Featured Posts

Saturday, August 31, 2013

Makala yangu ktk RAIA MWEMA la 28.08.13: Usalama wa taifa wamepitisha ‘unga’ Airport, kwa nini wasipitishe magaidi?


Askari trafiki feki akamatwa. Askari polisi feki akamatwa. Ofisa Usalama wa Taifa feki akamatwa. Hizo ni habari zilizotawala vyombo vya habari huko nyumbani hivi karibuni, ambazo kimsingi zinaashiria tatizo kubwa la uwepo wa watendaji feki wa taasisi za usalama.
Wakati lawama kubwa zinapaswa kuelekezwa kwa matapeli hao waliojipachika majukumu yasiyo yao, kwa hakika hatuwezi kutozinyooshea kidole taasisi husika kwa ‘kuruhusu’ wahalifu wafanikiwe kujivisha utumishi wa taasisi hizo pasi kujulikana kwa muda mrefu tu.
Binafsi sikushangazwa sana na taarifa za polisi na trafiki feki kwa sababu utendaji kazi wa baadhi ya polisi hauna tofauti na wahalifu. Sasa kama polisi halisi wanaweza kujihusisha na uhalifu, kwa nini matapeli wasiige mfano kwa kujidai polisi, japo ni feki?
Mara kadhaa tumesikia taarifa kuhusu polisi wanaojihusisha na uhalifu, na ni majuzi tu kulikuwa na taarifa za kuchefua, baadhi ya polisi wakikamatwa na fuvu la binadamuAidha fuvu hilo ni la raia aliyeuawa na polisi hao au lilifukuliwa kutoka kaburini kwa minajili ya ushirikina au kutisha raia wasio na hatia watoe rushwa, si rahisi kufahamu.
Takriban kila mwananchi ‘wa kawaida’ ambaye amewahi kufika kituo cha polisi atakuwa anafahamu kuwa njia pekee ya kupata huduma inayostahili ni kwa ‘kumpatia chochote (rushwa) afande’ ili ashughulikie kilichompeleka mwananchi huyo kituoni hapo. Kwa kifupi, Jeshi la Polisi linanuka rushwa.
Kilichonishitua zaidi ni hiyo habari ya Ofisa Usalama wa Taifa feki. Kama nilivyotanabaisha awali, yayumkinika kuamini kuwa matapeli waliojifanya polisi walifanikiwa katika ‘upolisi’ wao feki kwa vile si jambo la ajabu kwa polisi kudai rushwa. Kwa lugha nyingine, sidhani kama kuna Mtanzania anayeweza kushtuka akiombwa rushwa na polisi kiasi cha kudhani kuwa polisi huyo ni feki.
Lakini kwa hili la matapeli kumudu kujifanya maofisa usalama wa taifa sio tu ni jambo la kuogopesha bali pia linalohitaji kuangaliwa kwa undani zaidi.
Itakumbukwa kuwa majuzi, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe alizungumzia tatizo la kushamiri biashara ya dawa za kulevya. Pamoja na mengi aliyoozungumzia, Mwakyembe alinukuliwa akishauri Idara ya Usalama wa Taifa ijiangalie upya.
Nadhani, kimsingi, Dk Mwakyembe alitumia lugha ya kistaarabu badala ya kutamka bayana kuwa miongoni mwa wanaofanikisha dawa za kulevya kuingia au kupita katika mipaka ya nchi ni baadhi ya maofisa wa usalama wa taifa.
Na hata kama Mwakyembe asingesema hayo (na hakutamka waziwazi), mtu yeyote anayeelewa utendaji kazi wa Idara hiyo hatoshindwa kuelewa kwamba taasisi hiyo ni sehemu ya tatizo hilo la kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya.
Ninaandika haya kwa sababu nina uhakika idara hiyo inawafahamu kwa majina, sura na makazi wahusika wa biashara hiyo hatari. Na ufahamu huo sio jambo la jana au juzi. Wahusika wanaofahamika kwa muda mrefu, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
