Featured Posts

Tuesday, May 29, 2012

I Miss You So Much,Mom: Kumbukumbu ya Miaka Minne ya Kifo cha Mama Chahali


Mama mpendwa,ilikuwa siku kama yale leo,miaka minne iliyopita,uliondoka hapa duniani wakati tunakuhitaji sana.Japo miaka minne inaweza kuonekana ni muda mrefu kusahau machungu,kwangu mwanao imeshindikana.Kila siku ya Mungu ninaposali kukuombea pumziko na raha ya milele huko ulipo,hujikuta napatwa na uchungu usioelezeka.Kwa kifupi,mama mpendwa,kila siku baada ya kifo chako-siku kama ya leo miaka minne iliyopita,imeendelea kuwa ni hudhuni na majonzi yasiyoelezeka.

Mama mpendwa,ulikuwa ni zaidi ya mama kwangu,kwa mumeo-Baba Mzee Chahali,na kwa wanao wote na ndugu na jamaa.Nakumbuka mwaka 2005 nilipokuja likizo nyumbani,ulirukaruka kwa furaha,ukanikumbatia na kunipakata mwanao,ukaniandalia maji ya kuoga,ukanifanya nijsikie kama mtoto mchanga.Sikujua kuwa furaha ile ya mzazi kumwona mwanae waliopoteana kitambo kidogo sintoipata tena maishani.Inaniuma sana.

Nakumbuka wakati huo ambapo wewe na Baba mlikuwa mnasherehekea miaka 50 ya ndoa yenu,ulinipa mafundisho mengi kuhusu maisha,ndoa,upendo na zaidi ni kumweka mbele Mungu katika kila ninalofanya.Kabla ya kifo chako,nilikuwa nauangalia mkanda niliowarekodi wewe na Baba,na kila nilipofanya hivyo niligundua kuwa nina bahati ya pekee kuwa na wazazi wanaonipenda kiasi hicho.Sikujua kuwa mahojiano yale ndio ulikuwa wosia wako kwangu mwanao.Kwa sasa sina nguvu ya kuangalia video hiyo,kwani kila nikijaribu naishia kububujikwa na machozi.

Nakumbua nilipokwenda chumba cha maiti na kukuona umelazwa kwenye zile friji wanzohifadhia maiti.Nilikugusa mama,nilitaraji muujiza kwamba ungeamka na ndoto ile mbaya ingeisha.Hukuamka hadi leo hii.

Mama,inaniuma sana kwani nilipokuja kukuuza Februari 2008 ulikuwa umeshapoteza fahamu.Ulipokuwa Muhimbili na baadaye St Francis,Ifakara,nilikuwa najaribu kukusemesha.Kama vile ulifahamu mwanao nimekuja kukuuguza,kuna nyakati ulikuwa unatoa tabasamu lako lenye mwanya ulionirithisha.Nikategemea utaamka na kunieleza japo neno moja.Kwa bahati mbaya hadi unafariki hukuweza kuniambia chochote.Inaniuma sana mama.

Inauma zaidi ninapopiga simu nyumbani.Nilizowea kuwa nikimaliza kuongea na Baba anakupa simu wewe tupige stori.Sasa,kila ninapompigia mzee huwa najikuta nataka kumwambia Mzee akupe simu niongee nawe,kisha nakumbuka kuwa hauko nasi.Kila simu ninayopiga nyumbani inanirejeshea kumbukumbu hizo na kuniacha mpweke,mkiwa na mwenye uchungu mkubwa.

Nyakati nyingine baadhi ya watu wangu wa karibu (ninao wengi kutokana na malezi bora uliyonipatia) huwa wananiona kama dhaifu ninapowaeleza uchungu nnilio nao takriban kila siku tangu ufariki.Siwalaum,kwani wanachojitahidi kufanya ni kunishawishi nikubali ukweli kuwa haupo nasi na haiwezekani kukurejesha.Kuna wakati wananichukiza kwani najihisi kama hawaelewi jinsi kifo chako kinavyoniathiri.Lakini baadaye akili hunirejea na kutambua wanachofanya ni kujaribu kunisaidia tu.

