Featured Posts

Showing posts with label Mafuriko Dar. Show all posts
Showing posts with label Mafuriko Dar. Show all posts

Sunday, April 13, 2014

Sikiza 'nyodo' za Meya Jerry Silaa akihalalisha uwepo wake Mwanza huku wananchi wake wakikabiliana na mafuriko



Huu ni mtizamo wangu, na nilimfahamisha Mstahiki meya Jerry Silaa pia: huyu mtu ana bahati sana kwamba ni Meya wa manispaa nchini Tanzania, ambapo ukisahapata uongozi upo huru kufanya lolote lile- baya au zuri, la busara au la kipuuzi- pasi kuchelea matokeo. Laiti huyu mtu angekuwa Meya wa eneo lolote lile hapa Uingereza, basi Jumatatu angekumbana na wito wa kumtaka aachie ngazi. Ndio, uwepo wake Dar (Ilala) usingezuwia mafuriko, lakini sote twatambua kuwa nyakati za majanga zinahitaji viongozi kuonyesha uongozi kwa dhati (showing leadership). Kilichompeleka Mwanza ni shughuli za kichama, ambazo ninaamini zingeweza kusubiri hadi janga linalowasibu anaowaongoza limeshughulikiwa. 

Japo mwanzoni alileta majibu ya dharau baada ya kusoma 'tweets' hizo mbili za mwanzo hapo juu, lakini akakumbana na hasira za wananchi wengi ambao hawakupendezwa na majibu yake. Lakini kwa vile neno 'samahani' halipo kwenye kamusi za wengi wa viongozi wetu, Mstahiki Meya 'aliingia mitini' kimyakimya...na hajaonekana tena huko twitter hadi wakati ninaposti bandiko hili.

Swali la msingi: Hivi Katiba Mpya tunayohangaika kuipata huko Dodoma itaweza kweli kutengeneza mazingira yatakayowawezesha wananchi kuwashughulikia 'wahuni wa kisiasa' (political thugs)? Jeuri kubwa inayowafanya watawala wetu kufanya (including kusema) chochote ni kutochelea matokeo. Na japo Katiba tuliyo nayo sasa ina sheria nzuri tu za kumpatia mwananchi kile anachostahili (kwa maana ya haki zake), tatizo limebaki katika usimamizi wa sheria hizo, na pengine kubwa zaidi, sheria hizo kubaki kama maandiko tu yasiyoheshimiwa. Je Katiba Mpya (laiti ikipatikana) itaheshimiwa?

Finally, ninaamini Mstahiki Meya Silaa nafsi itamsuta na atakatisha ziara yake huko Mwanza na kuungana na wananchi katika harakati za kukabiliana na athari za mafuriko Dar (kwa yeye ni Manisapaa ya Ilala). See, kwenda kumwona mgonjwa hakumaanishi kutamfanya aopone bali kwaonyesha kuwa flani anajali. Kadhalika, tunapokwenda kwenye misiba haimaanishi kuwa tutamfufua marehemu, lakini ile tu kuwafariji wafiwa kunaonyesha kuwa tunajali. Nam ,Meya Slaa akiwa Illa/Dar hatozuiwa athari za mafuriko (au kama alivyosema mwenyewe "hawezi kzuwia mvua") lakini kibanadamu tu anapaswa kuwa na wahanga wa mafuriko (japo yeye ana-pick and choose nani anastahili kuitwa mhanga).

Thursday, December 29, 2011

Makala Yangu ya Mwisho wa Mwaka Ndani ya RAIA MWEMA: "Tatizo Serikali au Wanaoishi Mabondeni?"




Tatizo Serikali au wanaoishi mabondeni?