Lakini licha ya kuwafahamu wahusika, kwa mujibu wa taratibu za kazi za taasisi hiyo, kila mpaka wa nchi yetu una Ofisa wa Idara hiyo ambaye ana jukumu la kuchunguza na kuzuia uwezekano wa watu wasiotakiwa au vitu visivyotakiwa kuingia nchini.
Sasa kama maofisa hao wanatimiza wajibu wao ipasavyo, iliwezekanaje, kwa mfano, shehena kubwa ya dawa za kulevya ya ‘akina Masogange’ ikaingia nchini na kusafarishwa hadi Afrika Kusini ilikokamatwa?
Jibu ni aidha maofisa husika walikuwa ‘busy’ na masuala yao binafsi, au wao pia walikuwa miongoni mwa waliofanikisha kuingizwa kwa shehena hiyo.
Katika mazingira ya kawaida, suala hili linaweza kuonekana dogo tu, na lisilopaswa kuumiza vichwa vyetu. Lakini kimsingi, kama tuna maofisa usalama wanaoweza ‘kuruhusu’ dawa za kulevya zipite chini ya uangalizi wao, kipi kitawazuia kuruhusu magaidi wasipite alimradi wana fedha za kuwafanya maofisa hao wapuuzie wajibu wao?
Pengine baadhi ya wasomaji wanaweza kuhisi kuwa nimekuwa nikiiandama sana taasisi hiyo muhimu. Ukweli ni kwamba kanuni za msingi kabisa za Idara ya Usalama wa Taifa wa nchi yoyote ile ni “Idara legelege husababisha taifa legelege.” Na moja ya viashiria vya udhaifu wa taasisi kama hiyo ni kushamiri kwa vitendo vinavyofanya umuhimu wa kuwa na taasisi kama hiyo.
Hapa ninamaanisha kuwa ukiona taifa fulani linaandamwa na matukio ya ufisadi, basi Idara yake ya Usalama wa Taifa ni legelege, sambamba na matukio mengine yanayohatarisha ustawi wa nchi kama vile ufisadi.
Kwa lugha nyepesi, kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya-kama ilivyo kushamiri kwa ufisadi - ni uthibitisho bayana kuwa taasisi hiyo muhimu imelegalega.
Ni katika mazingira hayo ya kulegalega kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa ndipo tunashuhudia matapeli wakipata ujasiri wa kujifanya maofisa wa Idara hiyo.
Kuna msemo kuwa ‘ili uongo ufanikiwe sharti uwe na ukweli ndani yake.’ Naam, matapeli wanaojifanya maofisa wa Idara hiyo wanafahamu fika kuwa kuna maofisa halisi wanaofanya yale yale yanayofanywa na baadhi ya polisi, yaani kutumia nyadhifa zao kwa minajili ya uhalifu.
Ningetamani sana kuhitimisha makala hii kwa kushauri nini kifanyike. Lakini nadhani nisipoteze muda wangu na wako msomaji kutoa ushauri utakaopuuzwa. Kutarajia uongozi wa taasisi hiyo ‘ujiangalie’ kama alivyoshauri Mwakyembe ni mzaha. Kwa nini watendaji wanaonufaika kwa kukiuka taratibu za kazi wajichunguze ilhali wanajua bayana hakuna ‘mwenye jeuri’ ya kuwachukulia hatua?
Kutarajia kwamba watawala wetu wanaweza ‘kuweka kando uoga’ na kuwavaa mashushushu wetu kuwaeleza kuwa ‘ndugu zetu, tunawatengea fedha nyingi kwa ajili ya usalama wa taifa letu, lakini hali inazidi kwenda kombo’ ni ndoto za mchana.
Labda, Rais Jakaya Kikwete, katika miezi takriban 20 iliyobaki kabla ya kumaliza awamu ya pili ya urais wake, atafakari upya kuhusu azma yake njema ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania, aamue ‘liwalo na liwe’ na kupambana kwa dhati na vyanzo halisi vya ufisadi na kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya. Akitaka anaweza, kwani uwezo anao, na sababu anayo, kinachohitajika ni nia tu.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/usalama-wa-taifa-wamepitisha-%E2%80%98unga%E2%80%99-airport-kwa-nini-wasipitishe-magaidi#sthash.LDXT2hxF.dpuf