Mama mpendwa,sijui nisemeje.Rafiki zako wakubwa,wanao vitinda-mimba,Kulwa na Doto,ndio wananitia uchungu zaidi,kama ilivyo kwa Baba.Watatu hao pamoja na wewe mlikuwa kama marafiki.Nakumbuka siku zile nawapigia simu na kuwasikia mnacheka,mnataniana na kunipa kila aina ya faraja.Kwa sasa imebaki kumbukumbu tu.

Mama mpendwa,siku ya mazishi yako Padre alituambia maneno haya: "Mama Adelina alikuwa mtu wa watu,na kila anayemjua anafahamu hilo.Japo mnaomboleza kifo chake,lakini mnapaswa kupata faraja kuwa kutokana na matendo yake mema,Baba Yake wa Mbinguni Ameamua kumchukua.Sote tulimpenda lakini Mungu alimpenda zaidi,na ndio maana amemchukua." Maneno hayo ndio nguvu pekee inayonisaidia kumudu kufanya mambo mengine maishani.

Basi naomba nikuage tena mama kwa kumwomba BWANA AKUPATIE PUMZIKO LA MILELE NA MWANGA WA MILELE AKUANGAZIE,UPUMZIKE KWA AMANI AMEEN.

Sunday, May 27, 2012

Makala Za Sauti Toleo La Tatu: Vurugu za Zanzibar Na Hatima ya Muungano

Naomba kuwaletea toleo la tatu la mfululizo wa Makala za Sauti.Kamanilivyobainisha katika matoleo mawili yaliyopita,hadi sasa bado nipo katika hatua ya majaribio.Ninafanya kila linalowezekana kupata vitendea kazi bora kabisa(ikiwa ni pamoja na softwares mwafaka) ili kukupatia wewe msikilizaji ubora unaostahili.

Katika toleo hili ninazungumzia Vurugu zinazoendelea huko Visiwani Zanzibar na sualazimala Muungano kwa ujumla.Kwa hakika,kiwango cha ubora wa makala hiyo bado sio cha kuridhisha,na pia sijapata kujiamini vya kutosha katika uwasilishaji wa mada husika (kwa mfano kutumia muda kidogo kuamua nitumie neno gani) lakini huu ni mwanzo,na ninadhamiria kwa zaidi ya asilimia 100 kuwa muda si mrefu nitawaletea kitu bora kabisa na mnachostahili kwa dhati.

Labda la mwisho ni kwamba ninafanya kila linalowezekana ili toleo zima la makala husika liwe kwa lugha ya taifa,yaani Kiswahili.Hiyo ni moja ya sababu ya wakati flani kuwa ninahangaika nitumie nheno gani mwafaka la kiswahili.Si kwamba nimesahau lugha yangu ila moja ya madhara ya kuwa huko nje kwa muda mrefu ni hilo.

Karibuni sana,na msisite kunitumia maoni (chagua player yoyote kati ya hizi mbili hapa chini)
 

Taswira za Mkutano wa Chadema KatikaViwanja vya Jangwani



Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Dk Wilbrod Slaa akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.




 Mwenyekiti wa Taifa Freeman Mbowe Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA  akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


Mbunge wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Singida Magharibi Mheshimiwa Tundu Lissu akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


 Mbunge Wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Ubungo Mheshimiwa John Mnyika akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


Mbunge  wa Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Mbeya Mjini Mheshimiwa Joseph Mbilinyi aka Mr II(SUGU) akiwahutubia wafuasi wa chama hicho leo katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa kampeni yao ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.


 Viongozi wa chadema wakifurahia kadi nyingi za CCM zilizorudishwa leo jioni kwenye mkutano
Deo Munish Katibu mkuu wa BAVICHA akiteta jambo na mmoja aliyehudhuria mkutano wa CHADEMA Wa uzinduzi wa kampeni ya VUA GAMBA VAA GWANDA ambayo itazunguka mikoa yote ya Tanzania.




  Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe akiwaaga wananchi waliokuwa wamefurika makao makuu ya chama kinondoni walikofika wakitokea jangwani usiku huu
 Mbowe akiwatania wanachama ofini kinondoni baada ya wananchi kuanza kudai chama kimfukuze John Shibuda.Alikuwa akijifanya hasikii wanachosema na hapa anajaribu kuwasikiliza zaidi.hata hivyo Mbowe aliwaondoa wasiwasi na kusisitiza kuwa chama kinao utaratibu wa kushughulika na viongozi wanaokiuka maadili ya chama na kuwaomba wawaamini kama viongozi kuwa wanaouwezo wa kulishughulikia jambo hilo na mengine
 Mh.Mbowe na Mnyika wakiwa wamesimama kwenye gari wakati wa matembezi wakitoka kwenye mkutano
Aliyekua Mbunge wa Arusha Mjini(CHADEMA)Mheshimiwa Godbless Lema akiwa juu ya gari huku akishangiliwa na vijana jioni baada ya mkutano
 Sehemu ya umati uliowasindikiza viongozi wa chadema toka jangwani hadi kinondoni.wamesambaa yapata saa 2 usiku.

PICHA ZOTE NA MAELEZOKWA HISANI YA BLOGU YA MHESHIMIWA HAKI NGOWI

Mheshimiwa Balozi Peter Kallaghe awasilisha Hati za Utambulisho Ireland,Aongea na Watanzania

 Mh. Balozi Peter Kallaghe akiwasilisha barua ya utambulisho kwa Rais wa Ireland Michael Higgins


 Mh. Balozi Peter Kallaghe katika picha ya pamoja  na Rais wa Ireland Michael Higgins mara baada ya kuwasilisha barua ya utambulisho

 Mh. Balozi Peter Kallaghe na mke wake Mama Balozi Joyce Kallaghe katika picha ya pamoja  na Rais wa Ireland Michael Higgins mara baada ya kuwasilisha barua ya utambulisho


Afisa ubalozi Amos Msanjila na Mh. Balozi Peter Kallaghe katika picha ya pamoja na Rais wa Ireland Michael Higgins mara baada ya kuwasilisha barua ya utambulisho.




 Mh. Balozi Peter Kallaghe akiwa na baadhi ya watanzania waishio Dublin, 
Ireland




Baadhi ya watanzania waishio Dublin wakichagua chakula kutoka kwenye menu huku maongezi yakiendelea.




Mh. Balozi Peter Kallaghe akikabidhiwa zawadi na watanzania waishio Dublin.




 Mh. Peter Kallaghe, mama Balozi Joyce Kallaghe, Afisa ubalozi Amos Msanjila wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watanzania waishio Dublin.


Picha na maelezo kwa hisani ya Jestina George Blog

Miss Dar Inter-College 2012 Kurindima Club SunCiro Juni 8



SHINDANO la kumsaka Miss Dar Intercollege 2012 linatarajiwa kufanyika Juni 8 kwenye ukumbi wa Sunciro, ulipo Sinza Shekilango jijini Dar es Salaam, imefahamika.
Mratibu wa Shindano hilo Dina Ismail (pichani juu) alisema jana kwamba warembo watakaoshiriki shindano hilo wanaendeleza na mazoezi kwenye hoteli ya Lamada jijini Dar es Salaam chini ya ukufunzi wa Marylidya Boniface, huku kwa upande wa shoo wakinolewa na Bob Rich.
Alisema mpaka sasa warembo 12 kutoka vyuo vya Biashara (CBE), Uandishi wa Habari (DSJ) na Time, Ustawi wa Jamii na kile cha Usimamizi wa Fedha (IFM) wamesharipoti kambini.
Dina aliwataja warembo hao kuwa ni pamoja na Hilda Edward, Nancy Maganga, Saada Seleman, Neema Nashon, Rose Muchunguzi, Fina Revocatus,Jane Augustino,Theresia Issaya na Natasha Deo.Taji la kitongoji hicho linashikiliwa na Rose Msuya kutoka IFM.
Kwa upande mwingine, mratibu huyo ameyaomba makampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini shindano hilo ambalo linatarajiwa kuwa la aina yake na hasa ikizingatiwa kuwa washiriki wake wana vigezo vya hali ya juu.
“Tunaomba makampuni mbalimbali yajitokeze kudhamini shindano letu…mpaka sasa wadhamini tulionao ni pamoja na kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Redd’s, Lamada Hotel, Ndege Insurance, Dodoma Wine na Clouds Fm.