Maafa ya mafuriko Dar
Mafuriko Dar es Salaam
Mafuriko Dar es Salaam
NIANZE kwa kutoa pole kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kutokana na janga la mafuriko ya wiki iliyopita. Inasikitisha kuona tunamaliza mwaka 2011 kwa majonzi, badala ya furaha (hata kama tuna vitu vichache vya kufurahia).
Kwa hakika si jambo jema kutumia janga kama hili kunyoosheana vidole, hususan katika kipindi hiki ambacho hata hatujafahamu kiwango cha athari kilichosababishwa na mafuriko hayo.
Hata hivyo, tunaweza kuendelea kusononeka na kuomboleza milele lakini pasipo kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa huko mbele tunajiandaa ipasavyo kukabiliana na majanga kama haya basi ni dhahiri tunaweza kujikuta tena katika hali kama hii inayotukabili sasa.
Ni ukweli usiofichika kuwa nchi yetu inaendeshwa kwa mtindo wa zimamoto. Tunasubiri litokee balaa kisha watawala wetu wapite huku na kule wakijifanya kuguswa na kusononeshwa na maafa yaliyowakumba watawaliwa.
Jiji la Dar es Salaam kama yalivyo maeneo mengine ya nchi yetu ni kama bomu linalosubiri kulipuka. Japo mafuriko ni janga la asili kwa maana hakuna namna ya kuyazuwia, kwa hakika kuna njia kadhaa za kujiandaa kukabiliana nayo na hata kupunguza madhara yake.
Kimsingi haya si mafuriko ya kwanza kuwakumba wakazi wa Jiji la Dar es Salaam au kusababisha madhara katika sehemu nyingine nchini.
Tofauti na mafuriko yaliyotangulia ni kiwango cha madhara ambacho yayumkinika kuhisi kwamba inaweza kuwa vigumu kufahamu kutokana na uzembe, ubabaishaji na kutowajibika ipasavyo kwa wahusika.
Janga hili la mafuriko jijini Dar es Salaam limeibua tena mjadala wa miaka nenda miaka rudi kuhusu makazi ya mabondeni. Swali ambalo limejitokeza katika mijadala mbalimbali ni nani alaumiwe kati ya Serikali na wakazi wa mabondeni.
Pengine cha muhimu si lawama bali kuangalia chanzo na utatuzi wa tatizo hili ambalo likiachwa liendelee litasababisha vilio vingine huko mbele (hata kama tunaombea isiwe hivyo).
Ni rahisi kuwalaumu wakazi wa mabondeni kwa hoja dhaifu kama “nani awalazimishe kuhama mabondeni kama wenyewe hawataki au hawajali maisha yao?”
Unaweza kutoa lawama hizo kirahisi kama hujui ugumu wa kupata sehemu ya kuishi jijini Dar es Salaam, achilia mbali ugumu wa kupata kiwanja cha kujenga nyumba mpya.
Ripoti kadhaa kuhusu utawala bora zimekuwa zikizitaja mamlaka za ardhi kama kiongozi wa muda mrefu katika rushwa. Na kama inavyoeleweka, waathirika wakubwa wa rushwa ni walalahoi wasio na uwezo wa kuhonga. Sitaki kabisa kuamini kuwa wakazi wa mabondeni wanaendelea kuhatarisha maisha yao katika maeneo hayo kwa vile wanapenda iwe hivyo.
Nani asiyeogopa kifo? Nani anayetaka kuishi sehemu ambayo kufikika kwake hata wakati wa kiangazi ni kwa shida? Nani anayependa kukaa eneo ambalo mvua kidogo tu ikinyesha basi inaweza kusababisha wakazi wa eneo husika kujifungia ndani kutwa nzima au usiku kucha kwa vile kila eneo limejaa maji?