Friday, August 30, 2013

EXCLUSIVE: Zari a.k.a "The Lady Boss" tells all on @thesporahshow

Wednesday, August 28, 2013

Magazeti ya Leo Jumatano 28.08.13: Usalama wa Taifa Wapitisha Unga Aiport, Magaidi je? (RAIA MWEMA)


.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.

NCHI INAUZWA: Mwarabu wa Oman anayedai kuwekeza wa Airport Dar ALISHAINGIA MITINI kuhusu ATCL


Naomba niwe mkweli. Kila nikiskia Mwarabu flani anawekeza sehemu, hisia ya kwanza ni jinsi twiga na wanyama pori wetu wanavyotoroshwa na Waarabu...na sakata la Loliondo lililopelekea kifo cha mwandishi mahiri wa habari za Uchunguzi, Marehemu Stan Katabalo.

Kwa kifupi, picha iko hivi: Mwaka jana Rais Jakaya Kikwete alipokwenda huko Uarabuni, aliwahamasisha wafanyabiashara wa huko kuja kuwekleza Tanzania akidai kuwa nchi yetu ina "fursa zisizo na kikomo" (unlimited opportunities) kwa Waarab hao.

Kufuatia ziara hiyo ya JK na wito wake kwa Waarabu hao, siku chache baadaye (Januari mwaka huu) zikapatikana taarifa kuwa kundi la wafanyabiashara wa Oman likiongozwa na kampuni ya AL-HAYAT DEVELOPMENT AND INVESTMENT COMPANY wanapanga kuwekeza dola za kimarekani milioni 100 kufufua shirka la ndege la Tanzania (ATCL), na memorundum of understanding ikasaniwa kati ya ATCL na bosi wa kampuni hiyo ya Oman Sheikh Salim Al-Harthy

Hata hivyo, mwezi Juni mwaka huu, Naibu wa Mawasiliano na Uchukuzi, Dkt Charles Tizeba, aliliambia Bunge kuwa 'mwekezaji huyo wa Oman ameingia mitini' Kadhalika, Naibu Waziri huyo alieleza kuwa hakukuwa na makubaliano yoyote yaliyosainiwa kati ya 'wawekezaji' hao na ATCL

Cha kushangaza, vyombo mbalimbali vya habari huko nyumbani vimeripoti jana kuwa mtu yuleyule SHEIKH SALIM AL-HARTHY na kampuni ileile ya AL-HAYAT DEVELOPMENT DEVELOPMENT AND INVESTMENT COMPANY inatarajia kuufanyia ukarabati Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar, kwa kutumia uwekezaji wa dola za Kimarekani milioni 100.

Hivi ndugu msomaji, hata tukiweka kando rekodi ya 'wawekezaji' wa Kiarabu katika kuhujumu uchumi wetu, inaingia akilini kweli kwa mtu yuleyule aliyeleta uzushi kuhusu uwekezaji kwenye ATCL, na kisha kuingia mitini, kukabidhiwa dhamana ya kuifanyia ukarabari aiport yetu kuu?

'Mwekezaji' huyo Mwarabu alinukuliwa na gazeti moja akida (nanukuu)

 Nimekuja kuwekeza hapa kwa kuitikia mwito wa Rais Jakaya Kikwete, amechoka sana inabidi sisi tumsaidie, ana nia nzuri ya kuhakikisha nchi hii inakuwa kiuchumi inabidi tumsaidie kuwekeza katika maeneo kama haya” alisema. Katika hatua nyingine mwekezaji huyo ametangaza kuwekeza ndege nane kwenye Shirika la Ndege la Tanzania(ATCL), mradi ambao unatarajiwa kugharimu dola za Marekani 100 milioni.

Tafadhali zinatia maneno hayo ya rangi nyekundu.

Cha kusikitisha zaidi, ni ukweli kwamba hata Waziri pekee anayeonekana kupigania haki za wanyonge, Dkt Harrison Mwakyembe, naye kaingia mkenge kwa kumsapoti Mwarabu huyo, na kunukuliwa akisema kuwa serikali imefanya kazi kubwa ya kuvutia wawekezaji hao...





Biashara ya UNGA imetufikisha mahala pabaya: Hawa ndio MAJAJI wanaowalinda wauza unga


Majaji wanaowalinda wauza 'unga' wabainika

* Gazeti hili sasa limeamua kuwataja kwa majina
* Mahakimu nao wanawaachia mapapa kienyeji
* Kigogo ofisi ya DPP, Mahakama Temeke, Kinondoni balaa