Ama Kweli Dunia Ina Vituko:Eti Mganga wa Kienyeji Kalazwa Hospitali



Ama kweli dunia haiishiwi vituko.Katika mazingira ya kawaida haingii akilini kusikia mganga wa kienyeji kalazwa hospitali "ya kawaida" (yaani inayotibu kwa kutumia dawa za kisasa badala ya mitishamba).Hivi,kama mganga anaweza kutibu wagongwa pasipo kutumia dawa za kisasa,iweje yeye akiugua anaenda hospitali kutumia dawa hizo badala ya mitishamba yake?

Hili linapaswa kuwa fundisho kubwa kwa wanaotegemea tiba za kienyeji.Ukiona waganga wanaotibu kwa ndumba wanakimbilia hospitali huhitaji kujiuliza mara mbili kuhusu ufanisi wa dumba hizo.

Pichani juu ni Mbunge wa Korogwe Vijijini kwa tiketi ya CCM, 'Profesa' Maji Marefu,ambaye imeripotiwa kuwa amelazwa nchini India kwa matibabu ya ugonjwa ambao haujafahamika.

Hata hivyo,blogu hii inamtakia mganga huyo apate nafuu katika matibabu anayopatiwa ili arejee nchini kuutumikia umma kisiasa na katika tiba zake za asili.

Thursday, May 24, 2012

Makala Yangu Ndani ya RAIA MWEMA Mei 23 "Uamuzi mgumu na ujasiri wa kisiasa"