Hawa ni watu wanaohitaji kusaidiwa. Lakini kwa vile sote tunajua kuwa si Serikali kuu wala mamlaka za Jiji zinazoguswa kwa dhati na tatizo hili, ni muhimu kuwaelimisha wakazi hao kudai haki zao za kibinadamu kuhusu makazi bora na usalama wa maisha yao kwa ujumla.
Mwaka unamalizika na janga hili la mafuriko, na japo nisingependa kuwa “nabii wa majanga” (prophet of doom) yayumkinika kubashiri kuwa safari yetu huko mbele si salama. Ni wazi kuwa laiti yakitokea mafuriko mengine iwe Dar es Salaam au kwingineko nchini, tutarejea katika hali hii ya huzuni na majonzi kwa vile mfumo wa kuzuia na kukabiliana na majanga ni sifuri.
Viongozi wetu ni wepesi kumbebesha Mungu mzigo wa lawama kwa kauli maarufu ya “ni mapenzi ya Mungu.” Kuna nyakati ninatamani Mungu apandwe na hasira na kuwaumbua viongozi wa aina hiyo kwa umma kwa yeye (Mungu) kujivua lawama hizo na kuwafumbua macho watawaliwa waelewe kuwa tatizo ni watu waliopewa jukumu la kuongoza lakini wasiotekeleza jukumu hilo ipasavyo.
Kuna janga jingine kubwa la kiuchumi. Kwa sisi tunaoishi kwenye nchi kama Uingereza ambayo ni miongoni mwa wafadhili wakubwa wa Tanzania tunaona kila dalili kuwa muda si mrefu wanaweza “kubwaga manyanga” kusaidia nchi masikini na kuelekeza nguvu kwenye kujisaidia wao wenyewe.
Hali ya uchumi wa dunia ni mbaya sana lakini pengine kinachoweza kusababisha msione hivyo huko nyumbani ni ukweli kwamba hali huko ni mbaya karibuni kila siku.
Sasa kama hali ni mbaya wakati huu ambapo wafadhili wanaendelea kumwaga misaada yao (huku sehemu kubwa ya misaada hiyo ikiishia kwenye mifuko na akaunti za mafisadi), ni wazi kuwa hali itakuwa mbaya zaidi pindi wafadhili hao wakilazimika kupunguza au kukata kabisa misaada hiyo.
Tofauti na mafuriko ambayo ni janga la asili (natural disaster), tatizo hili la uchumi ni la kibinadamu. Na wakati wenye jukumu la kujiandaa na kukabiliana na majanga ya asili wanaweza kuwa na kisingizio kwamba “sie ni masikini sana kumudu kuwa tayari muda wote kujiandaa na kukabiliana na majanga ya asili,” kwenye tatizo hili la uchumi hakuna kisingizio hasa kwa vile tuna raslimali za kutosha za kujiandaa kukabiliana na mtikisiko wa uchumi wa dunia.
Wanasema “kufa kufaana.” Janga hili la mafuriko linaweza kutoa nafasi nzuri kwa watawala wetu kukwepa kutueleza kwa nini tupo katika hali mbaya kiasi hiki katika kipindi hiki tunachoelekea mwisho wa mwaka huku ikiwa ni siku chache tu baada ya kuadhimisha miaka 50 ya uhuru wetu.
Watawala wamepata kisingizio cha “tupo kwenye kipindi cha majonzi na si vema kuanza kunyoosheana vidole kuhusu masuala mengine.” Na kwa vile Watanzania wengi sio tu ni wepesi wa kusahau lakini pia hawapendi kuunganisha mlolongo wa matukio (chain of events) basi ni wazi kuwa janga hili la mafuriko litawanusuru watawala wetu kutupatia majibu kuhusu matatizo mengine mengi ambayo pasi na shaka tutaingia nayo mwaka ujao 2012.
Sawa, kwa sasa tunapaswa kufanya kila linalowezekana kuwasaidia Watanzania wenzetu walioathirika kwa mafuriko. Lakini wakati tunafanya hivyo ni lazima tutambue kuwa laiti tungepata ufumbuzi wa matatizo yaliyokuwepo kabla ya janga hili la mafuriko ni wazi kuwa pindi wahanga hao wakishasaidiwa hawatakuwa na hofu nyingine za kukabiliana na matatizo hayo “ya kudumu.”
