Makamba awatukana wanaoshauri Kikwete asigombee 2010
Rais Kikwete kongamano la Nyerere limemweka katika lawama za kutokuwa na maamuzi na kuwa asipendekezwe kugombea awamu ya pili.
Na Leon Bahati
KATIBU mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ambaye katika miezi ya karibuni amekuwa akihaha kutoa ufafanuzi, kukanusha au kujibu tuhuma mbalimbali dhidi ya chama hicho tawala, jana alikuwa na kazi nyingine ya kumtetea Jakaya Kikwete baada ya waziri katika serikali ya awamu ya tatu kushauri asiteuliwe kugombea urais 2010 iwapo atashindwa kufanya maamuzi magumu dhidi ya mafisadi.
Safari hii, Makamba alitumia maneno makali kumjibu waziri huyo, Matheo Qares akisema watu wenye fikra kwamba CCM inaweza kumtosa mwenyekiti wake kwenye mbio za urais wakati wa uchaguzi mkuu wa mwakani, "ni wehu".
Qares, ambaye aliwahi kushika wadhifa nyeti wa Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma, alitoa rai hiyo juzi kwenye kongamano la kumuenzi muasisi wa taifa la Tanzania aliposema kuwa CCM haina budi kutafuta mwanachama mwingine wa kugombea nafasi ya urais mwaka 2010 iwapo Kikwete atashindwa kufanya maamuzi magumu dhidi ya mafisadi, ambao alisema hawakijui chama na wengine uraia wao una utata.
Lakini jana, Makamba alisema watu wenye fikra hizo ni wehu kwa kuwa uteuzi wa wagombea ndani ya CCM ni mchakato usiotoa ruhusa kwa mawazo binafsi ya watu.
"Mtu mwenye akili nzuri hawezi kusema kwamba Rais Kikwete ameshindwa kutekeleza wajibu wake. Anayefikiria hivyo, ni mwehu," alisema Makamba alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli hizo.
Alisema ni vyema watu hao wakafahamu kuwa mgombea urais wa CCM anateuliwa kwa mujibu wa taratibu za chama kupitia vikao mbalimbali hivyo, wazo binafsi halina nafasi.
Alipoulizwa kuhusu shutuma zinazoelekezwa kwa Rais Kikwete, Makamba alisema asingependa kujibu hoja zilizotolewa na mjumbe mmoja mmoja kwenye kongamano hilo.
Lakini akaeleza kwamba yupo tayari kutoa maoni yake binafsi baada ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuwasilisha kwake mapendekezo waliyofikia kwenye kongamano hilo.
"Mimi mwenyewe sikuwepo kwenye kongamano hilo. Wala sijui mapendekezo yao. Siwezi nikatolea maoni hoja za mtu mmoja mmoja alizotoa kwenye Kongamano hilo. Nitakapopata mapendekezo ya jumla ya taasisi hiyo, nitakawa katika nafasi nzuri ya kutoa maoni yangu."
Katika kongamano hilo, Rais Kikwete amekuwa akilaumiwa kwa kutochukua hatua dhidi ya watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wengi wao wakielezwa kuwa ni wafanyabiashara ambao wanatuhumiwa kukiteka chama kwa kutumia nguvu zao za pesa.
Wakati fulani Joseph Butiku, mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambayo iliandaa kongamano hilo, alisema Rais Kikwete amezungukwa na mafisadi ambao wanaitafuna nchi.
Akizungumza kwenye kongamano hilo juzi, Qares alisema rais hana budi kufumba macho na kuwashughulikia hao watuhumiwa ambao wanadai Kikwete hakujuana nao barabarani na kama atashindwa basi ashauriwe kuwa miaka yake mitano inamtosha.
Kabla ya Qares, Musa Nkangaa, ambaye aliwahi kuwa waziri kwenye serikali ya awamu ya pili, aliituhumu CCM kuwa imepoteza hadhi na kujikuta ikikumbatia matajiri wachafu.
Kwa mujibu wa Nkangaa, CCM imekuwa si chama cha wakulima na wafanyakazi tena, bali kimebaki kuwa chama cha matajiri.
"Ndiyo maana imekuwa ikiweweseka kuwashughulikia watuhumiwa wa Richmond na Kagoda," alisema akimaanisha kashfa ya utoaji zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa Richmond Development Company LLC na tuhuma za wizi wa mabilioni ya fedha kutoka BoT.
Si Wanasiasa peke yao wana sifa hiyo ya kujipendekeza kwa watawala hata wakiona kuwa wanakwenda ndipo sipo. Wahandishi wa habari wa Tanzania wengi sana ni wanafiki. Utakuta mwandishi wa habari anampinga Kocha wa taifa kwa sababu timu haifanyi vizuri, au kutokana na uteuzi wake. Ila huyo huyo mwandishi wa habari akiandika kuhusu raisi atakwambia mawaziri wake wanamuangusha. MIMI NASHINDWA KUELEWA HAWO MAWAZIRI NI NANI ANAWACHAGUA. kama mtu hawezi kuteua watu wa kufanya naye kazi, kweli mtu huyo ataweza kufanya kazi anayokusudiwa kufanya?. AU RAISI ANATEULIWA MAWAZIRI? Kama unaweza kumlaumu kocha na kujenga hoja ajiuzulu kwa kushindwa kuteua wachezaji bora na kuongoza timu kwenye ushindi, kwanini isiwe raisi. SWALA LA KUCHAGUA WATU WA KUFANYA NAO KAZI KWA KUTUMIA KIGEZO CHA KUJUANA ZAIDI KULIKO UWEZO WA MTU NI HATARI NA NI UDHAIFU MKUBWA KWA KIONGOZI WA NCHI. Mimi sioni tofauti ya makamba na mawaziri wengi wa serikali ya kikwete na wachangiaji wengi wa kwenye blog ya michuzi, wanaokosoa mtu badala ya hoja mtu aliyoiwakilisha. KAMA KIONGOZI MWENYE UZOEFU MKUBWA NAMNA HII KWENYE SIASA ANAWEZA KUTOA MAONI YA NAMNA HII. INANITIA WASIWASI MKUBWA SANA NA TIMU YA KIKWETE. Na waandishi wa habari wengi wa Tanzania wanaona hii ni hali ya kawaida. badala ya kuchambua hii habari wao wataripoti kama ilivyo tena kwa kuiremba. KAZI KWELI KWELI......
ReplyDelete