Uamuzi mgumu na ujasiri wa kisiasa

Evarist Chahali
Toleo la 240
23 May 2012
WIKI iliyopita, Rais wa Marekani, Barack Obama, aliingia kwenye vitabu vya historia ya taifa hilo kwa kuwa kiongozi wa kwanza kuunga mkono ndoa za watu wa jinsia moja. Kwa muda mrefu Obama alikuwa aidha akipinga suala hilo nyeti au kuchelea kuweka wazi msimamo wake.
Tayari suala hilo la ndoa za jinsia moja limezua mgawanyiko mkubwa wa kimtizamo ingawa kura mbalimbali za maoni zinaonyesha kuwa msimamo huo ‘mpya’ wa Obama hautoathiri kwa kiasi kikubwa maamuzi ya wapigakura katika uchaguzi mkuu wa Marekani unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa kura za maoni za hivi karibuni, takriban asilimia 60 ya Wamarekani wanasema kitendo cha Obama kuunga mkono ndoa za mashoga hakitowashawishi kumpigia au kutompigia kura.
Lakini moja ya makundi ambayo yanaonyesha kuguswa na suala hilo ni Wamarekani Weusi. Kama ilivyo kwetu Waafrika, Wamarekani Weusi wamekuwa wapinzani wakubwa si tu wa ndoa, bali hata uhusiano wa kawaida wa watu wa jinsia moja. Mara kadhaa wasanii wengi wa muziki wa kufokafoka (hip-hop/rap), ambao ni maarufu kwa Wamarekani Weusi, wamekuwa wakilaumiwa kwa tungo zao zenye kuonyesha bayana upinzani dhidi ya ushoga.
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, baadhi ya viongozi wa makanisa ya Wamarekani Weusi wameeleza bayana kuwa hawamuuingi mkono Obama katika suala hilo, huku wengine wakitishia kutompigia kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Japo Obama anaendelea kuungwa mkono na kundi hilo (la Wamarekani Weusi) huku akionekana kuwa ni ‘mwenzao’, kura za maoni zinaonyesha kuwa asilimia 49 inampinga katika msimamo wake kuhusu ndoa za mashoga kulinganisha na asilimia 43 ya Wamarekani Weupe.
Obama mwenyewe amekiri kuwa anafahamu bayana msimamo wake huo utawaudhi baadhi ya wanaomuunga mkono. Lakini akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha luninga cha ABC cha Marekani, Rais huyo alieleza kuwa inamwia vigumu kuendelea na ‘sintofahaumu’ katika ‘ubaguzi’ dhidi ya mashoga ilhali Wamarekani kadhaa anaowaongoza wamo kwenye kundi hilo.
Alifafanua kuwa kama mzazi, alikuwa anapata wakati mgumu kutokuunga mkono ndoa za mashoga ilhali wanae Sasha na Malia wana  baadhi ya marafiki zao ambao wazazi wao ni mashoga.
Kadhalika, alieleza kuwa ilikuwa inamsumbua pia kuendelea kutokuunga mkono ndoa za mashoga huku baadhi ya makundi muhimu katika nchi hiyo, kwa mfano, wanajeshi wanaolitumikia taifa hilo kwa uadilifu mkubwa, yakijumuisha mashoga.
Lengo la makala hii si kumuunga mkono au kumpinga Obama katika msimamo wake huo kwa ndoa za mashoga bali kupigia mstari nafasi ya ujasiri katika uongozi.
Kama alivyokiri mwenyewe kuwa anafahamu bayana uamuzi wake wa kutangaza hadharani msimamo wake kuhusu ndoa za mashoga utawakera wengi, na pengine kumgharimu katika uchaguzi mkuu ujao, lakini Obama ameweza kufanya ujasiri wa kusimamia kile anachokiamini.
Japokuwa kuna baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaotafsiri hatua hiyo ya Obama kama kigeugeu-kwa maana alishawahi kuwa mpinzani wa ushoga- huku wengine wakidai hatua hiyo ni ‘janja yake’ tu kusaka kura za mashoga, jambo la msingi hapa ni ukweli kwamba amediriki kuweka kando uoga (huku akijua madhara) na kuweka wazi wapi anasimamia katika suala hilo.
Kwa upande fulani, uamuzi huo unaweza kumnufaisha dhidi ya mpinzani wake mtarajiwa kutoka chama cha Republicans, Mitt Romney, ambaye kama ilivyo kwa wahafidhina wengi, suala la ushoga ni kama laana.
Sasa, kwa vile moja ya misingi muhimu ya taifa la Marekani ni uhuru wa mtu kufanya apendacho alimradi havunji sheria, sambamba na kupinga ubaguzi wa aina yoyote ile, Obama na wanaomuunga mkono wanaweza kuutumia upinzani wa Romney dhidi ya ndoa za mashoga kama mfano hai wa jinsi mgombea huyo (mtarajiwa) na chama chake cha Republicans walivyobobea kwenye ‘ubaguzi na kuminya uhuru’  wa Wamarekani.