Na Waandishi Wetu, Dar na Zanzibar
Mahakama kupitia baadhi ya majaji na mahakimu wasio waadilifu imebainika kuwa kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Pamoja na Mahakama, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP), nayo imelaumiwa kwa kufuta kesi katika mazingira ambayo hata mtu ambaye hakusoma sheria, anaweza kuyatilia shaka. 
Wakati vyombo hivi vikikwamisha vita hii, lawama zimekuwa zikielekezwa kwa polisi na vyombo vingine vya usalama, ambavyo watendaji kazi wake wanafanya kazi usiku na mchana. 
Juhudi zote zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama zinagonga mwamba mahakamani kwa msaada wa ofisi hiyo ya DPP.
Wakati kesi nyingine zikifutwa, nyingine hazisikilizwi, kiasi cha kusababisha zirundikane mahakamani tangu mwaka 2005. Kesi chache zinazohusu watuhumiwa wakubwa wa kuuza ‘unga’ zinamalizwa haraka kwa utaratibu wa ofisi ya DPP kuwasilisha nia ya kutoendelea na mashtaka mahakamani (nolle prosequi) au wasimamizi hao wa utoaji haki kutoa hukumu zinazoacha wengi vinywa wazi na kuwakatisha tamaa polisi.
Katika hali ya kushangaza, majaji na mahakimu wamekuwa wakikiuka wazi Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya Na, 9 ya Mwaka 1995 inayozuia mtu yeyote aliyekamatwa na dawa zenye thamani kuanzia Sh milioni 10 asipewe dhamana, lakini hilo halizingatiwi. JAMHURI haikubahatika kufahamu bayana nini kinawapofusha majaji na mahakimu wakati ‘mapapa’ wanapofikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuuza unga, lakini ni wazi kuwa kuna mtandao mkubwa wa kulindwa kwa watuhumiwa hao wenye ukwasi mkubwa.
Wakati polisi wanafanya kazi ya hatari usiku muda wote, wakipambana na wauaji, wahongaji na watu wanaouza dawa za kulevya, kesi za mapapa zinamalizwa kienyeji mahakamani.
Moja ya kesi inayotia shaka ni Na. 47 ya Mwaka 2011. Kesi hii ilifunguliwa dhidi ya watuhumiwa Fredy William Chonde, Kambi Zuberi Seif; ambao ni Watanzania na Abdulghan Peer Bux na Shaaban Malik ambao ni raia wa Pakistani.
Hawa walikamatwa eneo la Mbezi Beach, Dar es Salaam wakiwa na kilo 175 za heroin, ambako kesi dhidi yao ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini humo. Wakati kesi inaendelea Kisutu, mawakili wa vigogo hawa walikwenda Mahakama Kuu wakafungua shauri la kuomba wapewe dhamana chini ya Jaji Pendo Msuya, wakitambua kuwa sheria inazuia.
Bila kuchukua jalada wala kuwasiliana na Mahakama ya Kisutu, huku Jaji Msuya akijua fika kuwa kilo 175 ambazo thamani yake ni zaidi ya Sh bilioni tano, na watuhumiwa hawapaswi kupewa dhamana; yeye kwa mamlaka aliyonayo kama Jaji aliamua kuwapa dhamana watuhumiwa hawa. Baada ya kupata dhamana, Wapakistani walirejeshewa pasipoti zao na wakakimbia nchi. Hawajakamatwa hadi leo.
“Cha kusikitisha kesi iliendelea bila kujua kuwa watuhumiwa wamekwishapewa dhamana na hadi Aprili 8, mwaka huu 2013 kesi hiyo ilitajwa… baadaye Mahakama ikapewa taarifa kuwa watuhumiwa walishapewa dhamana na Mahakama Kuu ndiyo maana hawaonekani mahakamani. Tulishangaa sana,” kilisema chanzo chetu kutoka Mahakama ya Kisutu.
Kesi nyingine iliyomalizwa kienyeji ni ya Mwinyi Rashid Mkoko. Vyanzo vya JAMHURI vinaonesha kuwa huyu na familia karibu yote wanatuhumiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya. Ndugu zake waliokamatwa kwa nyakati tofauti na baba yao, ambako mmoja alidhulumiana, na ‘mzigo’ na wauza unga, hali iliyofanya wamuue kwa kumpiga risasi.
Katika familia hii, Rashid Ismail Mkoko ndiye aliyeuawa na wauza unga wenzake eneo la Ilala, Dar es Salaam. Huyu alipata kukamatwa kuhusiana na dawa za kulevya, ila pia kwa kosa la mauaji. Shuhuda wa tukio la Rashid Ismail Mkoko anasimulia kama ifuatavyo:“Huyu ndiye wa kesi ile ambayo kijana aliyemtuma mzigo Pakistan pipi zilipasukia tumboni akafia gesti kule Tabata, Dar es Salaam. Mmoja wa ndugu wa kijana huyu aliyefariki, alimpigia simu akamwambia ‘si unajua alikuwa na mzigo wako ndiyo umemuua? Sasa mbona umetususa? Hata maji ya kunywa hutupatii msibani?’
“Mkoko akamwambia nitakuja jioni. Na kweli jioni iliyofuata akampigia simu kuwa anakwenda hapo nyumbani msibani. Alipofika akampigia simu, akamwambia njoo tuonane. Huyu ndugu wa kijana aliyefariki akatoka nje, akaenda kwenye gari kuonana na Mkoko.“Alipofika Mkoko akamuuliza ndiye wewe uliyenipigia simu jana, yule ndugu wa marehemu akajibu ‘ndiyo’, basi Mkoko alichofanya akatoa bastola akampiga risasi ya usoni yule kijana…akafariki papo hapo, Mkoko akaondoka.