Tunamaliza mwaka huku Ripoti ya Bunge kuhusu sakata la akina Jairo likiwa limenyamaziwa na Rais Jakaya Kikwete. Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo bado hajachukuliwa hatua kama ilivyo kwa Waziri William Ngeleja na Naibu wake, Adam Malima, sambamba na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utoh.
Hivi Kikwete haelewi kuwa katika mazingira ya kawaida tu uwepo madarakani wa watu hawa unaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ya hayo yaliyosabisha Bunge liwachunguze?
Hapa ninamaanisha kuwa kwa vile wahusika hawa wanaweza kujiona wapo “mguu ndani, mguu nje” basi ni bora “wachukue chao mapema” kabla hawajawajibishwa.
Tunamaliza mwaka huku ahadi zilizozoeleka za Rais Kikwete kuhusu utatuzi wa tatizo sugu la umeme zikiendelea kuwa ahadi hewa. Mwaka unaelekea ukingoni lakini ahadi ya Rais kuwa ifikiapo mwezi huu Desemba, mpango wa dharura wa kuongeza nishati ya umeme (megawati 572) katika gridi ya taifa ungekamilika inabaki kuwa ndoto ya alinacha.
Mpango huo wa Serikali uliowasilishwa bungeni mwezi Agosti, mwaka huu ulieleza kuwa kati ya megawati hizo, 150 zilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano kati yake na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Mgawanyo wa megawati hizo ulionyesha kungeingizwa megawati 50 kwa kila mwezi, kati ya Septemba na Desemba 2011.
Hadi sasa hakuna hata megawati moja ya umeme iliyozalishwa na NSSF na taarifa zinaonesha kuwa mamilioni ya fedha za umma yamepotea kwa “safari za kutalii” kwenda Marekani na Ufaransa “katika mchakato huo” lakini mgawo wa umeme unazidi kudumisha makali yake.
Nimalizie makala hii kwa kurejea pole zangu kwa waathirika wa mafuriko ya Dar es Salaam, sambamba na kuwatakia wasomaji wote wa Raia Mwema na makala hii heri ya mwaka mpya 2012.
Wakati mwaka huu 2011 unamalizika huku tukiwa na mengi ya kulalamikia kuliko kupongeza au kujidai nayo, ninaomba kutoa wito kwa kila Mtanzania mwenye uchungu na nchi yetu kuukaribisha mwaka mpya kwa kauli ya “Enough is enough”(Imetosha); aidha tuendelee kuwaruhusu viongozi wazembe na mafisadi waipeleke nchi shimoni au tusimame kidete na kudai haki zetu za msingi za kuwa na maisha bora na salama.
Kama alivyowahi kutuasa aliyepata kuwa Waziri wa Fedha wakati wa Awamu ya Pili, Marehemu Profesa Kighoma Ali Malima (namnukuu); “haki haitolewi kama zawadi. Haki hudaiwa, hata kwa nguvu inapobidi.” (Atakayeniita mchochezi kwa nukuu hii lazima atakuwa fisadi asiyetaka kuona Watanzania “wanaamka”).
Mkoloni hakuondoka kwa vile tulikuwa tunanung’unika, Nduli Idi Amin hakuacha uharamia wake kwa vile tulimwita kila jina baya. Kilicholeta mwisho wa udhalimu wa mkoloni na Amin ni harakati za dhati za kukomesha maovu yao.
Manung’uniko na majina mabaya kwa mafisadi na wazembe hayawezi kutuletea “ukombozi” wetu. Kinachohitajika ni mwamko na jitihada za dhati za kukomesha uharamia huo.
Heri ya mwaka mpya  2012.