Kwa mtizamo wangu, ujasiri alionyesha Obama (bila kujali kama naafikiana au ninapingana naye katika suala la ndoa za mashoga) ninaulinganisha na kauli za hivi karibuni za aliyekuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa sasa wa Monduli (CCM), Edward Lowassa. Naomba niweke wazi kuwa ninaamini wasomaji wengi wa makala hizi wanafahamu fika msimamo wangu dhidi ya Lowassa, hususan kuhusiana na tuhuma za ufisadi. Lakini msimamo huo haumaanishi nichelee kumuunga mkono pale anapoonyesha ujasiri wa kisiasa.
Kwa muda mrefu sasa, Lowassa amejitokeza kuwa mmoja wa wanasiasa wachache ndani ya CCM wanaoeleza waziwazi mapungufu ya chama hicho na jinsi yanavyoliathiri taifa kwa ujumla. Lakini kama ilivyozoeleka, msimamo huo (ambao hapa ninauita ujasiri) umemfanya mwanasiasa huyo aonekane kama kiumbe hatari kabisa kwa ustawi na uhai wa chama hicho tawala.
Majuzi, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alinukuliwa akimpinga Lowassa kutokana na kauli yake katika mkutano wa hadhara huko Mto wa Mbu, Arusha, kuwa tatizo la CCM ni uongozi kuacha kusimamia misingi. Katika majibu yake kwa Lowassa, Mukama alimtaka mbunge huyo wa Monduli kushughulikia matatizo jimboni kwake kwanza.
Kuna wanaotafsiri kuwa msimamo wa Lowassa kukikosoa chama chake ni sehemu tu ya mikakati yake ya kuwania urais mwaka 2015. Lakini wanaofikiria hivyo wanapaswa kumtendea haki mwanasiasa huyo hasa kwa vile hajatangaza kuwa atagombea urais katika uchaguzi mkuu ujao. Kadhalika, ni muhimu kutanua upeo wetu na kuzichambua kauli za Lowassa pasipo kuzihusisha zaidi na malengo yake ya baadaye ya kisiasa.
Kimsingi, tukiweka kando hisia za ‘unafiki wa kisiasa’, anayoongea Lowassa kuhusu CCM ni ya kawaida sana kwa maana kwamba kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufikiri anaelewa ‘mchango wa CCM katika kukwaza maendeleo ya nchi yetu.’
Kama chama tawala, CCM haiwezi kujinusuru dhidi ya shutuma kwamba inachangia sana kukwaza jitihada za kulikwamua taifa kutoka kwenye lindi la umasikini unaochangiwa zaidi na vitendo vya ufisadi.
Kwamba Lowassa ni mmoja wa wana-CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi si sababu ya kumfanya mwanasiasa huyo kutozungumzia suala hilo. Na hata hizo tuhuma dhidi yake zinaweza kukosa nguvu kwa vile CCM yenyewe imeshindwa kuchukua hatua zozote dhidi yake.
Makala hii haina maneno ya kuitia moyo CCM katika msimamo wa baadhi ya viongozi wake wanaokerwa na kauli za Lowassa, hasa ikizingatiwa kuwa anachofanya mwanasiasa huyo ni kuwakilisha tu mtizamo wa Watanzania wengi (ikiwa ni pamoja na wana-CCM) dhidi ya chama hicho tawala. CCM inaweza hata kumtimua Lowassa lakini isipojirekebisha, kuna kila dalili kuwa itang’olewa madarakani huko mbeleni.
Japo ninaelewa msimamo wa Mukama kwamba kama kiongozi wa CCM Lowassa anapaswa kuongelea matatizo ya chama hicho kwenye vikao vya ndani, kimsingi hilo ni moja ya vyanzo vya matatizo yanayosababisha watu kama Lowassa kuamua kuweka hadharani matatizo hayo.
Ni hivi, kama chama hicho kina matatizo, kisha yanazungumzwa kwenye vikao vya ndani na hayapatiwi ufumbuzi, kwa nini basi kiongozi asishawishike kuyaongelea matatizo hayo hadharani?
Halafu kuna suala la maslahi ya taifa dhidi ya maslahi ya chama. Kwa vile CCM ni chama tawala, kila inachofanya au kuzembea kufanya kinaligusa taifa moja kwa moja. Kwa mantiki hiyo, wakati Mukama anaweza kuyaona matatizo ya CCM kuwa ni suala la kichama, kiuhalisi matatizo hayo si tu yanaligusa taifa bali pia ni suala la kitaifa. Na kwa vile Tanzania ni yetu sote, basi ni sahihi na halali kwa kila Mtanzania, ikiwa ni pamoja na Lowassa, kuyaongelea matatizo yanayolisumbua taifa letu pasi uoga wa kumuudhi mtu flani.
Naomba kuhitimisha makala hii kwa kurejea kuweka bayana msimamo wangu kuwa lengo halikuwa kuunga mkono msimamo wa Obama kuhusu ndoa za mashoga wala kugeuka muungaji mkono wa Lowassa (japo vyote si dhambi).
Makala hii imelenga kuwapongeza wanasiasa hao kwa ujasiri wa kuweka wazi misimamo yao hata pale kufanya hivyo kunapoweza kuwaingiza matatizoni. Kinyume cha ujasiri ni uoga na unafiki, na sote tunafahamu kuwa kiongozi mwoga na/au mnafiki si tu hawezi kusimamia yale anayoamini lakini pia ni kikwazo katika jitihada za kuleta mabadiliko muhimu kwa anaowaongoza.