“Polisi walimkamata wakamfikisha mahakamani. Mahakama ikamwachia kwa mizengwe. Ila Mungu si Athumani, ikatokea naye akadhulumu wauza unga wenzake huko Ilala, nao wakamuwinda wakampiga risasi akafa mwaka juzi.
“Huyu alikuwa muuza dawa za kulevya mkubwa. Mdogo wake Mwinyi Rashid Mkoko, naye anauza dawa. Tulimkamata na heroin gramu 250 zenye thamani ya Sh milioni 11, ikafunguliwa kesi Temeke Na. PI 26 chini ya Hakimu Mkwawa, lakini ajabu wakati kesi inaendelea kutajwa Temeke hadi leo, huyu Mwinyi Mahakama Kuu imekwishamwachia huru bila vielelezo vyovyote,” kilisema chanzo chetu kutoka mahakamani.Uchunguzi wa JAMHURI umeonesha kuwa awali mawakili wa Mwinyi waliwasilisha ombi la dhamana kwa Jaji Munisi, ambaye aliwaelekeza mawakili wa Serikali kuwa badala ya kumshtaki Mwinyi kwa kukutwa na dawa za kulevya, waiondoe kesi mahakamani na kuifungua upya kama kesi ya kusafirisha dawa za kulevya. Kwa kawaida tuhuma za aina hiyo huwa hazina dhamana.Mawakili walivyopata mwanya huo, wanajua jinsi walivyozungumza na wanasheria wa Serikali. Kesi hiyo badala ya kuiondoa kama alivyoelekeza Jaji Munisi wakaihamishia kwa Jaji Dk. Fauz Twalib, ambaye katika hukumu yake ya Julai 30, 2012 alikiri kuwa mbele yake halikufikishwa jalada la kesi hiyo na wala hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza kwani yeye si hakimu, ila akasema kwa kuwa Mahakama ya Temeke haina mamlaka ya kusikiliza kezi za dawa za kulevya kama cocaine, basi akatoa fursa ya kumsikiliza mtuhumiwa.“Kwa kasi ya aina yake, siku hiyo hiyo ya Julai 30, 2012 baada ya Jaji Dk. Fauz kutoa hukumu hiyo ya ajabu, mawakili wa Serikali ambao ni upande wa mashitaka wakawasilisha nolle chini ya Section 91 ya CPA (Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka), hivyo Mwanasheria wa Serikali Mpembo kwa niaba ya DPP akawasilisha hati hiyo, na Jaji Fauz akaifuta kesi dhidi ya Mwinyi.“Kisichoeleweka na kufahamika ni nini kilitokea na nini kiliendelea siku hiyo hiyo kutoa hukumu, na siku hiyo hiyo Mpembo akawasilisha nolle na kesi ikafutwa siku hiyo hiyo. Hapa kuna maswali mengi. Mwinyi amekimbilia Zanzibar. Yupo anaponda raha, kesi bado ipo Temeke na hakuna kinachoendelea,” kimesema chanzo chetu.Baba yao Mwinyi na Rashid, naye kwa nyakati tofauti anadaiwa kukamatwa na polisi akituhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Mtoto wake mwingine, Abubakar Mkoko, yeye alitolewa dawa za kulevya tumboni, lakini Mahakama ikampiga faini ya Sh milioni 1 na kumwachia huru.Kesi nyingine inayowakosesha usingizi polisi ni ile ya Dhoulkefly Awadh Abdallah Na. 238 ya Mwaka 2010. Kesi hii ilimhusisha Abdallah na mkewe Asha Seif Kiluvya. Asha ndiye aliyekamatwa na dawa za kulevya. Hata hivyo, katika mazingira ya kutatanisha, ofisi ya DPP ilipeleka nolle prosequi mahakamani Asha akaachiwa huru, na sasa anashitakiwa Abdallah ambaye hakukutwa na kitu chochote.Kioja kinginge kilifanywa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kinondoni anayetajwa kwa jina la Msongo. Kesi hii ilianza mwaka 2005 na kumalizika mwaka 2008. Mshitakiwa alikuwa Yusufu Hassan Yossye, mkazi wa Kinondoni A, Mtaa wa Togo, aliyekutwa na gramu 1,244 za heroin ambazo alikamatwa nazo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Aliwekwa chini ya ulinzi kwa lengo la kumfanya atoe ‘pipi’ kwa njia ya haja kubwa. Katika hukumu ambayo inatia shaka Hakimu Msongo aliandika hivi:“Katika ushahidi wote uliotolewa, hakuna ubishi kuwa ni kweli amekutwa na dawa za kulevya. Pia ushahidi unaonesha kuwa mshitakiwa alitoa madawa hayo kwa njia ya haja kubwa. Hata hivyo, upande wa mashitaka umeshindwa kueleza ni dalili zipi zilipelekea (zilisababisha) kushukiwa kuwa mshitakiwa ana madawa ya kulevya. Na pia hawakushirikishwa watu au wataalamu wa afya ya binadamu.