeshwa Hazina. 
Katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, orodha ya majina kutoka Hazina inaonyesha kuwa hata wale ambao si watumishi tena wa chuo hicho, majina yao yapo kwenye orodha ya wanaostahili kulipwa mishahara. Kuanzi Oktoba 2010, Machi 2011, Mei 2011 na Juni 2011 Sh milioni 194.4 zimetumika kuwalipa watu ambao si watumishi katika chuo hicho. 
Imebainika pia kwamba baadhi ya watumishi waliojiuzulu au kuacha kazi katika Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), majina yao yameendelea kuwa kwenye orodha ya Hazina ya watumishi wanaopaswa kulipwa. Sh milioni 181 zilikuwa zimetumika kuwalipa hadi wakati ambao CAG alikuwa akiandaa ripoti hii. 
Katika Chuo cha Elimu Dar es Salaam nako mambo ni kama hayo. Watu 56 ambao hawapo kwenye utumishi wameweza kulipwa Sh milioni 778.7 licha ya ukweli kwamba hawapo chuoni hapo. Hakuna rekodi inayoonyesha kuwa fedha hizo zilirejeshwa Hazina. 
Fedha za Mifuko ya Jamii hatarini
Ukaguzi umebaini kuwa upo udhaifu mkubwa na hatari ya kupotea kwa mabilioni ya shilingi zilizowekezwa na Mifuko ya Jamii katika miradi mbalimbali nchini. 
Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limetumia Sh bilioni 234.054 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma. Kati ya fedha hizo, ni Sh bilioni 35.218 pekee ambazo zilisainiwa katika ujenzi wakati wa awamu ya kwanza. Fedha zilizotolewa katika ujenzi wa awamu ya pili, hazikusainiwa. Majengo ya awamu ya kwanza yamekamilika, lakini Serikali haijaanza kurejesha fedha inazodaiwa na NSSF zenye riba ya Sh bilioni 14.157. 
Wabunge waondolewe kwenye Bodi
Kwa mara nyingine, CAG amependekeza wabunge wasiwemo kwenye Bodi za Mashirika ya Umma na bodi nyingine. Anasema mapendekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba kuwamo kwao kwenye bodi husababisha mgongano wa masilahi. 
Anasema ni Tanzania pekee ambayo wabunge ni wajumbe katika bodi za mashirika ya aina hiyo. Utaratibu kama huo haupatikani mahali kwingineko duniani wala katika vyombo ambavyo Tanzania ni mwanachama. 
Uteuzi wa wajumbe wa Bodi
CAG anatoa mapendekezo kwamba maofisa watendaji wakuu wa kampuni/mashirika ni vizuri wakateuliwa na Bodi za Wakurugenzi badala ya utaratibu wa sasa, ambako ni Rais anayewateua. Anapendekeza Rais aachiwe madaraka ya kuteua mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi. 
Mapendekezo hayo, kwa mujibu wa CAG, yanalenga kuifanya Bodi ya Wakurugenzi iweze kuisimamia vema menejimenti na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa. 

Serikali ibane ununuzi mashangingi
CAG anapendekeza kuwa ili fedha nyingi zielekezwe kwenye maendeleo, Serikali haina budi kuweka utaratibu madhubuti wa kudhibiti matumizi hasa kwenye ununuzi wa magari ya kifahari, gharama za semina na kupunguza idadi ya wanaosafiri kwenye misafara ya viongozi ndani na nje ya nchi.

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India