Wednesday, May 23, 2012

Taarifa Muhimu Kutoka kwa Mheshimiwa John Mnyika Kuhusu Hukumu Dhidi ya Ubunge wake Kesho




WEDNESDAY, MAY 23, 2012


Hukumu kesho itakuwa mahakama kuu kivukoni na sio mahakama ya kazi akiba

Nimepokea taarifa kwamba hukumu ya kesi ya uchaguzi dhidi ya ushindi wetu Jimbo la Ubungo kesho tarehe 24 Mei 2012 itatolewa katika Jengo la Mahakama Kuu (Kivukoni- Court No. 1) badala ya jengo ilipo mahakama ya kazi (akiba) ambapo kesi iliendeshwa. Kama tulivyotafuta kura pamoja, tukapanga mstari kupiga kura pamoja na tukakesha kuzilinda pamoja tujumuike pamoja kujua hatma ya kura zetu. Hukumu ya kesi inatarajiwa kuanza kusomwa saa nne asubuhi hata hivyo ni muhimu kuwahi mapema zaidi asubuhi kwa ajili ya itifaki za kuingia mahakamani. Maslahi ya Umma kwanza

Tuesday, May 22, 2012

Toleo la Pili la Makala za Sauti: Shukrani na Uhamasishaji Dhidi ya Ubinafsi

Kwanza ninawashukuru wote walionipatia mchango wao wa mawazo kuhusu idea hii ya Makala za Sauti.Ninasema ASANTENI SANA.Pili,wengi wa mlionitumia maoni yenu mmezungumzia uhafifu wa sauti.Nimelifanyia kazi hilo na ndio iliyopelekea kutengeneza makal nyingine leo ili kupata mawazo kama kiwango na ubora wa sauti vinaridhisha.

Kwahiyo,makala ya leo imelenga zaidi kutoa shukrani kwa mapokezi niliyopewa kuhusiana na makala za sauti,na kidogo nimejaribu kuongelea jinsi kila mmoja wetu anavyoweza ku-play role yake katika kuifanya Tanzania yetu kuwa bora zaidi.

Basi naomba nikuache unisikilize hapa chini

Kitu Kipya Bloguni: Makala za Sauti (AUDIO MESSAGES)

Ninafanya majaribio ya kuwaletea makala zilizorekodiwa (za sauti) ambapo kama ilivyo hapa bloguni na katika makala zangu gazetini,nitakuwa nikijadili masuala mbalimbali.Ninaanza na sekta ya huduma ambapo mlengwa mkuu ni TANESCO.Nakuomba sana msomaji na msikilizaji unipatie mawazo na ushauri kuhusu wazo hili (hata kuniambia kuwa ni wazo baya ni ushauri pia).

Toleo la kwanza (nataraji kufanya audio hizi angalau mara moja kwa wiki) ni hili hapa Natambua kuwa kiwango cha audio sio cha hali ya juu lakini toleo hili la kwanza ni la majaribio,na iwapo wasomaji mtaafiki wazo hili basi nitajitahidi kupata nyenzo bora ya kurekodia ujumbe husika.

Saturday, May 19, 2012

Tuwasapoti wadogo zetu wa Biafra Sports Club



Timu ya soka ya watoto ya Biafra Kids inashiriki katikamichuano ya soka ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 17 kanda ya Kinondoni.




