
"Dowans na Richmond ni mtu na binamu yake na si vigumu kukubali kuwa bado wao ni wabia hadi sasa: Pamoja na yote mkasa wa Richmond haufai kufufuliwaaa upya kupitia Dowans," alisisitiza Sitta.
Aliongeza kuwa kama kweli Tanesco na serikali inazo Dola 69 milioni za Kimarekani (sawa na Sh90 bilioni za Kitanzania) ambazo ni bei ya mtambo wa Dowans, ingezitumia fedha hizo kama sehemu ya malipo ya kununua mitambo mipya. Alisema Tanesco ingetafuta ushauri kutoka Mamlaka ya Ununuzi Serikalini (PPRA) ili taratibu za dharula zitumike kununua mitambo mipya kukabiliana na "dharula inayotabiriwa".
Sitta alihoji mantiki itakayotumiwa na Tanesco kutaka kununua mitambo ambayo inamilikiwa na kampuni ambayo imeishtaki kwenye Baraza la Usuluhishi ambalo makao yake makuu yako Paris, Ufaransa.
"Gharama za mitambo na gharama za kuikodi haviwezi kuepukwa kuwa ni sehemu ya shauri lililo Paris," anasema Sitta. "NI kwa mantiki ipi kesi baina yao iendelee na hapo hapo mdaiwa (Tanesco) anunue mitambo kutoka kwa mdai (Dowans.
"Tanzania ilikuwa ikilipa Dowans shilingi za Kitanzania milioni 152 kwa siku (Dola 120,000) sawa na Dola 42 milioni kwa mwaka).
"Pamoja na yote, mkasa wa Richmond haufai kufufuliwa upya kupitia Dowans. Tanesco/serikali waelekeze nguvu zao katika njia mbadala za kulipatia taifa umeme wa dharura, badala ya njia hii ya Dowans iliyojaa utata."
Kuhusu mvutano kati ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma na ile ya Nishati na Madini, Spika Sitta amsema si sahihi kwa kamati yoyote ya Bunge isiyo ya sekta husika, kutoa maoni yake hadharani na kuishawishi jamii kwamba Bunge lina ushauri unaopingana kuhusu suala husika.
"Si sahihi kwa Kamati yoyote ya Bunge isiyo ya sekta kutoa maoni yake hadharani na kujenga taswira kwa umma kwamba, Bunge lina ushauri unaokinzana kuhusu suala lililo mbele yake. Kamati nyingine, haina budi kupitisha ushauri na maoni yake kwenye kamati ya kisekta," alisema Sitta.
Zitto Kabwe, ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, alikaririwa na vyombo vya habari akieleza msimamo wa kamati yake kuunga mkono Shirika la Umeme (Tanesco), kuinunua mitambo ya Dowans kwa maelezo kuwa hatua itasaidia kulinusuru taifa katika janga kubwa la kukosa umeme na kwamba sheria ya manunuzi si msahafu, hivyo inaweza kubadilishwa.
Lakini Kamati ya Nishati na Madini, ambayo mwenyekiti wake ni William Shelukindo, inapinga hatua hiyo ikieleza kuw ainakiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma, inayokataza serikali kununua vitu ambavyo tayari vimetumika.
Alisema ushauri kwa serikali kuhusu Tanesco kununua au kutonunua mitambo ya Dowans ulikwishatolewa kwa Wizara ya Nishati na Madini na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Desemba 14 mwaka uliopita.
"Huo ndiyo ushauri rasmi na sahihi wa Bunge ninaoutambua. Kwa msingi huo hoja ya kuzikutanisha Kamati hizi mbili (ya Nishati na Madini na ya Hesabu za Mashirika ya Umma) ili kurejea uamuzi au maoni yaliyokwishatolewa na Kamati inayohusika, haina msingi," alisema Sitta.
Alisema mkondo rasmi wa ushauri kwa serikali uliokusudiwa kwenye Ibara ya 63 (2) ya katiba ikisomwa na pamoja na kanuni za Bunge za mwaka 2007 ni kupiti Bunge zima au kamati zake za kisekta kila kamati na sekta yake.
Wakati Spika Sitta akibainisha msimamo wake na wa Bunge, mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba ameunga mkono ununuzi wa mitambo hiyo huku akisema kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa jana inaweza kukwamisha mchakato wa ununuzi wa mitambo hiyo.
Lipumba alisema katika mfumo wa utawala bora wakati kamati za bunge zinazohusika na mambo hayo na bodi za mashirika zipo, rais hapaswi kujiingiza mapema katika mijadala.
“Katika mfumo wa utawala bora ambao una kamati za bunge zinazohusika na sekta ya umeme na manunuzi, kwa rais kujiingiza kunaweza kuwa ni kikwazo cha mchakato mzima wa ununuzi wa mitambo,” alisema Profesa Lipumba.
Alifafanua kuwa, sheria ya manunuzi ya Serikali ina upungufu kwa kuwa inalazimisha ununuzi wa mitambo mipya, jambo ambalo haliwezekani kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania.
“Ununuzi wa mitambo ya kibiashara katika sekta ya biashara huwezi kulazimisha ununuzi wa mitambo mipya hususan katika nchi zinazoendelea kama ya kwetu. Jambo la msingi ni kuangalia uwezo wa mitambo katika kufanya kazi na si kwamba ni mipya au mikongwe,” alifafanua Lipumba na kuongeza:
“Sheria yetu ya manunuzi ni nzuri na inafaa sana kwa kununua vitu vya huduma za serikali, kama magari na vifaa vingine.”
Aliitaka Tanesco kuwa wazi kwa kuwa ni wao waliosema mitambo hiyo hawaitaki hivyo kuamuwa kuvunja mkataba na Dowans iweje leo wanageuka na kusema mitambo hiyo ni mizuri na kuitaka serikali iinunuwe.
“Tanesco walituambia kuwa mitambo hiyo hawaitaki na walivunja mkataba na Dowans, sasa inakuaje leo wanageuka na kusema kwamba mitambo hiyo ni mizuri na inunuliwe kwa ajili ya kuzalishia umeme? Tunahitaji uwazi zaidi kutoka Tanesco,” alihoji Profesa Lipumba.
Naye Stephen Menad ambaye ni mshauri wa masuala ya nishati na mazingira, alisema hakuna kitu kipya kwenye mitambo hiyo ya Dowans hivyo isinunuliwe na badala yake itafutwe mipya ili kuondoa mvutano baina ya wananchi na serikali.
Mussa Hassan, mkazi wa jijini Dar es Salaam ambaye ni mfanyabiashara, alisema ni aibu kwa serikali kula matapishi na kwamba viongozi wasisahau yaliyotokea wakati mitambo ya Richmond ilipokuja na mwisho wake kuwaweka pabaya viongozi waliokuwa serikalini.
Anthony Chambi, ambaye ni mfanyabiashara katikati ya jiji la Dar es Salaam, alisema hataki kusikia kuhusu mitambo hiyo kwa kuwa tayari ilishaiabisha serikali. Alisema anasikia kuna kesi Ufaransa kuhusu mitambo hiyo kitu kinachomshangaza kwa nini serikali inataka kununua mitambo ambayo ina kesi.