“Upande wa mashitaka katika ushahidi wao umeonesha walipishana kutoa idadi [ya pipi alizotoa kwa haja kubwa]. Kutokana na hilo, ushahidi hautoshelezi na mshitakiwa namwachia chini ya Kifungu cha 235 cha CPA (Kanuni ya Mwenendo wa Mashitaka) katika mashitaka yote mawili.” Hukumu hii ilitolewa na Hakimu Msongo Mei 2, 2008. Yossye alikuwa akishitakiwa kwa kukutwa na dawa; na pia kwa kuwaambia polisi uongo kuwa hakuwa na dawa, lakini baadaye akazitoa kwa njia ya haja kubwa.Katika Mahakama ya Kisutu, mwanamke mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Pilly, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na zawadi ya kinyago ambacho ndani yake kilikutwa na dawa za kulevya, lakini Mahakama ya Kisutu wakati inatoa taarifa ilimwachia huru Pilly kwa maelezo kuwa wakati polisi wanamkamata, hakuwapo mwanamke, hivyo ni kosa mhalifu mwanamke kukamatwa na polisi mwanaume. Akaachiwa huru!
Kesi nyingine ni ya Kwaku Sarfo, raia wa Ghana, alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere mnamo Novemba 14, 2010. Thamani ya dawa ilikuwa Sh milioni 390. Kesi ilipelekwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Samora kwa Hakimu Mkazi Luago.“Tulishangaa, kwamba kwanza Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi hii, lakini pia baada ya kupita siku 60; bila mamlaka kisheria, Hakimu Luago akaifuta. Hakimu huyu ni kero. Amehamishiwa Lindi akagoma kwenda. Hatujui anapewa jeuri na nani. Tungeomba Rais Kikwete na mhimili wa Mahakama waingilie kati suala hili vinginevyo nchi inateketea,” kimesema chanzo chetu.Uchunguzi umebaini kuwa kati ya kesi 423 zilizofikishwa Mahakama Kuu kati ya mwaka 2005 na 2013 hadi leo kesi iliyokwisha ni moja tu ya Shaaban Mintanga, ambayo nayo imeisha kutokana na mashahidi muhimu kufariki dunia kabla kesi haijasikilizwa. Kati ya mashahidi waliofariki dunia ni Mkemia Mkuu, Dk. Ernest Mashimba, aliyefariki Septemba 2010.
Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa, alikiri matukio hayo kuwapo na akasema: “Mimi mamlaka yangu ni kukamata, na kuwafikisha mahakamani. Sasa huko kama mmekuta hali iko hivyo, ambayo ni kweli kimsingi inasikitisha na kukatisha tamaa, inabidi muwaulize huko mahakamani au kwa DPP wao ndiyo waeleze nini kinatokea.”
JAMHURI haikufanikiwa kuzungumza na Msajili wa Mahakama Kuu kwani mara zote kila mwandishi wetu alipofika aliambiwa yuko kwenye vikao kwa wiki nzima, na hata alipoacha ujumbe wa maandishi haukujibiwa.
Baada ya juhudi za kumpata Msajili wa Mahakama Kuu kugonga mwamba, JAMHURI iliwasiliana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, ambaye Kamisheni ya Dawa za Kulevya iko chini yake. Yeye alisema ni kweli tatizo hilo lipo, na kwamba kuna mengi zaidi ya hayo.
“Mimi nasema sheria zinapaswa kubadilishwa, na Serikali tayari imeanza mchakato. Mtu akipatikana na pipi za dawa za kulevya zikatolewa tumboni mwake, nataka sheria irahisishwe na kuwezesha ashitakiwe na kufungwa maisha ndani ya siku saba.
“Hali ilivyo sasa ambapo unapaswa kuhifadhi ushahidi kwa miaka hadi 10 ukiendesha kesi moja, ushahidi unapoteza ubora. Wakati mwingine mtuhumiwa anashindwa kesi anatozwa faini ya Sh 500,000. Hatuwezi kupambana na dawa za kulevya tukashinda vita hii kwa utaratibu huo.
“Sasa Serikali imejipanga, ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mahakama maalum ya kudhibiti dawa za kulevya na kwa kweli katika hili tunataka mchakato uwe mfupi kadiri inavyowezekana. Ndani ya muda mfupi kadiri inavyowezekana tupitishe sheria hii ili sheria iwe kali itoe adhabu itakayowazuia wengine kufanya biashara hii,” alisema Lukuvi.
Hivi karibuni, Tanzania imeanza kuzungukwa na sura ya kuwa Taifa la wauza dawa za kulevya baada ya Watanzania wengi kukamatwa ndani na nje ya nchi wakiwa na dawa hizo. Taarifa za uhakika zilizoifikia JAMHURI zinasema Rais Jakaya Kikwete ametoa maelekezo ya dhati kuhakikisha linafanyika jambo kubwa litakalowezesha kukamata mtandao wa wauza dawa za kulevya na kumaliza tatizo hili nchini.
Kwa mwezi mmoja sasa, JAMHURI imekuwa ikichapisha orodha ya wauza unga ‘dagaa’ na ‘mapapa’ hapa nchini, ambako hadi sasa gazeti hili limekwishatangaza