WADOGO ZETU HAWA WANAOMBA MSAADA WA HALI NA MALI KUWAWEZESHA WAFANIKIWE KATIKA NDOTO ZAO KISOKA.UNAWEZA KUANZA KWA KUWATEMBELEA KWENYE UKURASA WAO WA Google+ UNAOPATIKANA KATIKA ANUANI IFUATAYO 


Tuesday, May 15, 2012

Usikose Kutembelea Blogu Mpya ya Kiingereza ya EAST AFRICA HERALD


BONYEZA PICHA KUINGIA KWENYE BLOGU YA

Monday, May 14, 2012

We Are The Champions: Manchester City Watwaa Ubingwa Ligi ya England (PICHA)

Let's party! Manchester City's jubilant players lift the Premier League trophy after the late drama
Baada ya miaka 44,Manchester City ni mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya England

Ice cool: Aguero blasts home to seal the 3-2 victory that made City champions after a 44-year wait
GOOOOOAL: Bao la tatu na la ubingwa kutoka kwa Muajentina Sergio Aguero

Incredible: Goal hero Sergio Aguero celebrates winning the title at the final whistle
Kama ndoto vile,wakati kila mshabiki akidhani Man City wamepoteza nafasi ya kutwaa ubingwa,Aguero akapachika bao la tatu

Striking at the death: Aguero wheels away after his magical late goal sealed the title for City
Aguero,ambaye ni mkwe wa gwiji la soka duniani Diego Maradona,akiwa amevua jezi kushangilia bao lililopatikana muda wa nyongeza na lililoipa ubingwa Man City baada ya kusubiri miaka 44


Amazing: Aguero is mobbed as the City fans struggle to believe what they are seeing
Mario Balotelli na Edin Dzeko wakimkimbilia Aguero kumpongeza kwa kufunga bao la tatu

Can you believe it? City players go wild after Sergio Aguero's last-gasp heroics against QPR
Wachezaji wa Man City wakimzonga Aguero baada ya kufunga bao la tatu lililowapa ubingwa

Roberto Mancini celebrates with the trophy
Kocha Mtaliano Roberto Mancini akiwa na kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya England

Vincent Kompany the captain of Manchester City poses with the trophy
Nahodha Vincent Kompany akiwa na kombe

Beautiful moment: Mancini and Carlos Tevez hold the trophy after putting their troubles behind them
Uhasama kando: Mancini na Carlos Tevez wakiteta huku wameshikilia kombe

Star showing: Liam Gallagher (top middle) celebrates with the City fans at the end of the match
Shabiki mkubwa wa Man City,mwanamuziki mkongwe Liam Ghallagher (ex-Osias) akisherehekea

Never forget: City fans party on the pitch after their epic comeback against QPR
Furaha isiyoelezeka

Our moment: City supporters pour on to the pitch at the final whistle at the Etihad Stadium
Shangwe kubwa

Now we rule the city: Manchester City fans celebrate with a banner aimed at their rivals
Furaha tupu

Top of the tree: City's players throw their arms in the air after securing their long-awaited title
Furaha kubwa ya kutwaa ubingwa baada ya kusubiri kwa miaka 44

Smiles better: Mario Balotelli (centre) shares a joke with manager Roberto Mancini as they wear Italian flags
Kocha wa Man City Roberto Mancini akifurahi na wachezaji wake

Show us your medal: Joe Hart holds team-mate David Silva as they enjoy their moment
Kipa wa Man City Joe Hart akiwa amembeba mchezaji mwenzie David Silva

Shocked: Sir Alex Ferguson looks visibly stunned by the late news coming in from City
Kocha wa Man United Sir Alex Ferguson akiwa haamini macho na masikio yake kuwa timu yake imepoteza ubingwa kwa wapinzani wao wa Manchester City

Nightmare: United's players are helpless as they absorb the news coming in from the Etihad Stadium
Wachezaji waManchester United wakipokea habari za ushindi wa Manchester City kwa bumbuwazi
Chanzo: Daily Mail

 
Design by Free WordPress Themes | Bloggerized by Lasantha - Premium Blogger Themes | Hot Sonakshi Sinha, Car Price in India