Friday, December 23, 2011

Tamko la CHADEMA kuhusu Mafuriko Dar



CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SALAAM ZA RAMBIRAMBI NA POLE KWA WANAFAMILIA NA WANANCHI KUHUSIANA NA JANGA LA MAFURIKO YALIYOKUMBA JIJI LA DAR ES SALAAM, MBEYA NA DODOMA .
Usiku wa kuamkia tarehe 20.12.2011 Maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar Es Salaam, Mbeya na Dodoma yamekumbwa na maafa makubwa ya mafuriko ambayo yamesababishwa na mvua kubwa ambazo zimeendelea kunyesha mfululizo katika maeneo hayo.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapenda kutoa pole za dhati kwa wanafamilia na wananchi wote ambao wamekumbwa na janga hili kubwa , kwani limesababisha maafa makubwa sana ya vifo, kupoteza mali na miundombinu mbalimbali kuharibiwa vibaya kwenye maeneo husika. Tunapenda kuwahakikishia wananchi hawa kuwa tutakuwa nao pamoja katika kipindi hiki kigumu katika maisha yao kutokana na madhara waliyopata yaliyosababishwa na maafa haya.
Kutokana na janga hili limetukumbusha jambo moja kuwa kama Taifa hatujajiandaa kikamilifu kuweza kukabiliana na majanga kama haya pindi yanapotokea na hata vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeonyesha dhahiri kuwa havijaandaliwa kimfumo na kinyenzo katika kuweza kukabiliana na majanga kama haya na huu ni udhaifu mkubwa sana kwa taifa lenye miaka 50 baada ya uhuru wake .
Mathalani mpaka sasa hatujaona jitihada zozote ambazo zimechukuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa katika kuonyesha juhudi za kukabiliana na janga hili kubwa kwa taifa letu,hii inaonyesha wazi kuwa kitengo hiki hakijaandaliwa kuweza kukabiliana na maafa kama ambavyo majukumu yake yanavyopaswa kuwa . Na hii ni hatari kwani kama chombo cha kukabiliana na maafa hakiwezi kufanya hivyo kwa wakati ni kuendelea kuwaacha wananchi waendelee kupata madhara makubwa zaidi. Na haswa ikizingatiwa kuwa idara ya hali ya hewa ilishatahadharisha kuhusiana na mvua hizi.
CHADEMA tunapenda kuikumbusha serikali kuhusiana na ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo ilieleza wazi kuhusiana na kukosekana kwa mifumo thabiti ya kujulisha umma kuhusiana na majanga mbalimbali katika miji yetu (Early Warning Systems) kama ambavyo ipo katika nchi nyingi , mfumo huu ni muhimu sana katika kuweza kuufanya umma uwe na elimu ya jinsi ya kuweza kujikinga na majanga haya kwa lengo la kupunguza madhara yasiwe makubwa kama ambavyo taifa hivi sasa linashuhudia.
CHADEMA inapendekeza hatua zifuatazo ziweze kuchukuliwa haraka na serikali ili kuweza kukabiliana na majanga/maafa mbalimbali hapa nchini yanapojitokeza;
I) Kuandaa mfumo wa awali wa kutahadharisha umma juu ya ujio wa majanga (Early Warning Systems) kwa kutumia vyombo na nyenzo mbalimbali ili kuepusha madhara makubwa kwa watu na mali zao.
II) Kutunga sheria mpya ya ujenzi na kuweka viwango vya ujenzi viwe vyenye hadhi ya kimataifa na haswa ujenzi wa kuta mbalimbali na majengo marefu na kuhakikisha kuwa ujenzi holela haujitokezi kwenye miji na majiji yetu hapa nchini.
III) Kuhakikisha kuwa kwenye miji yote mikubwa mtandao wa mabomba ya maji ya dharura unawekwa ili kuweza kukabiliana na majanga ya moto pindi yanapotokea.
IV) Serikali ijiandae mara moja kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama vile kuhara ,kipindupindu na mengineyo ambayo yatajitokeza kutokana na mafuriko haya kuharibu miundombinu ya kusambaza maji, makazi ya watu n.k.
V) Kitengo cha maafa kiwe na vifaa wakati wote , na haswa vifaa kwa ajili ya uokoaji na wawe na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma jinsi ya kuweza kutumia vifaa hivyo kuweza kujiokoa na sio kuacha hali iwe kama ambavyo imejionyesha Dar Es Salaam jana baada ya baadhi ya majaketi okozi kufikishwa kwa wahanga na kushindwa kuyatumia kikamilifu.
VI) Serikali itoe elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa ya milipuko kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko haya ili kuepusha wananchi wengi kukumbwa na magonjwa hayo pindi yakijitokeza.
Mwisho tunapenda kuendelea kutoa pole kwa wanafamilia wote na wananchi kwa ujumla kutokana na madhara makubwa waliyoyapata , Mungu awajaze nguvu katika kipindi hiki kigumu.
Tamko hili limetolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu CHADEMA .
……………….
DR. Willbroad P. Slaa.
Katibu Mkuu –CHADEMA.

22/12/2011.

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India