hadharani majina ya wauza unga 504 katika matoleo manne yaliyotangulia.
CHANZO: Jarida la Jamuhuri

Kushamiri kwa biashara ya SEMBE: Mwanamke wa Kitanzania aliyedakwa Dubai adai alifanywa punda na mumewe

Woman caught with Dhs3 million of drugs blames husband for...

Mwanamke wa Kitanzania aliyekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai akiwa na madawa ya kulevya yenye thamani ya Dirham milioni tatu (takriban shilingi bilioni 1.3 za Kitanzania) amedai kuwa alifanywa 'punda' na mumewe.

Mwanamke huyo ambaye hata hivyo hajatajwa jina alikamatwa na kilo 3 za 'unga' (cocaine) akitokea nchini Brazil, ambapo alipita transit Dubai, kwa madhumuni ya kuja Tanzania.

Kwa mujibu wa Polisi wa Dubai, mwanamama huyo alieleza kuwa alitibuana na mumewe, na mumewe akaamua kumpeleka Brazil kwa mapumziko, na wakati anarejea kutoka huko alikabidhiwa suitcase ambayo baadaye iligundulika kuwa ina madawa hayo ya kulevya.

Polisi hao wanasema kilichopeleka mwanamke huyo kushtukiwa na hali yake ya kutia mashaka wakati akiwa airport hapo.

Kesi yake imewasilishwa kwa waendesha mashtaka kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria

iMETAFSIRIWA KUTOKA TOVUTI YA 7 Days in Dubai


Monday, August 26, 2013

Magazeti ya Tanzania Leo Jumatatu Agosti 26, 2013


Saturday, August 24, 2013

Magazeti ya Leo 24.08.13: Afisa Usalama feki MWINGINE anaswa, Ndege Ya Rais Yabeba Mkaa


.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
.

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India